Watu Wanaotafuta Usalama
Watu Wanaotafuta Usalama
“Umwagaji-damu na mnyanyaso unaowalazimisha watu kutoroka ili kuokoa uhai wao haukumalizika katika karne ya 20. Milenia mpya ilipoanza makumi ya mamilioni ya watu walikuwa katika kambi za wakimbizi na kwenye makao mengine ya muda, wakihofu kwamba watauawa wakijaribu kurudi makwao.”—Bill Frelick, Kamati ya Wakimbizi ya Marekani.
JACOB alitamani sana jambo fulani. Alitamani sana kuishi mahala penye amani, ambapo mbuzi wa familia yake hawangeuawa kwa mabomu, na mahala ambapo angeweza kwenda shuleni.
Watu wa mji wa kwao walimweleza kwamba mahala pa aina hiyo palikuwapo, ingawa palikuwa mbali sana. Babake alimwambia kwamba safari ya kwenda mahala hapo ilikuwa hatari sana, kwani watu fulani walikuwa wamekufa njaa na kwa kukosa maji njiani. Lakini wakati jirani yake, ambaye mume wake alikuwa ameuawa, alipoanza safari pamoja na watoto wake wawili, Jacob aliamua kusafiri peke yake.
Jacob hakubeba chakula wala nguo. Siku ya kwanza, alikimbia bila kusimama. Barabara ilikuwa imejaa maiti. Siku iliyofuata, alikutana na mwanamke mmoja wa mji wa kwao aliyemwambia kuwa angeweza kusafiri pamoja naye na rafikize. Walitembea kwa siku nyingi huku wakipita vijiji vilivyokuwa mahame. Siku moja walipita katikati ya eneo lililotegwa mabomu ya ardhini, na mtu mmoja katika kikundi chao akauawa. Walikula majani.
Siku kumi baadaye, watu wakaanza kufa kwa sababu ya uchovu na njaa. Punde baadaye, wakashambuliwa na ndege za vita. Hatimaye, Jacob alivuka mpaka na akafika kwenye kambi ya wakimbizi. Sasa yeye huenda shuleni, naye hatishwi tena na sauti ya ndege. Ndege zote anazoona siku hizi ni zile zinazobeba vyakula badala ya mabomu. Lakini anakosa sana familia yake, na angependa kurudi nyumbani.
Kuna watu wengi ulimwenguni wanaokumbwa na hali kama ya Jacob. Wengi wao wamefadhaishwa na vita na wanateseka kwa sababu ya njaa na kiu. Wengi wao hawajaishi kamwe na familia zao, na wengi hawatarudi
kamwe nyumbani kwao. Wao ni maskini hohehahe.Mkuu wa Tume ya Umoja wa Mataifa Inayoshughulikia Wakimbizi huwaainisha hao maskini wanaohamahama katika vikundi viwili. Mkimbizi ni mtu anayetoroka nchi yake kwa sababu ya kuhofu mnyanyaso au ujeuri. Kikundi cha pili ni cha watu waliolazimishwa kuhama makwao hadi eneo jingine la nchi yao kwa sababu ya vita au hatari nyingine kubwa. *
Hakuna ajuaye idadi kamili ya wakimbizi na watu waliolazimishwa kuhama makwao ambao wanaishi kwa shida katika kambi za muda au wanahamahama wakitafuta usalama. Kwa mujibu wa vyanzo fulani vya habari, huenda kuna wakimbizi milioni 40 hivi ulimwenguni pote na nusu ya idadi hiyo ni watoto. Wakimbizi wote hao hutoka wapi?
Tatizo la Siku Zetu
Tatizo la wakimbizi liliongezeka mwishoni mwa vita ya kwanza ya ulimwengu. Vita ilipokwisha, milki zilivunjika na makabila madogo-madogo yalikandamizwa. Kwa sababu hiyo, mamilioni ya Wazungu walikimbilia nchi nyingine. Vita ya pili ya ulimwengu—ambayo ilikuwa mbaya zaidi ya ile ya kwanza—iliwalazimu tena mamilioni ya watu kuondoka makwao. Tangu mwaka wa 1945, vita vimepiganwa katika nchi chache lakini bado vimewafadhaisha watu wanaoishi katika nchi hizo.
“Ingawa sikuzote vita vimetokeza wakimbizi, ni katika karne ya ishirini tu ambapo vita kati ya mataifa mbalimbali vimeathiri watu wote katika mataifa hayo,” ndivyo anavyoeleza Gil Loescher katika kitabu chake cha mwaka wa 1993 cha Beyond Charity—International Cooperation and the Global Refugee Crisis. ‘Kwa kuwa wapiganaji na vilevile watu wasiopigana waliuawa wakati wa vita, watu wengi wakawa wakimbizi ili kuepuka jeuri hiyo iliyoelekezwa kwa watu wote.’
Isitoshe, vita vingi vya leo ni vya wenyewe kwa wenyewe na vinawaathiri sana wanaume waliofikisha umri wa kwenda vitani na vilevile wanawake na watoto. Baadhi ya vita hivyo huendelea kwa muda mrefu kwa sababu vinachochewa na migawanyiko mikubwa ya kikabila na ya kidini. Katika nchi moja ya Afrika, ambako vita ya wenyewe kwa wenyewe imeendelea kwa miaka 18, kuna watu milioni nne waliolazimishwa kuhama makwao, huku mamia ya maelfu ya watu wengine wamekimbilia nchi nyingine.
