Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kanisa la Anglikana Limegawanyika

Kanisa la Anglikana Limegawanyika

Kanisa la Anglikana Limegawanyika

NA MWANDISHI WA AMKENI!NCHINI UINGEREZA

KONGAMANO la 13 la Lambeth la Kanisa la Anglikana lilifanywa huko Canterbury mwaka wa 1998 karibu na kanisa kuu ambalo limekuwepo kwa miaka 900. Akihutubia kongamano hilo, Askofu William E. Swing alitoa taarifa hii muhimu: “Ni lazima dini ikome kusababisha matatizo na ianze kutoa suluhisho. Mataifa hayawezi kuwa na amani iwapo dini hazina amani.”

Mgawanyiko uliopo kati ya dini mbalimbali unaonekana wazi kama vile mgawanyiko kati ya waumini na makasisi wa dini ileile. Askofu mmoja alikataa kuhudhuria kongamano hilo, ambalo limekuwa likifanywa baada ya kila miaka kumi tangu 1948, kwa sababu maaskofu wa kike walikuwepo. Watu fulani waliohudhuria walikataa kushiriki mazungumzo ya Biblia pamoja na wanawake hao.

Katika mkutano wa 1988, suala kuu lililojadiliwa lilihusu kuwaweka wanawake kuwa viongozi wa dini na katika mkutano wa 1998 suala kuu lilihusu ngono kati ya watu wa jinsia moja. Hatimaye, maaskofu waliamua kwamba ngono kati ya watu wa jinsia moja “imekatazwa na maandiko.” Mbona wakaamua hivyo?

Huenda ikawa Waanglikana walitaka sana kuimarisha uhusiano wao na Kanisa Katoliki. Na walitambua kwamba hakuwezi kuwa na majadiliano kati ya makanisa hayo mawili wakiendelea kuruhusu “makasisi wanaofanya ngono na watu wa jinsia yao.” Huenda pia walifikia uamuzi huo kwa kuhofu dini ya Uislamu. Kulingana na maaskofu wa Afrika, iwapo Waanglikana wangekubali kuwe na makasisi wanaofanya ngono na watu wa jinsia yao, wangekomesha kazi ya kueneza injili katika mataifa ya Kiislamu.

Kuhusiana na jambo jingine lililosababisha mgawanyiko kwenye kongamano hilo, gazeti la The Sunday Telegraph liliripoti hivi: “Katika sehemu fulani za Afrika, swala kuu la kidini ni ndoa ya wake wengi.” Askofu mmoja aliuliza hivi kuhusu tatizo linalowakabili Waanglikana huko Afrika: ‘Maaskofu hufanya nini wakati mtu aliye na wake wengi anapolitolea Kanisa mchango mkubwa?’ Gazeti la The Times la London lilitabiri hivi kuhusu matokeo ya mazungumzo hayo: “Maaskofu Waanglikana hawatapinga ndoa ya wake wengi.”

Hii ndiyo mara ya kwanza ambapo maaskofu Waanglikana wamezungumzia uhusiano wao na dini ya Uislamu. Askofu wa Kaduna huko Nigeria aliripoti kwamba “kuna chuki nyingi kati ya Wakristo na Waislamu nchini Nigeria” na akadai kwamba watu zaidi ya 10,000 wameuawa katika mapambano ya kidini nchini humo. Ilisemwa kwamba yawezekana kuepuka vita ya kidini huko Afrika kwa kuendelea tu kuelewa imani ya Kiislamu pole kwa pole.

Itakuwaje kwa wale watu milioni 70, ambao kulingana na kadirio fulani linalotiliwa shaka, ni washiriki wa Kanisa la Kianglikana? * Hakuna matumaini mazuri, kwani gazeti la The Times laripoti hivi: “Watazamaji na washiriki wengi wameshangazwa na kongamano hilo kwa sababu nyakati nyingine limefanana sana na mkutano wa chama cha kisiasa badala ya mkutano wa maombi ya kanisa la Kikristo.”

Basi haishangazi kwamba gazeti la The Sunday Times lilimalizia kwa kusema kwamba ‘kulikuwa na chuki na uhasama mwingi kwenye mkutano huo.’

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 9 Gazeti la The Times linasema kwamba idadi hiyo ya milioni 70 “inavutia,” lakini “jambo ambalo halisemwi mara nyingi ni kwamba milioni 26 kati ya idadi hiyo ni washiriki wa Kanisa la Anglikana. Watu wapatao milioni moja tu ndio huenda kanisani hapa [Uingereza], wengine ni Waanglikana kwa jina tu.”

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kanisa Kuu la Canterbury, limekuwepo kwa miaka 900