Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuendesha Baiskeli Hufurahisha na Huboresha Afya

Kuendesha Baiskeli Hufurahisha na Huboresha Afya

Kuendesha Baiskeli Hufurahisha na Huboresha Afya

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

NI CHOMBO kipi cha usafiri kinachouzwa kwa bei nafuu kuliko vingine vingi, kinachokwenda kasi zaidi ya gari katika miji mingi, kinachoboresha afya, na kinachofurahisha? Ni baiskeli. Kuendesha baiskeli huzoeza mwili na hufurahisha. Kwa kuwa watu wengi siku hizi wanahangaikia afya yao, huenda kuendesha baiskeli kukakufaa.

Inasemekana kwamba Baroni Karl von Drais, mbuni Mjerumani, ndiye aliyebuni baiskeli. Mnamo mwaka wa 1817, alibuni chombo sahili kilichokuwa kama kifaa cha mtoto cha kuchezea chenye magurudumu. Chombo hicho kiliitwa draisine, nacho kilikuwa na magurudumu mawili, kiti, na usukani lakini hakikuwa na makanyagio. Mnamo mwaka wa 1839, mhunzi mmoja wa Scotland, Kirkpatrick Macmillan, aliunganisha makanyagio na gurudumu la nyuma. Kisha, vyombo hivyo vya usafiri vikabadilika sana. Mfaransa mmoja, Pierre Michaux pamoja na mwanawe Ernest, waliunganisha makanyagio na gurudumu la mbele na hivyo wakabuni chombo kilichoitwa velocipede (kutokana na neno la Kilatini velox, “-enye kasi,” na pedis, “mguu”). Chombo hicho kilikwenda kasi na ilikuwa rahisi zaidi kukiendesha.

Vyombo hivyo vilikwenda kasi zaidi vilipowekwa gurudumu kubwa la mbele. Huko Uingereza, baiskeli iliyoitwa penny-farthing iliundwa ikiwa na gurudumu kubwa sana la mbele lenye kipenyo cha meta 1.5 na gurudumu dogo sana la nyuma. Baiskeli hiyo iliitwa penny-farthing kwa sababu kulikuwa na sarafu kubwa sana iliyoitwa penny na sarafu ndogo sana iliyoitwa farthing.

Kisha baiskeli salama ikabuniwa, ambayo pia ilikwenda kasi. Baiskeli hiyo ilikuwa na magurudumu yenye ukubwa sawa au yaliyokaribia kuwa sawa na haingeweza kuanguka kwa urahisi. Mnamo mwaka wa 1879, Mwingereza Henry Lawson alipeleka baiskeli yake kwenye maonyesho huko Paris. Baiskeli hiyo ilikuwa na mnyororo ambao ulizungusha gurudumu la nyuma. Baadaye, baiskeli hiyo ikaitwa bicyclette.

Baiskeli nyingi leo zina magurudumu yanayolingana kwa ukubwa. Hivyo, muundo wa awali umebadilika kidogo. Baiskeli mbalimbali zilizopo leo, kama vile baiskeli za kawaida, za kwenda safari ndefu, za mashindano, na za kupanda milima, huwawezesha waendeshaji kusafiri kwa starehe huku zikiwa na magurudumu mawili mepesi ya mpira.

Hufurahisha na Huboresha Afya

Katika nchi nyingi, baiskeli hutumiwa sana kwa usafiri kwa sababu hazisababishi uchafuzi wala makelele na zinawawezesha watu wanaosafiri mwendo mfupi kufika haraka kuliko wanaposafiri kwa gari. Katika Afrika, Asia, na kwingineko, baiskeli zimetumiwa na watu kusafirisha vitu vingi sana sokoni. Mara nyingi, baiskeli hutumiwa kubeba watu wawili au zaidi, huku watu wa ukoo na marafiki wakikalia chuma kinachounganisha sehemu za baiskeli au kukalia sehemu ngumu ya kuwekea mizigo.

