Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Wamasai Ni Watu wa Pekee Wanaovutia

Wamasai Ni Watu wa Pekee Wanaovutia

Wamasai Ni Watu wa Pekee Wanaovutia

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

WIMBO wa mvulana Mmasai (Mmaasai) ulitoa mwangwi bondeni na kusikika mbali kwa sababu ya unyevu mwingi hewani mapema alfajiri. Kijana huyo aliimba kwa nguvu zaidi huku jua likiendelea kuchomoza, kama vile ndege anavyoimba kunapopambazuka.

Nilimsikiliza yule kijana mchungaji aliyesimama akiimba katikati ya ng’ombe za babake mapema asubuhi. Kijana huyo alivalia kitambaa kirefu chekundu naye alisimama kwa mguu mmoja akiegemea mkuki wake na kuwaimbia ng’ombe zake waliotulia. Acha niwaeleze zaidi kuhusu Wamasai, watu wa pekee.

Karibuni Kwenye Eneo la Wamasai

Wamasai, watu wanaovutia na wanaofuga wanyama, wanaishi katika pori la Bonde Kuu la Ufa nchini Kenya na Tanzania huku Afrika Mashariki. Wao bado huishi kama vile mababu wao wa kale walivyoishi zamani. Watu hao hawajali saa, bali hufanya kazi zao kuanzia mapambazuko hadi machweo, na kwa kufuatana na majira.

Wamasai wana ustadi unaohitajika kuishi katika pori la Bonde la Ufa. Wao hutembea mbali sana kutafuta malisho na maji kwa ajili ya mifugo yao, nao huchunga mifugo miongoni mwa makundi ya kongoni, punda-milia, twiga, na wanyama wengine wanaoishi katika pori hilo.

Watu Wanaopenda Ng’ombe

Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe wote duniani ni mali yao. Imani hiyo inatokana na hekaya inayosema kwamba hapo mwanzoni Mungu alikuwa na wana watatu, naye alimpa kila mmoja zawadi. Yule wa kwanza alipokea mshale wa kuwindia, yule wa pili alipokea jembe la kulimia, na yule wa tatu alipokea fimbo ya kuchunga ng’ombe. Inasemekana kwamba yule mwana wa mwisho alikuwa babu wa kale wa Wamasai. Ijapokuwa watu wa makabila mengine wanafuga ng’ombe, Wamasai wanaamini kwamba ng’ombe hao ni mali yao.

Mwanamume mwenye ng’ombe na watoto wengi huheshimiwa na kupewa hadhi katika jamii ya Wamasai. Mwanamume aliye na ng’ombe wanaopungua 50 huonwa kuwa mtu maskini. Kwa msaada wa wake zake na watoto wake wengi mwanamume Mmasai hutarajia hatimaye kuwa na kundi kubwa linaloweza kufikia ng’ombe 1,000.

Wamasai hupenda ng’ombe zao. Kila mtu katika familia hutambua vizuri sauti na utu wa kila mnyama kundini. Mara nyingi, ng’ombe hurembeshwa kwa kuchorwa alama za mistari mirefu inayojipinda-pinda na mapambo mengine kwa kutumia chuma chenye moto. Nyimbo hutungwa juu ya sura nzuri za ng’ombe mbalimbali na jinsi wanavyopendwa. Fahali wenye pembe kubwa zilizojipinda hupendwa sana, na ndama mdogo hutunzwa na kushughulikiwa kana kwamba ni mtoto aliyezaliwa karibuni.

Nyumba za Wamasai hujengwa na wanawake, nazo hujengwa kwa matawi na nyasi na kisha hukandikwa kwa samadi ya ng’ombe. Nyumba za Wamasai ni zenye umbo la mstatili nazo huzunguka boma ambamo ng’ombe hulala usiku. Nje ya nyumba hizo kuna ua wa matawi yenye miiba unaowalinda Wamasai na ng’ombe zao dhidi ya fisi, chui, na simba wanaowinda usiku.

