Ulimwengu Ambao Kila Mtu Atafurahia
Ulimwengu Ambao Kila Mtu Atafurahia
“Kwa kuwa tatizo la wakimbizi linakumba ulimwengu wote, ni lazima masuluhisho yatafutwe ulimwenguni pote.”—Gil Loescher, profesa wa mahusiano ya kimataifa.
WENZI wawili wachanga walianza safari usiku. Kwa kuwa alihangaikia usalama wao, mume huyo hakupoteza wakati, hata ingawa walikuwa na mtoto mchanga. Alikuwa amesikia kwamba mtawala mkatili wa nchi hiyo alipanga njama kutekeleza mauaji katika mji huo. Baada ya safari ngumu ya zaidi ya kilometa 160 hivi, hatimaye familia hiyo ilivuka mpaka na kupata usalama.
Baadaye, familia hiyo maskini ikawa maarufu ulimwenguni pote. Mtoto huyo aliitwa Yesu, na wazazi wake waliitwa Maria na Yosefu. Wakimbizi hao hawakuhama ili kutafuta mali. Badala yake, maisha yao yalikuwa hatarini. Kwani, mtoto wao ndiye aliyekuwa shabaha ya shambulizi hilo!
Sawa na wakimbizi wengine, Yosefu na familia yake hatimaye walirudi nyumbani kwao hali ya kisiasa ilipotulia. Lakini, pasipo shaka uhai wa mtoto wao mchanga uliokolewa kwa sababu walikimbia bila kukawia. (Mathayo 2:13-16) Misri, nchi waliyokimbilia, ilijulikana kwa kukubali wakimbizi wa kisiasa na wa kiuchumi. Karne nyingi kabla ya hapo, babu za Yesu walikuwa wamekimbilia Misri wakati nchi ya Kanaani ilipokumbwa na njaa.—Mwanzo 45:9-11.
Wako Salama Lakini Hawajatosheka
Mifano ya Biblia na ya siku hizi huonyesha wazi kwamba kukimbilia nchi nyingine kwaweza kuokoa uhai. Hata hivyo, familia hufadhaika sana wakati inapolazimika kuacha makao yake. Ijapo makao yao yaweza kuwa madogo, huenda walitumia pesa na miaka mingi ili kuyatengeneza. Na huenda ikawa walirithi makao hayo ambayo yanawahusianisha na utamaduni wao na nchi yao. Isitoshe, wakimbizi wanaweza kukimbia na mali chache tu au hata bila chochote. Hivyo, mara nyingi wakimbizi hutumbukia katika umaskini, haidhuru jinsi hali yao ya kiuchumi ilivyokuwa hapo awali.
Wakimbizi wanaweza kusahau haraka kwamba wamepata usalama iwapo hawana tumaini jingine ila tu kuishi katika kambi ya wakimbizi daima. Na hali yao huwa yenye kufadhaisha zaidi inapoendelea kwa muda mrefu na hasa wasipochangamana na wenyeji wa eneo walilokimbilia. Sawa na watu wengine, wakimbizi hutaka kuwa na makao ya kudumu. Kambi ya wakimbizi si mahala pazuri pa kuwalea watoto. Je, kuna wakati ambapo kila mtu atakuwa na makao ya kudumu?
Je, Warudishwe Makwao?
Katika miaka ya 1990, watu milioni tisa hivi waliokuwa wamelazimishwa kuhama makwao walirudi nyumbani hatimaye. Baadhi ya watu hao walifurahia jambo hilo, na walianza mara moja maisha mapya. Lakini wengine walikuwa wamekata tamaa. Walirudi tu kwa sababu hali ilikuwa mbaya katika nchi waliyokuwa wamekimbilia. Matatizo waliyokabili katika nchi hiyo yalikuwa makubwa sana hivi kwamba waliona ilikuwa afadhali kurudi nyumbani, japo hawangekuwa salama.
Hata katika hali nzuri kabisa, watu wanaorudishwa makwao hukabili magumu kwa sababu inawabidi kuhama kwa mara ya pili.
Kitabu The State of the World’s Refugees 1997-98 chasema hivi: ‘Kila mara wakimbizi wanapohamishwa, wanapoteza mashamba, kazi, nyumba, na mifugo. Na wanakabili ugumu wa kuanza maisha mapya.’ Uchunguzi mmoja uliofanywa kuhusu wakimbizi waliorudishwa makwao huko Afrika ya kati uliripoti kwamba ‘huenda wakimbizi waliosaidiwa walipokuwa uhamishoni wakakabili magumu mengi zaidi makwao kuliko yale waliyokuwa nayo uhamishoni.’Hata hivyo, hali ya mamilioni ya wakimbizi wanaolazimishwa kurudi nchini kwao inasikitisha hata zaidi. Wao hupata nini wanaporudi? Ripoti moja ya shirika la Umoja wa Mataifa ilisema hivi: “Huenda ikawabidi wakimbizi hao wanaorudishwa makwao kuishi mahala ambapo hakuna sheria, mahala penye wavamizi na uhalifu wa kijeuri, mahala ambapo maaskari walioondolewa jeshini wanawashambulia raia na mahala ambapo watu wengi wanaweza kupata silaha ndogondogo.” Kwa wazi, watu waliorudishwa makwao hawawezi kuwa salama hata kidogo katika mazingira hayo magumu.
