Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Myanmar “Nchi ya Kidhahabu”

Myanmar “Nchi ya Kidhahabu”

Myanmar “Nchi ya Kidhahabu”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MYANMAR

“NCHI ya Kidhahabu” iko katikati ya milima inayoitenganisha na nchi jirani za Asia. Ghuba ya Bengal na Bahari ya Andaman ziko upande wa kusini-magharibi wa nchi hiyo iliyo na pwani yenye urefu wa kilometa 2,000 hivi. Bangladesh na India ziko magharibi; China iko kaskazini; na Laos na Thailand ziko mashariki. Nchi hiyo ni kubwa kidogo kuliko Madagascar na ni ndogo kuliko jimbo la Texas la Marekani. Nchi hiyo huitwaje? Myanmar, na hapo zamani iliitwa Burma.

Wakazi wa kwanza kabisa wa Myanmar waliiita nchi hiyo Nchi ya Kidhahabu. Nchi hiyo ina mali asili nyingi muhimu, kama vile: mafuta na gesi, shaba, bati, fedha, tang’isteni, na madini mengine. Pia, kuna vito vyenye thamani kama vile yakuti, zumaridi, rubi, na vito vyenye rangi ya kijani. Mali asili nyingine zatia ndani misitu ya mvua ya kitropiki yenye miti isiyopatikana sana, kama vile msaji, rosewood, na padauk. Misitu hiyo pia ina wanyama-pori wengi kama vile, tumbili, simba-milia, dubu, nyati, tembo, na kadhalika. Lakini wenyeji wa Nchi ya Kidhahabu ndio wenye thamani zaidi.

Wenyeji wa Myanmar

Kwa kawaida, wenyeji wa Myanmar ni wapole na watulivu, nao wana adabu nzuri na ni wakarimu. Wao huwatendea wageni kwa heshima na adhama. Kwa kawaida, watoto huwaita wanaume wenye umri mkubwa mjomba, na wanawake wenye umri mkubwa shangazi.

Mara nyingi wageni wanaotembelea Myanmar hushangazwa na ngozi laini ya watu wazee. Wanawake wa huko wanasema kwamba ngozi hiyo laini kama ya kijana hutokezwa na kipodozi cha rangi hafifu ya dhahabu kinachoitwa thanaka. Kipodozi hicho hutengenezwa kutokana na mti wa thanaka. Wanawake hufanyiza rojorojo laini kwa kusaga tawi la mti huo kwenye jiwe gumu tambarare kisha wanaongeza maji kidogo. Wao hupamba nyuso zao kwa kutumia kipodozi hicho. Kipodozi cha thanaka hulainisha, hutuliza, na kulinda ngozi na jua kali la tropiki.

Vazi la lungi ndilo huvaliwa kwa kawaida na wanaume na wanawake nchini Myanmar. Vazi hilo hutengenezwa kwa urahisi kwa kushona ncha mbili za kitambaa chenye urefu wa meta mbili hivi. Wanawake hulivaa kwa kuingia ndani yake, kisha wanalizungusha kama sketi, na kuingiza kiunoni ncha moja inayoning’inia. Nao wanaume hulivaa kwa kufunga ncha zote mbili za vazi hilo kiunoni. Kwa kuwa vazi la lungi ni nadhifu na halibani, linafaa kabisa maeneo ya tropiki.

Ukitembelea masoko utaona kwamba watu wa Myanmar wana vipawa vingi. Wana ustadi wa kufuma hariri, kutengeneza vito, na kuchonga vinyago vya mbao. Vinyago vinavyovutia vya wanadamu, simba-milia, farasi, nyati, na tembo vimetengenezwa kwa mbao za msaji, padauk, na miti mingine. Hata vitu vya kawaida kama meza, kuta zinazotenganisha vyumba, na viti vimechongwa mapambo mengi sana. Lakini iwapo unataka kununua vitu hivyo, uwe tayari kupigania bei!

