Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Magumu na Hatari za Ualimu

Magumu na Hatari za Ualimu

Magumu na Hatari za Ualimu

‘Walimu wana majukumu mengi mazito, hata hivyo, jitihada za waelimishaji hao katika shule zetu husifiwa mara chache sana.’—Ken Eltis, Chuo Kikuu cha Sydney, Australia.

KAZI ya ualimu imetajwa kuwa “kazi muhimu zaidi.” Hata hivyo, walimu hukabili matatizo mengi kama vile, mapato ya chini, madarasa mabaya, kushughulikia karatasi nyingi, wanafunzi wengi mno darasani, ukosefu wa heshima, ujeuri, na wazazi wasiojali. Walimu hushughulikia matatizo hayo jinsi gani?

Ukosefu wa Heshima

Tuliwauliza walimu wanne wa New York City ni matatizo gani wanayoona kuwa makubwa. Wote walijibu: “Ukosefu wa heshima.”

William, anayeishi Kenya, alisema kwamba hata watoto barani Afrika hawana heshima kama zamani: “Utii wa watoto unapunguka. Nilipokuwa mtoto [sasa ana umri wa miaka 40 na kitu], walimu walikuwa kati ya watu walioheshimiwa zaidi huku Afrika. Wazee kwa vijana walimwona mwalimu kuwa mfano wa kuigwa. Heshima hiyo inapunguka. Utamaduni wa nchi za Magharibi unawaathiri watoto pole kwa pole hata mashambani. Kutoheshimu mamlaka husifiwa kuwa ushujaa katika sinema, video, na vitabu.”

Giuliano, anayefanya kazi ya ualimu huko Italia, analalamika hivi: “Watoto huathiriwa na roho ya kuasi, ya ukaidi, na ya kutotii inayoenea kotekote katika jamii.”

Dawa za Kulevya na Ujeuri

Kwa kusikitisha, utumizi wa dawa za kulevya ni tatizo kubwa sana shuleni hivi kwamba mwalimu na mwandishi, Mmarekani, LouAnne Johnson, aliandika: ‘Mtaala wa karibu kila shule, kuanzia shule za watoto wadogo, unatia ndani masomo ya kukinza dawa za kulevya. Watoto hujua mengi kuhusu dawa za kulevya kuliko watu wazima wengi. Wanafunzi wanaoanza kutumia dawa za kulevya hasa ni wale wasiojiamini, wanaohisi kwamba hawapendwi, wapweke, au waliochoshwa.’—Two Parts Textbook, One Part Love.

Ken, mwalimu anayeishi Australia, aliuliza hivi: “Walimu wetu watamfundisha jinsi gani mtoto aliye na umri wa miaka tisa, ambaye amezoea kutumia dawa za kulevya nyumbani?” Michael, mwenye umri wa miaka 30 na kitu, ambaye ni mwalimu wa shule moja huko Ujerumani, anaandika hivi: “Tunajua kwamba watoto hutumia na kuuza dawa za kulevya shuleni; lakini ni wachache sana wanaogunduliwa.” Anataja pia kutotii. Anasema kwamba ishara ya kutotii ni ‘mielekeo ya kuharibu vitu. Meza na kuta huchafuliwa, na dawati na viti huharibiwa. Baadhi ya wanafunzi wangu wamekamatwa au kuhojiwa na polisi kwa sababu ya kuiba dukani, na kadhalika. Si ajabu kwamba watoto huiba sana shuleni!’

Amira, anayefundisha katika Jimbo la Guanajuato, Mexico, anasema: “Ujeuri na utumizi wa dawa za kulevya nyumbani huwaathiri watoto moja kwa moja. Wao hufundishwa lugha chafu na maovu mengine nyumbani. Tatizo jingine kuu ni umaskini. Ijapokuwa masomo ni ya bure katika nchi yetu, bado wazazi wana daraka la kuwanunulia watoto vitabu vya kuandikia, kalamu, na vitu vinginevyo. Lakini mara nyingi wao huwa na pesa za kununua chakula tu.”

Bastola Shuleni?

