Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Siku Ambayo Ile Minara Miwili Iliporomoka

Siku Ambayo Ile Minara Miwili Iliporomoka

Siku Ambayo Ile Minara Miwili Iliporomoka

MATUKIO ya Septemba 11, 2001, katika jiji la New York City, Washington, D.C., na Pennsylvania yatakumbukwa daima na mamilioni, au labda mabilioni ya watu ulimwenguni. Ulikuwa wapi ulipoona au kusikia habari ya kuvamiwa kwa majengo ya World Trade Center huko New York na makao makuu ya kijeshi ya Pentagon huko Washington?

Uharibifu huo mbaya sana wa mali nyingi na zaidi sana uhai umewapa wanadamu sababu ya kutua na kufikiri.

Tumejifunza nini kuhusu mambo tunayopaswa kutanguliza na maamuzi tunayofanya maishani? Watu walionyeshaje sifa bora za kujitolea, huruma, uvumilivu, na ukarimu wakati wa msiba huo? Makala hii na ile inayofuata zitajibu swali hilo la pili.

Masimulizi ya Waokokaji

Mara tu baada ya msiba huo huko New York, reli za chini ya ardhi zilifungwa, na maelfu ya watu walitoka upande wa kusini wa Manhattan kwa miguu—wengi wao wakivuka daraja la Brooklyn na la Manhattan. Waliona wazi majengo ya ofisi na kiwanda ya makao makuu ya Mashahidi wa Yehova. Punde, baadhi ya wakimbizi kutoka kwenye msiba huo walikimbilia majengo hayo.

Alisha (aliye upande wa kulia), binti ya Shahidi mmoja, alikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kufika hapo. Alikuwa amefunikwa na vumbi na majivu. * Yeye alieleza: “Nilipokuwa ndani ya gari-moshi kuelekea kazini, niliona moshi kutoka kwenye ile minara miwili inayoitwa World Trade Center. Nilipofika kwenye eneo la msiba, kulikuwa na vioo vilivyotapakaa kila mahali, nami nilihisi joto sana. Watu walikimbia huku na huku na polisi walijaribu kuhamisha watu wengine. Lilikuwa kama eneo la vita.

“Nilitafuta usalama katika jengo lililokuwa karibu. Kisha nikasikia mlipuko wakati ndege ya pili ilipogonga mnara wa kusini. Lilikuwa tukio lenye kuogofya sana. Moshi mweusi ulienea kila mahali. Tuliagizwa tutoke katika eneo hilo hatari. Niliingizwa kwenye feri iliyovuka Mto wa East kwenda Brooklyn. Nilipofika upande ule mwingine, niliangalia juu, na kuiona ile ishara kubwa ya ‘WATCHTOWER.’ Makao makuu ya dini ya mama yangu! Mara moja nilielekea kwenye jengo la ofisi. Nilijua kwamba nilikuwa nimefika mahali salama. Nilioga kisha nikawapigia wazazi wangu simu.”

Wendell (aliye upande wa kulia) alikuwa bawabu katika Hoteli ya Marriott, iliyo katikati ya ile minara miwili. Yeye alieleza: “Nilikuwa nikifanya kazi sebuleni wakati niliposikia mlipuko wa kwanza. Niliona vifusi vikianguka kila mahali. Nilipoangalia upande mwingine wa barabara, nilimwona mwanamume aliyekuwa amelala chini huku akiteketea. Nilipasua koti langu na shati na kukimbia ili kujaribu kuuzima moto huo. Mtu mwingine aliyekuwa anapita alikuja kunisaidia. Nguo zote za mwanamume huyo ziliteketea ila tu soksi na viatu vyake. Kisha wazimamoto wakaja na kumpeleka hospitalini.

“Punde tu baada ya hapo, Bryant Gumbel wa shirika la habari za televisheni la CBS alipiga simu ili mtu amsimulie yaliyokuwa yakitendeka. Kupitia kwa mazungumzo hayo ya televisheni, familia yangu ikiwa katika Visiwa vya Virgin ilipata habari na kujua kwamba nilikuwa hai.”