Wenyeji wa Myanmar pia hutengeneza vyombo vinavyopendeza kwa vanishi kama vile, mabakuli, sahani, na masanduku yenye vifuniko. Lakini vyombo vyao ni vya pekee hasa kwa sababu michoro na mapambo yake si ya kawaida. Wao huanza kufuma vyombo vyao kwa kutumia kamba za mwanzi. (Vyombo vya hali ya juu hufumwa kwa mwanzi na manyoya ya farasi.) Chombo kilichofumwa hupakwa vanishi mara saba. Vanishi hiyo hutengenezwa kwa kuchanganya mafuta ya mti wa thisei, au mti wa lacquer, pamoja na mifupa ya wanyama iliyochomwa na kusagwa.

Vanishi hiyo inapokauka, msanii huchonga mchoro kwenye chombo hicho kwa kutumia kifaa cha kuchora cha chuma. Kisha, chombo hicho hupakwa rangi na kung’arishwa nacho huvutia sana na kinaweza kutumiwa nyumbani.

Dini Imeathiri Mambo Mengi

Asilimia 85 hivi ya wenyeji wa Myanmar ni Wabudha; na watu wale wengine ni Waislamu na Wakristo. Kama ilivyo katika nchi nyingi za Kusini-Mashariki mwa Asia, dini ni muhimu kwa wenyeji wengi wa Myanmar. Hata hivyo, wageni wengi hawafahamu desturi fulani za dini za huko.

Kwa mfano, watawa Wabudha wameweka nadhiri kutomgusa mwanamke. Hivyo, kwa heshima, wanawake huwa waangalifu wasiwakaribie sana watawa hao. Desturi za kidini huathiri watu pia wanaposafiri kwa basi. Mtu wa nchi ya Magharibi aweza kushangazwa anapoona ishara kwenye basi inayosema hivi: “Tafadhali usimuulize dereva tutafika lini.” Je, ishara hiyo imewekwa kwa sababu madereva hukasirishwa na abiria wenye haraka? La. Wabudha wa huko huamini kwamba akina nat (roho) watakasirishwa na swali hilo na huenda wakachelewesha basi.

Historia ya Myanmar

Historia ya mapema kabisa ya Myanmar haijulikani sana, lakini yaonekana kwamba makabila fulani yalihamia huko kutoka maeneo ya karibu. Watu wa kabila la Mon waliiita nchi hiyo Suvannabhumi—maana yake ni, “Nchi ya Kidhahabu.” Watu walioongea Kitibeti-Burma walihamia huko kutoka sehemu ya mashariki ya milima ya Himalaya na watu wa kabila la Tai walitoka mahala ambapo sasa ni kusini-magharibi mwa China. Milima mingi ya Myanmar ilitenganisha makabila. Hiyo ndiyo sababu kuna makabila mengi na lugha nyingi.

Mapema katika karne ya 19, Waingereza walioishi katika koloni yao mpya ya India walianza kuwasili. Kwanza walikaa kwenye eneo la kusini halafu wakamiliki nchi yote. Kufikia 1886, Burma, jina la Myanmar la zamani, ikawa sehemu ya British India.

Wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu, nchi hiyo ilikuwa eneo la vita, na baada ya miezi michache mnamo mwaka wa 1942, majeshi ya Wajapani yaliwaondoa Waingereza. Kisha, reli yenye sifa mbaya iliyoitwa “Reli ya Kifo” ilijengwa. Reli hiyo yenye urefu wa kilometa 400 ilipita kwenye maeneo hatari ya msituni na milimani nayo iliunganisha mji wa Thanbyuzayat huko Burma na mji wa Nong Pladuk nchini Thailand. Kwa sababu kulikuwa na uhaba wa metali, sehemu kubwa ya reli hiyo ilitengenezwa kwa vyuma vya reli vilivyotolewa katikati ya nchi ya Malaya (ambayo sasa ni Malaysia). Sehemu ndogo ya mradi huo—kujenga daraja juu ya Mto Kwai—ilitumika baadaye kama habari kuu ya filamu moja maarufu.

