Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupata Makao ya Kudumu

Kupata Makao ya Kudumu

Kupata Makao ya Kudumu

“Hata ikiwa ni kwa hali ya chini sana, kwetu ndiko kuzuri.”—John Howard Payne.

KWANZA vita ilizuka, vita iliyodumu muda mrefu. Kisha ukame ukatokea, ukame uliodumu muda mrefu. Baada ya ukame, kukaja njaa. Na watu wakalazimika kuhama makwao ili kutafuta maji, chakula, na kazi.

Maelfu ya watu walifika mpakani. Lakini kwa kuwa katika miaka ya karibuni wakimbizi milioni moja walikuwa tayari wameingia katika nchi hiyo jirani, haikukubali wakimbizi wengine. Mapolisi wa mpakani wenye marungu, waliwazuia watu wasivuke mpaka.

Afisa mmoja wa uhamiaji katika eneo hilo alitaja wazi sababu za kuwazuia wakimbizi hao wasiingie nchini humo. Alisema hivi: “Hawalipi kodi. Wao huharibu barabara. Wao hukata miti. Wao humaliza maji. La, hatutaki wakimbizi wengine.” *

Matukio hayo ya kuhuzunisha yameongezeka sana. Watu waliolazimishwa kuhama hukabili ugumu wa kupata makao ya kudumu. Ripoti moja ya hivi majuzi ya shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International ilisema hivi: ‘Idadi ya wakimbizi inapoongezeka, nchi mbalimbali zinakataa hata zaidi kuwasaidia.’

Huenda wale wanaofanikiwa kufika kwenye kambi ya wakimbizi wakapata usalama wa kadiri, lakini hawajihisi kwamba wako nyumbani. Na hali katika kambi zaweza kuwa ngumu sana.

Hali Katika Kambi za Wakimbizi

Mkimbizi mmoja huko Afrika alilalamika hivi: “Unaweza kufa kwa kupigwa risasi [huko nyumbani], lakini hapa [katika kambi ya wakimbizi] watoto wako watakufa njaa.” Kama vile baba huyo alivyong’amua, kambi nyingi huwa chafu nazo hukumbwa na uhaba wa chakula, maji na makao. Sababu za hali hiyo ni wazi. Huenda serikali za nchi zinazoendelea, ambazo hukumbwa na maelfu ya wakimbizi kwa ghafula, tayari zinashindwa kulisha raia zake. Serikali hizo haziwezi kuwasaidia sana wakimbizi wote wanaotaka kuingia katika nchi zao. Na kwa kuwa mataifa tajiri yana matatizo yao yenyewe, yanaweza kusita kuwasaidia wakimbizi walio katika nchi nyingine.

Wakati watu zaidi ya milioni mbili walipokimbia nchi moja ya Afrika mwaka wa 1994, kambi za wakimbizi zilizojengwa haraka zilikuwa chafu na hazikuwa na maji. Jambo hilo lilitokeza ugonjwa wa kipindupindu ambao uliua maelfu ya watu kabla haujadhibitiwa. Isitoshe, wapiganaji wenye silaha walichangamana na wakimbizi wengine na punde baadaye wakaanza kusimamia ugawanyaji wa misaada. Tatizo hilo halikutokea tu wakati huo. Ripoti moja ya shirika la Umoja wa Mataifa yasema hivi: ‘Kuwepo kwa vikundi vyenye silaha katika kambi kumewahatarisha sana wakimbizi wengine. Wametishwa, wamenyanyaswa, na kulazimishwa wajiunge na jeshi.’

Huenda wenyeji pia wakaumia kwa sababu ya ongezeko kubwa la wakimbizi wenye njaa. Katika eneo la Maziwa Makuu ya Afrika, maafisa fulani walilalamika hivi: “[Wakimbizi] wameharibu maghala yetu, mashamba yetu, mifugo yetu, mbuga zetu, wamesababisha njaa na kueneza magonjwa . . . [Wao] hupata misaada ya chakula lakini sisi hatupati chochote.”

