Asali Ni Dawa Bora
Asali Ni Dawa Bora
WATAFITI fulani wa mambo ya tiba wamesisimuka sana kutambua jinsi asali inavyoweza kuzuia bakteria na uvimbe. Gazeti la The Globe and Mail la Kanada laripoti hivi: “Tofauti na vile viuavijasumu vingi ambavyo vimeshindwa kuua bakteria sugu, asali yaweza kuua bakteria fulani sugu kwenye vidonda vilivyoambukizwa.”
Asali huponyaje? Jibu la swali hilo lahusisha yule nyuki ambaye hukusanya umajimaji mtamu kutoka kwenye maua. Mate ya nyuki huyo yana kimeng’enya ambacho huvunja sukari iliyo katika umajimaji huo. Sukari hiyo inapovunjwa haidrojeni peroksaidi hufanyizwa, ambayo kwa kawaida hutumiwa kusafisha na kutibu vidonda. Kwa kawaida, haidrojeni peroksaidi inapowekwa kwenye kidonda, haifanyi kazi kwa muda mrefu. Lakini asali ni tofauti. Ripoti hiyo ya gazeti la Globe yasema hivi: “Asali ikiwekwa kwenye kidonda, umajimaji ulio mwilini unaifanya kuwa majimaji, na hiyo hupunguza ukali wa asidi iliyo katika asali.” Ukali wa asidi ukiisha pungua, kimeng’enya huanza kufanya kazi. Kimeng’enya hicho huvunja sukari iliyo katika asali polepole na kwa kiwango kilekile. Utaratibu huo hufanyiza haidrojeni peroksaidi polepole na kwa kadiri ya kutosha ili kuua bakteria bila kuathiri sehemu zisizoambukizwa.
Gazeti la Globe linasema kwamba vitu kadhaa katika asali huiwezesha kuponya vidonda. “Utando mwembamba wa asali hufanya kidonda kiwe na unyevunyevu ambao unalinda ngozi na kuzuia ufanyizaji wa ngozi ngumu. Asali huchochea ukuzi na ufanyizaji wa mishipa midogo ya damu na huchochea chembe zinazofanyiza ngozi mpya.” Pia, vitu fulani katika asali “huzuia uvimbe, huboresha mzunguko wa damu na kuzuia kidonda kisitokwe na umajimaji.”
Ripoti hiyo yatoa tahadhari hii: “Hata hivyo, si kila mtu anayeweza kuponywa kwa asali.” Yakadiriwa kwamba asilimia 5 ya asali ina bakteria zenye sumu. Mashirika fulani kama vile shirika la Afya la Kanada la Huduma za Kuchunguza Bakteria na mashirika mengine yanayoshughulikia magonjwa ya watoto hushauri watu wasiwape watoto walio na umri wa chini ya mwaka mmoja asali kwani “watoto hawana vijidudu fulani vya kutosha katika matumbo yao ili kuwalinda na bakteria hiyo.”