Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kea Kasuku wa Milimani Apendaye Kucheza

Kea Kasuku wa Milimani Apendaye Kucheza

Kea Kasuku wa Milimani Apendaye Kucheza

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NEW ZEALAND

KASUKU anayeitwa kea ni ndege anayeishi katika maeneo ya milimani ya New Zealand. Kwa kuwa ndege huyo anapenda sana kucheza, amewachekesha na kuwafurahisha watu—au kuwaudhi—kwa michezo yake.

Hebu wazia umepanda milima kutwa nzima. Unafika kwenye kibanda fulani mlimani ukiwa umechoka. Baada ya kula, unataka tu kuingia kitandani ili ulale fofofo. Lakini kasuku hao wanataka kukuvuruga. Wanatua juu ya paa la mabati la kibanda hicho na kuanza kujitelezesha kimchezo. Wanapokwaruza mabati hayo ni kana kwamba wanafikiri wanapiga muziki. Ili kuonyesha kwamba wanafurahia mchezo huo, wanatoa milio mikali wanapoteleza. Kisha, wanapigapiga mabawa yao na kujikakamua kurudi juu ili waanze tena kujitelezesha kwa sauti.

Hata hivyo, ndege hao hubuni njia nyingine za kujifurahisha, kwani wanaweza kuchoshwa na mchezo huo. Wao wanabingirisha mawe kwenye paa, kisha wanayafukuza mawe hayo huku wakitoa milio mikali. Ndege hao hujining’iniza juu chini kwenye dari la kibanda na kuchungulia dirishani ili kuona jinsi watu wanavyoitikia. Ni kana kwamba ndege hao wanafikiri kuwa watu hao waliochoka wanafurahia mchezo wao. Lakini kabla hujasema kwamba kasuku hao wa milimani wanapenda kucheza, tutajifunza mambo fulani juu yao.

Kasuku anayeitwa kea alipewa jina hilo kutokana na mlio anaotoa wakati anaporuka ambao unaandikwa hivi, kee-a. Makao yao ya asili ni New Zealand na wanapatikana tu kwenye eneo la mlimani la Kisiwa cha Kusini. Makao yao yanaanzia kwenye misitu ya milimani kufikia kwenye maeneo yasiyokuwa na mimea na wao hula miche na matunda ya beri.

Kasuku hao wana nguvu nyingi. Uzani wa kea wa kiume unaweza kufikia kilogramu 1.2 na urefu wa sentimeta 50. Wao huwa na rangi ya kijani-kibichi. Ijapokuwa wao hufichika wanapokuwa katikati ya majani, bado wao hutambulika. Wao huonekana tofauti na ndege wengine kwa sababu ya ujasiri wao, sauti zao za kipekee, ukubwa wao, na rangi nyekundu kwenye upande wa chini wa mabawa.

Mara nyingi wao hucheza wanapokuwa angani, wakifuata mikondo ya upepo wa milimani inayobadilika-badilika. Wao huvutia sana wanapoelea juu ya mabonde, wakifukuzana na kuhepana. Wanasemwa kuwa ni miongoni mwa ndege werevu zaidi ulimwenguni. Huenda werevu wao ndio unawafanya wapende mchezo sana.

Wanapenda Kucheza

Sifa moja kubwa ya ndege hao ni kupenda kucheza. Kwa kuwa ndege hao ni wadadisi, wao huchunguza kila kitu mahala walipo, hasa kitu kigeni. Zaidi ya kukichunguza kitu hicho kwa macho yao, wao hukigonga-gonga na kukidunga-dunga kwa midomo yao yenye nguvu hadi wanapochoshwa na kitu hicho au wanapokiharibu.

Kasuku mmoja alionekana kwenye stesheni ya gari-moshi la mlimani. Alikuwa akichunguza mikebe miwili iliyojaa maziwa iliyokuwa imewekwa mahala palipoinuka kando ya reli. Kasuku huyo mtundu alifunua mkebe mmoja na kuanza kunywa maziwa. Ndege huyo alifukuzwa, na fimbo ya chuma ikawekwa kati ya vishikio vya mikebe hiyo ili kumzuia asifunue mikebe. Kasuku huyo hakuvunjika moyo. Alirudi, akachunguza fimbo hiyo kwa muda mfupi, halafu akaiondoa kwa ustadi akitumia mdomo wake. Kisha akafunua mkebe na kunywa maziwa tena. Ndege hao ni wakorofi lakini wanafurahisha!

Kasuku Hao na Wapiga-Kambi

Wapiga-kambi wanaobaki karibu na kambi ili kulinda mizigo yao hustaajabishwa na michezo ya ndege hao wanaovutia. Hata hivyo, usipoacha mtu kambini kulinda mizigo, ndege hao wanaweza kuharibu vitu sana. Wanaweza kurarua hema kabisa kwa midomo yao yenye nguvu. Wanaweza kurarua godoro lenye manyoya na kuyatawanya kotekote.