Hivi majuzi kumekuwa na visa kadhaa vya kupiga risasi katika shule huko Marekani. Visa hivyo huonyesha kwamba ujeuri unaohusisha bastola ni tatizo kubwa katika nchi hiyo. Ripoti moja inasema hivi: “Inakadiriwa kwamba kila siku bastola 135,000 hupelekwa kwenye zile shule 87,125 za umma za nchi hiyo. Ili kupunguza idadi ya bastola shuleni, wenye mamlaka hutumia vifaa vya kugundua silaha za metali, kamera za upelelezi, mbwa waliozoezwa kunusa bastola, ukaguzi wa kabati za wanafunzi, vitambulisho, na kupiga marufuku mikoba ya vitabu shuleni.” (Teaching in America) Ulinzi mkali kama huo unazusha swali hili, Je, tunaongea juu ya shule au magereza? Ripoti hiyo inasema vilevile kwamba zaidi ya wanafunzi 6,000 wamefukuzwa shuleni kwa sababu ya kubeba bastola!

Iris, aliye mwalimu huko New York City, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Wanafunzi huleta silaha shuleni kisirisiri. Vifaa vya kugundua metali haviwezi kugundua silaha zote zinazopelekwa shuleni. Kuharibu vitu kimakusudi ni tatizo jingine kubwa.”

Katika hali hiyo ya vurugu, walimu wenye bidii hujaribu kuwaelimisha watoto na kuwafundisha maadili. Si ajabu kwamba walimu wengi sana wameishiwa nguvu kabisa kimwili na kiakili, na kushuka moyo. Rolf Busch, aliye msimamizi wa Shirika la Walimu huko Thuringia, Ujerumani, alisema hivi: “Karibu theluthi moja ya walimu milioni moja huko Ujerumani huwa wagonjwa kwa sababu ya mfadhaiko. Wameishiwa nguvu kabisa kwa sababu ya kazi yao.”

Watoto Wanaozaa Watoto

Vijana wanaofanya ngono ni tatizo jingine kuu. George S. Morrison, mwandishi wa kitabu Teaching in America, anasema hivi kuhusu nchi hiyo: “Wasichana milioni 1 hivi (asilimia 11 ya wasichana walio na umri wa kati ya miaka 15 na 19) hupata mimba kila mwaka.” Wasichana wengi wenye umri wa kati ya miaka 13 na 19 hupata mimba huko Marekani kuliko katika nchi nyingine zilizoendelea.

Iris anakubaliana na maoni hayo na kusema: “Vijana huongea kuhusu ngono na karamu tu. Ni kama ugonjwa. Na sasa tuna mtandao wa Internet kwenye kompyuta za shule! Hiyo inamaanisha kwamba wanafunzi wanaweza kupiga gumzo na kuangalia picha chafu kwenye Internet.” Angel, anayeishi Madrid, Hispania, alisema hivi: “Uasherati ni jambo la kawaida miongoni mwa wanafunzi. Wanafunzi wachanga sana wanapata mimba.”

“Mayaya Wenye Cheo cha Juu”

Lalamiko jingine la walimu ni kwamba wazazi wengi hawawafundishi watoto wao. Walimu husema kwamba wazazi ndio wanaopaswa kuwa wa kwanza kuelimisha watoto wao. Adabu inapaswa kufundishwa nyumbani. Sandra Feldman, msimamizi wa Shirika la Walimu la Marekani anasema kwamba ‘tunapaswa kuwaona walimu kuwa wataalamu, wala si mayaya wenye cheo cha juu.’

Mara nyingi wazazi hawaungi mkono nidhamu inayotolewa shuleni. Leemarys, aliyenukuliwa katika sehemu iliyotangulia, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Ukimripoti mwanafunzi mhalifu kwa mkuu wa shule, utashambuliwa na wazazi hivi punde!” Busch, aliyenukuliwa mapema, alisema hivi kuwahusu wanafunzi wakaidi: “Watoto hawafundishwi nyumbani tena. Siku hizi si kawaida watoto kufundishwa vizuri na kwa busara nyumbani.” Estela, anayeishi Mendoza, Argentina, alisema hivi: “Sisi walimu huwaogopa wanafunzi. Tukiwapa maksi za chini, wataturushia mawe, au kutushambulia. Tukiwa na gari, wataliharibu.”

Si ajabu kwamba kuna upungufu wa walimu katika nchi nyingi. Vartan Gregorian, msimamizi wa Shirika la Carnegie la New York, alionya hivi: ‘Shule zetu [za Marekani] zitahitaji walimu wapya milioni 2.5 katika miaka kumi ijayo. Walimu hutafutwa huko India, West Indies, Afrika Kusini, Ulaya na popote pale ambapo walimu wazuri wanaweza kupatikana ili wafundishe katika shule’ za majiji makubwa. Yaelekea maeneo hayo yatakumbwa na upungufu wa walimu.

Kwa Nini Kuna Upungufu wa Walimu?