Wanaume zaidi ya 300,000—watu waliotekwa vitani na wenyeji wa India na Burma—walijenga reli hiyo wakisaidiwa na tembo 400. Makumi ya maelfu ya watu walikufa wakifanya kazi hiyo. Reli hiyo ilishambuliwa sana na ndege za kurusha mabomu za majeshi ya Muungano. Hivyo, haikutumika sana na mwishowe iliacha kutumiwa kabisa. Baadaye, vyuma vingi vya reli viling’olewa na kutumiwa kwingineko.

Hatimaye, Waingereza wakafanikiwa kumiliki nchi hiyo tena walipowashinda Wajapani mnamo mwaka wa 1945. Lakini Waingereza hawakutawala kwa muda mrefu, kwani Burma ilipata uhuru mwezi wa Januari 4, 1948. Mnamo Juni 22, 1989, shirika la Umoja wa Mataifa liliidhinisha jina jipya la nchi hiyo, Myanmar.

Nchi Yenye Majiji Makuu ya Kidhahabu

Nchi ya Myanmar imekuwa na majiji mengi makuu katika karne zilizopita. Kwa mfano, katikati ya Myanmar, utapata jiji la Mandalay ambalo kwa kawaida huitwa Jiji la Kidhahabu. Jiji hilo lenye minara mingi ya kila aina inayoitwa pagoda, lina watu 500,000 nalo ndilo lililokuwa jiji kuu kabla ya Waingereza kumiliki nchi hiyo. Mfalme Mindon alifanya jiji la Mandalay kuwa jiji la kifalme alipojenga jumba kubwa la kifalme huko mnamo mwaka wa 1857 kwa ajili yake na malkia zake. Jiji hilo la kale lenye ukubwa wa kilometa za mraba 4 limezingirwa na ukuta wenye kimo cha meta 8 na upana wa meta 3. Handaki la maji lenye upana wa meta 70 huzunguka ukuta huo.

Mnamo mwaka wa 1885, Waingereza walimpeleka mwandamizi wa Mindon, Mfalme Thibaw, uhamishoni huko India, lakini hawakuharibu jumba hilo la kifalme. Hata hivyo, jumba hilo la kifalme liliteketezwa kabisa kwa moto wakati wa Vita ya Pili ya Ulimwengu. Watu wa Myanmar hawakukata tamaa, bali walijenga tena jumba jingine la kifalme lililofanana kabisa na lile la kwanza pamoja na majengo yake ya mbao ya rangi nyekundu na ya dhahabu kwenye eneo hilohilo. Watu wanaweza kutembelea jumba hilo.

Jiji la Pagan liko umbali wa kilometa 200 kutoka Mandalay. Hilo lilikuwa jiji kuu jingine lililojengwa katika milenia ya kwanza ya Wakati wa Kawaida na liliendelea sana katika karne ya 11. Lakini, jiji hilo liliachwa miaka 200 baadaye. Hata hivyo, katikati na karibu na vijiji vichache kuna mamia ya minara na mahekalu mazee ya Kibudha yanayoonyesha jinsi jiji hilo lilivyokuwa lenye fahari hapo kale.

Jiji kuu la sasa, Yangon (ambalo lilikuwa likiitwa Rangoon hadi mwaka wa 1989), ambalo lina zaidi ya watu milioni tatu, ni jiji lenye utendaji mwingi. Magari, mabasi, na teksi zisizo na madirisha hupita huku zikipiga honi. Ingawa kuna majengo mengi ya kale yaliyojengwa kando ya barabara za Yangon zenye miti wakati wa ukoloni wa Waingereza, sasa jiji hilo pia lina hoteli na majengo marefu sana ya kisasa ya ofisi.

