Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jinsi Divai Yenye Mapovu Inavyotengenezwa

Jinsi Divai Yenye Mapovu Inavyotengenezwa

Jinsi Divai Yenye Mapovu Inavyotengenezwa

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UFARANSA

ULIMWENGUNI POTE, CHAMPAGNE, (shampeni) divai yenye mapovu, hupendwa sana wakati wa sikukuu na sherehe mbalimbali. Hata kutaja tu jina hilo hufanya watu wakumbuke sherehe ya shangwe.

Wengi wanadhani kwamba Dom Pérignon alibuni champagne. Kwa vyovyote vile, alifanya mengi ili kukiboresha kinywaji hicho. Kuanzia mwaka wa 1668 hadi alipokufa mwaka wa 1715, mtawa huyo wa kundi la St. Benedict alikuwa msimamizi wa chakula katika Kao la Watawa la Hautvillers (lililopo katikati ya eneo la Champagne la Ufaransa). Baadhi ya watu humwona Dom Pérignon kuwa mwanzilishi wa mbinu nyingi zinazotumiwa kutengeneza kinywaji hicho hata leo.

Waingereza walikuwa wa kwanza kupenda divai inayotoa povu, lakini katika karne ya 18, watu kwenye jumba la mfalme la Ufaransa walianza kutumia kinywaji hicho cha fahari. Hata hivyo, kumbuka kwamba divai inayoitwa champagne, ni ile inayotengenezwa katika eneo la Champagne tu huko Ufaransa. Hata ni lazima zabibu ziwe zimekuzwa katika eneo hilo!

Udongo katika eneo la Champagne ni wenye chokaa kufikia kina cha meta 100 na juu yake kuna tabaka jembamba la udongo wa kitope. * Kwa sababu hiyo, udongo huo ni wenye unyevu daima, nao hutoa joto usiku. Isitoshe, mizizi ya mizabibu hupenya hadi kwenye kina cha meta 10, nayo hufyonza madini yaliyo muhimu ili kutokeza divai bora.

Eneo linaloitwa champagne lina ukubwa wa ekari 90,000, na mizabibu imepandwa kwenye ekari 70,000 hivi za eneo hilo. Mizabibu hupandwa kwenye sehemu ya juu ya pande za milima ili isiathiriwe na baridi kali inayokumba sehemu ya chini nyakati nyingine, kama ile iliyokuwapo mwaka wa 1985, wakati halijoto iliposhuka hadi nyuzi 30 Selsiasi chini ya kiwango cha kuganda. Mizabibu ya aina tatu hupandwa: Pinot Meunier na Pinot Noir ambayo huzaa zabibu nyeusi, na Chardonnay ambayo huzaa zabibu nyeupe. *

Divai Isiyo na Mapovu

Zabibu zilizochumwa huwekwa mara moja katika vyombo vikubwa vya kukamulia vyenye kina kifupi ili rangi ya maganda isiathiri maji ya matunda. Tani nne za zabibu zinapokamuliwa mara ya kwanza hutokeza lita 2,050 za maji bora ya matunda yanayotumiwa kutengeneza divai bora. Zinapokamuliwa mara ya pili na ya tatu, zinatokeza lita 410 na lita 205 za maji duni ya matunda. Maji yoyote yanayokamuliwa baada ya hapo hayafai kwa kutengeneza champagne.

Kwa majuma kadhaa maji hayo ya matunda huchacha polepole katika vyombo vikubwa vya mbao ya mwaloni au chuma. Vijidudu vinapoendelea kula sukari ya maji hayo ya matunda ndipo yanapokuwa divai yenye kileo. Kaboni dioksidi hutokezwa pia wakati huo. Divai zote huchachishwa kwa njia hiyo. Matokeo ni divai isiyo na mapovu. Lakini wakati umewadia kubadili divai hiyo isiyo na mapovu iwe kinywaji bora chenye mapovu.

Kiasi cha sukari katika divai hiyo isiyo na mapovu hupimwa na kudumishwa kuwa gramu 25 hivi kwa lita moja ya divai, inapoongezwa divai ya zamani iliyo na sukari ya miwa. Kisha divai hiyo inayotengenezwa huwekwa katika chupa zinazofungwa kwa kizibo cha muda. Chupa hizo huhifadhiwa zikiwa zimelala katika ghala za chini ya ardhi zenye halijoto ya nyuzi 10 Selsiasi kwa muda wa miezi kadhaa. Kwa muda huo vijidudu hula sukari na polepole uchachishaji wa pili huanza. Uchachishaji huo wa pili hutokeza kaboni dioksidi tena. Lakini sasa kaboni dioksidi haiwezi kutoka kama vile ilivyofanya divai ilipokuwa katika vile vyombo vikubwa. Badala yake imefungwa ndani ya chupa na shinikizo linaendelea kuongezeka hadi litakapofikia kipimo cha sita kwenye kipima-hewa. Chupa inapofunguliwa lita tano au sita za gesi huachiliwa, ndipo yale mapovu maarufu huonekana.

Ili kustahimili shinikizo hilo, lazima chupa ziwe zenye nguvu na zifungwe barabara. Jambo hilo liliwatatanisha watengenezaji wa zamani. Kwa mfano, katika kitabu chake cha The Story of Wine, Hugh Johnson anasema kwamba mwishoni mwa miaka ya 1800, “ilikuwa hatari kuingia katika ghala ya champagne, hasa katika miezi ya tatu na nne, bila kufunika uso kwa bati la chuma ili kujilinda kutokana na vipande vya chupa zilizolipuka.”