Ndege hao hupenda kubingirisha kitu chochote chenye umbo la duara kilimani. Ndege hao hupenda kitu chochote kinachong’ara. Wanapenda hasa kucheza na kamba za viatu. Wanapenda pia mchezo wa kuokota vitu na kuviangusha wakiwa juu sana, kana kwamba wanafurahia kuona vikianguka.

Watu wanaofanikiwa kuwaona kasuku hao hufurahishwa sana na ustadi wao wa kucheza na kutumbuiza. Kwa sababu ya michezo yao ya kuchekesha, wameitwa tumbili wa New Zealand wenye mabawa.

Kasuku Hao na Watelezaji wa Skii

Kasuku hao hupenda kukusanyika mahala ambako kuna watu wengi, kama vile kwenye maeneo ya kuteleza kwenye theluji. Watelezaji wa skii huvutiwa pia na ndege hao. Ni kana kwamba ndege hao hutaka kuteleza kwenye theluji pia. Wao huwafuata watelezaji huku wakirukaruka. Ndege hao hufurahia hasa kuteleza kama kigari cha kutelezea kwenye theluji. Wanapofanya hivyo, wao hupunguza mwendo wao kwa kupanua miguu yao kama vile watelezaji wanavyofanya kwa vifaa vyao vya kuteleza. Ni kana kwamba kasuku huyo anatangaza kuwa yeye pia anapaswa kufurahia kuteleza kwenye theluji.

Michezo yao pia husababisha usumbufu na uharibifu. Wasimamizi wa maeneo ya kuteleza kwenye theluji wanasema kwamba inawabidi kulinda vifaa vyao ili ndege hao wasiweze kuviharibu. Ni lazima vifaa vya pekee vifunikwe. Hata hawatumii kamba bali wanatumia waya. Ndege hao wana ustadi wa kufunua pipa za takataka za aina yoyote ile. Watelezaji hulazimika kulinda mali zao kutokana na ndege hao machachari. Kwa mfano, usipolinda kamera yako, kea ataanza kuichezea.

Watelezaji hulazimika kulinda magari yao kwa kuyafunika kwa wavu maalumu. Kwa nini? Kwa sababu kasuku hao hupenda kugongagonga magari. Wao hupenda sana kuharibu mipira ya waipa na vidude vingine vya mpira na kuvunja taa za plastiki za nyuma ya gari. Dirisha la gari likiachwa wazi, kasuku hao huingia ndani. Kisha wao hupigapiga kelele huku wakiharibu vitu vilivyoachwa. Kwelikweli, kasuku hao ndio wakora pekee wanaolindwa na sheria huko New Zealand.

Kwenye Maeneo ya Ujenzi

Kasuku hao hupenda kucheza pia kwenye maeneo ya ujenzi milimani. Wakati vibanda vilipokuwa vikijengwa kwenye njia maarufu ya Milford huko New Zealand, kasuku hao walijitokeza. Kasuku mmoja alianza kuiba misumari. Wakati mjenzi aliyechokozwa alipokuwa akimfukuza, kasuku mwingine akaiba sigara zake. Ndege huyo mkorofi alirarua karatasi za sigara hizo huku kasuku wengine wakipiga makelele kana kwamba walikuwa wakimuunga mkono. Kati ya ndege wote, kea ndiye ndege mdadisi na mkorofi zaidi. Wanapowaona watu wakitembelea makao yao, kasuku hao hukusanyika na kuwafuata kana kwamba wanafikiri wamekuja kuiba.

Ni kana kwamba ni lazima washikeshike au wachunguze kitu chochote kilicho karibu nao. Michezo yao huwafurahisha watu wanaowaona mara mojamoja lakini huwaudhi watu wanaowaona kila siku. Watu wengine huwapenda na wengine huwachukia. Hata hivyo, kila mtu anaweza kukubali kwamba kasuku hao ni ndege wenye urafiki na wenye kufurahisha. Na wamelindwa kabisa na sheria za kuhifadhi viumbe.

Ndege wa Milimani Apendaye Kucheza

Ukiwaona ndege hao werevu, wanaopenda kucheza, utakubali kwamba wao hufurahisha sana. Wao hupenda kuwakaribia watu wote wanaotembelea makao yao ya milimani, na kuwachekesha. Inapendeza sana kuwaona wakicheza na kujifurahisha.

Naam, tabia yao ya kisilika ya kupenda kucheza na kufurahi hutukumbusha kwamba waliumbwa na Yehova, Mungu mwenye furaha.—1 Timotheo 1:11.

[Picha katika ukurasa wa 19]

“Kea” anaharibu mwavuli

[Picha katika ukurasa wa 20]

“Kea” wanaharibu gari

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 18]

Courtesy of Willowbank Wildlife Reserve, Christchurch, New Zealand