Ulimwengu Ambamo Watu Wote Watakuwa Salama
Pasipo kushughulikia visababishi vyenyewe, matatizo ya wakimbizi hayawezi kamwe kusuluhishwa kwa kuwalazimisha kurudi nyumbani. Bi. Sadako Ogata, aliyekuwa mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi, alisema hivi mnamo mwaka wa 1999: “Matukio ya mwongo huu—na hasa yale ya mwaka uliopita—yanaonyesha wazi kwamba haiwezekani kuzungumzia masuala ya wakimbizi bila kuongea juu ya usalama.”
Na mamilioni ya watu ulimwenguni pote hawaishi kwa usalama. Kofi Annan, katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, anasema hivi: “Katika sehemu fulani za ulimwengu, mataifa yameanguka kwa sababu ya vita vya kikabila na vya wenyewe kwa wenyewe na hivyo yameshindwa kuwalinda raia wake. Kwingineko, serikali zimehatarisha usalama wa watu kwa kukataa kutimiza masilahi ya watu wote, kwa kuwanyanyasa wapinzani wake na kuwaadhibu watu wasio na hatia wa makabila madogo.”
Kwa kawaida, vita, mnyanyaso, na ujeuri wa kikabila—visababishi vya ukosefu wa usalama ambavyo Kofi Annan alitaja—husababishwa na chuki, ubaguzi, na dhuluma. Maovu hayo hayatamalizwa kwa urahisi. Je, hilo lamaanisha kwamba tatizo la wakimbizi litazidi?
Tatizo hilo lingezidi ikiwa wanadamu wangeruhusiwa waendelee kushughulikia mambo. Lakini katika Biblia, Mungu anaahidi ‘kuvikomesha vita hata mwisho wa dunia.’ (Zaburi 46:9) Pia, kupitia nabii wake Isaya, yeye asema kuhusu wakati ambao watu “watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. . . . Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na BWANA, na watoto wao pamoja nao.” (Isaya 65:21-23) Bila shaka, hali hizo zitakomesha kabisa tatizo la wakimbizi. Je, inawezekana hali hizo ziwepo?
Utangulizi wa hati ya Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa wasema hivi: ‘Kwa kuwa vita huanza katika akili za watu, vivyo hivyo amani yapaswa kuanza katika akili za watu.’ Muumba wetu anajua kwamba watu wanapaswa kubadili mawazo yao. Nabii huyohuyo anaeleza ni kwa nini siku moja watu wote duniani wataishi wakiwa salama: “Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua BWANA, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”—Isaya 11:9.
Tayari Mashahidi wa Yehova wanajua kwamba ujuzi juu ya Yehova unaweza kushinda ubaguzi na chuki. Kupitia kazi yao ya ulimwenguni pote ya kuhubiri, wao hufundisha kanuni za Maandiko ambazo zinawatia watu moyo kupendana badala ya kuchukiana, hata katika nchi zenye vita. Pia, wao huwasaidia wakimbizi kadiri wawezavyo.
Kwa upande mwingine, wanafahamu kwamba suluhisho la kudumu kwa tatizo la wakimbizi litaletwa na Mfalme aliyewekwa na Mungu, Yesu Kristo. Yeye anajua jinsi chuki na ujeuri zinavyoweza kuharibu maisha ya watu kwa urahisi. Biblia hutuhakikishia kwamba atahukumu maskini kwa uadilifu. (Isaya 11:1-5) Chini ya utawala wake wa mbinguni, mapenzi ya Mungu yatafanywa duniani, kama huko mbinguni. (Mathayo 6:9, 10) Wakati huo utakapofika, hakuna mtu atakayelazimika kuwa mkimbizi tena. Na kila mtu atakuwa na makao yake mwenyewe ya kudumu.
[Sanduku katika ukurasa wa 12]
Ni Nini Kinachohitajiwa Ili Kusuluhisha Tatizo la Wakimbizi?
“Kutosheleza mahitaji ya wakimbizi wote na ya watu wote waliolazimishwa kuhamia maeneo mengine ya nchi yao, kunahusisha mengi zaidi ya kuandaa usalama na msaada wa muda. Kunahusisha kuondoa mnyanyaso, ujeuri, na mapambano yanayowalazimisha watu kuhama. Kunahusisha kufahamu kwamba wanaume, wanawake, na watoto wote wana haki ya kuwa na amani, usalama, na adhama bila kulazimika kukimbia makwao.”—The State of the World’s Refugees 2000.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 13]
Ufalme wa Mungu Utaleta Suluhisho Gani?
“Haki itadumu katika nchi iliyokuwa nyika, uadilifu utatawala katika mashamba yenye rutuba. Kutokana na uadilifu watu watapata amani, utulivu na usalama utadumu milele. Watu wangu watakaa katika makao ya amani, katika maskani salama na mazingira matulivu.”—Isaya 32:16-18, Biblia Habari Njema.