Donald, mwanamume kibonge mwenye urefu wa meta 1.95 anayefanya kazi katika World Financial Center, alikuwa kwenye orofa ya 31 ya jengo la shirika hilo akitazama ile Minara Miwili na Hoteli ya Marriott. Alisema: “Nilipigwa na butaa na hofu kwa yale niliyoona. Watu walianguka na wengine wakaruka kutoka kwenye madirisha ya ule mnara wa kaskazini. Nilivurugika sana, nikakimbia upesi iwezekanavyo kutoka kwenye jengo hilo.”

Tukio jingine ni la mama mmoja mwenye umri wa miaka 60 na kitu na binti zake wawili walio na umri wa miaka 40 na kitu. Ruth na dadake Joni pamoja na mama yao Janice, walikaa katika hoteli moja karibu na ile Minara Miwili. Ruth, aliye muuguzi asimulia: “Nilikuwa bafuni. Kwa ghafula, mamangu na dadangu wakaniambia nitoke upesi. Tulikuwa kwenye orofa ya 16, na waliona dirishani vifusi vikianguka. Mama aliona mwili ukianguka kutoka kwenye paa iliyokuwa karibu kana kwamba ulikuwa umerushwa kutoka mahali fulani.

“Nilivaa haraka, na tukaanza kuteremka ngazi. Kulikuwa na makelele mengi. Tukatoka kwenye jengo hilo na kufika barabarani. Tulisikia milipuko na kuona miali ya moto. Tuliamuriwa tuharakishe kwenda upande wa kusini penye Bustani ya Battery, mahali ilipokuwa Feri ya Kisiwa cha Staten. Tukiwa njiani, tulipoteana na mama yetu anayeugua ugonjwa wa pumu. Angeokokaje moshi, majivu na vumbi yote hiyo? Tulimtafuta kwa nusu saa bila kufanikiwa. Hata hivyo, mwanzoni hatukuwa na wasiwasi sana kwa sababu yeye ana ujuzi mwingi na ni mtulivu.

“Hatimaye, tuliambiwa tutumie Daraja la Brooklyn ili tuvuke kwenda upande ule mwingine. Wazia jinsi tulivyohisi tulipofika upande ule mwingine wa Daraja la Brooklyn na kuona ile ishara kubwa ya ‘WATCHTOWER’! Tulijua tulikuwa salama salimini.

“Tulikaribishwa na kupewa mahali pa kulala. Tulipewa mavazi pia kwa sababu hatukuwa na chochote ila tu nguo tulizokuwa tumevaa. Lakini mama alikuwa wapi? Tulimtafuta usiku wote katika hospitali mbalimbali bila kufanikiwa. Tulipata habari karibu saa tano na nusu asubuhi siku iliyofuata. Mama alikuwa sebuleni! Ni nini kilichompata?”

Mama yao, Janice, aendelea kusimulia: “Tulipokuwa tukiharakisha kutoka hotelini, nilimfikiria mwanamke mmoja mzee rafiki yangu, ambaye hangeweza kuondoka pamoja nasi. Nilitaka kurudi ili nimbebe na kumwondoa humo ndani, lakini ilikuwa hatari sana. Katika vurugu hilo tulitengana na binti zangu. Hata hivyo, sikuwa na wasiwasi sana, kwani wao ni watulivu na Ruth ni muuguzi mwenye ujuzi.

“Kila mahali nilipotazama, watu walihitaji msaada—hasa watoto wachanga. Nilisaidia wengi kadiri nilivyoweza. Nilienda kwenye sehemu ambayo majeruhi walikaguliwa na kutibiwa kulingana na majeraha yao. Nilisaidia kuosha mikono na nyuso za polisi na wazimamoto waliokuwa wamefunikwa na moshi na vumbi. Nilikaa huko mpaka karibu saa tisa asubuhi. Kisha nikapanda feri ya mwisho kwenda Kisiwa cha Staten. Nilifikiri labda binti zangu walipata usalama huko. Lakini hawakuwepo.

