Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wauzaji wa Kale wa Vitabu na Bidhaa

Wauzaji wa Kale wa Vitabu na Bidhaa

Wauzaji wa Kale wa Vitabu na Bidhaa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

MIAKA kadhaa iliyopita, “jumba [dogo] la makumbusho” lilianzishwa kwenye kituo cha kuteleza kwa ski cha Deux-Alpes, chini ya mlima wa Jandri Glacier, kusini-mashariki mwa Ufaransa. Sanamu moja ya barafu iliyoonyeshwa hapo ilikuwa sanamu ya mwuzaji wa vitabu na bidhaa. Sanamu hiyo ilikuwa ukumbusho wa biashara ya kale ya milimani ya wauzaji wa vitabu na bidhaa.

Kwa karne nyingi wauzaji hao wa vitabu na bidhaa walitembea kutoka soko hadi soko na nyumba kwa nyumba wakiuza bidhaa walizokuwa wakizibeba shingoni (jina la muuzaji wa vitabu katika Kifaransa ni colporteur, nalo linatokana na neno col linalomaanisha shingo, na porter linalomaanisha kubeba). Watu wengi leo hawajawahi kusikia juu yao. Na wale ambao wamekwisha sikia juu yao, huenda wakadhani kwamba walikuwa wachuuzi duni wa vitu visivyo na maana. Hata hivyo, wauzaji hao wa vitabu na bidhaa wangali na uvutano mkubwa katika maisha ya mamilioni ya watu hadi leo hii.

Kuichunguza Kazi Yao

Wauzaji hao wa vitabu na bidhaa hawakuwa watu maskini wa hali ya chini bali wengi wao walikuwa wanabiashara waliopanga kazi yao kwa utaratibu, wakisambaza vitu vipya kotekote Ulaya. Hata hivyo, si wote waliofanya kazi ya kutembeza vitabu ili wapate faida ya kifedha. Wengine wao walifanya hivyo ili kueneza imani yao. Baadhi yao hata waliuawa kwa sababu ya kazi hiyo.

Yaelekea wauzaji hao walianza kufanya kazi hiyo mwishoni mwa kipindi kinachoitwa Enzi ya Kati (500-1500 W.K.). Wale wa kwanza walikuwa watu wa eneo la milima ya Alps lenye umbo la mwezi mwandamo, milima ya Pirenia, na Milima ya Scotland. Wengi walikuwa wakulima ambao walifanya kazi hiyo ya kutembeza bidhaa baada ya kumaliza kuvuna.

Mmojawapo alikuwa mwanamume Mfaransa aliyeitwa Jehan Gravier. Yeye na familia yake waliishi katika eneo la milimani linaloitwa La Grave katika karne ya 16. Alikubali kufanya kazi ya kuwapelekea wenyeji wa miji ya bondeni bidhaa za maeneo ya milimani kama vile mbao, ngozi, sufu, na chumvi, kwa sababu shamba lake halikutoa mazao ya kutosha. Watu kama Gravier walipeleka bidhaa hizo mjini na kuzibadili kwa nguo za wanaume, vyanuo, miwani, vitabu, dawa, tumbaku, na picha zilizochongwa. Kisha wakazi wa miji au wakulima walioishi mbali na duka waliuziwa bidhaa hizo. Baadhi ya wauzaji hao walitembea kilometa 20 kila siku! Watu wa ukoo walitunza mashamba yao na familia zao wakati hawakuwapo.

