Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Pesa Chafu
Gazeti la The Globe and Mail la Kanada lasema kwamba “noti za pesa zimejaa bakteria.” Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Marekani ulionyesha kwamba karibu noti zote zinazotumika zina viini vya streptococcus, enterobacter, pseudomonas, na viini vingine. Gazeti la The Globe lasema kwamba viini hivyo “vyaweza kuhatarisha wagonjwa walio na mfumo wa kinga ulio dhaifu kama vile wazee-wazee walio dhaifu au watu walio na virusi vya UKIMWI.” Noti nyingine huwa na bakteria hatari hata zaidi. Watafiti wanadokeza kwamba inafaa “pesa zisafishwe.” Huko Japani watu wanaweza kupata pesa zao zilizo kwenye benki kupitia mashine za ATM ambazo ‘hutoa pesa ambazo zimepashwa joto hadi nyuzi 200 Selsiasi—halijoto inayotosha kuua bakteria nyingi bila kuchoma pesa hizo.’ Gazeti la The Globe lashauri kwamba baada ya kushika pesa “nawa mikono yako!”
Kupunguza Matumizi ya Chumvi Barabarani
Gazeti la mazingira la Terre sauvage laripoti kwamba wakati wa majira ya baridi kali, kati ya tani 400,000 na milioni 1.4 za chumvi humwagwa juu ya barabara nchini Ufaransa ili kuondoa theluji na barafu. “Chumvi yote hiyo inasababisha madhara katika mazingira ambayo yanagunduliwa pole kwa pole.” Chumvi iliyomwagwa kwenye barabara hurundamana udongoni na inaweza kuchafua visima, matabaka ya maji ya ardhini, maziwa, na vidimbwi. Chumvi hiyo hukausha mimea dhaifu inayopatikana meta 50 kutoka kwenye barabara zilizomwagwa chumvi na inaharibu mizizi ya miti. Chumvi hiyo huzuia usanidimwanga wakati inapofyonzwa na mizizi ya miti. Miti hudhoofika na kunyauka inapozidi kufyonza chumvi hiyo. Mara nyingi, wanyama wanaokwenda kwenye barabara hizo kulamba chumvi, hugongwa na magari au kufa kwa sababu ya kulamba chumvi nyingi upesi. Katika hali fulani, chumvi yaweza kufanyiza tabaka jembamba la barafu isiyoonekana barabarani. Madereva huwa waangalifu wanapoendesha gari kwenye barabara zenye theluji, lakini wengi hawawi waangalifu wanapokuwa kwenye barabara zisizo na theluji kwani hawajui kwamba kuna barafu hiyo isiyoonekana. Wataalamu wanapendekeza hivi: ‘Msimwage chumvi nyingi barabarani.’
Milio ya Bundi Huonyesha Hali Yao ya Afya
Gazeti la The Economist lasema kwamba milio ya bundi wa kahawia huonyesha hali yao ya afya. “Stephen Redpath wa Kituo cha Uingereza cha Sayansi ya Mazingira na ya Maji na wataalamu wenzake walichunguza bundi wa kahawia 22 katika Msitu wa Kielder, kaskazini mwa Uingereza.” Watafiti hao walichezesha kaseti ya “milio ya bundi mgeni wa kiume na wakahesabu muda uliopita kabla ya bundi hao kuitikia milio hiyo.” Bundi waliokuwa na vimelea vingi katika damu walichukua muda mrefu kabla ya kuitikia. Walichukua muda unaozidi mara mbili ule wa bundi wasiokuwa na vimelea. Kwa kuongezea, wakati bundi wenye vimelea vingi walipolia, milio yao ilikuwa ya chini kuliko ile ya bundi wenye afya. Gazeti la The Economist lasema hivi: “Pasipo shaka, bundi hao hujishtaki kwa milio yao.”