“Kulipopambazuka, nilijaribu kuingia feri ya kwanza kurudi Manhattan, lakini sikuweza kuipanda kwani sikuwa mfanyakazi wa dharura. Kisha nikamwona John, mmoja wa wale polisi niliosaidia. Nilimwita na kumwambia kwamba nilitaka kurudi Manhattan. Kisha akaniambia niambatane naye.

“Nilipofika Manhattan, nilirudi kwenye Hoteli ya Marriott. Nilifikiri kwamba nilikuwa bado na fursa ya kumsaidia rafiki yangu, yule mwanamke mzee, lakini haikuwezekana! Hoteli hiyo ilikuwa magofu. Jiji lilikuwa kimya bila mtu yeyote ila tu polisi na wazimamoto waliokuwa wamechoka na kuhuzunika sana.

“Nilianza kuelekea kwenye Daraja la Brooklyn. Nilipokaribia upande ule mwingine wa Daraja hilo, niliiona ile ishara mashuhuri ya ‘WATCHTOWER.’ Niliwaza kwamba huenda ningewapata binti zangu huko. Na hakika walikuwa huko, wakaja chini sebuleni kunisalimu. Jinsi tulivyokumbatiana na kulia!

“Jambo la kushangaza ni kwamba licha ya kuwepo kwa moshi, vumbi, na majivu, sikupatwa na shambulio la pumu hata kidogo. Niliendelea kusali kwa sababu nilitaka kusaidia, sikutaka kuwa mzigo.”

“Hakukuwa na Mahali pa Kutua!”

Rachel, mwanamke aliye katika mwanzo wa miaka yake ya 20, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Nilisikia sauti ya ndege nilipokuwa nikitembea karibu na jengo letu katika upande wa kusini wa Manhattan. Kwa sababu ilitoa sauti kubwa sana, niliangalia juu. Sikuweza kuamini—niliona jeti kubwa ambayo bila shaka ilielekea kutua. Nilishangaa kwa nini ilikuwa karibu na ilienda kwa kasi sana. Hakukuwa na mahali pa kutua! Niliwaza kwamba huenda rubani alishindwa kuidhibiti. Kisha nikamsikia mwanamke mmoja akipiga mayowe na kusema, ‘Ndege hiyo imegonga lile jengo!’ Kukatokea moto mkubwa kutoka kwenye mnara wa kaskazini. Nikaona shimo kubwa jeusi katika mnara huo.

“Hilo ndilo jambo baya sana nimewahi kuona maishani mwangu. Ilikuwa kama ndoto. Nilisimama hapo nikiwa nimeduwaa. Baada ya muda mfupi tu, ule mnara wa pili uligongwa na ndege nyingine, na hatimaye minara yote miwili ikaporomoka. Nilivurugika sana. Sikuweza kuvumilia mambo yote hayo!”

“Ikiwa Ni Lazima Niogelee, Nitaogelea”

Denise, mwenye umri wa miaka 16, alikuwa tu amefika shuleni karibu na jengo la Soko la Hisa la Marekani, lililopo kusini mwa Jengo la World Trade Center. “Ilikuwa tu baada ya saa 3:00 asubuhi, nami nilijua kuna jambo lililokuwa limetendeka, lakini sikujua lilikuwa nini. Tulikuwa tukifundishwa historia kwenye orofa ya 11. Wanafunzi wote walionekana kuwa na wasiwasi. Na mwalimu bado alitaka tufanye mtihani. Sisi tulitaka kwenda nyumbani.

