Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Mavazi ya Pengwini

Zaidi ya mavazi 1,000 yaliyoshonwa na watu waliojitolea ulimwenguni pote yametumwa Tasmania, Australia. Ni nani watakaoyavaa? Pengwini aina ya fairy—ndege wadogo wenye uzito wa kilogramu moja hivi wanaoishi katika eneo linalochafuliwa mara nyingi na mafuta yanayomwagika baharini. Gazeti National Post la Kanada laeleza hivi: “Ndege hao humeza mafuta yenye sumu yaliyoko kwenye manyoya yao wanapojisafisha. Watu wanajitolea kuwavalisha ndege walioloweka mafuta ili wasiweze kula mafuta hayo [kabla ya] kusafishwa.” Gazeti hilo linaripoti kwamba mavazi hayo pia hukinza baridi. Msemaji wa Idara ya Uhifadhi ya Tasmania, Jo Castle, anasema kwamba ndege wa baharini wa Kizio cha Kaskazini pia walivalishwa mavazi nyakati nyingine, lakini mtindo wa mavazi “ulibadilishwa kwa ajili ya ndege hao wadogo wa kizio cha kusini.”

Kula kwa Sauti

Kula kwa sauti hubishaniwa na wateja wa mikahawa ya supu ya tambi inayopendwa sana huko Japani. Wajapani wengi wa makamo na wazee huhisi kwamba tambi ndefu ni tamu zaidi zikiliwa kwa sauti pamoja na supu, zikiwa bado moto. Wanaona kula kwa sauti kuwa mazoea ya kuonyesha kwamba wanafurahia chakula. Lakini vijana Wajapani wana maoni tofauti kuhusu jinsi ya kula tambi ndefu. Gazeti The Japan Times laripoti hivi: “Vijana Wajapani huogopa kumwaga supu kwenye tai na nguo zao [za mitindo maalumu]. Kwa kuwa wamezoea adabu za nchi za Magharibi tangu utotoni, na vilevile chakula cha Magharibi, yaelekea wataudhika iwapo watu walio karibu nao watakula kwa sauti.” Ubishi juu ya kula kwa sauti umewafanya Wajapani wazee waogope kula kwa sauti wanapokula tambi katika mikahawa. Gazeti moja kuu la Japani liliwaunga mkono wazee lilipolalamika hivi: ‘Ingesikitisha sana kama watu wangeacha kabisa kula kwa sauti.’

Hatari za Kileo

Jarida la tiba la Uingereza, The Lancet, laripoti kwamba “idadi ya vijana waliojeruhiwa, kupooza, na kufa huko Ulaya kwa sababu ya kileo imeongezeka sana katika miaka ya karibuni.” Huko Ulaya, kileo hutumiwa zaidi kuliko mahali pengine ulimwenguni na husababisha vifo vya vijana 55,000 kila mwaka. Theluthi moja ya wanafunzi waliohojiwa huko Denmark, Finland, Greenland, Ireland, na Uingereza walikiri kwamba walikuwa wamelewa angalau mara tatu mwezi uliotangulia. Uchunguzi mmoja wa wanafunzi 100,000 wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 16 katika nchi 30 za Ulaya, ulionyesha kwamba idadi ya vijana waliotumia kileo iliongezeka zaidi katika Jamhuri ya Slovakia, Lithuania, Poland, na Slovenia. Gazeti Independent la London liliripoti kwamba Chuo cha Royal College of Physicians cha Uingereza chaonya kwamba sasa, wanawake walio katika miaka yao ya mapema ya 20 hupata ugonjwa fulani wa ini, ambao hapo awali uliwapata tu wanaume walevi katika miaka yao ya 40 na 50. Chuo hicho kilisema kwamba “utumiaji wa kileo ni mojawapo ya matatizo ya afya yanayogharimu serikali ya Uingereza fedha nyingi sana.”

Kuvuka Pasifiki kwa Mashua ya Makasia

Mtu mmoja amevuka Bahari ya Pasifiki kwa kutumia mashua ndogo ya makasia isiyo na matanga wala injini. Gazeti El Comercio la Lima lasema kwamba Mwingereza Jim Shekhdar alianza safari huko Peru mnamo Juni 2000. Baharia huyo mjasiri alichukua kifaa cha kuondoa chumvi kwenye maji ya baharini, redio, simu nne za setilaiti, na kifaa cha kutokezea umeme kwa miale ya jua ili awe na umeme wa kuendesha vifaa hivyo. Mwanamume huyo, aliyeitwa “baharia mwenye kichaa” na watu fulani, aliwasili Australia mnamo Machi 2001. Alikuwa amesafiri kilometa 15,000 baharini kwa muda wa miezi tisa. Katika safari yake alikuwa karibu kugongwa na meli ya mafuta na aliponea chupuchupu mashambulio kumi ya papa. Lakini msiba wa mwisho ulimpata siku ya mwisho wakati mawimbi makubwa yalipopindua mashua yake juu chini na ilimbidi kuogelea umbali wa meta 100 hadi pwani ambapo watu wa familia yake walikuwa wanamngojea.