Katika nchi za Magharibi, ambako magari hutumiwa sana kwa usafiri, watu wameanza kutumia baiskeli kwa sababu ya mahangaiko ya afya na kutaka kubadili kawaida ya maisha. Njia maalumu za baiskeli zimetengenezwa kandokando ya barabara nyingi. Kwa mfano, huko Uingereza, maafisa wengi wa serikali za mitaa hujivunia jinsi wametengeneza vijia vingi vya baiskeli.

Kuendesha baiskeli kwaweza kuboresha afya hata ingawa mtu aweza kuathiriwa na moshi wa magari. Mtaalamu wa usafiri, Adrian Davis, asema kwamba kuendesha baiskeli “humlinda mtu asipate ugonjwa wa moyo, kisababishi kikuu cha kifo na kifo cha mapema huko Uingereza.” Mtu anapoendesha baiskeli yeye hutumia nguvu nyingi sana. Yeye hutumia asilimia 60 hadi 85 hivi ya nguvu zake zote, tofauti na zile asilimia 45 hadi 50 anazotumia anapotembea. Kwa kuwa miguu yake hailemewi na uzito mwingi, haielekei sana kwamba mifupa yake itajeruhiwa kama anapotembea au anapokimbia.

Isitoshe, uendeshaji wa baiskeli hufurahisha na hiyo ni faida nyingine ya afya. Uchunguzi unaonyesha kwamba kuendesha baiskeli huchochea kemikali zinazoitwa endorphin zifanyizwe ubongoni. Kemikali hizo zaweza kumfanya mtu ajihisi vizuri zaidi. Mbali na kumfanya mtu ajihisi vizuri, kuendesha baiskeli kwaweza kumfanya mtu awe na umbo zuri. Jinsi gani? Gazeti la The Guardian laripoti kwamba “mwendeshaji [baiskeli] atachoma kalori saba hivi kila dakika, au kalori 200 kila nusu saa akisafiri kwa mwendo wa wastani.” Matokeo huwa nini? Huenda akawa na kiuno chembamba na kupunguza uzito mwingi mapajani.

Usalama Unapoendesha Baiskeli

Kuna hangaiko kubwa kuhusu usalama wa waendeshaji baiskeli katika nchi zenye magari mengi. Kwa mfano, je, yafaa mtu avae kofia ya kujikinga? Ni jambo la hekima kutahadhari. Kwa upande mwingine, kuvaa kofia ya kujikinga tu hakuonyeshi kwamba mwendeshaji hataumia. Mwandishi wa habari Celia Hall aliandika juu ya uchunguzi uliowahusu waendeshaji baiskeli 1,700 wenye umri mbalimbali ambao walivaa kofia ya kujikinga. Jambo moja la kushangaza lililobainika ni kwamba waendeshaji hufikiri kuwa hawawezi kuumia wanapovaa kofia ya kujikinga. Isitoshe, asilimia 6 kati yao walivaa kofia za kujikinga ambazo hazikuwatosha. Wakati wa msiba wa barabarani, kofia ya kujikinga isiyomtosha mwendeshaji huongeza uwezekano wa kujeruhiwa kwa asilimia 50. Ukivaa kofia ya kujikinga, hakikisha kwamba inakutosha. Chunguza kofia ya kujikinga ya mtoto wako kwa ukawaida. Kofia ya kujikinga ambayo ni kubwa kupita kiasi yaweza kusababisha kifo.

Mara nyingi, madereva huudhiwa na waendeshaji baiskeli na kuwapuuza. Kwa hiyo, hakikisha unaonekana. Vaa mavazi yatakayokulinda, yaani, mavazi yanayong’aa mchana na yanayoweza kumulika usiku. Baiskeli yako pia yapasa kuonekana wazi, hata gizani. Mara nyingi, ni takwa la sheria na ni jambo la hekima kuwa na vifaa vya kumulika kwenye makanyagio na kudumisha taa za mbele na za nyuma zikiwa safi. Hakikisha kwamba uchaguzi wako wa vifaa vya kujilinda unapatana na sheria ya nchi yako.