Hata hivyo, huenda tatizo kubwa zaidi likawa kwamba kambi nyingi za wakimbizi za muda hugeuzwa kuwa makao ya kudumu. Kwa mfano, katika nchi moja ya Mashariki ya Kati, wakimbizi 200,000 hivi wamesongamana katika kambi iliyojengwa kwa ajili ya wakimbizi 50,000 hivi. Mmoja wao alisema hivi kwa huzuni: “Hatuna mahala pengine pa kwenda.” Wakimbizi hao ambao wameteseka kwa muda mrefu, wamewekewa vikwazo vikali vya kuajiriwa kazi katika nchi hiyo, na asilimia 95 kati yao hawana kazi au wameajiriwa kazi yenye mshahara mdogo. Afisa mmoja wa wakimbizi alisema hivi: ‘Sijui jinsi wanavyojiruzuku.’

Lakini ikiwa hali ni mbaya katika kambi za wakimbizi, huenda zikawa mbaya hata zaidi kwa watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao.

Majonzi ya Kulazimishwa Kuhama

Kwa mujibu wa mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi, ‘kiwango cha tatizo hilo la kulazimishwa kuhamia eneo jingine, kuteseka kwa wanadamu ambako husababisha tatizo hilo, na pia athari yake juu ya amani na usalama ulimwenguni, imesababisha hangaiko kubwa ulimwenguni pote.’ Watu hao wasio na makao hukabili hatari kubwa kuliko wakimbizi kwa sababu kadhaa.

Hakuna shirika la kimataifa ambalo hushughulikia mahitaji ya watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao, na matatizo yao hayatajwi mara nyingi kwenye vyombo vya habari. Serikali zao, zinazohusika katika vita ya aina fulani, hushindwa au hukataa kuwasaidia. Mara nyingi familia hugawanyika wakati zinapokimbia maeneo hatari. Kwa kuwa mara nyingi wao hutembea, watu fulani wanaolazimishwa kuhama hufa safarini wanapokimbilia mahala salama.

Wengi kati ya watu hao waliolazimishwa kuhama hukimbilia majiji, nao huishi katika hali ngumu kwenye vibanda au majengo yaliyoachwa ukiwa. Wengine huenda kwenye kambi za muda, ambazo hushambuliwa nyakati nyingine. Kwa kawaida, wao hukabili hatari kubwa ya kufa kuliko watu wengine katika nchi hiyo.

Hata jitihada zinazofanywa kwa nia nzuri ili kuwasaidia watu hao waliolazimishwa kuhama zaweza kuwadhuru. Kitabu The State of the World’s Refugees 2000 chasema hivi: ‘Katika mwongo wa mwisho wa karne ya 20, mashirika ya ufadhili yanayohudumia watu katika nchi zilizokumbwa na vita yaliokoa maelfu ya watu na kupunguza sana kuteseka. Hata hivyo, somo moja muhimu ambalo watu walijifunza katika mwongo huo ni kwamba wakati wa vita, vikundi vinavyopigana vinaweza kwa urahisi kutumia misaada vibaya, na kuimarisha watu wenye mamlaka wanaokandamiza haki za binadamu. Pia, misaada inayotolewa na mashirika ya ufadhili inaweza kutumiwa kuinua uchumi wa makundi yanayopigana, na hivyo kuendeleza vita.’

Kutafuta Maisha Bora

Mbali na wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao, kuna ongezeko la wakimbizi wa kiuchumi. Kuna visababishi kadhaa vya tatizo hilo. Tofauti iliyopo kati ya nchi tajiri na nchi maskini za ulimwengu inazidi, na kila siku watu fulani walio maskini hohehahe hutazama vipindi vya televisheni vinavyoonyesha maisha ya hali ya juu ya watu wanaoishi katika nchi fulani. Imekuwa rahisi kusafiri duniani na kuvuka mipaka. Pia, vita vya wenyewe kwa wenyewe na ubaguzi wa kikabila na wa kidini umewachochea sana watu kuhamia nchi zenye ufanisi.

Na ijapo wahamiaji fulani—hasa wale walio na watu wa jamaa katika nchi zilizoendelea kiviwanda—hufanikiwa kuhama, wengine huharibu maisha yao. Wale wanaodanganywa na wahalifu huwa hatarini. (Ona masanduku.) Familia yapaswa kufikiria kwa makini hatari hizo kabla ya kuhama kwa sababu za kiuchumi.

