Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Viatu vya Ngozi ya Samaki

Gazeti la El Comercio la Lima laripoti kwamba katika kiwanda kipya kilicho kwenye Milima ya Andes ya Peru, viatu vinatengenezwa kwa ngozi ya samaki wa trauti. Ngozi za samaki wanaofugwa kwenye vidimbwi vya kuzalishia husafishwa na kutengenezwa kwa dawa za asili. Kisha ngozi hizo hupakwa mafuta na kutiwa rangi kwa vitu vya asili kama vile bizari, kochinili, au achiote. Vitu hivyo haviharibu yale mapambo yenye umbo la almasi kwenye ngozi ya trauti. Ngozi hizo hutumiwa pia kutengeneza “vibeti, kanda za saa, au vifuko vya simu za mkononi.” Barbara León, mhandisi wa kiwanda, aliyesimamia mradi huo asema hivi: ‘Jambo la maana zaidi ni kwamba vitu vya kutengeneza ngozi visivyo vya asili havitumiwi, kama vile kromiamu. Hiyo inazuia uchafuzi. Kwa hiyo, utengenezaji wa ngozi ya trauti hauharibu mazingira.’

Bado Kucheka Ndiyo Dawa Bora!

“Imegunduliwa kwamba dalili za watu walioshuka moyo zilipungua sana walipochekeshwa kila siku kwa muda wa majuma manne,” laripoti gazeti la The Independent la London. “Baadhi ya wagonjwa walioambiwa wasikilize kaseti za vichekesho kwa dakika 30 kila siku walipona na dalili za wengine zilipungua kwa asilimia 50.” Zaidi ya miradi 100 ya uchunguzi huko Marekani imeonyesha kwamba mtu anayecheka anapochekeshwa anaweza kufaidika. Mbinu hiyo imewasaidia watu walioshuka moyo, walio na mizio, wenye shinikizo la juu la damu, wenye mifumo dhaifu ya kinga, na hata wagonjwa wa kansa na yabisi-kavu. Kwa muda mrefu imejulikana kwamba kicheko huboresha afya, lakini haieleweki waziwazi namna jambo hilo linavyowezekana. Hata hivyo, Dakt. Ed Dunkleblau anatoa onyo hili: Epuka matusi na kejeli, na usiwe mcheshi kupita kiasi. La sivyo, mgonjwa aweza kudhania kwamba watu hawajali sana hali yake.

“Dini Si Muhimu Sana”

Uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Brazili uliohusisha watu wazima maskini wanaoishi mijini, umeonyesha kwamba ingawa asilimia 67 hudai kuwa Wakatoliki, ni asilimia 35 tu wanaoamini Yesu, Maria, na mafundisho ya kanisa. Asilimia 30 tu huenda kanisani kila juma. Uchunguzi huo, ulioanzishwa na Kongamano la Kitaifa la Maaskofu wa Brazili, ulionyesha kwamba Wakatoliki wengi hawakubali mafundisho ya Kanisa la Katoliki kuhusu ngono kabla ya ndoa (asilimia 44), talaka (asilimia 59), kuoa tena (asilimia 63), na kutumia vifaa vya kuzuia mimba (asilimia 73). Kulingana na mwanatheolojia Severino Vicente, kanisa linapata hasara kwa sababu ya upungufu wa makasisi, kufifia kwa uvutano wake juu ya mfumo wa elimu wa Brazili, na kwa kufundisha kijuujuu tu. Yeye anasema hivi: “Wakatoliki wa siku hizi wanaamini kwamba lililo sawa huamuliwa na mtu mwenyewe na kwamba dini si muhimu sana.”

Hatari Nyumbani!

Takwimu za hospitali za mwaka wa 1999, zilizochapishwa na Idara ya Biashara na Viwanda ya Uingereza, zilionyesha kwamba “watu 76 walikufa kila juma kwa kujeruhiwa nyumbani—zaidi ya wale waliokufa katika misiba ya barabarani,” laripoti gazeti la The Guardian la London. “Vifaa vya kazi, ngazi, mazulia na mabirika ya kuchemsha maji” yalisababisha vifo vingi. Zaidi ya watu 3,000 kila mwaka walipelekwa hospitalini haraka kwa sababu ya kutegwa na vikapu vya kuweka nguo chafu, zaidi ya watu 10,000 walilazwa hospitalini walipojiumiza wakivaa soksi au soksi za wanawake zinazobana, na zaidi ya watu 13,000 walijeruhiwa walipokuwa wakikata mboga. Misiba 100,000 hivi ilisababishwa na kunywa kileo. Msemaji mmoja mwanamke wa Shirika la Royal la Kuzuia Misiba alisema hivi: ‘Tunapokuwa kazini na barabarani tunajihadhari kwa sababu tunaongozwa na sheria, lakini tunapokuwa nyumbani hatujihadhari. Unaweza kujiumiza vibaya sana ukiondoa kifuniko cha birika kisha maji ya moto yakumwagikie mguuni.’

Jinsi Maharamia Waskandinavia Walivyohifadhi Vyakula

Miaka elfu moja iliyopita, maharamia Waskandinavia waliposafiri, walibeba maji kutoka kwenye mashimo yenye kuvumwani zilizooza kwani maji hayo yangeweza kunywewa hata baada ya miezi mingi. Na Waskandinavia walihifadhi samaki na mboga kama karoti na tanipu katika mashimo yenye majani yaliyooza. Kwa muda mrefu watafiti wamefikiri kwamba kemikali fulani zinazopatikana katika mashimo hayo au ukosefu wa oksijeni humo huzuia vitu visioze haraka. Shirika la habari la CNN laripoti kwamba Dakt. Terence Painter, wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Tekinolojia huko Norway, na watu wengine wawili, sasa wamepata aina fulani ya sukari katika kuvumwani hizo. Na wanaamini kuwa sukari hiyo ndiyo inayohifadhi vitu. Ili kuonyesha jinsi sukari hiyo inavyohifadhi vitu vizuri, walifukia ngozi za samaki wa salmoni ndani ya unga wa mbao na kufukia ngozi nyingine katika majani yaliyooza au kuzipaka umajimaji wa kuvumwani. Ripoti hiyo yasema hivi: ‘Samaki waliohifadhiwa katika mashimo yenye majani yaliyooza au katika umajimaji wa kuvumwani hawakuoza kwa zaidi ya mwezi mmoja, huku samaki waliofukiwa katika unga wa mbao walinuka baada ya siku mbili.’

