Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea Mbuga ya Taifa ya Olympic

Kutembelea Mbuga ya Taifa ya Olympic

Kutembelea Mbuga ya Taifa ya Olympic

NILILELEWA karibu na Mlima Olympus huko kusini mwa Ulaya, kwa hiyo nilitaka kujua ni kwa nini rasi (ardhi nyembamba inayopenyeza baharini) moja ya Pasifiki huko Amerika Kaskazini, iliitwa kwa jina la mlima huo. Eneo hilo liko umbali wa maelfu ya kilometa kutoka kwa Mlima Olympus huko Ugiriki. Nilichochewa kutembelea Mbuga ya Taifa ya Olympic wakati rafiki mmoja alipotaja kwamba kuna misitu ya mvua huko. Misitu hiyo iko umbali wa kilometa 8,000 kaskazini-magharibi mwa msitu wa mvua wa Amazoni huko Brazili.

Kabla ya kuanza safari nilijifunza kwamba kuna maajabu mengi ya maumbile katika mbuga hiyo yenye ukubwa wa ekari 900,000 iliyo katika jimbo la Washington, kaskazini-magharibi mwa Marekani. Eneo hilo lina miti mikubwa, pwani yenye miamba iliyochongoka, mvua nyingi sana, na ukungu wa bahari ya Pasifiki ambao huenea kutoka pwani hadi sehemu ya juu isiyo na miti. Katika mbuga hiyo kuna milima mirefu iliyofunikwa kwa theluji na barafu inayoteleza polepole, na msitu wa mvua ulio na miti mingi sana kama misitu ya eneo la Amazoni.

Mwaka wa 1788, nahodha Mwingereza alikiita kilele kirefu zaidi, chenye kimo cha meta 2,500 hivi, Mlima Olympus kwa jina la makao ya miungu ya kihekaya ya Ugiriki. Ili kuihifadhi, pori hiyo ilifanywa kuwa Mbuga ya Taifa ya Olympic mwaka wa 1938.

Kumbe Kuna Misitu ya Mvua Huko Amerika Kaskazini!

Mike, aliye mwenyeji na kiongozi, alitungojea mimi na mke wangu asubuhi moja nzuri kwenye makao makuu ya mbuga hiyo huko Port Angeles. Mike ambaye ni mwanamume mwenye mwili mkubwa hufurahia kuonyesha wageni kama sisi maajabu ya msitu huo wa mvua. Alisema kwa shauku kwamba ‘misitu ya mvua huenda ni kitu kinachostaajabisha hasa hapa mbugani, kwa sababu misitu ya mvua hupatikana hasa katika maeneo ya joto jingi tu. Misitu yetu ni midogo kuliko misitu mingine ya mvua katika maeneo yasiyo ya joto jingi.’ Nilipomwomba aeleze zaidi, Mike alitutajia takwimu mara moja: Misitu hiyo hupata maji mengi sana kwa sababu mvua nyingi hunyesha upande wa magharibi wa Milima ya Olympic. Kila mwaka sentimeta 200 hivi za mvua hunyesha karibu na eneo la pwani na sentimeta 400 au zaidi hunyesha katika mabonde ya mito chini ya milima. Sehemu kubwa ya misitu ya mvua iko katika mabonde ya Mto Hoh, Mto Queets, na Mto Quinault.

Tabaka ya majani yanayooza yenye kina cha nusu meta hivi ilipunguza kelele ya hatua zetu za miguu. Miti huzuia upepo msituni; na mvua inayonyesha mara nyingi sana huwa kama ukungu tu kwa sababu huzuiwa na miti na mimea. Miale michache tu ya jua hufika chini. Sauti nyororo zaidi ya ndege ilisikika bila tatizo, tuliwaona mbawala wakipita mara kwa mara katikati ya mashina ya miti yenye kuvumwani.

Miti Huchipuka Kwenye Magogo ya Miti Mingine

Kwa sababu kuna tabaka ya majani yaliyooza chini, si rahisi mbegu zimee. Ndiyo sababu miti mingi mikubwa katika msitu huo ilichipuka kwenye magogo ya miti. Miti hiyo inapooza inakuwa mahali pazuri pa mbegu kumea. Ni jambo la kawaida kuona miti kadhaa mikubwa ikikua katika mstari kwenye gogo la mti mkubwa ulioanguka. Kwa hiyo, kuna safu za miti msituni zinazoonekana kana kwamba zilipandwa hivyo kwa mpangilio.

Tulipoacha vijia kwenye sehemu tambarare na kupanda mlimani tuliona msitu wa aina nyingine. Miti mingi huko juu ni misonobari mikubwa sana aina ya Pacific silver na aina ya Alps. Kwenye pande za Mlima Olympus kuna tabaka 7 za barafu zinazoteleza ambazo ni zenye kina cha meta 300, na juu milimani kuna zaidi ya tabaka 50 za barafu.

