Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Punda-Mwitu wa Afrika

Punda-Mwitu wa Afrika

Punda-Mwitu wa Afrika

NA MWANDISHI WA AMKENI! KATIKA AFRIKA

KUNDI la punda-milia elfu moja hivi lakimbia-kimbia kwa uhuru katika ukanda wa mbuga ya Afrika. Mabavu ya punda-milia hao yainuka na kushuka juu-chini, juu-chini huku shingo zao zilizojaa manyoya zikisonga kulingana na miendo yao kabambe. Sauti ya kwato zao zinazoikanyaga ardhi iliyokauka zanguruma kwenye nyanda tambarare. Wingu la vumbi jekundu lapeperuka nyuma yao nalo laweza kuonekana kwa mbali sana. Wanakimbia na kurandaranda kwa uhuru.

Wanaanza kutembea polepole, kisha wasimama kana kwamba wameonyeshwa ishara fulani isiyoonekana. Wanauma nyasi kavu kwa meno yao mapana yenye nguvu. Kundi hilo liko chonjo, linatazama huku na huku, linasikiliza, na kunusanusa hewa mara kwa mara. Linasikia sauti ya ngurumo ya simba kwa sababu upepo unalielekea, nalo lashikwa na wasiwasi. Laijua sauti hiyo vizuri sana. Masikio yao yakiwa wima, nyasi nazo zingali zaning’inia midomoni, punda-milia hao wanatazama upande walikosikia sauti hiyo. Wakiwa hawaoni hatari yoyote karibu, wainamisha shingo zao tena na kuendelea kula.

Joto lianzapo kuongezeka, wanaendelea tena na mwendo wao. Wakati huu ni harufu ya maji inayovuta punda-mwitu hao kuelekea mtoni. Wanasimama katika sehemu iliyoinuka ya ukingo wa mto na kukodolea macho maji ya rangi ya mchanga yanayotiririka polepole, wakitoa pumzi puani na kukwangua vumbi. Wanasitasita, wakitambua hatari inayoweza kutokea chini ya mto uliotulia. Lakini wana kiu kali, na wengine wanaanza kusukumana. Wanakimbia kwa kishindo hadi ukingoni mwa mto. Kila mmoja anakunywa maji hadi wanapokata kiu, kisha wageuka na kurudi kwenye nyanda tambarare.

Kufikia jioni, kundi hilo latembea bila haraka kwenye nyasi ndefu. Umbo lao laonekana kama kivuli katika mwanga mwekundu unaong’aa wa jua linalotua, huku wakiwa wamezungukwa na mbuga maridadi ya Afrika, wanavutia wee!

Wenye Milia na Wenye Ushirikiano

Maisha ya kila siku ya punda-milia hayabadiliki. Harakati yao ya kutafuta chakula na maji daima huwafanya waendelee kurandaranda. Wakiwa malishoni kwenye nyanda tambarare, punda-milia huonekana wakiwa safi na wanono, ngozi yao yenye milia ikiwa imejinyoosha kwenye maungo yao yenye nguvu. Milia ya punda hao ni ya pekee, na kama vile ambavyo watu wengine hudai, milia ya punda mmoja haifanani na ile ya mwingine. Milia yao myeupe na myeusi yenye kutokeza huonekana tofauti na wanyama wale wengine wa mbuga. Hata hivyo sura yao yapendeza na yafaana kabisa na mbuga ya Afrika.

Kwa kawaida punda-milia ni wenye ushirikiano sana. Wakiwa mmoja-mmoja wao huwa na muungano thabiti unaoweza kudumu muda wote wa maisha yao. Kundi kubwa la punda-milia laweza kuwa na maelfu kadhaa ya wanyama. Katika kundi hilo kubwa kuna vikundi vidogo-vidogo vya familia vilivyo na punda dume aliye na punda majike. Vikundi hivyo vidogo vya familia hugawanya washiriki wake kulingana na utaratibu fulani. Punda jike mwenye kuongoza huamua mahali watakapoenda. Yeye huongoza, huku punda majike wengine na watoto wao wakifuatana mmoja-mmoja kwa safu. Ingawa hivyo, punda dume ndiye mwenye madaraka. Akitaka familia yake ibadili mwendo, yeye humwendea punda jike aliye kiongozi na kumwashiria kwa kumgusa akimwelekeza upande mwingine.