Ukungu Wenye Moshi Husababisha Mshtuko wa Moyo

Gazeti la National Post la Kanada laripoti kwamba “ukungu wenye moshi unaokuwa katika majiji mengi ya Kanada wakati wa kiangazi unaweza kusababisha mshtuko wa moyo katika muda wa saa mbili.” Ukungu huo huwa na chembe ndogo zisizoonekana zinazosababisha uchafuzi kutokana hasa na magari, mitambo ya nguvu za umeme, na kwenye sehemu za kuotea moto. Gazeti hilo lasema kwamba ‘wagonjwa walio katika hatari ya kupata mshtuko wa moyo, kama vile wagonjwa wa kisukari, wagonjwa wa moyo au wazee, walikabili hatari kubwa zaidi kwa asilimia 48 saa mbili baada ya kupumua hewa yenye chembe hizo ndogo. Baada ya kupumua hewa hiyo kwa saa 24, hatari ya kupatwa na mshtuko wa moyo iliongezeka kufikia asilimia 62.’ Dakt. Murray Mittleman wa shule ya tiba ya Chuo Kikuu cha Harvard adokeza kwamba watu wanapoonywa kwamba kutakuwapo na ukungu wenye moshi ‘ni vizuri wakae ndani ya nyumba kwa muda mrefu, na huenda ikafaa watumie kifaa cha kufanya hewa kuwa baridi. Chembe hizo ni ndogo sana na huingia ndani ya nyumba lakini vifaa vya kufanya hewa kuwa baridi huziondoa.’

Faida ya Kulala Kidogo Mchana

Gazeti la The Times la London laripoti kwamba kulingana na Mwingereza mmoja ambaye ni mtaalamu wa usingizi, Profesa Jim Horne wa Chuo Kikuu cha Loughborough, dawa bora ya kutokuwa na usingizi wakati wa alasiri “ni kulala kidogo kwa dakika kumi.” Horne anasema hivi: ‘Ukilala kabla tu ya kuhisi usingizi, hutahisi usingizi kabisa.’ Makampuni fulani huko Marekani yamewajengea wafanyakazi vyumba vya kulala—vyenye vitanda, mablanketi, mito, na sauti zinazotuliza akili, pamoja na saa zinazolia baada ya kila dakika 20. Lakini Profesa Horne anaonya kwamba ukilala sana—labda, kwa dakika 25—huenda ukaamka ukijihisi vibaya. ‘Ukilala kwa zaidi ya dakika kumi, mwili utalegea kama vile unavyofanya usiku na utaanza kulala usingizi mzito.’

Kunenepa Kupita Kiasi na Kansa

Gazeti la The Times la London laripoti kwamba “kunenepa kupita kiasi ndicho kisababishi kikuu cha kansa miongoni mwa watu wa nchi za Magharibi wasiovuta sigara.” Uchunguzi uliofanywa kwa muda wa miaka 50 umeonyesha kwamba kubadili hali ya maisha—kutia ndani kupunguza uzito iwapo mtu ni mnene kupita kiasi—kwaweza kupunguza uwezekano wa kupata kansa kwa asilimia 50 miongoni mwa watu wasiovuta sigara. Profesa Julian Peto wa Taasisi ya Uchunguzi wa Kansa huko Uingereza, anasema kwamba ‘iwapo wewe si mvutaji wa sigara, unapaswa kuepuka kunenepa kupita kiasi na virusi vinavyosababisha kansa ya tumbo na ya mlango wa kizazi. Majaribio yaliyofanywa kwa kutumia wanyama yameonyesha kwamba lishe ya kadiri hupunguza sana uwezekano wa kupata kansa.’ Mtu husemwa kuwa amenenepa kupita kiasi iwapo uzito wake wa mwili umezidi uzito wa wastani wa watu wa umri wake, jinsia yake, kimo chake, na umbo lake kwa asilimia 20.

Kuishi Pamoja Kabla ya Ndoa

Gazeti la Kanada la National Post lasema kwamba ‘wazazi wanaoishi pamoja kabla ya kufunga ndoa wanakabili uwezekano mkubwa zaidi wa kutengana.’ Heather Juby, mwandishi-msaidizi wa uchunguzi uliofanywa na shirika la Takwimu la Kanada, alisema kuwa watafiti walitarajia kwamba wenzi walio na mtoto wangejitoa kabisa kudumisha uhusiano wao. Yeye asema hivi: “Lakini wenzi wanaokubali haraka kuishi pamoja kabla ya kufunga ndoa hutengana haraka pia.” Watafiti waligundua kwamba asilimia 25.4 ya watu walioishi pamoja kabla ya kufunga ndoa walitengana, huku asilimia 13.6 ya wazazi ambao hawakuishi pamoja kabla ya kufunga ndoa walitengana. Juby asema kwamba ‘uhusiano wa watu wanaoishi pamoja kabla ya kufunga ndoa haudumu, kwani huenda ikawa walikuwa tayari kuishi pamoja bila kufunga ndoa kwa sababu hawakuona ndoa kuwa muungano wa kudumu.’