Sikuzote, inawabidi watu wanaoishi katika maeneo yenye vita wahame makwao ili kuepuka jeuri. Kitabu The State of the World’s Refugees 1997-98 chasema hivi: “Wakimbizi huhama makwao na kuingia katika nchi nyingine kwa sababu inawalazimu kufanya hivyo, wala si kwa sababu ya starehe au kwa kupenda.” Hata hivyo, siku hizi si rahisi kupata kibali cha kuingia katika nchi nyingine.
Katika miaka ya 1990, idadi ya wakimbizi ulimwenguni ilipungua kutoka milioni 17 hivi hadi milioni 14. Hayo yanaonekana kuwa maendeleo, lakini sivyo ilivyo. Katika mwongo huohuo, inakadiriwa kwamba idadi ya watu waliolazimishwa kuhamia sehemu nyingine ya nchi yao ilifikia
milioni 25 hadi milioni 30. Mbona kukawa na ongezeko hilo?Imekuwa vigumu zaidi kupata hati rasmi za kuwa mkimbizi kwa sababu mbalimbali. Huenda nchi zikakataa kukubali wakimbizi, ama kwa sababu haziwezi kushughulikia wakimbizi wengi au kwa sababu zinahofu kwamba idadi kubwa ya wakimbizi inaweza kusababisha hali mbaya ya kiuchumi na ya kisiasa. Hata hivyo, nyakati nyingine wakimbizi wenye hofu hukosa nguvu, chakula, au fedha za kuwategemeza wanapotembea hadi mpakani. Wao hukosa la kufanya ila tu kuhamia eneo lenye usalama katika nchi yao.
Ongezeko la Wakimbizi wa Kiuchumi
Kuongezea mamilioni ya wakimbizi wa kawaida, kuna mamilioni ya watu wengine maskini ambao hutaka kuboresha hali yao ya maisha wakitumia njia moja tu wanayojua—kuhamia nchi nyingine ambako hali za maisha ni afadhali.
Mnamo Februari 17, 2001, meli moja kuukuu ilikwama kwenye pwani ya Ufaransa. Wanaume, wanawake na watoto elfu moja hivi walikuwa wamesafiri kwa meli hiyo kwa muda wa juma moja hivi bila kula chochote. Kila abiria alikuwa amelipa dola 2,000 za Marekani kwa ajili ya safari hiyo hatari, bila hata kujua nchi aliyokuwa akielekea. Nahodha na mabaharia wa meli hiyo walitoweka mara tu walipopandisha meli hiyo ufukoni. Lakini abiria hao wenye hofu waliokolewa, na serikali ya Ufaransa ikaahidi kushughulikia maombi yao ya kuishi nchini humo. Watu wengi kama hao hujaribu kufunga safari kama hizo kila mwaka.
Wengi kati ya wahamiaji hao wa kiuchumi huwa tayari kukabili magumu na hatari kubwa. Wao hujaribu juu chini kupata nauli ya safari hiyo kwa sababu umaskini, ujeuri, ubaguzi, au serikali katili—na nyakati nyingine mambo yote hayo manne—hufanya wakose tumaini maishani.
Wengi wao hufa wanapojaribu kutafuta maisha bora. Katika mwongo uliopita, wahamiaji 3,500 hivi walizama au kutoweka wakati walipojaribu kuvuka Mlango-Bahari wa Gibraltar walipokuwa wakisafiri kutoka Afrika hadi Hispania. Katika mwaka wa 2000, wahamiaji 58 Wachina walikufa kwa kukosa hewa walipokuwa wamefichwa ndani ya lori lililokuwa likiwasafirisha kutoka Ubelgiji hadi Uingereza. Wahamiaji wengi sana hufa kwa kukosa maji kwenye jangwa la Sahara wakati malori yao makuukuu, yanayobeba watu wengi mno, yanapoharibika jangwani.
Licha ya hatari hizo, kuna ongezeko kubwa la wakimbizi wa kiuchumi ulimwenguni. Kila mwaka, watu wapatao nusu milioni huingizwa Ulaya kiharamu; na watu 300,000 huingizwa Marekani vivyo hivyo. Mnamo mwaka wa 1993, Hazina ya Idadi ya Watu ya Umoja wa Mataifa ilikadiria kwamba kulikuwa na wahamiaji milioni 100 ulimwenguni, na theluthi moja kati yao walihamia Ulaya na Marekani. Tangu wakati huo, idadi ya wahamiaji imeongezeka sana.
Wahamiaji wengi hawapati kamwe usalama wanaotafuta. Na ni wakimbizi wachache tu wanaopata makao salama na ya kudumu. Mara nyingi, wahamiaji hao hukimbia matatizo fulani na kuingia katika matatizo mengine. Makala inayofuata itazungumzia baadhi ya matatizo hayo na mambo yanayoyasababisha.
[Maelezo ya Chini]
^ fu. 8 Katika mfululizo huu, tunapozungumzia watu waliolazimishwa kuhama makwao, hatuzungumzii wale watu milioni 90 hadi milioni 100 ambao wamelazimishwa kuhama makwao kwa sababu ya miradi ya maendeleo kama ujenzi wa mabwawa, kuchimba migodi, kupanda miti, au miradi ya kilimo.