Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutafuta Pomboo Huko New Zealand

Kutafuta Pomboo Huko New Zealand

Kutafuta Pomboo Huko New Zealand

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NEW ZEALAND

MWANDISHI Mgiriki Plutarch aliandika: “Huyu ndiye mnyama pekee anayempenda mwanadamu bila kutarajia chochote kutoka kwake.” Aliongea juu ya mnyama yupi? Aliongea kuhusu pomboo, mnyama wa jamii ya nyangumi.

Kulingana na kitabu The World Book Encyclopedia, “wanasayansi wengi huwaona pomboo kuwa wenye akili nyingi sana kama vile sokwe-mtu na mbwa.” Lakini, kama vile Plutarch alivyosema, pomboo hawapendi wanadamu kwa sababu ya chakula tu. Badala yake, ni kana kwamba wengi wao wanapenda kucheza nasi. Kitabu cha Mysteries of the Deep chasema kwamba “ijapokuwa pomboo hategemei wanadamu, huenda ikawa anafurahia kutazama michezo yetu kama vile sisi tunavyofurahishwa na michezo yake.” Kuna aina 32 za pomboo wa baharini, na 4 kati ya hizo hupatikana New Zealand: pomboo wa kawaida, pomboo mwenye pua pana, pomboo mweusi (dusky), na yule mdogo kuliko wote ulimwenguni—pomboo wa Hector. *

Kuna pomboo wengi sana huko Ghuba ya Visiwa, ambayo ni eneo maridadi kwenye pwani ya New Zealand. Tulikuwa na hamu ya kuwaona, kwa hiyo tulianza safari yetu kwa mashua katika mji wa Russell. Kiongozi wetu alituambia kwamba mbali na pomboo wenye pua pana na pomboo wa kawaida, huenda tukaona nyangumi mwenye meno meusi na nyangumi mwuaji (killer)—ambao ni wa jamii ya pomboo. Alitushauri kwamba ili kujua mahali wapo tujaribu kuona maji yanayopulizwa wanapopumua au pezi lao la mgongoni. Alisema kwamba “nyakati nyingine pomboo hutuona kabla hatujawaona!”

Kuogelea Pamoja na Pomboo

Punde, pomboo wakubwa wenye pua pana—wengine wenye urefu wa meta nne—walitukaribia. Mapezi yao ya mgongoni yalionekana katikati ya mawimbi. Walipocheza wakiwa karibu na gubeti, walisafiri kwa kasi sawa na mashua bila kufanya jitihada yoyote. Mashua iliposimama mimi na kiongozi wetu tuliingia ndani ya maji yenye rangi ya kijani-kibichi, ambamo pomboo walituruhusu kuogelea pamoja nao.

Mwanzoni nilipozungukwa na mapezi mengi ya mgongoni nilishindwa la kufanya. Nilivuta pumzi na kuwatazama kwa mshangao na wasiwasi wanyama hao wenye rangi ya kijivu walioogelea chini yangu. Pomboo mmoja alitokea chini na kunichunguza, kisha akageuka kidogo na kunionyesha tumbo lake jeupe. Ijapokuwa pomboo hao hawakutukaribia sana, tuliwasikia walipopiga mbinja. Nilijaribu kuiga sauti yao, lakini pomboo hao hawakuvutiwa, walirudi nyuma, kisha wakaendelea kuzunguka tena.

Kuwinda na Kucheza

Baada ya kurudi kwenye mashua tena, tulifuata pomboo hadi ghuba moja tulivu. Huko kulikuwa na pomboo wengi sana waliorukaruka na kurusharusha maji kotekote! Pomboo hao walikuwa wakiwinda. Pomboo hula hasa ngisi, samaki, na wanyama wenye magamba. Hata tulimwona pomboo aliyemzoeza mtoto wake kuwinda. Pomboo huyo alimduwaza samaki mdogo kwa kupiga mbinja, na mtoto alijaribu kumkamata kwa kumpiga na mkia wake. Yaelekea mtoto huyo angehitaji mazoezi zaidi!