Hata hivyo, kinywaji chetu hakijakamilika bado. Ili divai hiyo iwe safi ni lazima kuondoa chembe za chachu na chumvi yenye madini. Kazi hiyo inafanywa na wafanyakazi wanaogeuza chupa wanaoitwa remueur. Watu hao wanaziinamisha chupa hatua kwa hatua, juu chini, na kila siku wanazigeuza kidogo wakifuata taratibu fulani. Baadhi ya wafanyakazi wanaweza kugeuza chupa 10,000 kwa saa moja! Hata hivyo, siku hizi chupa za champagne ya kawaida mara nyingi hugeuzwa kwa mashine.

Mambo ya Mwisho-Mwisho

Hatimaye, takataka imeshuka chini katika shingo ya chupa. Kuondolewa kwa takataka hiyo kunaitwa dégorgement (yaani, kutapisha). Chupa ikiwa juu chini, shingo yake huingizwa katika maji baridi ya chumvi ya nyuzi 27 Selsiasi chini ya kiwango cha kuganda. Kisha chupa hufunguliwa upesi. Takataka iliyoganda husukumwa nje na shinikizo la ndani. Kileo kitamu huongezwa ili chupa ijae tena. Utamu wa divai utategemea utamu wa kileo hicho. Divai itabainishwa kuwa ama tamu, tamu kiasi, au kali, kulingana na mapendezi ya wateja. Mwishowe chupa zinaweza kufungwa kabisa kwa vizibo maalum vitakavyopata umbo la uyoga pole kwa pole. Hivyo ni kitambulisho kimoja cha champagne.

Hata hivyo, ni lazima kizibo kikazwe barabara. Mwanzoni kamba za katani zilitumiwa, lakini hizo zilioza chupa zilipowekwa katika ghala za chini ya ardhi zenye unyevu. Baadaye, waya za kawaida zilitumiwa, lakini hizo ziliathiriwa na kutu, nazo zilikata kizibo. Mwishowe, njia nyingine iligunduliwa: Kifuniko cha chuma kiliwekwa juu ya kizibo na kufungwa kwa nyaya kadhaa zilizopindwa. Mbinu hiyo ya kufunga chupa imetumiwa kwa miaka 150 iliyopita. Hatimaye, kibandiko cha chupa huwekwa na vilevile karatasi inayong’aa kwenye shingo.

Kinywaji Kinachotamaniwa

Watengenezaji wengi wa divai katika sehemu nyingine wamejaribu kutengeneza divai zenye mapovu. Lakini, hata kama wangetumia njia iyo hiyo kutengeneza divai yenye mapovu, hawangeweza kuiita champagne kihalali. Hivi majuzi, Mfaransa aliye mbuni wa mitindo alipelekwa mahakamani kwa sababu aliyaita marashi aliyobuni, Champagne. Mwingereza fulani pia alipelekwa mahakamani kwa sababu alikiita kinywaji kilichotengenezwa kwa maua ya msambuku, Elderflower Champagne, na kukiuza katika chupa zilizofanana na chupa za champagne.

Kama vile biashara nyingine, biashara ya champagne imekumbwa na tatizo la uchumi. Chupa milioni 249 za champagne zilitengenezwa katika mwaka wa 1989, lakini mauzo yalishuka na chupa nyingi hazikuuzwa. Leo, watengenezaji wa divai, wanajitahidi kutengeneza divai bora badala ya divai nyingi.

Divai ya champagne inaweza kuhifadhiwa kwa miaka michache ikiwekwa mahali penye giza na halijoto isiyobadilika. Lakini divai hiyo inaweza kutumiwa mara inaponunuliwa. Inapasa kuwa baridi sana inapotumiwa, kati ya nyuzi 6 hadi 9 Selsiasi. Njia nzuri ya kupunguza joto ni kuweka chupa katika ndoo ndogo yenye maji na barafu. Bilauri ndefu zilizo na mapambo yaliyochongwa hutumiwa ili mapovu yaonekane vizuri.

Kwa hiyo ukipata nafasi kuonja kinywaji hicho kizuri, kumbuka jinsi kilivyotengenezwa. Na ufurahie yale mamilioni ya mapovu, kwa sababu sasa unajua hutokana na nini.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 6 Kwa sababu udongo una chokaa nyingi katika eneo hilo, ilikuwa rahisi kuchimba vyumba chini ya ardhi ambavyo hutumiwa kama ghala. Vyumba hivyo vina urefu wa zaidi ya kilometa 250 na vina halijoto ya nyuzi 10 Selsiasi. Ghala nyingi katika eneo la Reims ni machimbo ya mawe ya kale ya Waroma.

^ fu. 7 Aina fulani za champagne hutengenezwa kwa zabibu ya Chardonnay pekee, kama vile divai maarufu ya Blanc de Blancs (linamaanisha nyeupe inayotokana na nyeupe), inayotengenezwa kwa zabibu zinazokuzwa kwenye eneo la Côte des Blancs, kusini ya mji wa Épernay.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Chardonnay

Pinot Noir

Pinot Meunier

[Hisani]

Photo DUBOIS-Collection C.I.V.C.

Photo collection C.I.V.C.

[Picha katika ukurasa wa 15]

1 Zabibu huchumwa kwa mkono kwa uangalifu na kukamuliwa katika mashine ya kukamulia

2 Kwa muda wa majuma kadhaa divai huendelea kuchacha katika vyombo vya mbao ya mwaloni

3 Chupa huwekwa kwenye rafu kwa uchachishaji wa pili

4 Katika hatua inayoitwa “dégorgement” takataka husukumwa nje

[Hisani]

Photo M. HETIER-Collection C.I.V.C.

Photo collection C.I.V.C.