Je, Tunaharibu Chakula Chetu?
Je, Tunaharibu Chakula Chetu?
KUJARIBU kuboresha vyakula kwa njia mbalimbali si jambo jipya. Kwa vizazi vingi wanadamu wamejaribu kuboresha vyakula kwa ukuzaji na uzalishaji mzuri ambao umetokeza namna mbalimbali za mazao, ng’ombe, na kondoo. Mwakilishi mmoja wa Usimamizi wa Chakula na Dawa wa Marekani alisema kwamba “karibu vyakula vyote unavyonunua vimeboreshwa kwa ukuzaji na uzalishaji.”
Lakini wanadamu wamejaribu kuboresha vyakula kwa njia nyingine pia. Mbinu nyingi za kutengeneza vyakula zimebuniwa ili kuboresha ladha au rangi yake, kuvihifadhi au kuvifanya viwe na umbo na ladha inayotakiwa. Watu wamezoea kula vyakula vilivyoboreshwa kwa njia hizo.
Lakini watu wengi wana wasiwasi kwamba mbinu mpya za kujaribu kuboresha vyakula huviharibu. Kwa nini? Baadhi ya watu wanahofu kwamba mbinu za siku hizi hufanya vyakula viwe hatari kwa afya. Je, hivyo ndivyo ilivyo? Tuchunguze mbinu tatu zinazotiliwa shaka. *
Homoni na Viuavijasumu
Katika miaka ya 1950, kiasi kidogo cha viuavijasumu kilianza kuongezwa kwenye chakula cha kuku, nguruwe, na ng’ombe katika nchi
kadhaa. Dawa hiyo inaongezwa ili kupunguza magonjwa, hasa mahali ambapo wanyama wanasongamana sana. Katika nchi fulani, vyakula vya wanyama huongezewa pia homoni, ili wanyama wakue haraka. Inadhaniwa kwamba homoni na viuavijasumu hulinda wanyama wasiambukizwe magonjwa na kufanya ufugaji ulete faida nyingi za kifedha. Wateja hunufaika kwa kuwa vyakula hivyo ni vya bei nafuu.Sababu hizo zinaonekana zinafaa. Lakini, je, nyama ya wanyama waliolishwa dawa hizo inaweza kumdhuru mlaji? Ripoti ya Kamati ya Jumuiya ya Ulaya ya Uchumi na Jamii ilionya kwamba mlaji anaweza kuambukizwa bakteria zisizouawa na viuavijasumu. Ripoti hiyo ilisema kwamba “baadhi ya bakteria hizo, kama vile Salmonella na Campylobacter, huenda zikasababisha magonjwa mabaya.” Isitoshe, vipi ikiwa vyakula vina mabaki ya viuavijasumu pia? Inahofiwa kwamba magonjwa yasiyotibika kwa viuavijasumu yangeweza kutokea hatua kwa hatua.
Namna gani nyama ya wanyama waliolishwa homoni? Profesa mmoja wa Munich huko Ujerumani, Dakt. Heinrich Karg anasema: “Wataalamu wote wanakubaliana kwamba nyama ya wanyama waliolishwa homoni haitadhuru afya, iwapo wanyama hao watalishwa homoni hiyo kwa kiwango kinachotakikana.” Hata hivyo, gazeti la Die Woche linaripoti kwamba ‘watafiti wamebishana kwa miaka 15 na hawajaweza kukubaliana’ kwamba nyama hiyo haidhuru afya. Na nchini Ufaransa kuwalisha wanyama homoni kumekatazwa katakata. Ni wazi kwamba mgogoro bado unaendelea.
Vyakula Vilivyonururishwa
Tangu majaribio yalipoanzishwa Sweden mwaka wa 1916, angalau nchi 39 zimekubali kuua viini kwenye chakula kama viazi, mahindi, matunda, na nyama kwa kiwango kidogo cha mnururisho. Kwa nini? Inasemekana kwamba mnururisho huua karibu bakteria, vimelea, na wadudu wote, hivyo mlaji anaepuka kuambukizwa magonjwa yanayosababishwa na vyakula. Mnururisho pia hufanya vyakula visiharibike.
