Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Kifungo cha Maisha Katika Mzinga wa Nyuki
Gazeti la New Scientist linasema kwamba “nyuki wa Afrika wamegundua mbinu bora isiyo ya kawaida ya kuwazuia wadudu wanaovamia mzinga. Nyuki hao huwafunga wadudu hao ndani ya vyumba vya gereza katika mizinga yao. Wadudu hao wanapofungwa, nyuki hupata nafasi ya kukimbia iwapo itakuwa lazima.” Watafiti “walichunguza jinsi nyuki huko Afrika Kusini wanavyojihami dhidi ya mbawakawa mdogo wa mzinga, Aethina tumida, ambaye ni nusu ya ukubwa wa nyuki.” Mmojawapo wa watafiti hao, Peter Neumann, anasema kuwa mbawakawa huyo ana mabawa magumu hivi kwamba nyuki wanaomshambulia hawawezi kumdhuru. Hivyo, nyuki wanaweza kujikinga tu kwa kuwafunga mbawakawa hao. Neumann anaeleza kwamba “baadhi ya nyuki hujenga gereza huku wengine wakiwalinda mbawakawa wasitoroke.” Nyuki hukusanya utomvu wa miti ili kujenga gereza hilo na ujenzi huendelea kwa siku nne. Nyuki wa Ulaya, na wale wa Amerika Kaskazini, hawajagundua mbinu hiyo. Kwa hiyo, mbawakawa hao, walioingizwa Marekani bila kukusudia miaka mitano hivi iliyopita, wakivamia mojawapo ya mizinga ya nyuki huko, mzinga huo “utakuwa taabani.”
Wanyama Wanaopima Uchafuzi
Mtaalamu wa wanyama, Steve Hopkin, anadai kwamba minyoo fulani ni wastadi wa kupima uchafuzi wa hewa na wa udongo. Wanyama hao duni hupatikana kwa wingi na kwa bei nafuu, nao hufanya kazi hiyo vizuri kuliko vifaa vya hali ya juu vilivyotengenezwa na wanadamu. Kome fulani hutumiwa kupima uchafuzi katika maji. Chombo chenye ukubwa wa ndoo na chenye kome wanane walio hai, hutumiwa kwa mafanikio kupima uchafuzi katika mto wa Rhine na wa Danube. Kees Kramer aliyebuni chombo hicho alisema kwamba “uchafuzi ukiongezeka kwa ghafula, kome watatambua jambo hilo.” Kome hao hufunga magamba yao wanapogundua uchafuzi mwingi wa kikemikali, na wanapofanya hivyo king’ora kilicho katika chombo hicho hulia. Gazeti la El País linasema kwamba chombo hicho ni bora kwa sababu huonyesha jinsi uchafuzi unavyoathiri viumbe.
Watoto Wanaoandikishwa Jeshini
Ripoti moja ya shirika la habari la Associated Press ilisema kwamba “zaidi ya watoto 300,000—baadhi yao wakiwa na umri wa miaka 7 tu—wanapigana vita katika nchi 41 kotekote duniani.” Wengi wao wana umri wa kati ya miaka 15 na 18. “Shirika la Muungano wa Kukomesha Uandikishaji wa Watoto Jeshini linasema kwamba mbali na kuwatuma watoto wapigane katika mstari wa mbele, watoto hutumiwa pia kutafuta mabomu yaliyotegwa ardhini, na vilevile kama wapelelezi, wachukuzi, na kwa kusudi la umalaya.” Mara nyingi watoto hao hupewa dawa za kulevya ili kuondoa woga. Mwanamgambo mmoja mwenye umri wa miaka 14 huko Sierra Leone alisema kwamba wale wanaokataa kutumia dawa hizo huuawa. Kijana mmoja wa Afrika Kaskazini alisema hivi kuhusu vita alivyopigana mwaka wa 1999 alipokuwa na umri wa miaka 15: “Vijana wote wenye umri wa miaka 15 na 16 waliwekwa kwenye mstari wa mbele huku jeshi likirudi nyuma. Nilikuwa pamoja na vijana wengine 40. Nilipigana kwa muda wa saa 24. Nilipoona kwamba ni watatu tu kati ya marafiki wangu waliokuwa hai, nilikimbia.” Ripoti ya Muungano huo ilisema kwamba serikali huandikisha watoto ‘kwa sababu kuandikisha watoto hakugharimu pesa nyingi, na wakiuawa, ni rahisi kupata wengine, wala si vigumu kuwazoeza kuua bila woga, na kutii bila kufikiri.’
Biblia Imetafsiriwa Katika Lugha Nyingi Zaidi
Shirika la Biblia la Uingereza linaripoti kwamba ‘sasa, Biblia ikiwa nzima au sehemu, inapatikana katika lugha 2,261. Tafsiri za lugha 28 zimeongezwa katika miezi 12 iliyopita. Sasa [Biblia] nzima inapatikana katika lugha 383. Lugha 13 ziliongezwa mwaka uliopita.’ Sasa Biblia zenye Maandiko yote ya Kiebrania au Maandiko yote ya Kigiriki, yaani Agano la Kale na Agano Jipya, zinapatikana katika lugha 987.
