Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuambatana na Upepo

Kuambatana na Upepo

Kuambatana na Upepo

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

“NIPE KITAMBAA NA KAMBA, NAMI NITAWAONYESHA JAMBO LITAKALOSTAAJABISHA ULIMWENGU!” —JOSEPH-MICHEL MONTGOLFIER, 1782.

MIALI ya moto inayotokea ghafula hufanya puto la hewa ya joto lianze kupaa polepole. Kusafiri hewani kwa puto maridadi lenye rangi nyingi huwachangamsha na kuwapumzisha watu wenye shughuli nyingi. Mshabiki mmoja wa puto la hewa ya joto alisema kwamba kusafiri kwa puto “hutuliza na husisimua.”

Kusafiri kwa maputo kumewavutia watu tangu Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, wapange safari ya kwanza kwa puto la hewa ya joto, mapema katika miaka ya 1780. (Ona sanduku chini.) Hata hivyo, wengi walianza kupenda kusafiri kwa maputo tangu miaka ya 1960. Wakati huo ndipo vitambaa visivyoshika moto vilipoanza kutumiwa, na mbinu mpya za bei nafuu na zisizo hatari za kupasha hewa moto na kudhibiti joto ndani ya puto zilipobuniwa.

Jinsi Maputo Yanavyotengenezwa

Puto maridadi hutengenezwa kwa kuunganisha sehemu ndefu za vitambaa vyenye rangi nyingi, zilizo nyembamba kuelekea ncha zote mbili. Maputo mengine yana upana wenye meta 15 na urefu unaozidi meta 25.

Marubani wabunifu hutengeneza maputo yenye ukubwa na maumbo mbalimbali kama vile ya wanyama, chupa, wacheshi, na mengineyo. Maputo yote yenye maumbo mbalimbali husafiri bila kupiga kelele, na yote huendeshwa kwa njia sawa.

Abiria na rubani hupanda kikapu kikubwa cha matete kilichounganishwa na puto kwa kamba nzito za waya. Kikapu hicho huning’inia chini ya mdomo wa puto. Baadhi ya vikapu vimetengenezwa kwa alumini. Unapoangalia juu ukiwa kikapuni utaona kwamba chombo cha kupasha moto na kidhibiti-joto vimekazwa kwenye kipande cha chuma chini tu ya mdomo wa puto. Mitungi ya gesi imo ndani ya kikapu.

Matayarisho ya Kupaa

Ndege huhitaji uwanja mrefu ili iweze kupaa, lakini puto la hewa ya joto huhitaji tu kiwanja kidogo. Kupata kiwanja kisicho na vizuizi vyovyote juu ni muhimu. Je, ungependa kusafiri kwa puto? Kabla hujapanda kikapuni, matayarisho fulani huhitajika.

Kwanza, puto lisilo na hewa hutandazwa chini karibu na kikapu. Kikapu hicho huwekwa upande ambao upepo unaelekea. Kisha, hewa hupuliziwa ndani ya puto kwa kutumia kipepeo kikubwa kinachoendeshwa kwa injini. Baadaye, hewa iliyopashwa moto huingizwa ndani ya puto ili kulipandisha na kusimamisha kikapu. Kisha, vifaa vyote hukaguliwa, kutia ndani mipira ya gesi. Ni muhimu kuhakikisha kwamba kamba za kupunguza hewa zinaning’inia hadi kikapuni. Sasa, abiria wanaweza kupanda na rubani yu tayari kuanza safari. Marubani fulani huwasiliana kwa redio na watu wanaofuata puto kwa gari ili wachukue puto na abiria wakati wanapotua.

Kuambatana na Upepo

Wengi wanaosafiri kwa maputo hupenda kupaa kwenye kimo cha chini ya karibu meta 100 ili waweze kupeperuka polepole na kutazama mandhari yanayovutia na mambo yanayoendelea kule chini. Kwenye kimo hicho hata kicheko na sauti kubwa za watu walio chini husikika. Ni jambo la kuvutia sana kuona puto likipeperushwa na upepo huku ukiwa chini. Watu wengine hupaa hadi kimo cha meta 600 au zaidi kwa ukawaida. Hata hivyo, si jambo la hekima kuruka kwa muda mrefu kwenye kimo cha zaidi ya meta 3,000 bila kuwa na akiba ya hewa.—Soma sanduku la “Kupaa Hadi Kimo cha Juu.”