Wataalamu wanasema kwamba, vyakula bora ni vyakula safi visivyotengenezwa viwandani. Lakini ni watu wachache sana katika nchi zilizoendelea wanaotumia wakati mwingi kupika. Gazeti la Test linasema kwamba kwa kawaida watu katika nchi hizo wanatumia “muda wa dakika kumi kupika kiamsha kinywa, na dakika kumi na tano kupika chakula cha mchana na muda huohuo kupika mlo wa jioni.” Kwa hiyo, si ajabu kwamba watu wengi hupendelea vyakula vya mikebe na vinavyodumu kwa muda mrefu. Lakini, je, vyakula vilivyonururishwa vinadhuru afya?
Katika mwaka wa 1999, Shirika la Afya Ulimwenguni lilichapisha matokeo ya uchunguzi uliofanywa na wataalamu wa mataifa mbalimbali. Walifikia mkataa kwamba vyakula vilivyonururishwa “havidhuru afya navyo vina virutubishi vya kutosha.” Wale wanaounga mkono mbinu hiyo wanasema ni kama kunururisha vitambaa vya kufunga vidonda hospitalini ili kuua vijidudu, au kuchunguza mizigo kwenye uwanja wa ndege kwa kutumia mnururisho. Hata hivyo, wachambuzi wanasisitiza kwamba mnururisho huharibu vyakula
na huenda pia kukawa na madhara yasiyojulikana bado.Kubadilisha Maumbile ya Mbegu
Kwa muda fulani wanasayansi wameweza kubadilisha maumbile ya mbegu kwa kuingiza chembe ya urithi ya kiumbe kimoja ndani ya kiumbe kingine cha aina hiyohiyo. Hata hivyo, wanasayansi wanaweza kufanya mengi zaidi leo. Kwa mfano, wanasayansi wamebadilisha maumbile ya aina fulani za nyanya na vilevile tunda la stroberi (strawberry) kwa kuingiza chembe ya urithi ya samaki ili matunda hayo yaweze kusitawi katika hali ya baridi.
Mbinu ya kubadilisha maumbile ya vyakula kwa kuingiza chembe tofauti za urithi imetetewa sana na vilevile kushutumiwa vikali. * Watetezi wa mbinu hiyo wanasema kwamba inaweza kutegemeka zaidi kuliko ukuzaji wa kawaida, na kwamba itaongeza mazao na kupunguza njaa. Lakini je, vyakula hivyo vinaweza kudhuru afya?
Wanasayansi wa vyuo vya elimu ya juu katika nchi ya Uingereza na Marekani, na vilevile Brazili, China, India, Mexico, na nchi nyingine zinazoendelea, waliandika ripoti kuhusu habari hiyo. Ripoti hiyo iliyochapishwa mwezi wa Julai, 2000 ilisema: “Kufikia leo, mbegu zilizorekebishwa maumbile zimepandwa kwenye mashamba ya hektari zaidi ya milioni 30 [ekari milioni 70], na mazao hayo hayajasababisha madhara yoyote ya afya.” Katika maeneo fulani vyakula hivyo huonwa kuwa vyenye kujenga afya kama tu vyakula vya kawaida.
Hata hivyo, watu katika maeneo mengine wana wasiwasi mwingi. Baadhi ya watu nchini Austria, Ufaransa, na Uingereza, wanatilia shaka ubora wa vyakula hivyo. Mwanasiasa mmoja wa Uholanzi alisema hivi juu ya vyakula vilivyobadilishwa maumbile: “Hatuvipendi vyakula vya aina hiyo.” Watu wanaopinga vyakula vya aina hiyo wanasema kwamba mbinu hiyo si ya asili, na huenda ikadhuru mazingira.
Baadhi ya wanasayansi huonelea kwamba uchunguzi zaidi unahitajika ili kuona ikiwa vyakula vilivyoongezwa chembe tofauti hudhuru walaji au la. Kwa mfano, Shirika la Tiba la Uingereza linaonelea kwamba vyakula hivyo vitanufaisha watu. Hata hivyo, shirika hilo linasema kwamba kwa kuwa kuna wasiwasi fulani kuhusu mambo kadhaa—kama vile mizio (allergy) ya vyakula hivyo—“ni lazima uchunguzi zaidi ufanywe.”