Kemikali Mpya Nzito
Gazeti la Ujerumani la Süddeutsche Zeitung linaripoti kwamba wanasayansi ‘wameanza kutumia metali nzito ya hassium katika kazi yao.’ Wanasayansi kwenye kituo cha Gesellschaft für Schwerionenforschung (Kituo cha Utafiti wa Ioni Nzito) huko Darmstadt, Ujerumani, wamefaulu kwa mara ya kwanza kuchanganya atomi za hassium pamoja na oksijeni, na hivyo kutengeneza kemikali mpya. Hassium ambayo imetengenezwa na mwanadamu, imeitwa kwa jina la jimbo la Hesse huko Ujerumani. Wanasayansi wa nyuklia walitengeneza metali hiyo kwa mara ya kwanza mwaka wa 1984. Metali ya hassium na kemikali hiyo mpya ni zenye mnururisho, zinabadilika-badilika, na hazidumu kwa muda mrefu, kwa hiyo hazina faida yoyote kwa wakati huu.
Hatari za Kuongezwa Damu
Gazeti la Sydney Morning Herald la Australia linaripoti kwamba ‘kulingana na miongozo ya Tiba ya [New South Wales] theluthi moja ya wagonjwa wanaoongezwa damu hawahitaji damu. Miongozo hiyo inasema kwamba mgonjwa anahitaji kuongezwa damu iwapo kiwango chake cha damu ni saba au chini.’ Dakt. Ross Wilson, aliyesimamia uchunguzi huo kuhusu utumizi wa damu, alisema hivi: “Kuongeza damu isivyo lazima kunaweza kufanya moyo uache kupiga na hivyo kumwua mgonjwa.” Kulingana na uchunguzi ambao Dakt. Wilson alisimamia miaka sita iliyopita, “[Waaustralia] 18,000 hivi hufa kila mwaka kwa sababu ya magonjwa yanayosababishwa na matibabu.” Dakt. Wilson anapendekeza kuwa madaktari wakumbushwe kile ambacho miongozo hiyo kuhusu kuongezwa damu inasema kila wanapotaka kutumia damu, na wagonjwa vilevile waarifiwe juu ya miongozo hiyo ili waweze kuizungumzia pamoja na daktari.
Adhabu Kali kwa Kusambaza Picha Chafu Kwenye Internet
Shirika la habari la Associated Press linaripoti kwamba “mahakama kuu ya jinai ya Ujerumani ilitangaza . . . kwamba kusambaza picha chafu za watoto kwenye Internet ni sawa na kuzichapisha, na wanaofanya hivyo watahukumiwa kifungo cha kufikia miaka 15.” Gazeti hilo lilisema kwamba ‘uamuzi huo wa Mahakama Kuu utatumiwa ili kuwaadhibu wale wanaosambaza picha chafu za watoto kwenye Internet, kwa kuwa hakukuwapo sheria kuhusu jambo hilo hapo awali.’ Mahakama kuu ilibatilisha uamuzi wa mahakama nyingine ambayo ilionelea kwamba kusambaza picha chafu za watoto kwenye Internet si kosa zito kama kuchapisha habari za aina hiyo.
Bangi na Moyo
Gazeti la Globe and Mail la Kanada linasema kwamba uchunguzi mpya wa ‘watu wa makamo wanaovuta bangi unaonyesha kwamba uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo unaongezeka mara tano katika muda wa saa moja baada ya kuvuta bangi. Kuvuta bangi huongeza mpigo wa moyo—mara nyingi mpigo huongezeka maradufu kuliko ilivyo kawaida—na kubadili msukumo wa damu. Pia, kunaweza kusababisha mshtuko wa moyo kwa kufanya damu igande na kuizuia isifike kwenye msuli wa moyo.’ Dakt. Harold Kalant wa Chuo Kikuu cha Toronto alisema hivi: “Wazee wamo hatarini kupata mshtuko wa moyo kwa sababu ya moyo kufanya kazi zaidi.” Ripoti hiyo inasema kwamba kokeini ni hatari hata zaidi kwa kuwa uwezekano wa kupata mshtuko wa moyo huongezeka mara 25 katika muda wa saa moja baada ya kuitumia.
Waridi Lipewe Jina Lipi?
Kuipa mimea majina kumekuwa kazi ngumu sana, kwa sababu mimea mingi mipya huzalishwa. Gazeti la The Wall Street Journal linasema kwamba ‘tayari kuna aina ya yungiyungi 100,000 hivi zilizo na majina, angalau waridi 100,000, na zaidi ya dalia 14,000. Maneno ambayo hutumiwa katika mashairi kama vile maridadi, rangi ya waridi, pendeza, ndoto, fahari, malkia, mapambazuko, machweo, mahameli, manukato, na mwujiza, tayari yametumiwa na kurekodiwa. Watu wanaofanya kazi ya kuipa mimea majina wamebuni majina mapya mazuri, lakini pia wameishia kubuni majina duni kwelikweli.’ Kwa mfano, gazeti hilo linasema kwamba, “kwenye maduka ya mimea unaweza kununua ua aina ya iris liitwalo Taco Supreme, waridi aina ya Macho Man, hosta aina ya Abba Dabba Do, yungiyungi aina ya Primal Scream, au dalia aina ya Kung Fu.” Hata ua fulani linaweza kuitwa kwa jina lako ukiwa tayari kulipa kiasi fulani cha fedha. Kampuni moja huko California hutoza dola 10,000 za Marekani ukitaka kulipatia waridi jina, lakini ni lazima uchague jina lisiloudhi. Kampuni nyingine hutoza dola 75,000, na kuwalipia wateja ili wakae katika hoteli kwa mwisho-juma mmoja jijini Los Angeles.