Faida za Kumsomea Mtoto
Gazeti la kila juma la Poland la Przyjaciółka lasema kwamba: “[Watoto] wanapoona kwamba mama na baba wanapenda kusoma, wao hujaribu kuwaiga.” Makala hiyo yasema kwamba katika enzi hizi ambapo watoto wanapenda kutazama sana televisheni, kuna faida kuwasomea watoto na kuwaonyesha picha na kuzieleza hata wanapokuwa na umri wa miaka miwili tu. Wazazi wanaweza kumuuliza mtoto kuhusu yale ambayo wamesoma ili kuona kama ameelewa habari hiyo. “Na mtoto anapochoshwa ghafula . . . , jaribu kufanya usomaji usisimue kwa kutumia ishara za mwili na kubadili sauti.” Wazazi wanashauriwa wafahamu na kuzungumza kuhusu mapendezi ya mtoto wao. “Zungumza kuhusu vitabu ulivyopenda ulipokuwa mtoto, na utaje vichwa vyenye kupendeza. . . . Usiache kuwasomea watoto wako, hata wanapojua kusoma,” lasema gazeti la Przyjaciółka. “Nyakati nyingine inatosha kusoma kurasa chache za kwanza ili kumtia mtoto moyo, kisha mtoto ataendelea kujisomea kwa furaha.”
Vionjio Visivyofanya Kazi
Kulingana na makadirio yaliyofanywa na Hiroshi Tomita, ambaye ni mtaalamu wa magonjwa ya masikio, pua, na koo, kila mwaka zaidi ya watu 140,000 nchini Japani, kutia ndani vijana wengi, hupoteza hisi ya kuonja. Ripoti hiyo ya gazeti la The Daily Yomiuri yasema kwamba dawa na matatizo ya afya yanaweza kusababisha ugonjwa huo. Hata hivyo, Tomita anaamini kwamba asilimia 30 hivi ya visa hivyo husababishwa kwa kutopata madini ya kutosha ya zinki, ambayo ni muhimu
sana. Makala hiyo yasema hivi: “Zinki huchangia sana kufanyizwa kwa chembe mpya za vionjio, na upungufu [wa zinki] husababisha ukosefu wa hisi hiyo pole kwa pole.” Tatizo hilo husababishwa na vyakula visivyokuwa na lishe, vyakula vinavyotengenezwa viwandani, na kutokula vyakula mbalimbali. Makala hiyo yaeleza kwamba “kemikali ya fosfati, ambayo hupatikana katika vyakula vingi vilivyotengenezwa viwandani, huzuia zinki isiingie mwilini na kupunguza kiwango chake.” Kwa watu wasiohisi ladha katika chakula, Tomita anapendekeza wale vyakula vilivyo na zinki nyingi. Hivyo vyatia ndani chaza, samaki wadogo, na maini. Tomita asema kwamba kula vyakula mbalimbali vyenye lishe kwaweza kurudisha hisi kwenye vionjio, lakini hali mbaya zaidi isipotibiwa kwa zaidi ya miezi sita, kuna uwezekano mkubwa wa kutopona.Misikiti Yaongezeka Marekani
Gazeti la The New York Times lasema hivi: “Idadi ya misikiti nchini Marekani imeongezeka kwa asilimia 25 hivi katika miaka sita, kufikia misikiti 1,200.” Hiyo inaonyesha kwamba Waislamu wameongezeka nchini humo. John Esposito, msimamizi wa Kituo cha Maelewano Kati ya Waislamu na Wakristo kwenye Chuo Kikuu cha Georgetown, anasema kwamba sasa kuna Waislamu “milioni nne hadi milioni sita hivi.” Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa hivi majuzi na mashirika manne ya Kiislamu ya Marekani, idadi hiyo yaweza kuwa kubwa hata zaidi. Vyovyote iwavyo, kulingana na Esposito ‘kwa kuwa Waislamu wanaendelea kuhamia huko na kwa sababu familia zao nyingi ni kubwakubwa’ ongezeko hilo litaendelea. “Baada ya miongo michache, dini ya Uislamu itakuwa dini ya pili kwa ukubwa nchini Marekani.” Gazeti la Times lilisema kwamba “wanaume hasa” ndio wanaohudhuria ibada misikitini. Uchunguzi huo pia ulionyesha kwamba “waumini wanatoka katika jamii mbalimbali: theluthi moja wametoka Asia Kusini, asilimia 30 ni Wamarekani wenye asili ya Kiafrika, asilimia 25 ni Waarabu.”