Kufanya Maamuzi Yanayofaa
Katika nchi fulani asilimia 80 ya vyakula vinatengenezwa viwandani. Mara nyingi vyakula hivyo huongezewa kemikali mbalimbali ili viwe na ladha na rangi inayotakiwa, na visiharibike. Kitabu kimoja chasema kwamba “ni lazima kemikali ziongezwe kwenye vyakula vingi vya kisasa, kama vile vyakula visivyo na
kalori nyingi, vitafunio, na vyakula vya mikebeni.” Mara nyingi vyakula hivyo vina viungo vilivyobadilishwa maumbile.Kwa miaka mingi ukulima ulimwenguni pote umeendeshwa kwa njia ambazo watu wengi wanaona ni zenye madhara. Kwa mfano, dawa za kuua wadudu zimetumiwa. Isitoshe, vyakula vinavyotengenezwa viwandani vimetiwa kemikali ambazo zimeathiri baadhi ya walaji. Je, mbinu mpya za ukuzaji ni hatari zaidi kuliko hizo za hapo awali? Hata maoni ya wataalamu hutofautiana. Uthibitisho mbalimbali wa kisayansi huunga mkono pande zote mbili.
Kwa kuwa watu wengi leo wanaona ni vigumu sana kuepuka vyakula vilivyotengenezwa na kukuzwa kwa mbinu za kisasa, na kwa sababu wana matatizo mengine makubwa zaidi, wameazimia kutohangaikia jambo hilo. Hata hivyo, wengine wana wasiwasi mwingi. Wewe na familia yako mnaweza kufanya nini endapo mna wasiwasi juu ya vyakula vilivyotengenezwa na kukuzwa kwa mbinu za kisasa? Huenda mwongozo unaotolewa katika sehemu inayofuata unaweza kuwasaidia. Hata hivyo, ni jambo la busara kwanza kuhakikisha kwamba tuna maoni yanayofaa kuhusu habari hiyo.
Chakula ni kama afya. Kwa sasa hatuna njia ya kupata wala chakula wala afya kamili. Kulingana na gazeti natur & kosmos la Ujerumani, hata watu wanaochagua vyakula na kuvitayarisha kwa uangalifu sana hawawezi kuhakikisha kwamba vyakula vyote wanavyokula vinajenga afya kabisa. Chakula kinachofaa mtu mmoja kinaweza kumdhuru mwingine. Kwa hiyo, tunahitaji kutumia busara tunapofanya uamuzi juu jambo hilo.
Biblia haituelezi uamuzi unaofaa kuhusu vyakula vilivyopo leo. Hata hivyo, inatufundisha sifa moja ambayo itatusaidia. Andiko la Wafilipi 4:5 linasema: “Hali yenu ya kukubali sababu na ijulikane kwa watu wote.” Tukiwa na busara tunaweza kufanya maamuzi mazuri bila kupita kiasi. Busara inaweza kutuzuia tusiwashurutishe wengine kukubali maoni yetu. Na inaweza kutuepusha tusibishane na wale walio na maoni tofauti.
Hata hivyo, hatari nyingi zinazohusu vyakula hazibishaniwi. Baadhi ya hatari hizo ni zipi, na unaweza kufanya nini uziepuke?
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 4 Kwa kawaida, kila mtu hula vyakula anavyopendelea. Gazeti la Amkeni! halipendekezi vyakula mbalimbali vinavyozungumziwa, wala halipendekezi kutokula vyakula fulani, iwe vimetengenezwa kwa njia gani. Mfululizo huu umeandikwa ili kuwajulisha wasomaji juu ya mambo yanayojulikana sasa kuhusiana na habari hiyo.
^ fu. 15 Tafadhali soma toleo la Amkeni! la Aprili 22, 2000.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Je, mla-nyama anaathiriwa na homoni na viuavijasumu ambavyo ng’ombe hulishwa?
[Picha katika ukurasa wa 6]
Ni jambo la busara kusoma maandishi kwenye vyakula vilivyotengenezwa viwandani
[Picha katika ukurasa wa 7]
Kuna faida kununua vyakula vilivyotolewa shambani karibuni