Vilima Vilivyochongoka na Migongo ya Milima Yenye Barafu

Tulikuwa tumetumia nguvu nyingi tulipopanda mlimani. Kwa hiyo, kesho yake tulikula kiamsha-kinywa cha kutosha kwenye mkahawa mmoja huko Port Angeles, ili tupate nguvu tena. Arlene, mhudumu wetu wa mezani mwenye urafiki, alituambia kwamba anapenda sana theluji ya eneo hilo lakini hapendi mvua. Alisisitiza kwamba ni lazima tupande hadi vilele vyenye theluji upande wa mashariki ili tuweze kuona sehemu maridadi zaidi ya Mbuga ya Olympic.

Tuliposafiri kwenye barabara iliyo mashariki ya Port Angeles kuelekea Deer Park, punde tulijikuta kwenye barabara isiyotiwa lami iliyopinda-pinda na yenye mwinuko mkali. Tuliona mandhari yenye fahari kuelekea kaskazini na kusini. Tuliona Kisiwa cha Vancouver, Mlango wa Bahari wa Juan de Fuca na Milima mirefu ya Olympic iliyofunikwa kwa barafu. Kwenye konde za milimani tuliwaona mbawala wengi na mimea kadhaa isiyopatikana mahali pengine, kama vile ua la piper bellflower na la Flett violet.

Kisha tukafika kwenye mgongo wa mlima wa Hurricane Ridge. Barabara ya kwenda huko inapendwa sana. Hiyo ni barabara nzuri inayoanzia karibu na makao makuu ya Mbuga ya Olympic na kufikia konde zenye maua kwenye kimo cha meta 1,755. Kutoka hapo vilele vingi vya milima vyenye theluji na barafu katika mabonde vinaonekana kuelekea kusini. Tuliitazama mandhari hiyo huku mawingu mazito yakitokea upesi kutoka upande wa magharibi.

Aina fulani ya maua ya yungiyungi huchanua mara theluji inapotoweka kondeni, na kwa muda wa miezi mitatu maua mengi yenye rangi mbalimbali huchanua kwenye konde hizo. Mbawala wanaolisha wanaweza kuonekana hapo na nyakati nyingine mbuzi wa milimani huonekana kwenye majabali yenye miteremko mikali.

Mawimbi ya Bahari ya Pasifiki

Pwani bora ya mbuga ya Olympic inaweza kufikiwa kwa miguu wala si kwa magari. Tulianzia mji wa Forks upande wa mashariki na kupita msituni kwa miguu, kisha tukawasili pwani ambako kuna vidimbwi vya maji vyenye viumbe wengi wa baharini. Baada ya kupita rasi ya Teahwhit Head, tulifikia Giants Graveyard, ambapo mawimbi huwa povu yanapovunjwa kwenye miamba iliyokaa shaghalabaghala baharini. Miti kwenye pwani hizo inakua ikiwa imelala kwa sababu ya upepo mkali wa bahari unaovuma daima. Tulipotembea pwani huku upepo ukivuma tuliona vipande vingi vya mbao vyenye maumbo mazuri vilivyopeperushwa pwani na mawe yasiyokuwa na mikwaruzo kana kwamba yamepigwa msasa.

Tulifurahia Mbuga ya Taifa ya Olympic kwa sababu tuliweza kutembea kwenye pori isiyo na watu ambayo haijabadilika tangu zamani za kale. Ilifanya tumtukuze Muumba ambaye, “mkononi mwake zimo bonde za dunia, hata vilele vya milima ni vyake. Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya, na mikono yake iliumba nchi kavu.” (Zaburi 95:4, 5)—Imechangwa.

[Sanduku katika ukurasa wa 25]

Kwa Nini Kuna Mvua Nyingi Hivyo?

Mawingu yenye unyevu hupelekwa kuelekea barani na mkondo wa joto wa Pasifiki nayo hulazimishwa kupaa kwa sababu ya Milima mirefu ya Olympic. Mawingu hayo huwa baridi yanapopaa, na unyevu hugeuka kuwa mvua kubwa au theluji. Kwa hiyo, upande wa magharibi wa milima hupata sentimeta 350 za mvua kwa mwaka. Mlima Olympus hupata sentimeta 500 hivi za mvua, ambayo mara nyingi hunyesha ikiwa theluji. Hata hivyo, hakuna mvua nyingi upande wa mashariki wa milima.

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

BAHARI YA PASIFIKI

KANADA

MAREKANI

MBUGA YA TAIFA YA OLYMPIC

[Picha katika ukurasa wa 23]

Chini ya Mlima Olympus uliofunikwa kwa theluji kuna msitu wa mvua unaoitwa Hoh

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ziwa la Home katika bonde la Mto wa Dungeness

[Picha katika ukurasa wa 24]

Pwani ya Pasifiki inayoitwa Pwani ya Kalaloch

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kwenye konde za milimani, kuna mbawala wengi na mimea ya kipekee kama vile “Flett violet”

[Picha katika ukurasa wa 25]

Maporomoko ya Sol Duc

[Picha katika ukurasa wa 25]

Mti uliosukumwa na maji kwenye Pwani ya Rialto