Hata hivyo, Gravier alifanya mengi zaidi ya kuuza tu vitu vidogo-vidogo. Rekodi zinaonyesha kwamba alidaiwa na mchapishaji fulani anayeitwa Benoît Rigaud. Jambo hilo linaonyesha kwamba Gravier aliuza vitabu, kama vile wauzaji wengine wengi walivyofanya. Gravier aliishi katika kipindi cha Mvuvumuko (1400-1700 W.K.) huko Ulaya, na biashara ya vitabu ilisitawi sana. Kati ya mwaka wa 1500 na 1600, vitabu milioni 140 hadi milioni 200 vilichapishwa Ulaya. Robo ya vitabu hivyo vilichapishwa Ufaransa. Mji wa Lyons, ulioko chini ya milima ya Alps, ulikuwa mji mkuu wa biashara nchini Ufaransa. Mji huo ulikuwa pia kitovu cha uchapishaji huko Ulaya, na vilevile cha uchapishaji wa vitabu vya Kifaransa. Kwa hiyo, Gravier alipata vitabu vingi vya kuuza. Hata hivyo, ijapokuwa wanaume kama vile Gravier waliuza vitabu kwa sababu tu ya faida za kifedha, wengine walisambaza vitabu kwa sababu za kidini pekee.

‘Wafanya-Magendo wa Imani’

Mtambo wa kuchapa ulipovumbuliwa, watu walianza kusoma vitabu, vijarida, na vijitabu vya dini kwa hamu. Biblia ilichapwa kwanza katika Kilatini na baadaye katika lugha za kawaida. Mamilioni ya Biblia zilichapwa Ujerumani, na wauzaji wa vitabu walizisambaza haraka kwa watu walioishi mashambani. Hata hivyo, ugawaji huo haukupendwa na wote.

Yapata mwaka wa 1525, Bunge la Ufaransa lilipiga marufuku utafsiri wa Biblia katika Kifaransa, na mwaka uliofuata, watu walikatazwa wasimiliki Biblia ya Kifaransa. Licha ya marufuku hayo, maelfu ya Biblia zilichapwa, na wauzaji jasiri wa vitabu walisambaza Biblia nyingi kotekote Ufaransa kisiri. Mmojawapo wa wauzaji hao alikuwa kijana aliyeitwa Pierre Chapot. Alikamatwa mwaka wa 1546 na kuuawa.

Hatimaye, katika mwaka wa 1551, Serikali ya Kikatoliki ya Ufaransa ilipiga marufuku kazi ya wauzaji hao ya kuuza vitabu, kwa kuwa waliuza “kisiri” vitabu “vilivyotoka Geneva,” yaani, kutoka kwa Waprotestanti. Hata hivyo, mambo hayakubadilika. Biblia nyingi ziliingizwa Ufaransa kwa njia zozote zile. Biblia nyingi zilikuwa ndogo, nazo zilifichwa kisiri chini ya pipa za divai, katika pipa za kokwa aina ya chestnut, au mahali pa mizigo katika merikebu. Mwanamume hodari aliyeitwa Denis Le Vair alikamatwa alipokuwa akisafirisha pipa lililojaa Biblia. Yeye pia aliuawa. Mkatoliki mmoja aliyechukia wauzaji hao wa vitabu alisema kwamba “kwa muda mfupi, walisambaza Agano Jipya la Kifaransa kotekote nchini Ufaransa.”

‘Wafanya-magendo [hao] wa imani,’ kama mwandishi mmoja anavyowaita, walikuwa hatarini daima katika karne ya 16. Wauzaji wengi wa vitabu walikamatwa, walifungwa gerezani, walipelekwa kuvuta makasia katika merikebu, walifukuzwa nchini, au kuuawa. Baadhi yao walichomwa kwa moto pamoja na vitabu vyao. Ni wauzaji wachache tu wa vitabu wanaojulikana kwa majina. Hata hivyo, kwa sababu ya jitihada za wauzaji wengi sana jasiri, familia nyingi za Waprotestanti walipata Biblia.

Maktaba Zilizohama-Hama

Katika karne ya 17, Kanisa Katoliki liliendelea kuzuia watu wa kawaida wasiisome wala kuimiliki Biblia. Waumini walipewa vitabu vya saa na vitabu vya maisha ya watakatifu badala ya Biblia—vibadala duni kwelikweli! * Lakini, Wakatoliki wa kikundi kilichoitwa Jansenists waliokuwa eti, “waasi wa dini,” waliunga mkono usomaji wa Maandiko Matakatifu. Kwa hiyo, wauzaji wa vitabu walishiriki kugawanya Maandiko ya Kigiriki (“Agano Jipya”) ya kikundi cha Jansenists, ambayo Le Maistre de Sacy alikuwa ametafsiri.