Punda-milia hupenda kusafishwa na kuchanwa, na ni kawaida kuwaona wakisugua na kukunakuna kwa meno mabavu, mabega, na migongo ya wenzao. Yaelekea kufanya hivyo huwafanya wawe na ukaribu sana kati yao na huanza watoto wanapokuwa na umri wa siku chache tu. Ikiwa hakuna mshiriki wa familia anayepatikana ili afanye hivyo, punda-milia hao wanaowashwa hujibingirisha mchangani au kujisugua kwenye miti, kilima cha mchwa, au kitu chochote kilichosimama.

Pambano la Kuishi

Maisha ya punda-milia yamejaa hatari. Simba, mbwa-mwitu, fisi, chui, na mamba, humwona punda huyo mwenye uzani wa kilogramu 250 kuwa windo rahisi sana. Punda-milia anaweza kukimbia kilometa 55 kwa saa, lakini mara nyingi hushikwa ghafula na wanyama wawindaji ambao hutumia ujanja. Simba huvizia, mamba nao hujibanza chini ya maji yenye topetope, nao chui huotea gizani.

Mbinu za punda-milia za kujikinga zategemea kama washiriki wengine wa kundi lake wako chonjo na chapuchapu. Ingawa walio wengi hulala usiku, sikuzote kuna wale ambao huwa macho, wakisikiliza, na kulinda. Punda-milia anapomwona mnyama mwindaji akikaribia, yeye hutahadharisha kundi lote kwa kutoa mlio fulani. Mara nyingi, ikiwa mnyama mmoja katika kundi ni mgonjwa au mzee na hawezi kutembea haraka, punda-milia wenzake watatembea polepole au watangoja hadi mnyama huyo atakapoweza kujiunga nao. Watishwapo na hatari, punda dume husimama bila woga kati ya mnyama mwindaji na punda majike, huku akimwuma na kumpiga mateke adui ili kulipatia kundi nafasi ya kukimbia.

Ushirikiano huo wa kifamilia waonyeshwa katika kisa kimoja kilichotokea kwenye Nyanda za Serengeti, Afrika, kama ilivyoshuhudiwa na mwanamazingira Hugo van Lawick. Akisimulia jinsi kundi la mbwa-mwitu lilivyoanza kufukuza kundi la punda-milia, alisema kwamba mbwa hao walitenga punda jike, na watoto wake wawili. Kundi lote la punda-milia lilipotoroka, mama na mtoto wake mmoja walipigana kwa ushujaa na mbwa-mwitu hao. Upesi mbwa hao wakawa wakali zaidi, na punda jike na yule mtoto wake wakaanza kuchoka. Kwa kweli ilionekana kwamba watakufa. Van Lawick akumbuka hali hiyo yenye kusikitisha akisema: “Kwa ghafula nilisikia ardhi ikitetemeka, na nilipotazama huku na huku, nilishangaa kuona punda-milia kumi wakija kwa kasi. Baada ya muda mfupi kundi hilo lilizingira walio wake, yule mama na watoto wake wawili, kisha wakatimua mbio ghafula kuelekea upande ambao wale punda-milia walitoka. Mbwa hao waliwafuata kwa meta 50 hivi lakini walishindwa kupenya kwenye kundi hilo na upesi wakakata tamaa.”

Kulea Familia

Punda-milia jike humlinda sana mtoto wake mchanga na mwanzoni huwa hataki wengine katika kundi wamkaribie. Wakati huo wa kujitenga, mtoto huwa na uhusiano wa karibu sana na mama yake. Mtoto huyo mchanga hukumbuka muundo wa milia myeupe na myeusi ya mama yake. Baadaye, atatambua sauti, harufu, na milia ya mama yake, naye hatamkubali punda-milia jike yeyote yule.