Lakini puto huteremshwa jinsi gani? Nguvu za uvutano hufanya puto literemke, na rubani hudhibiti mshuko akivuta kamba ya kupunguza hewa ili kuachilia kiasi fulani cha hewa yenye joto. Hata hivyo, kusafiri sambamba na upeo wa macho ni tofauti na kupaa juu. Puto hupelekwa na upepo. Rubani mmoja stadi anasema hivi: “Kila safari ni tofauti, kwa kuwa puto hupeperushwa kwa kufuatana na mwendo na mwelekeo wa upepo.” Mwendo na mwelekeo wa puto hubadilika-badilika kulingana na jinsi upepo unavyovuma. Kwenye kimo cha meta 100 upepo unaweza kuelekea upande mmoja, huku ukielekea upande ule mwingine kwenye kimo cha meta 200.

Kwa kuwa puto husafiri kwa mwendo sawa na upepo, abiria huhisi kana kwamba puto linasimama tuli, huku dunia ikizunguka kule chini. Gazeti la Smithsonian linasema kwamba “watu wanaosafiri kwa puto husafiri sambamba na upepo hivi [kwamba] wanapofungua ramani haipeperushwi na upepo.”

Kuwa Rubani Stadi

Wakati bora wa kusafiri kwa puto ni baada tu ya mapambazuko au kabla ya machweo, kwa kuwa mara nyingi hali ya hewa huwa tulivu wakati huo. Wengi hupenda kusafiri asubuhi kwa kuwa kuna hali ya hewa baridi wakati huo na puto hupaa kwa urahisi. Wale wanaosafiri saa za alasiri huenda wakakuta kwamba usiku umeingia kabla hawajatua.

Rubani hupata ustadi kwa kusafiri mara kwa mara. Jambo la maana ni kupata upepo unaoelekea upande unaotakikana na kufuatana nao. Marubani stadi hupaa hatua kwa hatua. Wao hupaa hadi kimo fulani na kusimamisha puto hapo, kisha hewa hupashwa moto kwa ghafula. Hewa hiyo yenye joto hupaa hadi kwenye sehemu ya juu kabisa ya puto, na kuinua puto juu zaidi.

Kuongeza joto kwa kadiri inayofaa na kuwa makini ni kwa maana ili rubani aweze kuongoza puto ifaavyo. Rubani akikosa kuwa makini hata kwa muda mfupi puto linaweza kuteremka. Rubani stadi hukumbuka kwamba chombo cha kupasha moto kiko meta 15 hadi 18 chini ya sehemu ya juu kabisa ya puto, kwa hiyo, inaweza kuchukua sekunde 15 hadi 30 kabla ya puto kuanza kupaa baada ya hewa kupashwa moto.

Kutua kunaweza kusisimua, hasa kukifanywa wakati upepo unapovuma na katika kiwanja kidogo! Mtaalamu mmoja wa maputo anasema kwamba katika hali hiyo, “ni afadhali kutua kwa haraka na kwa kishindo katika eneo linalofaa, badala ya kuteremka polepole na kujikuta katikati ya simba katika hifadhi fulani ya wanyama.” Hata hivyo, kuteremka polepole kunafurahisha zaidi wakati ambapo hakuna upepo mwingi.

Yaelekea watu wataendelea kufurahia kusafiri kwa maputo yenye rangi nyingi nyangavu; huku wengi wakishiriki katika mashindano na sherehe, na wengine wakifurahia tu kupeperushwa na upepo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14, 15]

SAFARI ZA KWANZA ZA PUTO

Inasemekana kwamba Joseph-Michel na Jacques-Étienne Montgolfier, wana wa tajiri mmoja aliyekuwa mtengenezaji wa karatasi huko Annonay, Ufaransa, ndio waliotengeneza puto la kwanza la hewa ya joto, na kupanga safari ya kwanza ya puto. Walifanya majaribio ya kwanzakwanza na maputo ya karatasi, mapema katika miaka ya 1780, nao walifikiri maputo hayo yalipaa kwa sababu ya moshi wa majani makavu na sufu zilizowaka moto. Punde si punde, wakagundua kwamba ilikuwa hewa yenye joto iliyofanya maputo yapae.