Wakati huohuo, wauzaji wa vitabu walianza kuuza vitabu vipya vya bei nafuu. Vitabu hivyo vilisaidia Wafaransa wengi kujifunza kusoma, navyo viliwaelimisha na kuwaburudisha hadi vilipotoweka katika karne ya 19. Wafaransa waliviita bibliothèque bleue, yaani, maktaba ya samawati, kwa kuwa majalada ya vitabu hivyo yalikuwa ya samawati. Huko Uingereza viliitwa chapbook; na nchini Hispania viliitwa pliégos de cordel. Vilikuwa na masimulizi juu ya mashujaa hodari waungwana wa Enzi ya Kati, habari za utamaduni na mila, masimulizi ya maisha ya watakatifu, na kadhalika. Kama unavyoweza kuwazia, wauzaji wa vitabu walitarajiwa kwa hamu, iwe walikuja katika majira ya kiangazi, kama wale waliotoka Pirenia walivyofanya, au katika majira ya baridi kali, kama wale wa Milima ya Alps ya Dauphiné.

Jambo la kupendeza ni kwamba, kazi ya wauzaji wa vitabu ilinufaisha watu walioelimika na wasioelimika. Uchunguzi uliofanywa katika karne ya 18 kuhusu wakulima wa eneo la kusini-magharibi la Ufaransa la Guienne, unasema hivi: “Wakati wa usiku mrefu wa majira ya baridi kali [wakulima] huwasomea watu waliokusanyika wa nyumba yao kwa muda wa nusu saa kuhusu maisha ya watakatifu, au sura moja ya Biblia. . . . Kama hakuna vitabu vingine vya kusoma, wanasoma . . . vile vitabu vya samawati na vitabu vingine visivyo na maana ambavyo wauzaji wa vitabu huwaletea watu wa mashambani kila mwaka.” Hata hivyo, Biblia ndiyo iliyopendwa sana, nayo ilipatikana hata katika nyumba za hali ya chini.

Mahali Wateja Walipopatikana

Wauzaji wa vitabu walitembeza bidhaa zao katika Milima ya Alps ya Ufaransa na ya Italia, Pirenia, Normandy, na kaskazini-magharibi mwa Ufaransa. Wauzaji wa vitabu kutoka Milima ya Alps ya Dauphiné pekee ndio walioongoza robo ya uuzaji wa vitabu kusini mwa Ulaya. Mwuza-duka mmoja wa vitabu mjini Geneva aliyeishi wakati huo alisema hivi: “Biashara ya kuuza vitabu nchini Hispania na Ureno, na hali kadhalika katika miji mingi ya Italia, inaongozwa na Wafaransa wa kijiji kimoja . . . cha Milima ya Alps ya Dauphiné.”

Wauzaji wa vitabu walifanikiwa kwa kuwa walikuwa “wafanyakazi wenye juhudi, bidii, na busara,” lakini mbali na hayo walifanikiwa pia kwa sababu walipenda familia yao, kijiji chao, na dini yao. Wengi wao walikuwa Waprotestanti ambao waliendelea kuwasiliana na wale waliokuwa wamehama nchi zao kwa sababu ya mnyanyaso. Kwa hiyo, wateja wa kawaida wa wauzaji hao wa vitabu walikuwa watu wa ukoo, wananchi wenzi, na watu wa dini zao walioishi kotekote Ulaya. Kwa mfano, familia ya Gravier, walitembeza vitabu katika nchi ya Ufaransa, Hispania, na Italia. Wauzaji wengine wa vitabu walisafiri hadi Uajemi na Amerika.

