Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Samaki wa Mtakatifu Petro

Samaki wa Mtakatifu Petro

Samaki wa Mtakatifu Petro

UKITEMBELEA mkahawa fulani karibu na Bahari ya Galilaya * huko Israel, huenda ukapendezwa kuona jina “Samaki wa Mtakatifu Petro” kwenye orodha ya vyakula. Mhudumu wa mezani anaweza kukuambia kwamba watu wengi, hasa watalii, hupenda mlo huo sana. Samaki huyo ni mtamu, hasa akiwa ametoka tu kukaangwa. Lakini samaki huyo ana uhusiano gani na mtume Petro?

Jibu linapatikana katika simulizi la Biblia la Mathayo 17:24-27. Kulingana na simulizi hilo, Petro alipotembelea mji wa Kapernaumu karibu na Bahari ya Galilaya, aliulizwa iwapo Yesu alikuwa akilipa kodi ya hekalu. Baadaye, Yesu alieleza kwamba hakuwa na wajibu wa kulipa kodi hiyo, kwani alikuwa Mwana wa Mungu. Lakini, ili wengine wasikwazwe, alimtuma Petro aende ziwani, atupe ndoana, achukue samaki wa kwanza ambaye angetokea, na alipe kodi hiyo kwa kutumia sarafu ambayo angepata katika mdomo wa samaki huyo.

Jina “Samaki wa Mtakatifu Petro” linatokana na tukio hilo linalosimuliwa katika Biblia. Lakini Petro alivua samaki wa aina gani?

Ziwa Lenye Samaki Wengi

Yadhaniwa kwamba aina 10 tu kati ya aina 20 hivi za samaki wanaopatikana katika Bahari ya Galilaya, wanaweza kuwa aina ya samaki ambaye Petro alivua. Aina hizo kumi zimeainishwa katika vikundi vitatu vya samaki wa kuuzwa.

Kikundi kikubwa ni kikundi cha musht. Neno hilo linamaanisha “chanuo” katika Kiarabu, kwa kuwa zile aina tano za samaki katika kikundi hicho wana pezi la mgongoni linalofanana na chanuo. Aina moja ya samaki wa musht anaweza kufikia urefu wa sentimeta 45 hivi na uzito wa kilogramu mbili hivi.

Kikundi cha pili ni dagaa wa Kinerethi (Bahari ya Galilaya). Uvuaji wa dagaa unapopamba moto, maelfu ya kilogramu ya dagaa hukamatwa kila usiku. Karibu tani elfu moja huvuliwa kila mwaka. Tangu zamani watu wamezoea kumhifadhi samaki huyo katika maji ya chumvi.

Kikundi cha tatu ni kikundi cha biny, au barbel. Kuna aina tatu za biny, nao wamepewa jina hilo la Kisemiti, linalomaanisha “unywele,” kwa kuwa wana nywele kwenye pembe za midomo. Chakula chao ni chaza, konokono, na samaki wadogo. Samaki aina ya barbel mwenye kichwa kirefu anaweza kufikia urefu wa sentimeta 75 hivi na uzito wa zaidi ya kilogramu saba. Samaki aina ya barbel wana nyama nyingi, na Wayahudi hupenda kuwala katika siku za Sabato na katika karamu zao.

Mbali na vikundi hivi, kuna samaki aina ya kambare. Samaki huyo ndiye mkubwa kushinda wote katika Bahari ya Galilaya. Anaweza kufikia urefu wa sentimeta 120 na uzito wa kilogramu 11 hivi. Lakini kambare hana magamba, kwa hiyo, alikuwa kitu kisicho safi kulingana na Sheria ya Musa. (Mambo ya Walawi 11:9-12) Kwa hiyo, Wayahudi hawali kambare, basi haielekei kwamba alikuwa yule samaki ambaye Petro alivua.

Petro Alivua Samaki wa Aina Gani?

Samaki aina ya musht anajulikana kuwa “Samaki wa Mtakatifu Petro,” naye anaitwa hivyo katika mikahawa iliyoko karibu na Bahari ya Galilaya. Ni rahisi kutayarisha na kula samaki huyo kwa kuwa hana mifupa mingi. Lakini je, huyo ndiye samaki ambaye Petro alivua?

Mendel Nun, mvuvi ambaye ameishi kwenye pwani ya Bahari ya Galilaya kwa zaidi ya miaka 50 anajua mengi kuwahusu samaki wa ziwa hilo. Yeye anasema hivi: “Samaki aina ya musht hula viumbe vidogo vya majini na hapendi vyakula vingine. Kwa hiyo, samaki huyo huvuliwa kwa wavu, wala si kwa ndoana.” Basi, haielekei Petro alivua samaki huyo. Na kwa kuwa dagaa ni samaki mdogo sana, hawezi kuwa samaki wa Mtakatifu Petro.

Hivyo, baadhi ya watu wanaona kwamba bila shaka samaki aina ya barbel ndiye “samaki wa Mtakatifu Petro.” Nun alisema hivi: “Tangu siku za kale, wavuvi wa [Bahari ya Galilaya] wametumia ndoana yenye chambo cha dagaa ili kuvua samaki aina ya barbel. Huyo ni samaki-mwindaji anayekula viumbe wa majini wanaoishi chini ziwani.” Alifikia uamuzi kwamba “yaelekea Petro alivua samaki aina ya barbel.”

Basi, kwa nini samaki aina ya musht anaitwa “samaki wa Mtakatifu Petro” katika mikahawa? Nun anajibu hivi: “Kuna sababu moja tu. Ili kuwavutia watalii! . . . Bila shaka, ilionekana kuwa biashara ingesitawi ikiwa samaki aliyeandaliwa kwenye mikahawa iliyoko karibu na ziwa angeitwa ‘samaki wa Mtakatifu Petro,’ watu kutoka maeneo ya mbali walipoanza kutembelea sehemu hiyo. Samaki anayependwa sana na aliye rahisi kutayarisha alipewa jina linalovutia wateja wengi!”

Ijapokuwa hatuwezi kusema kwa uhakika ni samaki wa aina gani ambaye Petro alivua, bila shaka, samaki yeyote ambaye utaletewa ukiagiza “samaki wa Mtakatifu Petro” atakuwa mtamu sana.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 2 Bahari ya Galilaya ni ziwa lenye maji yasiyo na chumvi.

[Picha katika ukurasa wa 19]

“Musht”

[Picha katika ukurasa wa 19]

“Barbel”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 19]

Garo Nalbandian