Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Afya Bora Nilifarijiwa na kutiwa moyo sana na ule mfululizo wa makala “Je, Watu Wote Wanaweza Kuwa na Afya Bora?” (Juni 8, 2001) Ninaugua ugonjwa fulani wa akili, na nimewahi kufikiria kujiua. Kila siku mimi hujiuliza iwapo nitaweza kuvumilia siku hiyo. Gazeti hilo lilinikumbusha ahadi ya Yehova kwenye Ufunuo 21:4 ya ‘kufuta kabisa kila chozi kutoka katika macho yetu.’
C. T., Japani
Asanteni kwa makala zenu nzuri. Mimi ni daktari anayetumia matibabu ya asili, na ninatazamia wakati ambapo hakutakuwa na magonjwa. Wakati huo utakapofika, nitaacha kazi yangu na kuanza ukulima. Hiyo ni kazi nyingine ninayopenda sana!
B. C., Marekani
Mashairi Nilifurahia sana kusoma makala yenu ya “Kutokeza Taswira kwa Kutumia Maneno.” (Juni 8, 2001) Nilipostaafu, nilianza kuandika mashairi. Mimi hufurahi na kuridhika sana ninapofanya hivyo.
J. B., Uingereza
Tangu nilipokuwa mtoto nilipenda sana kusoma, na hivyo nikapenda mashairi. Asanteni sana kwa kusema kwamba “mtu anayechukua mambo kijuujuu tu hawezi kuandika mashairi yanayopendeza.” Watu wengi huamini kwamba kuandika mashairi huonyesha udhaifu. Ushairi ni aina ya uandishi unaopendeza sana na ninafurahi kujua kwamba Muumba wetu ana maoni hayo pia.
M. T., Chile
Makanisa Makuu Nilifurahia makala yenye kichwa “Je, Makanisa Makuu Yamejengwa kwa Sifa ya Mungu au ya Wanadamu?” (Juni 8, 2001) Lakini je, Mashahidi wa Yehova hawajengi Majumba makubwa ya Ufalme na Majumba makubwa ya Makusanyiko?
R. B., Marekani
“Amkeni!” linajibu: Tulishutumu ujenzi wa makanisa makuu si kwa sababu ni makubwa bali kama vile mwanahistoria mmoja alivyosema “kiburi” cha viongozi wa kidini ndicho mara nyingi kilichochochea makanisa hayo yajengwe. Pia, mara nyingi waumini waliumia sana walipogharimia ujenzi wa majengo hayo makubwa. Tofauti na hilo, Majumba ya Ufalme na Majumba ya Makusanyiko ni majengo ya kiasi ambayo hayajengwi ili kumtukuza mwanadamu yeyote. Badala yake, majengo hayo ni mahala pa ibada. Majengo hayo hujengwa kwa michango ya hiari wala hakuna yeyote anayelemewa kwa sababu ya gharama yake.
Nondo Nina umri wa miaka 14, na nilifurahi niliposoma makala yenye kichwa “Nondo Maridadi.” (Juni 8, 2001) Nilidhani kwamba nondo wana sura ya kutisha, lakini baada ya kusoma makala hiyo nimeamua sitawaua ovyoovyo!
D. S., Marekani
Nilipokuwa nikisoma makala hiyo, nondo alitua mguuni pangu. Alikuwa nondo maridadi wee! Viumbe hupendeza sana, na tunapowatazama, upendo wetu kwa Mungu huongezeka.
G. P., Italia
Kwa kuwa sikujua umaridadi na unamna-namna wa nondo ambao Yehova ameumba, nilidhani wao ni wadudu wasiopendeza. Muda mfupi baada ya kusoma makala hiyo, nilimwona nondo mmoja maridadi nilipokuwa nikimwagilia mimea maji. Nilimshukuru Yehova kwa uumbaji wake na kwa makala hiyo iliyonisaidia nitazame vitu kwa makini zaidi.
C. S., Marekani
Maji Mekundu Mimi ni mwalimu, na nimekuwa nikifundisha somo linalohusu utunzaji wa mazingira na viumbe wa pwani. Nilikuwa nimetafuta sana makala inayozungumza wazi kuhusu maji mekundu baharini. Kisha nikapata makala yenye kichwa “Maji Yanapokuwa Mekundu” (Juni 8, 2001) ambayo ilinisaidia sana. Asanteni sana kwa kuichapisha.
J.O.P., Ufilipino