Nyumba Zinazosababisha Magonjwa
Gazeti la New Scientist lasema hivi: “Nyumba zilizojengwa muda usiozidi mwaka mmoja uliopita katika eneo la Melbourne [Australia] zinatokeza mvuke wenye sumu unaozidi kwa mara 20 kiwango kinachokubaliwa na Baraza la Taifa la Utafiti wa Afya na Tiba.” Mojawapo ya kemikali hizo ni formaldehyde, “ambayo hufanya ngozi iwashe na hata labda kusababisha kansa.” Kemikali hiyo huenea hewani kutoka kwenye vifaa vya ujenzi kama vile mbao za sakafu na fanicha. Mazulia mapya hueneza kemikali ya styrene, ambayo labda husababisha kansa pia, “na rangi na viyeyusho hutokeza kemikali mbalimbali zenye sumu,” yasema ripoti hiyo. “Haielekei kemikali hizo zitasababisha madhara makubwa ya afya kwa watu wengi. Lakini zinaweza kusababisha maumivu ya kichwa na kuwadhuru sana watu wachache wanaoathiriwa kwa urahisi.”
Nchi Inayotokeza Maziwa Mengi Zaidi Ulimwenguni
Kwa sasa, India ndiyo nchi inayotokeza maziwa mengi zaidi ulimwenguni, lasema gazeti la The Hindustan Times. Ripoti hiyo yasema hivi: “Taasisi ya Worldwatch inayoshughulikia masuala ya mazingira [huko Washington, D.C.] imesifu maendeleo hayo ya India ya kutokeza maziwa mengi. Tangu mwaka wa 1994 maziwa yalianza kuwa bidhaa kuu ya kilimo iliyotokezwa nchini India na mnamo mwaka wa 1997, nchi hiyo ilipita Marekani na ikawa nchi inayotokeza maziwa mengi zaidi ulimwenguni.” Lester Brown, mwenyekiti wa Taasisi ya Worldwatch, alinukuliwa akisema hivi: ‘Kwa kupendeza, India ilitimiza hilo kwa kulisha mifugo yake mazao mengine ya shambani na masazo ya mavuno badala ya kutumia nafaka. India iliweza kutokeza maziwa mengi zaidi bila kulisha ng’ombe nafaka ambazo zingewafaidi wanadamu.’
Imekuwa Rahisi Kutumia Fedha
Gazeti la Calgary Herald laripoti kwamba maendeleo ya kitekinolojia yamewawezesha Wakanada wengi kununua vitu wakati wowote kila siku ya juma. “Wateja wanaweza kununua vitu wakati wowote kupitia Internet, Stesheni ya Ununuzi kwenye televisheni, kwa kutumia vitabu vya orodha ya bei vinavyotumwa kupitia posta au kununua bidhaa mara moja wakitumia kadi ya mkopo.” Kadi za mikopo mikubwa huwachochea watu kutumia fedha kupita kiasi. Kadi fulani za mkopo hutoa zawadi za ziada. Larry Wood, profesa wa fedha kwenye Chuo Kikuu cha Calgary, alisema hivi: “Watu wanaweza kuwa na fedha taslimu za kununua bidhaa lakini wanatumia kadi zao za mkopo ili wapate zawadi hizo, wakiwaza kwamba watatumia fedha taslimu kulipa mkopo huo mwishoni mwa mwezi. Kisha wanakula fedha zote wakibaki na deni la mkopo.” Hata hivyo, Wood anaamini kwamba tatizo hilo linasababishwa na mambo mengine pia. Yeye anasema kwamba wateja wanapojaribu kudumisha hali ya maisha waliyozoea, wao huona ni afadhali wawe na madeni badala ya kupunguza matumizi yao. Kulingana na uchunguzi uliofanywa mwaka wa 1999 kuhusu Takwimu za Kanada, madeni ya kadi za mikopo ya nchi hiyo yalikuwa zaidi ya dola bilioni 14 za Kanada.