“Kisha jengo likatikisika wakati ndege ya pili ilipougonga ule mnara wa kusini. Lakini bado hatukujua kilichokuwa kimetendeka. Ghafula nikasikia ujumbe fulani kwenye redio ya mkononi ya mwalimu: ‘Ndege mbili zimegonga ile Minara Miwili! Niliona haikufaa kubaki shuleni. Hili lilikuwa tendo la ugaidi, na huenda jengo la Soko la Hisa lingelipuliwa.’ Basi tukatoka nje.

“Tulikimbia kuelekea Bustani ya Battery. Nilipogeuka kuona kilichokuwa kikitendeka, niliona kwamba mnara wa kusini ulielekea kuporomoka. Kisha nikafikiri kwamba huenda majengo yote marefu yangeporomoka. Kwa sababu pua na koo langu lilijawa na majivu na vumbi, ilikuwa vigumu sana kupumua. Nilikimbilia Mto East nikijua kwamba, ‘Ikiwa ni lazima niogelee, nitaogelea.’ Nilipokuwa nikikimbia nilimwomba Yehova aniokoe.

“Hatimaye, niliwekwa kwenye feri kwenda New Jersey. Ingawaje ilimchukua mama yangu zaidi ya saa tano kunipata, nilikuwa salama!”

‘Je, Hii Ndiyo Siku Yangu ya Mwisho Kuwa Hai?’

Joshua, mwenye umri wa miaka 28, kutoka Princeton, New Jersey, alikuwa darasani akifunza kwenye orofa ya 40 ya mnara wa kaskazini. Yeye akumbuka: “Kwa ghafula nilihisi kana kwamba bomu lilikuwa limelipuka. Kulikuwa na matetemeko, kisha nikafikiri kwamba tetemeko la ardhi lilikuwa limetokea. Nilipotazama nje, sikuamini nilichoona—moshi na vifusi vilitapakaa kuzunguka jengo hilo. Niliwaambia wanafunzi waache kila kitu na tuondoke!

“Tuliteremka ngazi zilizojaa moshi na maji yaliyotiririka kutoka miferejini. Lakini hatukuwa na wasiwasi. Nilitumaini kwamba tulikuwa tumechagua ngazi iliyofaa ili kuuepuka moto.

“Nilipokuwa nikikimbia chini, niliwaza ikiwa hiyo ndiyo iliyokuwa siku yangu ya mwisho kuwa hai? Niliendelea kusali kwa Yehova nami nikahisi nikiwa na amani isiyo ya kawaida. Sijawahi kuwa na amani ya moyoni ya aina hii. Sitasahau kamwe pindi hiyo.

“Hatimaye tulipotoka ndani ya jengo hilo, polisi waliendelea kuwaondosha watu wote kutoka mahali hapo. Nilipoiangalia ile minara, niliona kuwa yote ilikuwa imekatwa na kuachwa wazi. Lilikuwa jambo lisiloweza kuwaziwa.

“Kisha nikasikia sauti ya kiajabu—kimya kisicho cha kawaida kana kwamba maelfu ya watu waliacha kupumua. Ni kana kwamba mji wa New York haukuwa na watu wowote. Baadaye nikasikia mayowe. Mnara wa kusini ulianza kuporomoka wenyewe! Moshi, majivu, na vumbi zilipeperushwa kutuelekea. Ilikuwa kama kutazama sinema. Lakini hili lilikuwa tukio halisi. Ikawa vigumu kupumua kwa sababu ya vumbi nyingi.

“Nilipofika kwenye Daraja la Manhattan, niligeuka na kuuona ule mnara wa kaskazini ukiporomoka pamoja na antena yake ya televisheni. Nikiwa darajani, niliendelea kusali niweze kufika Betheli, makao makuu ya Mashahidi wa Yehova. Nilifurahi sana kuyaona majengo hayo. Na kwenye ukuta wa kiwanda niliyaona yale maandishi makubwa ambayo maelfu ya watu huyasoma kila siku, ‘Soma Neno la Mungu Biblia Takatifu Kila Siku’! Nilikuwa karibu kufika. Nilijitahidi sana nifike huko.