Mnamo mwaka wa 1996, meli moja kuukuu ilizama katika Bahari ya Mediterania, na watu 280 wakafa. Watu hao waliokufa walikuwa wakihama kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka nao walikuwa wamelipa kati ya dola 6,000 na dola 8,000 za Marekani ili wapelekwe Ulaya. Kabla ya tukio hilo, walikuwa tayari wameteseka kwa majuma kadhaa kutokana na njaa, kiu, na kuteswa kimwili. Safari yao ya kuboresha maisha iligeuka kuwa msiba.

Kila mkimbizi, mtu aliyelazimishwa kuhama, au mhamiaji haramu amewahi kupatwa na matatizo hayo. Iwe watu hao wamehamia mahala pengine kwa sababu ya vita, mnyanyaso, au umaskini, kuteseka kwao hutokeza maswali haya: Je, tatizo hilo litasuluhishwa? Au, je, wakimbizi watazidi kuongezeka daima?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Hali iliyotajwa hapo juu ilitokea mnamo Machi 2001 katika nchi moja ya Asia. Lakini matatizo kama hayo yametokea pia katika nchi kadhaa za Afrika.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Matatizo ya Wahamiaji Haramu

Mbali na wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao, idadi ya “wahamiaji haramu” ulimwenguni ni kati ya milioni 15 na milioni 30. Wengi kati ya watu hao ni wale wanaotaka kuhepa umaskini—na labda dhuluma na mnyanyaso pia—kwa kuhamia nchi tajiri.

Kwa kuwa imekuwa vigumu kupata hati halali za uhamiaji katika miaka ya karibuni, biashara haramu ya kuhamisha wahamiaji imeanzishwa. Kwa hakika, mashirika mengi ya wahalifu ya kimataifa yanachuma pesa nyingi kupitia biashara hiyo ya kuhamisha wahamiaji. Wapelelezi fulani wanakadiria kwamba biashara hiyo huleta faida ya dola bilioni 12 za Marekani kila mwaka bila kuwahatarisha sana wahalifu hao. Pino Arlacchi, msaidizi mmoja wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa alisema kwamba “hiyo ndiyo biashara haramu inayositawi haraka sana ulimwenguni.”

Wahamiaji haramu hawalindwi na sheria, na wahalifu hao huwanyang’anya pasipoti zao. Wahamiaji hao huajiriwa kazi kwenye karakana ambako wanafanya kazi katika hali mbaya na kulipwa mshahara mdogo, huajiriwa kazi za nyumbani, kazi ya kilimo, au katika biashara ya uvuvi. Wengine huwa makahaba. Wanapokamatwa na wenye mamlaka, wanaweza kufukuzwa nchi hiyo, bila hata ndururu. Wanapolalamika kuhusu hali ngumu za kikazi, huenda wakapigwa, wakabakwa au hata familia zao walizoacha nchini kwao zikatishwa.

Mara nyingi magenge ya wahalifu wanaowahamisha watu kiharamu huwavutia watu kwa kuwaahidi kazi zenye mishahara minono. Hivyo, huenda familia maskini ikawakabidhi wahalifu hao mali zake zote ili kumpeleka mshiriki mmoja wa familia yao Ulaya au Marekani. Iwapo mhamiaji hawezi kugharimia nauli yake, itampasa kufanya kazi ili kulipa deni hilo. Deni hilo laweza kuwa dola 40,000 za Marekani. Badala ya kupata maisha mazuri kama alivyoahidiwa, mhamiaji anakuwa mtumwa.

[Picha]

Wakimbizi haramu huko Hispania

[Sanduku/ Picha katika ukurasa wa 9]

Watoto Wazuri Huharibiwa

Familia ya Siri iliishi katika vilima vilivyoko Kusini-Mashariki mwa Asia, ambako wazazi wake walikuza mpunga. Siku moja mwanamke mmoja aliwaambia wazazi wa Siri kwamba angemtafutia kazi yenye mshahara mzuri jijini. Aliahidi kuwapa dola 2,000 za Marekani nao wakakubali kwani hizo zilikuwa pesa nyingi sana kwa wakulima hao. Hata hivyo, punde si punde Siri akaajiriwa kazi kwenye nyumba ya makahaba. Waajiri wake walimwambia kwamba alihitaji kulipa dola 8,000 za Marekani ili awekwe huru. Wakati huo Siri alikuwa na umri wa miaka 15.

