Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Chai Inayoua Virusi
Taasisi ya Afya ya Reuters inaripoti kwamba majaribio katika maabara yameonyesha kwamba “yaelekea aina nyingi za majani-chai ya kawaida huzuia virusi visiongezeke na kuviua.” Aina mbalimbali za chai nyeusi na za kijani-kibichi, moto na baridi, zilitumiwa katika majaribio ya kuua virusi kama vile herpes simplex 1 na 2 na virusi-bakteria T1. Mtafiti Dakt. Milton Schiffenbauer wa Chuo Kikuu cha Pace huko New York alisema kwamba “chai baridi au ya moto huua virusi [vya herpes] katika muda wa dakika chache.” Matokeo hayohayo yameonekana katika majaribio ya kuua virusi T1. Ijapokuwa haijulikani bado jinsi chai inavyoua virusi hivyo, watafiti wamegundua kwamba hata chai isiyo nzito sana huua virusi hivyo. Chai nyeusi ina nguvu zaidi ya kuua virusi kuliko chai ya kijani-kibichi.
Kufilisika kwa Sababu ya Simu
Gazeti la The Sunday Telegraph laripoti kwamba vijana Waaustralia “wenye umri wa miaka 18 wanasema kwamba wamefilisika kwa sababu ya madeni makubwa ya simu za mkononi.” Vijana fulani wana madeni ya maelfu ya dola kwa sababu wamevutiwa na matangazo ya biashara na kwa sababu wameweza kupata mikopo ya kupiga simu kwa urahisi. Waziri wa Australia wa Biashara ya Haki, John Watkins, alisema hivi juu ya tatizo hilo: “Baadhi ya vijana wana madeni makubwa wanapomaliza shule. Huo ni mwanzo mbaya sana wa maisha.” Gazeti hilo lawapa vijana mapendekezo yafuatayo ya kuepuka madeni hayo: Hakikisha umejua bei unapopiga simu. Afadhali utumie simu ya mkononi iliyolipwa kimbele isiyokuruhusu kutumia njia ya mkopo na kurundika madeni. Jaribu kupiga simu wakati bei ni nafuu ili kupunguza gharama.
Hatari Zilizofichika Nchini Ufaransa
Gazeti la Le Figaro linaripoti kwamba tani milioni 1.3 hivi za vifaa vya kuua vya Vita ya Kwanza na ya Pili ya Ulimwengu bado vimefichika ardhini huko Ufaransa. Kuna makombora mengi yenye kemikali yanayoendelea kuhatarisha watu na mazingira kwenye maeneo ya vita. Wataalamu wanaoondoa makombora huitwa mara nyingi sana kila mwaka, kwa kuwa maeneo mengi yaliyokuwa bila majengo mbeleni sasa ni mitaa ya makazi au maeneo ya viwanda. Mamia ya aksidenti yametukia kati ya mwaka wa 1945 na 1985, na zaidi ya wataalamu 600 wameuawa wakifanya kazi hiyo. Kazi ikiendelea kwa kiwango cha leo, itachukua miaka 700 kuondoa makombora yote.
Maji kwa Watalii?
Gazeti la The Guardian la London laripoti hivi: “Idadi ya watalii inaongezeka kwenye hoteli za ulimwengu, kwa hiyo, mabwawa mengi ya kuogelea hujengwa na viwanja vingi vya gofu hutengenezwa, nazo humaliza akiba ya maji.” Tricia Barnett wa shirika la Tourism Concern anasema kwamba “hilo ni tatizo kubwa ulimwenguni pote. Nyakati nyingine unaweza kuona kijiji [huko Afrika] chenye mfereji mmoja tu, lakini kila chumba katika hoteli kina bafu yenye mfereji.” Shirika moja la kuhifadhi mazingira linakadiria kwamba mtalii mmoja huko Hispania hutumia lita 880 za maji kila siku, lakini mwenyeji hutumia lita 250 tu. Uwanja wa gofu wenye mashimo 18 katika nchi yenye ukame unaweza kumwagiliwa kiasi cha maji ambacho watu 10,000 hutumia kwa kawaida. Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa lakadiria kwamba kiasi cha maji kinachotumiwa na watalii 100 kwa muda wa siku 55 kingetosha kukuza mchele wa kutosha ili kulisha watu 100 kwa muda wa miaka 15.
Hatari za Kuvuta Sigara
Naohito Yamaguchi wa Taasisi ya Taifa ya Kitovu cha Uchunguzi wa Kansa huko Japani alisema kwamba “mtu mmoja kati ya wanane waliokufa kutokana na kansa ya mapafu walipata ugonjwa huo kwa sababu ya kuvuta moshi uliopulizwa na wavutaji wa sigara.” Wanasayansi walipata matokeo hayo kwa kuchunguza watu 52,000 waliokufa kutokana na kansa ya mapafu. Gazeti la Asahi Shimbun linasema kwamba “utafiti ambao umeendelea kwa muda mrefu unaonyesha kwamba kaboni monoksaidi na visababishi vingi vya kansa viko katika moshi unaopulizwa na wavutaji wa sigara kuliko katika moshi unaovutwa nao.” Uchunguzi wa serikali huko Japani wa mwaka wa 1999 wa watu 14,000 ulionyesha kwamba asilimia 35 ya wafanyakazi na wanashule na asilimia 28 ya watu nyumbani waliathiriwa na moshi uliopulizwa na wavutaji wa sigara. Yamaguchi anasema kwamba “wavutaji wa sigara wanapaswa kuelewa kwamba wanawadhuru wasiovuta kwa kadiri kubwa hivi kwamba vikundi hivyo viwili vyapaswa kutenganishwa.”