“Ninapokumbuka matukio hayo, ninaona uhitaji wa kutanguliza mambo muhimu maishani.”

“Niliona Watu Wakiruka Kutoka Kwenye Ule Mnara”

Jessica, mwenye umri wa miaka 22, aliona matukio hayo akitoka kwenye stesheni ya gari-moshi la chini ya ardhi mjini. “Nilipoangalia juu, niliona majivu, vifusi, na kila aina ya vipande vya chuma vikianguka chini. Watu walikosa subira na walivurugika sana huku wakingoja kupiga simu. Nilisali niwe mtulivu. Kisha kukawa na mlipuko mwingine. Vyuma na vioo vilianguka kutoka angani. Nikasikia makelele haya, ‘Ilikuwa ndege nyingine!’

“Nilipotazama juu, nilisikitika kuona watu wakiruka kutoka orofa za juu zilizokuwa na mawimbi ya moshi na moto mkali. Bado ninaweza kukumbuka mwanamume na mwanamke mmoja waliokuwa wameshikilia dirisha kwa muda, kisha wakaliachilia, na kuanguka, na wakaanguka na kuanguka. Lilikuwa jambo lenye kusikitisha sana.

“Hatimaye nilifika kwenye Daraja la Brooklyn, nikatoa viatu vyangu na kukimbia kuelekea upande ule mwingine wa Brooklyn kutoka kwenye Mto wa East. Niliingia kwenye jengo la ofisi ya Watchtower, ambapo nilitulizwa.

“Nikiwa nyumbani, usiku huo, nilisoma ule mfululizo wa makala katika toleo la Amkeni! la Agosti 22, 2001, ‘Kupambana na Mfadhaiko wa Tukio Lenye Kutisha.’ Jinsi nilivyohitaji habari hiyo!”

Msiba huo mkubwa uliwachochea watu kusaidia katika njia yoyote waliyoweza. Makala ifuatayo inaeleza jinsi misaada hiyo ilivyotolewa.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Mwandishi wa Amkeni! aliwahoji waokokaji wengi ingawaje haikuwezekana kuandika maelezo yao yote kwenye makala hizi. Ushirikiano wao ulisaidia kukamilisha na kuthibitisha masimulizi haya.

[Mchoro/Picha katika ukurasa wa 8, 9]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

YALIYOHARIBIWA KABISA

1 MNARA WA KASKAZINI 1 World Trade Center

2 MNARA WA KUSINI 2 World Trade Center

3 HOTELI YA MARRIOTT 3 World Trade Center

7 WORLD TRADE CENTER

YALIYOHARIBIWA SANA

4 WORLD TRADE CENTER

5 WORLD TRADE CENTER

L ONE LIBERTY PLAZA

D DEUTSCHE BANK 130 Liberty St.

6 U.S. CUSTOMS HOUSE 6 World Trade Center

N S MADARAJA YA KASKAZINI NA KUSINI YA WATU WANAOTEMBEA KWA MIGUU

YALIYOHARIBIWA KIDOGO

2F 2 WORLD FINANCIAL CENTER

3F 3 WORLD FINANCIAL CENTER

W WINTER GARDEN

[Hisani]

Kufikia Oktoba 4, 2001 3D Map of Lower Manhattan by Urban Data Solutions, Inc.

[Picha]

Juu kabisa: Mnara wa kusini uliporomoka kwanza

Juu: Wengine walikimbia kutafuta usalama katika majengo ya Watchtower

Kulia: Mamia ya wazimamoto na vikundi vya waokoaji walifanya kazi kwa bidii katika eneo la mlipuko

[Hisani]

AP Photo/Jerry Torrens

Andrea Booher/FEMA News Photo

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

AP Photo/Marty Lederhandler

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 4]

AP Photo/Suzanne Plunkett