Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Historia ya Marashi

Historia ya Marashi

Historia ya Marashi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO

Historia ya marashi ilianza zamani za kale. Inafikiriwa kuwa marashi yalianza kutokezwa kwa kuchoma gundi na utomvu wa mmea ili kutokeza ubani katika sherehe za kidini. Kwa hiyo, neno la Kiingereza la marashi, perfume, linatokana na neno la Kilatini per fumum linalomaanisha “kupitia moshi.” Rekodi ya mapema kuhusu marashi inatoka Misri. Wakati kaburi la Farao Tutankhamen lilipofunguliwa, humo mlipatikana zaidi ya chupa 3,000 za marashi yaliyokuwa bado yamehifadhi baadhi ya manukato yake kwa zaidi ya karne 30!

Miaka 1,500 kabla ya Wakati wa Kawaida, Mungu aliagiza “manukato yaliyo bora” yaongezwe katika mafuta matakatifu yaliyotumiwa na makuhani Waisraeli. (Kutoka 30:23-33) Waebrania walitumia marhamu yaliyotiwa marashi kujipodoa na katika tiba, vilevile kwa kutayarisha maiti kwa ajili ya maziko—bila shaka yakitumika kama dawa na pia inaondoa harufu mbaya. Kwa mfano, wanawake walipeleka manukato na mafuta yaliyotiwa marashi kwenye kaburi ili kuyatumia kwenye mwili wa Yesu. (Luka 23:56; 24:1) Kumpaka mgeni mafuta yaliyotiwa marashi kwenye miguu yake kulionwa kuwa tendo la ukaribishaji katika nyumba ya Mwisraeli.—Luka 7: 37-46.

Katika karne ya kwanza, iliripotiwa kwamba Roma ilikuwa ikitumia karibu tani 2,800 za ubani na tani 550 za manemane kwa mwaka mmoja. Viungo kama hivyo vyenye harufu tamu ndizo zawadi alizopelekewa mtoto Yesu. (Mathayo 2:1, 11) Inasemekana kwamba katika mwaka wa 54 W.K., Maliki Mroma Nero alitumia fedha zinazolingana na dola 100,000 (za Marekani) kutia harufu nzuri kwenye karamu. Mabomba yaliyofichwa katika vyumba vyake vya kulia yaliwanyunyizia wageni maji yaliyotiwa marashi. Kuanzia karne ya saba W.K. na kuendelea, Wachina walitumia manukato, kutia ndani vifuko vilivyotiwa marashi. Katika Zama za Kati, Waislamu walikuwa wakitumia marashi, hasa manukato za waridi.

Utengenezaji wa marashi uliimarika sana nchini Ufaransa katika karne ya 17 hivi kwamba makao ya Mfalme Louis wa 15 yaliitwa makao ya marashi. Manukato yalitiwa kwenye ngozi na hata kwenye mavazi, glavu, pepeo, na fanicha.

Marashi aina ya Cologne yaliyovumbuliwa katika karne ya 18 yalitiwa katika maji ya kuogea, yalichanganywa na divai, yaliliwa kwenye donge la sukari ili kusafisha kinywa, na pia yaliingizwa mkunduni na kutumiwa kama dawa kwenye vidonda. Katika karne ya 19, manukato yasiyotokana na vitu vya asili yalianza kutengenezwa. Hivyo, marashi ya kwanza yasiyo na manufaa ya kitiba yalianza kuuzwa. Leo biashara ya marashi inatokeza mabilioni ya dola. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 7 Habari kuhusu hali ya kuathiriwa na marashi imezungumziwa katika toleo la Agosti 8, 2000.

[Picha katika ukurasa wa 31]

Misri, chupa ya marashi kutoka kaburi la Tutankhamen, karne ya 14 K.W.K.

[Hisani]

Werner Forman/Egyptian Museum, Cairo, Egypt/Art Resource, NY

[Picha katika ukurasa wa 31]

Ugiriki, karne ya 5 K.W.K.

[Hisani]

Musée du Louvre, Paris

[Picha katika ukurasa wa 31]

Ufaransa, karne ya 18 W.K.

[Hisani]

Avec lʹaimable autorisation du Musée de la Parfumerie Fragonard, Paris

[Picha katika ukurasa wa 31]

Chupa ya kisasa ya marashi