Biashara ya Watumwa ya Kisasa
“Utumwa umeongezeka sana [leo] kuliko katika pindi nyingine yoyote kulingana na utafiti wa karibuni uliofanywa na mtaalamu mmoja huko Uingereza,” linaripoti gazeti la The Independent la London. Gazeti hilo linasema kwamba profesa wa mambo ya kijamii, Kevin Bales, wa Chuo Kikuu cha Surrey huko Roehampton, “amekadiria kwamba watu milioni 27 wanaishi kama watumwa sasa. Hao ni wengi zaidi kuliko watumwa wa Milki ya Roma au wakati biashara ya watumwa ilipokuwa imepamba moto.” Bales anasema kwamba ijapokuwa utumwa wa leo hutofautiana na utumwa uliokuwapo miaka 150 iliyopita, mamilioni ya watu “hukandamizwa na watu wengine wanaowatisha au kuwatenda kwa ujeuri, nao hawalipwi chochote.” Watumwa wa kawaida leo ni watu ambao wamefanya maagano kulipa kiasi fulani cha fedha ili wasafirishwe hadi nchi nyingine. Watu wanaowasafirisha huwaahidi kazi yenye mshahara mnono. Hata hivyo, wanapoingizwa katika nchi nyingine isivyo halali, wafanyakazi hao hulazimika kufanya kazi ya hali ya chini ili walipe deni lao.
Mazoezi ya Mwili Yanaweza Kupunguza Kushuka Moyo
Jarida la The Harvard Mental Health Letter larejezea uchunguzi uliofanywa kwenye Kituo cha Tiba cha Chuo Kikuu cha Duke huko Marekani na kusema “huenda mazoezi ya mwili yakawasaidia wagonjwa fulani zaidi kuliko dawa ya kushuka moyo.” Vikundi vitatu vya watu 50 waliokuwa wameshuka moyo sana walitibiwa kwa njia tofauti-tofauti kwa muda wa miezi minne. Wale wa kikundi cha kwanza walitumia dawa, wa kikundi cha pili walifanya mazoezi ya mwili, na wa kikundi cha tatu walitumia dawa na pia walifanya mazoezi. Jarida hilo lilisema kwamba baada ya miezi minne, kati ya asilimia 60 na 70 ya wagonjwa hao katika vikundi vyote vitatu “walikuwa wamepona.” Hata hivyo, baada ya miezi sita, wagonjwa waliofanya mazoezi “walikuwa na afya nzuri kihisia na kimwili kuliko wale wengine; asilimia nane pekee kati yao walirudiwa na ugonjwa.” Lakini asilimia 38 kati ya wale waliotumia dawa na asilimia 31 kati ya wale waliotumia dawa na kufanya mazoezi walirudiwa na ugonjwa huo.
Je, Matumbawe ya Jamaika Yanasitawi Tena?
Gazeti la The Dallas Morning News lasema kwamba nyamizi wa baharini wameanza kusitawi tena kwenye pwani ya kaskazini huko Jamaika. Isitoshe, “wanasayansi wamegundua kwamba matumbawe mengi mapya, kutia ndani matumbawe magumu yanayofanyiza miamba, yanasitawi palepale.” Miamba ya matumbawe imekuwa katika hali mbaya tangu nyamizi aina ya Diadema antillarum walipotoweka kwa ghafula mwaka wa 1983 na 1984. Aina fulani za nyamizi huzuia mwani usisitawi sana. Mwani ukiachwa kusitawi bila kizuizi unaweza kuharibu kabisa miamba ya matumbawe. Hata hivyo, gazeti hilo lasema kwamba “uchunguzi mpya unaonyesha kwamba nyamizi aina ya Diadema wanasitawi tena, na huenda matumbawe yanasitawi vilevile.” Mtaalamu wa bahari Nancy Knowlton anasema kwamba “hilo ndilo jambo zuri zaidi kutokea kwa matumbawe ya Karibea katika miaka ya karibuni.”
Viumbe wa Baharini Hutiwa Sumu kwa Vidonge vya Plastiki
Gazeti la New Scientist lasema kwamba “kotekote duniani viumbe wa baharini hutiwa sumu kwa vidonge vidogo vya plastiki vinavyoelea baharini.” Meli husafirisha mitumba ya vidonge vidogo vya plastiki kutoka viwanda vinavyotengeneza plastiki hadi kwenye viwanda vingine vinavyovitumia ili kutengeneza vifaa mbalimbali. Hata hivyo, maelfu ya kilogramu ya vidonge hivyo huingia baharini vikiwa takataka au huanguka baharini kutoka melini au humwagwa kwa kusudi la kusawazisha mizigo. Watafiti wa Chuo Kikuu cha Tokyo cha Kilimo na Tekinolojia huko Japani waligundua kwamba vidonge hivyo hufyonza kemikali nyingi zenye sumu baharini—kemikali hizo huharibu uwezo wa kuzaa na mfumo wa kinga wa mwili na wa homoni wa wanyama hao. Ndege, samaki, na kasa hula vidonge hivyo wakifikiri ni mayai ya samaki au chakula kingine, kwa hiyo jambo hilo linaweza kuwaathiri wanyama wengine wengi hatimaye.