Pomboo hutumia muda mwingi kucheza na kuwa pamoja. Mmoja alipita akijivunia mwani aliobeba kwenye pezi la mgongo. Kiongozi wetu alitueleza kwamba pomboo hupenda sana kucheza na mwani. Wao huuweka kwenye pezi au pua na kucheza nao kwa muda mrefu. Mmoja anapochoka kucheza nao mwingine huuchukua na kuendelea.

‘Picha’ za Akilini Zinazotokezwa kwa Sauti

Ili “kuyaona” mazingira yao ya baharini vizuri, pomboo hutumia mwangwi wenye mawimbi ya sauti yanayokwenda kasi sana. Pomboo hutoa sauti ya mialiko, na “picha” ambazo hutokezwa na sauti hiyo huwawezesha kujua mahali ambapo chakula na vitu vingine—kama vile sisi—hupatikana. Pomboo huwasiliana kwa kupiga mbinja kwa sauti nyembamba iliyo kali mara kumi ya sauti ya mwanadamu. Wanatokeza mawimbi ya sauti yanayokwenda kasi mara nne na nusu ya mawimbi ya sauti ya mwanadamu. Yaelekea, pomboo huwasiliana kwa kuchora ‘picha’ za akilini kwa kutumia sauti.

Kuna mengi ya kujifunza juu ya pomboo. Huenda siku moja tutawaelewa kabisa—jinsi wanavyofikiri na jinsi wanavyotuona. Tuliacha pomboo wakiendelea kucheza kwenye ghuba hiyo maridadi yenye miamba, ukungu, na pwani yenye mchanga mweupe tukiwa tumefurahishwa na kustaajabishwa sana. Safari hiyo ilitufanya tuvutiwe na wanyama hao na kusukumwa kumcha Muumba zaidi.—Ufunuo 4:11.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Pomboo wengine wanaofika New Zealand nyakati nyingine ni hourglass dolphin na pomboo aina ya finless southern right whale.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18, 19]

Kumlea Mtoto

Pomboo si samaki bali ni wanyama wanaonyonyesha watoto wao. Kwa hiyo, chakula cha mtoto wa pomboo ni maziwa yanayotokezwa katika mwili wa mamake. Katika miaka mitatu ambayo mama humnyonyesha mtoto, atamfundisha mtoto huyo kile anachohitaji kujua maishani. Kwa mfano, atamfundisha jinsi ya kutumia mwangwi ili kupima umbali, na vilevile jinsi anavyopaswa kumaliza kila “sentensi” kwa sauti maalumu ambayo inamtambulisha. Pia, atamzoeza kuwinda, kujamiiana, na jinsi ya kuishi pamoja na pomboo wengine.

Mtoto wa pomboo huzaliwa mkia ukitangulia. Anapokuwa tumboni huwa amejipinda. Kuna mistari kwenye miili ya watoto waliotoka tu kuzaliwa inayoonyesha jinsi walivyokuwa wamejipinda tumboni. Mtoto hunyonya mama anapoogelea, huku akibaki karibu na mama ili asukumwe mbele kwa kani zinazotokezwa wakati mamake anapoogelea.

[Hisani]

© Jeffrey L. Rotman/CORBIS

[Ramani katika ukurasa wa 19]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

NEW ZEALAND

Ghuba ya Visiwa

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pomboo mwenye pua pana

[Hisani]

© Jeff Rotman

[Picha katika ukurasa wa 17]

Pomboo wa “Hector”

[Hisani]

Photo by Zoe Battersby

[Picha katika ukurasa wa 18]

Pomboo mweusi

[Hisani]

Mark Jones

[Picha katika ukurasa wa 18]

Pomboo wa kawaida

[Hisani]

© R.E. Barber/Visuals Unlimited