Wamasai hutegemea sana mifugo yao, kwa hiyo ni lazima ng’ombe wawe na afya na nguvu. Wamasai hunywa maziwa ya ng’ombe na kutumia samadi ya ng’ombe kujenga nyumba. Wamasai huchinja ng’ombe mara chache sana. Wao hufuga mbuzi na kondoo wachache kwa ajili ya chakula. Lakini ng’ombe anapochinjwa, kila sehemu ya mnyama hutumiwa. Pembe hutumiwa kutengeneza vyombo, na kwato na mifupa hutumiwa kutengeneza mapambo; na ngozi zilizolainishwa hutumiwa kutengeneza viatu, nguo, matandiko, na kamba.

Watu Wenye Kuvutia na wa Pekee

Wamasai ni watu warefu, wembamba, na wenye sura nzuri. Wao hufunga mashuka yenye rangi nyangavu nyekundu na samawati. Wanawake hujirembesha kwa kuvalia mkufu mpana wenye shanga, na mapambo ya vichwani yenye rangi nyingi. Nyakati nyingine mikono na miguu hukazwa kikiki kwa nyaya nyingi nene za shaba. Wanawake na wanaume hurefusha masikio yao kwa kuvaa mapambo na vipuli vizito vyenye shanga. Madini mekundu yaliyosagwa huchanganywa na mafuta ya ng’ombe nayo hutumiwa kupamba mwili.

Nilikaa karibu na moto jioni moja nikiwatazama Wamasai fulani waliokusanyika ili kucheza ngoma. Walisimama katika duara na kusogea kwa kufuatana na mdundo. Mdundo wa ngoma ulipozidi, ile mikufu mipana mizito yenye shanga kwenye mabega ya wasichana iliruka-ruka kwa kufuatana na mdundo. Kisha, moran (mpiganaji) mmoja baada ya mwingine aliingia katikati ya duara na kuanza kurukaruka juu sana. Wacheza-ngoma wanaweza kuendelea kucheza usiku kucha hadi wote watakapochoka kabisa.

Maisha ya Jamaa ya Wamasai

Mchana kutwa, niliketi pamoja na wanawake kadhaa Wamasai chini ya mti aina ya mgunga, na kuwatazama waliposhona shanga kwenye ngozi laini. Waliendelea kushona na kuongea bila kujali ndege aina ya mnana waliopiga kelele mtini huku wakijenga viota vyao kwa nyasi zilizonyauka. Kila siku wanawake hao huchota maji, huokota kuni, hurekebisha nyumba zao, na kuwatunza watoto.

Jua lilipoanza kutua, wachungaji walirudi nyumbani na mifugo yao. Ng’ombe walitembea polepole huku wakitifua vumbi jekundu. Wanawake walipoona vumbi kule mbali, waliacha kazi zao mara moja na kuanza kufanya matayarisho kwa ajili ya ng’ombe waliorudi.

Ng’ombe walipokuwa ndani ya boma, wanaume walitembea-tembea katikati ya wanyama wao, huku wakipapasa pembe za fahali na kusifu uzuri wao. Mvulana mdogo alikamua maziwa kidogo mdomoni, na akakemewa na mamake mara moja. Wasichana walipitapita katikati ya ng’ombe hao wengi wakiwakamua kwa ustadi, na kujaza pomoni vibuyu vyao virefu.

Jioni tulikusanyika karibu na moto kwa sababu ya baridi. Tulisikia harufu ya moshi na nyama-choma na vilevile harufu ya ng’ombe waliokuwa karibu. Mzee mmoja alisimulia hadithi za kale za Wamasai na vitendo vya kishujaa vya moran. Alitua tu aliposikia simba akinguruma kwa mbali, kisha akaendelea kusimulia hadithi yake ndefu iliyofurahisha wasikilizaji wake. Hatimaye, wote, mmoja baada ya mwingine, waliingia kulala katika nyumba zao zenye giza tititi. Ijapokuwa ng’ombe waliolala walisikika wakipumua, kila sehemu ya pori ilikuwa kimya kabisa.

Kulea Watoto

Watu wote kijijini huamka mapema alfajiri. Watoto wadogo wanaovalia tu mikufu na mishipi yenye shanga tumboni, hucheza nje asubuhi. Kicheko chao hufurahisha Wamasai, wanaowapenda watoto wao sana. Wamasai huwategemea watoto wao wawatunze wanapozeeka.