Ili uwe salama, ni muhimu utunze baiskeli yako. Ichunguze, na uisafishe na uirekebishe kwa ukawaida. Baada ya kuchukua tahadhari hizo, huenda likawa jambo la hekima kuendesha baiskeli kwenye vijia vilivyo kando ya barabara kuu. Lakini ili ufanye hivyo kwa usalama, utahitaji baiskeli inayofaa.—Ona sanduku lenye kichwa “Baiskeli Inayokufaa.”

Mashindano ya Kuendesha Baiskeli

Watu wengine hushiriki katika mashindano ya kuendesha baiskeli. Hivi majuzi kumekuwa na kashfa fulani kuhusu mashindano maarufu ya Tour de France ambazo zimehusianisha mashindano ya kuendesha baiskeli na matumizi ya dawa za kulevya na udanganyifu. Katika makala yenye kichwa “Dawa Bora na Ishinde!,” gazeti la Time lilidai kwamba mashindano hayo “yameharibika.” Watu wengi wameacha kuuheshimu mchezo huo baada ya kusikia madai kuhusu matumizi ya dawa za kulevya na kemikali zinazoongeza nguvu.

Waendeshaji wa baiskeli wenye hekima hufikiria kwa uangalifu muda na jitihada wanazotumia katika mchezo huo. Hata ingawa kuendesha baiskeli huleta faida za afya, watu wenye usawaziko hufahamu kwamba mazoezi ya mwili ni jambo moja tu kati ya mengi yanayomwezesha mtu kuishi kwa muda mrefu akiwa na afya nzuri. Hata hivyo, utakapoendesha baiskeli yako wakati ujao, na ufurahie kutumia chombo hicho kinachoboresha afya!

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 21]

Baiskeli Inayokufaa

Baiskeli za kupanda milima zaweza kutumiwa katika maeneo yote. Baiskeli hizo zina kiunzi kidogo kilicho imara, usukani ulionyooka, makanyagio yaliyowekwa juu kuliko yale ya baiskeli za kawaida, na magurudumu mapana yanayofaa barabara mbovu. Gia mbalimbali zilizopo humwezesha mwendeshaji kupanda vilima kwa urahisi.

Iwapo unataka kusafiri kwenye barabara ngumu na zenye mawemawe, utahitaji baiskeli inayofanana na ile ya kupanda milima na vilevile kama ile ya kawaida. Baiskeli hiyo ina magurudumu membamba na makanyagio yaliyo chini kidogo. Baiskeli za kawaida humwezesha mwendeshaji kuketi wima na zina gia chache.

Unapochagua baiskeli yoyote ile, hakikisha kwamba ukubwa wake unakufaa. Kwanza iendeshe. Rekebisha usukani, kiti, na makanyagio ili vifaane nawe. Unapopanda baiskeli, miguu yako yapasa kufika chini (ona juu).

Utaweza kuendesha baiskeli yako kwa starehe na kwa usalama iwapo utarekebisha kiti ili uweze kunyoosha mguu wako huku kisigino kikikanyaga kanyagio hadi chini kabisa (ona kushoto). Urefu wa usukani wapasa kulingana na ule wa kiti.—Chanzo: Gazeti la Which?

[Picha katika ukurasa wa 19]

Baiskeli ya “penny-farthing”

[Hisani]

Police Gazette, 1889

[Picha katika ukurasa wa 19]

Baiskeli ya “velocipede”

[Credit Line]

Wanaume: A Pictorial Archive from Nineteenth-Century Sources/ Dover Publications, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 20]

Katika sehemu fulani kuvaa kofia ya kujikinga ni takwa la sheria

[Picha katika ukurasa wa 20]

Baiskeli hutumiwa sana kwa usafiri katika nchi nyingi