Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Sala Makala ya “Vijana Huuliza . . . Je, Mungu Atasikiliza Sala Zangu?” (Juni 22, 2001) ilinitia moyo sana. Nilipokea gazeti hilo nilipokuwa nimelazwa hospitalini. Sikuweza kuhudhuria mikutano kwenye Jumba la Ufalme wala kusanyiko letu. Nilikuwa nimeshuka moyo na sikuweza kudhibiti hisia hizo. Nilipotoa sala kwa Yehova nilitulia, nikatiwa moyo kwa kadiri ambavyo sikutarajia. Nimefarijika kujua kwamba Yehova hataniacha kamwe.
A. O., Japani
Nina umri wa miaka 18, nami ni painia wa kawaida, mhubiri wa wakati wote. Nilikuwa nimeshuka moyo kwa muda wa miezi michache iliyopita. Nilikuwa na maoni kama ya Steve, kijana aliyetajwa katika makala hiyo aliyesema kwamba nyakati nyingine alihisi kwamba hakupaswa kumsumbua Mungu na matatizo yake. Lakini nilifikiria kwa uzito ushauri wa Luka 12:6, 7. Nilianza kutulia na nikasukumwa kumwelezea Yehova yaliyokuwa moyoni mwangu.
M. D., Nikaragua
Kulelewa Katika Nyumba ya Watawa Makala “Niliachwa na Wazazi—Nikapendwa na Mungu” (Juni 22, 2001) ilinikumbusha mambo mengi. Nakumbuka kile ambacho mama yangu alitueleza kuhusu maisha yake katika nyumba ya watawa na jinsi watawa hao walivyomtenda vibaya. Alikuwa na umri wa miaka 16 alipoondoka katika nyumba hiyo na hakuwa na mahali pa kukaa. Watu wengi sana wameteseka hivyo, nao huogopa kusema juu ya mateso yao. Ninafurahi kwamba mlichapisha makala hiyo.
G. E., Marekani
Afya Nilisoma makala “Je, Matibabu ya Kisasa Yanaweza Kufaulu?” katika toleo lenu la Juni 8, 2001. Kwa kuwa mimi si mtaalamu wa tiba wala wa sayansi, nilipendezwa sana na nikafaidika na maelezo na marejeo yenu kuhusu historia ya matibabu. Nitahifadhi toleo hilo.
E. F., Ujerumani
Dawa za Kulevya Mfanyakazi mwenzangu huniletea magazeti yenu kwa ukawaida, nami huyasoma. Lakini siwezi kukubaliana nanyi kwamba wanamuziki wote wa roki hutumia dawa za kulevya, kama mlivyodokeza katika mfululizo wa makala wa “Matumizi ya Dawa za Kulevya—Yatakomeshwa!” (Julai 8, 2001) Kuna wanamuziki wengi wa roki ambao hawatumii dawa za kulevya nao huchukua kazi yao kwa uzito.
M. M., Japani
“Amkeni!” linajibu: Kusudi letu halikuwa kudokeza kwamba wanamuziki wote wa roki hutumia dawa za kulevya. Hata hivyo, inajulikana kwamba wanamuziki wengi wa roki na mashabiki wao hutumia dawa za kulevya mara nyingi kwenye maonyesho yao.
Maporomoko ya Niagara Nimemaliza tu kusoma makala ya “Maporomoko ya Maji ya Niagara—Yalinistaajabisha.” (Julai 8, 2001) Nilifurahia sana kusoma makala hiyo. Hivi majuzi, mume wangu alinipeleka huko ili kuadhimisha ukumbusho wa siku yetu ya arusi. Sikufikiri nitafurahia safari hiyo. Lakini nilifurahia kama nini! Kuyaona na kuyasikia maporomoko hayo kulivutia sana.
C. K., Marekani
Mlisema kwamba mmomonyoko wa maporomoko hayo umeendelea kwa muda wa miaka 12,000 iliyopita. Jambo hilo halilingani na simulizi la Biblia juu ya ile gharika ya duniani pote.
R. P., Uingereza
“Amkeni!” linajibu: Tulitaja tu makadirio ya wanasayansi, na hatukusema kwamba makadirio hayo ni sahihi. Wanasayansi wanaofanya makadirio hayo hawafuati simulizi la Biblia juu ya Furiko la Siku za Noa, ambalo lilitukia miaka 5,000 hivi iliyopita.—Mathayo 24:37.