Katikati ya majengo hayo, kwenye jengo la Shwedagon Pagoda, kuna mnara-pia wenye kimo cha meta 98 ambao umefunikwa kwa dhahabu. Jengo hilo lilijengwa miaka 2,500 iliyopita nalo linaonyesha ufanisi na usanifu-ujenzi bora wa kale. Yasemekana kwamba mnara-pia huo ulirembeshwa na vito na almasi 7,000 hivi. Sehemu ya juu kabisa ya mnara-pia huo ina almasi yenye uzito wa karati 76. Kama ilivyotokea kwa majengo mengi ya kale huko Myanmar, jengo la Shwedagon pia limeharibiwa na matetemeko ya ardhi na vita, na sehemu kubwa ya jengo hilo imejengwa upya.

Hata hivyo, watu fulani hudai kwamba mnara wa kidhahabu wa Sule Pagoda ndio mnara unaovutia zaidi huko Yangon. Mnara huo wenye kimo cha meta 46, ambao ulijengwa miaka 2,000 iliyopita, uko kwenye makutano ya barabara nne kuu za jiji hilo. Mnara huo umezungukwa na maduka.

Dhahabu ya Kiroho

Mnamo mwaka wa 1914, Wanafunzi wawili wa Biblia wa Kimataifa (kama Mashahidi wa Yehova walivyojulikana wakati huo) waliwasili Rangoon kutoka India wakiwatafuta watu waliothamini dhahabu yenye thamani kubwa zaidi—dhahabu ya kiroho. Mnamo mwaka wa 1928 na 1930, wamishonari wengine walifika huko. Kufikia mwaka wa 1939, makutaniko matatu yenye Mashahidi 28 yalikuwa yameanzishwa. Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya India, iliyokuwa Bombay, ilisimamia kazi huko hadi mwaka wa 1938. Kuanzia mwaka huo hadi mwaka wa 1940, ofisi ya tawi ya Australia ilisimamia kazi iliyofanywa Myanmar. Baada ya Vita ya Pili ya Ulimwengu, ofisi ya tawi ya kwanza ya Myanmar ilianzishwa huko Rangoon katika mwaka wa 1947.

Mnamo Januari 1978, ofisi ya tawi ilihamishwa kwenye Barabara ya Inya. Makao makuu hayo yenye orofa tatu yanaitwa Betheli ya Myanmar. Washiriki 52 wa familia ya Betheli hushughulikia mahitaji ya Mashahidi wapatao 3,000 nchini humo. Kwa kuwa lugha nyingi za kienyeji hutumiwa nchini Myanmar, sehemu kubwa ya kazi inayofanywa kwenye ofisi hiyo ni ya kutafsiri. Kazi nyingi inayofanywa na Mashahidi wa Yehova inaongeza ‘dhahabu’ zaidi katika Nchi ya Kidhahabu.

[Ramani katika ukurasa wa 17]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BANGLADESH

INDIA

CHINA

LAOS

THAILAND

MYANMAR

Mandalay

Pagan

YANGON

GHUBA YA BENGAL

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 17]

Kutoka juu: Wanaume na wanawake huvaa mavazi ya “lungi”; mtawa mchanga wa Kibudha; wanawake waliojipaka kipodozi cha “thanaka”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kuhubiri katika shamba la njugu

[Picha katika ukurasa wa 18]

Vinyago vya mbao huuzwa masokoni

[Hisani]

chaang.com

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kuchonga pambo kwenye ubao wa juu wa meza uliotengenezwa kwa vanishi

[Picha katika ukurasa wa 18]

Bakuli linalopendeza lililotengenezwa kwa vanishi

[Hisani]

chaang.com

[Picha katika ukurasa wa 20]

Ofisi ya tawi ya Mashahidi wa Yehova ya Myanmar

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]

© Jean Leo Dugast/Panos