Daktari Mwenye Urafiki Husaidia Wagonjwa Kupona

Gazeti The Times la London lasema kwamba “daktari mwenye urafiki anayewatuliza wagonjwa huwa na matokeo mazuri zaidi.” Baada ya kuchanganua uchunguzi 25 uliofanywa kuhusiana na jambo hilo, watafiti wa chuo kikuu cha York, Exeter, na Leeds, huko Uingereza, walikata kauli hivi: “Madaktari waliojaribu kuwa wachangamfu na wenye urafiki pamoja na wagonjwa, na kuwahakikishia kwamba wangepona karibuni, walikuwa na matokeo mazuri zaidi kuliko wale walioshughulikia wagonjwa kwa ubaridi, bila urafiki, na bila kuwatuliza.” Uchunguzi mmoja huko Sweden ulionyesha kwamba wagonjwa “walifurahi na kupona haraka zaidi walipotibiwa na daktari aliyewahakikishia kwamba wangepona, daktari aliyekuwa tayari kujibu maswali, na daktari aliyetumia muda mrefu zaidi kuwashughulikia.”

Faida ya Kufanya Mazoezi kwa Ukawaida

Watu wengi hufanya mazoezi ya mwili kwa bidii sana mara mojamoja ili kujaribu kuepuka unene, ugonjwa wa moyo, na matatizo mengine ya afya yanayosababishwa na kazi ya ofisini. Hata hivyo, gazeti la Süddeutsche Zeitung la Ujerumani laripoti kwamba uchunguzi wa karibuni unaonyesha kwamba kufanya mazoezi ya wastani kwa ukawaida huboresha usagaji wa chakula kuliko kufanya mazoezi ya bidii mara mojamoja. Mtafiti Mholanzi Dakt. Klaas Westerterp aliwachunguza watu 30 waliojitolea ili kuona kiasi cha nguvu walichotumia kila dakika. Matokeo yalionyesha kwamba ni afadhali kufanya mazoezi kidogo kila siku kuliko ‘kujaribu kufanya mazoezi kwa bidii sana mara mojamoja.’ Ripoti hiyo yapendekeza: “Jaribu kutembea na kupanda baiskeli mara nyingi iwezekanavyo ikiwa kazi yako ni ya kukaa au kusimama.”

Magari-Moshi ya Ufaransa Yanayoenda Kasi

Katika mwaka wa 1867 safari ya gari-moshi kutoka Paris hadi Marseilles ilichukua zaidi ya saa 16. Katika miaka ya 1960, safari hiyo ilichukua muda wa saa saba na nusu. Lakini, mnamo Juni 2001, shirika la Kitaifa la Reli la Ufaransa lilizindua reli mpya ya magari-moshi yanayoenda kasi kati ya majiji hayo mawili. Sasa abiria wanaweza kusafiri kwa mwendo wa kilometa 300 kwa saa, na kusafiri zile kilometa 740 kati ya majiji hayo kwa muda wa saa tatu tu. Reli yenye urefu wa kilometa 250 iliyo kusini ya Lyons hupitia kwenye zaidi ya madaraja 500. Kilometa nane hivi za reli hiyo zinapitia chini ya ardhi na kilometa 17 hupitia kwenye madaraja marefu ya chuma. Gazeti Le Monde la Ufaransa lasema kwamba “magari-moshi 20 yanayoelekea pande zote mbili yanaweza kusafiri katika hali ya usalama kabisa kwenye reli hiyo katika muda wa saa moja.” Hiyo ingemaanisha kwamba gari-moshi moja lingepita kila dakika tatu.

Watoto Waliofadhaika

Gazeti El Universal la Mexico City lasema hivi: “Siku hizi, watoto hawachezi nje, hawastarehe na hawana utulivu, jinsi ilivyokuwa miaka kadhaa iliyopita.” Watafiti wameona kwamba mtoto aliye na umri wa miaka 10 anakabili kiwango cha mfadhaiko ambacho mtu mwenye umri wa miaka 25 alikabili mwaka wa 1950. Mfadhaiko huo hutokana na masomo na mambo mengine ambayo wazazi hufikiri yatamsaidia mtoto wao kuwa na wakati ujao mzuri. Lakini gazeti hilo lasema kwamba masomo hayo ya ziada “huathiri afya yake, starehe yake, na maendeleo yake.” Ripoti hiyo inapendekeza kwamba wazazi wapunguze shughuli za ziada za watoto wao, ili watoto waweze kutumia wakati mwingi nyumbani. Lakini haimaanishi wanapaswa kukaa kitako tu au kutazama televisheni au kucheza michezo ya kompyuta baada ya shule, bali “wanapaswa kucheza nje pamoja na watoto wengine, kukimbia, kupanda baiskeli, kucheza michezo ya kuchemsha bongo, au kuchora.”

Joto la Bahari Linaloongezeka Huathiri Wanyama na Mimea

Hivi majuzi, wanasayansi waliotembelea Kisiwa cha Heard kilichopo umbali wa kilometa 4,600 kusini-magharibi ya Australia waligundua kwamba idadi ya wanyama na mimea imebadilika sana. Gazeti la West Australian lasema kwamba “pengwini aina ya king, sili wenye manyoya, na ndege aina ya mnandi wameongezeka sana, na mimea mingi inasitawi kwenye maeneo yaliyofunikwa kwa barafu hapo mbeleni.” Mwanabiolojia Eric Woehler alisema kwamba kulikuwa na pengwini sita tu aina ya king waliojamiiana kwenye kisiwa hicho mwaka wa 1957. Anasema, “sasa kuna zaidi ya pengwini 25,000.” Woehler alisema kwamba halijoto ya uso wa bahari imeongezeka kwa robo tatu ya digrii moja Selsiasi katika miaka 50 iliyopita. Aliongeza kwamba “ongezeko hilo linaloonekana kuwa dogo sana, ndilo limesababisha mabadiliko hayo tunayoona.” Woehler alidhani kwamba hatimaye huenda joto litazidi sana hivi kwamba mimea na wanyama fulani watatoweka kabisa katika kisiwa hicho.