Watoto waliozaliwa karibuni hawawi na milia myeupe na myeusi kama ya wazazi wao. Milia yao huwa na rangi ya nyekundu-kahawia nayo hugeuka kuwa myeusi wanapoendelea kukua. Katika kundi kubwa, watoto kutoka katika vikundi mbalimbali vya familia hukusanyika na kucheza pamoja. Wao hukimbizana, hupigana mateke na kukimbia katikati ya punda-milia wakubwa, ambao nyakati nyingine hucheza nao. Watoto hao hufanya michezo ya kufukuza ndege na wanyama wengine wadogo-wadogo huku wakitimua mbio kwa miguu yao mirefu myembamba. Miguu yao mirefu myembamba, macho meusi makubwa na yenye kope nyingi, ngozi yenye manyoya mororo, yanawafanya wawe wanyama wadogo wenye kupendeza.

Walio Huru na Wazuri Ajabu

Leo makundi makubwa ya punda-milia yanaweza kuonekana yakirandaranda na yakiwa huru kwenye nyanda za rangi ya njano-njano za Afrika. Inavutia kuwatazama tu.

Ni nani anayeweza kukana kwamba punda huyo, mwenye milia myeupe na myeusi isiyo na kifani, mwaminifu kabisa kwa familia yake, na mwenye uhuru wa kutembea, ni kiumbe mwenye fahari na mzuri ajabu? Kupata kumjua mnyama huyo hujibu swali lililoulizwa maelfu ya miaka iliyopita: “Ni nani aliyempeleka punda-milia aende huru?” (Ayubu 39:5) Jibu liko wazi. Ni Mfanyi wa viumbe vyote vilivyo hai, Yehova Mungu.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Kwa Nini Punda Hao Wana Milia?

Wale wanaoamini mageuzi hushindwa kueleza kwa nini punda hao wana milia. Wengine wamefikiria kwamba huenda ikawa inatumika kama ishara fulani ya kutoa onyo. Hata hivyo, ni dhahiri kwamba, simba na wanyama wengine wawindaji hawaogopeshwi kamwe na milia ya punda.

Wengine wamedokeza kwamba milia hiyo hutumika kama njia ya kuvutia kingono. Hata hivyo, kwa kuwa punda-milia wote wana milia ileile, hii haielekei kuwa sababu inayofaa.

Wengine husema kwamba milia myeupe na myeusi ilitokea ili kuwasaidia wakabiliane na jua kali la Afrika. Lakini basi, kwa nini wanyama wengine hawana milia?

Habari nyingine ya kuwaziwa tu yasema kwamba milia ya punda humsaidia kujificha. Wanasayansi wamegundua kwamba jua kali la nyanda za Afrika kwa kweli hukengeusha na kuzuia umbo la punda-milia, likifanya iwe vigumu kumwona akiwa mbali. Hata hivyo, kujificha huko kwa mbali hakuwezi kusaidia sana kwa kuwa simba, ambaye ni adui mkubwa wa punda-milia, hushambulia tu akiwa karibu.

Pia imedaiwa kwamba wanapotimua mbio kwa hofu, kundi kubwa la punda-milia huvuruga simba wanaowinda na kuwafanya wasiweze kukazia fikira mnyama mmoja. Lakini, ukweli ni kwamba, uchunguzi wa wanyama-mwitu umeonyesha kwamba simba ni wenye ustadi na wenye mafanikio wanapowinda punda-milia kama tu vile wanapowinda wanyama wengine.

Jambo hilo hutatanisha hata zaidi kwa kuwa nyakati nyingine milia ya punda huyo humhatarisha. Usiku, kwenye nyanda zilizomulikwa na mbalamwezi, milia myeupe na myeusi ya punda huyo humfanya aonekane zaidi ya wanyama wengine walio na rangi moja. Kwa kuwa mara nyingi simba huwinda usiku, hiyo humfanya punda-milia awe hatarini.

Kwa hiyo punda huyo alitoa wapi milia yake? Jibu ni rahisi: “Ni mkono wa BWANA uliofanya haya.” (Ayubu 12:9) Naam, Muumba aliumba viumbe wa dunia na sifa mbalimbali zinazowafaa katika maisha yao, ambazo huenda binadamu asizielewe kabisa. Muundo wa ajabu wa viumbe hai huwa na kusudi jingine. Huwafurahisha wanadamu. Kwa kweli, uzuri wa uumbaji umewachochea wengi kuhisi kama alivyohisi Daudi wa kale: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako.”—Zaburi 104:24.