Mwanzo Mpya wa Kazi ya Kuuza Vitabu

Viwanda vikubwa vilipoanzishwa katika karne ya 19 hali ilibadilika sana na kazi ya kutembeza vitabu iliyokuwa imeendelea kwa vizazi vingi ilikoma kabisa. Hata hivyo, tangu mashirika mbalimbali ya Biblia yaanzishwe, Biblia imesambazwa kwa kiasi kisicho na kifani. Lakini, Kanisa Katoliki bado lilipinga ugawanyaji wa Biblia. Watu waliosambaza Biblia waliendelea kunyanyaswa na kushtakiwa mahakamani mpaka mwishoni mwa miaka ya 1800. Hata hivyo, kuanzia mwaka wa 1804 hadi 1909, waligawanya nakala milioni sita za Biblia nzima au za sehemu ya Biblia nchini Ufaransa pekee.

Lakini kazi ya kuelimisha watu juu ya Biblia haikuwa imemalizika. Katika mwaka wa 1881, gazeti la Zion’s Watch Tower and Herald of Christ’s Presence (lililochapwa Marekani) lilitoa mwito kwa Wakristo kufanya kazi ya kuhubiri habari njema. Lengo lilikuwa nini? “Kusambaza kweli ya Biblia kwa kuwafanya watu wasome.” Kufikia mwaka wa 1885, wahubiri 300 hivi walikuwa wameitikia mwito huo, nao walikuwa wakifanya kazi ya kuhubiri. Baadhi yao walisafiri hadi nchi za mbali, kama vile Barbados, Burma (sasa Myanmar), El Salvador, Finland, Guatemala, na Honduras. Vita ya Kwanza ya Ulimwengu ilipoanza, wahubiri hao walikuwa wamekwisha eneza ujuzi wa Biblia huko China, Kosta Rika, New Zealand, Norway, Poland, Sweden, Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, na Uswisi.

Wahubiri wa wakati wote wa kwanza miongoni mwa Wanafunzi wa Biblia (wanaojulikana kama Mashahidi wa Yehova leo) waliitwa colporteur. Baadaye jina hilo likabadilishwa, kwa kuwa maana yake haikuonyesha kwa usahihi lengo kuu la kazi yao—yaani, kufundisha Biblia. (Mathayo 28:19, 20) Isitoshe, jina hilo halikuonyesha kwamba walijitolea kufanya kazi yao pasipo kupata faida ya kifedha. Kwa hiyo, leo, wahudumu wa wakati wote wa Mashahidi wa Yehova wanaitwa mapainia.

Mwaka uliopita, mapainia 800,000 waligawa Biblia na vitabu vya Biblia bila malipo. Hawafanyi hivyo ili wapate faida ya kifedha, bali ‘kwa weupe wa moyo, ndiyo, wakiwa waliotumwa kutoka kwa Mungu, mbele ya Mungu, kwa ushirika na Kristo.’ (2 Wakorintho 2:17) Kwa hiyo, wahudumu hao mapainia wanafanya kazi kubwa zaidi kuliko kazi ile iliyofanywa na wale wauzaji wa vitabu. Hata hivyo, wauzaji wengi wa kale wa vitabu waliwawekea mfano bora wa bidii na imani.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 16 Kitabu hicho cha saa kilikuwa na sala zilizopasa kutolewa kwa heshima ya Maria katika saa maalumu.

[Picha katika ukurasa wa 24, 25]

Wauzaji wa vitabu na bidhaa waliwapelekea watu vitu vipya

Wauzaji wa vitabu walitarajiwa kwa hamu

[Hisani]

© Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris ▸

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Agano Jipya” la Le Maistre de Sacy, na kitabu kimoja cha maktaba ya samawati

[Hisani]

Kushoto kabisa: © Cliché Bibliothèque nationale de France, Paris Kushoto: © B.M.V.R de Troyes/Bbl.390/Photo P. Jacquinot

[Picha katika ukurasa wa 26, 27]

Wahubiri waligawanya vitabu vya Biblia

[Picha katika ukurasa wa 26]

Leo wahubiri wa wakati wote wanawatolea watu elimu ya Biblia bila malipo