Siri hangeweza kulipa deni hilo. Alipigwa na kubakwa ili akubali kufanya kazi hiyo. Maadamu angewaletea faida, hangeachiliwa huru. Jambo la kusikitisha ni kwamba hatimaye makahaba wengi huachiliwa wanapopata UKIMWI ili warudi wakafe kwenye vijiji vyao.

Biashara kama hiyo inasitawi katika nchi nyingine. Ripoti moja ya 1999 yenye kichwa International Trafficking in Women to the United States ilikadiria kwamba wanawake na watoto kati ya 700,000 na 2,000,000 huhamishwa kiharamu kila mwaka, hasa ili wawe makahaba. Baadhi yao huenda wakadanganywa, wengine hutekwa nyara; lakini karibu wote hulazimishwa kufanya kazi hiyo. Kijana mmoja wa Ulaya Mashariki aliyeokolewa kutoka kwenye genge la makahaba alisema hivi kuhusu watu hao waliomteka: “Sikufikiria jambo hilo linaweza kutukia. Watu hao ni wanyama.”

Baadhi ya watu hao wanaodhulumiwa wamechukuliwa kwenye kambi za wakimbizi na kuahidiwa kuwa wataajiriwa kazi zenye mishahara minono huko Ulaya au Marekani. Wanawake wengi waliotaka kuboresha maisha yao wamelazimishwa kuwa makahaba.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Chunguza Mambo kwa Makini Kabla ya Kuhama kwa Sababu za Kiuchumi

Kwa sababu kuna magenge mengi ya wahalifu wanaohamisha wahamiaji kiharamu na kwa sababu ya ugumu wa kupata hati halali za kuhamia nchi zilizoendelea, waume na akina baba wapaswa kufikiria kwa makini maswali yafuatayo kabla ya kufanya uamuzi.

1. Je, hali yetu ya kiuchumi ni mbaya sana hivi kwamba ni lazima mshiriki mmoja wa familia au familia yote kuhamia nchi ambako mishahara ni minono?

2. Tutahitaji kukopa pesa ngapi ili kulipia safari hiyo, na deni hilo litalipwaje?

3. Je, kuna faida kutenganisha familia ili kutafuta faida za kiuchumi ambazo huenda tukakosa kupata? Wahamiaji wengi haramu hushindwa kupata kazi ya kudumu katika nchi zilizoendelea.

4. Je, niamini habari ninazosikia kuhusu mishahara minono na misaada inayotolewa na serikali katika nchi hiyo? Biblia husema kwamba “mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.”—Mithali 14:15.

5. Nina uhakika gani kwamba hatutajihusisha na shirika la wahalifu?

6. Ikiwa shirika la wahalifu litapanga safari hiyo, je, ninafahamu kwamba huenda mke wangu—au binti yangu—akalazimishwa kuwa kahaba?

7. Je, ninang’amua kwamba nikihamia nchi nyingine kiharamu, ninaweza kukosa kuajiriwa kazi ya kudumu na huenda nikafukuzwa, na kupoteza pesa zote nilizotumia kulipia safari hiyo?

8. Je, ninataka kuwa mhamiaji haramu au kutumia njia zisizo halali ili kuingia katika nchi yenye ufanisi?—Mathayo 22:21; Waebrania 13:18.

[Mchoro/Ramani katika ukurasa wa 8, 9]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Jinsi Wakimbizi na Wafanyakazi Wahamiaji Wanavyohama

Maeneo yenye idadi kubwa ya wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao

Jinsi wafanyakazi wahamiaji wanavyohama hasa

[Hisani]

Vyanzo: The State of the World’s Refugees; The Global Migration Crisis; na World Refugee Survey 1999.

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mkimbizi asubiri kupelekwa kwenye makao mapya

[Hisani]

UN PHOTO 186226/M. Grafman