Wote katika jamii hushirikiana kuwalea watoto—mtu yeyote mwenye umri mkubwa anaweza kumtia nidhamu na kumwadhibu mtoto mwasi. Watoto hufundishwa kuwaheshimu wazee, nao hujifunza upesi desturi za jamaa za Wamasai. Wakiwa wadogo hawana jukumu lolote, lakini wasichana wanapokua, wao hufundishwa kazi ya nyumbani na wavulana hufundishwa kutunza na kulinda mifugo. Wazazi huwafundisha watoto wao juu ya mitishamba na mila na mapokeo ya Wamasai.

Jinsi Vijana Huwa Watu Wazima

Vijana wanapokuwa wakubwa, wao hujifunza mila na sherehe wanazohitaji kupitia ili wawe watu wazima. Miongoni mwa mila ambazo wao hujifunza ni zile zinazohusu magonjwa, bahati mbaya, ndoa, na kifo. Wamasai huamini kwamba wasipofuata mila hizo watapatwa na balaa.

Wazazi wa msichana Mmasai wanaweza kupanga ndoa yake akiwa kitoto. Msichana huyo huposwa na mwanamume aliye na mifugo ya kutosha kulipa mahari ambayo babake atatoza. Mara nyingi wasichana huolewa na wanaume walio na umri mkubwa kuliko wao, ambao tayari wana wake wengine.

Wavulana Wamasai wanapokua, wao hushirikiana sana na marika wao. Uhusiano wa pekee wa marika hao unaweza kudumu maisha yao yote. Wakiwa pamoja wataendelea kupata uzoefu na hatimaye kustahili kuwa moran. Wakiwa moran watakuwa na wajibu wa kulinda boma, kuhakikisha maji yanapatikana, na kulinda mifugo na wanyama wawindaji na wezi. Wamasai wanajulikana sana kwa sababu ya ushujaa na ujasiri wao, na sikuzote wao hubeba mikuki yao yenye ncha kali.

Moran wanapofikia umri wa miaka 30, wao hufikia hatua ya mwisho ya kuwa watu wazima. Wakati huo ndipo wanapoitwa wazee. Hatua hiyo husherehekewa kwa shangwe nyingi. Baada ya sherehe hiyo, wanaume hao huruhusiwa kuoa. Wakifikia cheo hicho, wataanza kutafuta mke na kuongeza mifugo, nao wanatazamiwa kutoa ushauri na kusuluhisha mabishano.

Wakati Ujao wa Wamasai

Mila za pekee na utamaduni wa Wamasai unatoweka kwa haraka siku hizi. Katika maeneo mengine, Wamasai hawawezi tena kuhamahama na mifugo yao ili kutafuta malisho bora. Sehemu nyingi za nchi yao ya zamani zinafanywa kuwa mbuga za wanyama, au kutumiwa kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, na ukulima. Wamasai wengi hulazimika kuuza ng’ombe zao wapendwa kwa sababu ya ukame na hali mbaya ya kiuchumi. Wamasai wanapohamia miji mikubwa, wanakumbwa na matatizo yaleyale yanayowapata watu wengine siku hizi.

Mashahidi wa Yehova huhubiri katika eneo la Wamasai huku Afrika Mashariki. Zaidi ya nakala 6,000 za kichapo Furahia Milele Maisha Duniani! zimechapishwa katika Kimasai. Kwa hiyo, Wamasai husaidiwa kuona tofauti iliyopo kati ya ushirikina na kweli ya Biblia. Ni jambo la kufurahisha kwamba Muumba wetu, Yehova Mungu, amewapa watu hao wa pekee na wanaovutia nafasi ya kuwa kati ya watu wa ‘mataifa na makabila na vikundi vya watu na lugha’ watakaookoka uharibifu wa ulimwengu huu wenye taabu.—Ufunuo 7:9.

[Picha katika ukurasa wa 25]

Nyumba ya Wamasai

[Picha katika ukurasa wa 26]

Wamasai wanakusanyika ili kucheza ngoma

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mashahidi wawili Wamasai