Baadaye, walipoanza kutengeneza maputo kwa kitambaa, waliona kwamba maputo makubwa zaidi yaliweza kupaa juu zaidi, kubeba mizigo mizito zaidi, na abiria wengi zaidi. Mnamo Juni 1783, walirusha puto kubwa kuliko yote ambayo walikuwa wamewahi kutengeneza kufikia wakati huo kutoka kwenye mtaa wa Annonay. Lilipaa kwa muda wa dakika kumi hivi, kisha likateremka.

Walipoona mafanikio hayo waliazimia kurusha puto lenye watu. Hata hivyo, kwanza walirusha puto lililobeba jogoo, bata, na kondoo. Maelfu ya watu walikusanyika kuangalia tukio hilo huko Versailles, mnamo Septemba 1783. Wanyama wote watatu hawakufa wala hawakuathiriwa hata kidogo na safari hiyo ya dakika nane. Punde baadaye, mnamo Novemba 21, 1783, puto lililobeba watu lilirushwa kwa mara ya kwanza. Mfalme Louis wa 16 alishawishiwa kuwaruhusu waungwana wawili kwenda safari hiyo. Walianza huko Château de la Muette, na kupeperuka kwa umbali wa kilometa nane hivi juu ya Paris. Baada ya dakika 25 hivi, wakalazimika kutua kwa kuwa puto lilikuwa linawaka moto.

Yapata wakati huo, wanasayansi wa Chuo cha Sayansi huko Paris walipendezwa na uvumbuzi huo. Profesa Jacques Charles, mmojawapo wa wanafizikia mashuhuri wa wakati huo, alishirikiana na mafundi wawili werevu, Charles na M. N. Robert, kutengeneza puto la kwanza lililojazwa gesi ya hidrojeni. Puto hilo lilijaribiwa Agosti 27, 1783. Puto hilo lilipeperuka kwa umbali wa kilometa 24 hivi, kwa muda wa dakika 45, nalo likapewa jina Charlière. Maputo ya aina hiyo hutumiwa hata leo hii.

[Sanduku katika ukurasa wa 17]

KUPAA HADI JUU

Mwingereza Henry Coxwell ni rubani mashuhuri aliyepaa hadi kimo cha juu. Mnamo Septemba 1862, alipewa kazi ya kumpeleka James Glaisher wa Shirika la Uingereza la Utabiri wa Hali ya Hewa hadi kimo cha juu ili Glaisher afanye uchunguzi wa kisayansi. Walipaa hadi kimo cha kilometa tisa hivi, bila vifaa vya kuongeza hewa ya kupumua!

Baada ya kufikia kimo cha meta 8,000 Coxwell alianza kufanya matayarisho ya kuteremka, huku akiwa na tatizo la kupumua kwa sababu ya upungufu wa hewa. Hata hivyo, kwa sababu ya kuzunguka-zunguka kwa puto, kamba ya kupunguza hewa ilikuwa imejipinda na Coxwell alilazimika kupanda juu ili kunyosha kamba hiyo. Glaisher tayari alikuwa amepoteza fahamu, na ilimbidi Coxwell kuivuta ile kamba kwa meno kwa kuwa mikono yake ilikuwa imepooza kwa sababu ya baridi. Hatimaye wakaanza kuteremka.

Wanaume wote wawili walipata nafuu kiasi cha kuweza kupunguza mwendo wa puto ili lisiteremke kwa kasi mno. Walikuwa wamefikia kimo cha meta 10,000 hivi. Rekodi hiyo haikuvunjwa kwa muda wa miaka 100. Safari yao ya puto, ni mojawapo ya safari maarufu za angani, kwa kuwa walisafiri katika kikapu kisichofunikwa, hawakuwa na akiba ya hewa, walivalia tu nguo za kawaida, na hawakujua mengi kuhusu anga la juu.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Sehemu ya ndani ya puto linalopuliziwa hewa

[Picha katika ukurasa wa 15]

Puto huongezwa hewa yenye joto linapoanza safari na wakati wa safari

[Picha katika ukurasa wa 16]

Maputo yenye maumbo yasiyo ya kawaida