Yoshinori, ambaye amekuwa mwalimu kwa muda wa miaka 32 huko Japani, alisema kwamba “ualimu ni kazi ya fahari yenye malengo mazuri, nayo huheshimiwa huko Japani.” Kwa kusikitisha, walimu hawaheshimiwi katika tamaduni fulani. Gregorian, aliyenukuliwa hapo awali, alisema kwamba walimu “hawaheshimiwi, hawatambuliwi kuwa wataalamu, wala hawalipwi mshahara wanaostahili. . . . Katika majimbo mengi [ya Marekani], walimu huchuma pesa kidogo kuliko watu wanaofanya kazi nyingine zozote zinazohitaji shahada ya kwanza au shahada ya pili.”

Ken Eltis, aliyenukuliwa hapo awali, aliandika hivi: “Itakuwaje wakati walimu watakapogundua kwamba kazi nyingi zisizohitaji elimu nyingi huleta mapato makubwa kuliko ualimu? Au watakapoona kwamba wanafunzi ambao waliwafunza miezi kumi na miwili iliyopita . . . huchuma kiasi kikubwa cha fedha kuliko wanavyochuma sasa, au kwamba hawataweza kufikia kiasi hicho hata katika miaka mitano ijayo? Bila shaka jambo hilo lingemfanya mwalimu ajione kuwa yeye si wa maana.”

William Ayers aliandika hivi: “Walimu hupata mshahara mdogo sana . . . Tunalipwa tu robo ya mshahara wa wakili, nusu ya mshahara wa mhasibu, na kidogo kuliko madereva wa lori na watu wanaofanya kazi kwenye kiwanja cha kutengenezea meli. . . . Hakuna kazi nyingine yenye madaraka mazito hivyo na mshahara mdogo hivyo.” (To Teach—The Journey of a Teacher) Janet Reno, aliyekuwa Mkuu wa Sheria wa Marekani, alisema hivi mnamo Novemba 2000: “Tunaweza kuwatuma watu hadi kwenye mwezi. . . . Tunawalipa wanariadha wetu mishahara minono. Kwa nini walimu wetu hawalipwi mshahara wa kutosha?”

“Kwa kawaida, walimu hawalipwi vya kutosha,” alisema Leemarys. “Baada ya miaka mingi ya masomo, mimi hulipwa mshahara wa chini, licha ya mfadhaiko na magumu ya maisha ya jiji hili kubwa la New York City.” Valentina, mwalimu mmoja huko St. Petersburg, Urusi, alisema hivi: “Kazi ya mwalimu haithaminiwi. Mapato yamekuwa chini sikuzote.” Marlene, anayeishi Chubut, Argentina, anakubaliana naye kwa kusema hivi: “Inatubidi kufanya kazi katika shule mbili au tatu, na kukimbia kutoka mahali pamoja hadi pengine kwa sababu mshahara wetu ni mdogo. Kwa hiyo, tunashindwa kufanya kazi yetu ifaavyo.” Arthur, mwalimu mmoja anayeishi Nairobi, Kenya, alimwambia mwandishi wa Amkeni! hivi: “Kwa sababu uchumi unazorota, maisha yangu kama mwalimu hayajakuwa rahisi. Wafanyakazi wenzangu watakubaliana nami kwamba sikuzote watu huepuka kazi hiyo kwa sababu ya mshahara mdogo.”

Diana, mwalimu mmoja huko New York City, alilalamika kwamba walimu hutumia muda wa saa nyingi kushughulikia karatasi nyingi. Mwalimu mwingine aliandika hivi: ‘Karibu siku nzima hutumiwa kurudia-rudia mambo tu.’ Lalamiko moja la kawaida lilikuwa: ‘Siku nzima tunajaza fomu zisizo za maana.’

Walimu Wachache, Wanafunzi Wengi

Berthold, anayeishi huko Düren, Ujerumani, alitaja tatizo jingine la kawaida: “Madarasa yana wanafunzi wengi mno! Madarasa fulani yana wanafunzi 34. Hivyo, hatuwezi kuwasaidia wanafunzi walio na matatizo. Wao hawatiwi maanani. Mahitaji ya mwanafunzi mmoja-mmoja hupuuzwa.”

Leemarys, aliyenukuliwa hapo awali, alieleza hivi: “Mwaka uliopita, tatizo langu kuu, mbali na wazazi wasiojali, lilikuwa kwamba nilikuwa na wanafunzi 35 katika darasa langu. Wazia kujaribu kuwafundisha watoto 35 wenye umri wa miaka sita!”

Iris alisema hivi: “Huku New York kuna upungufu wa walimu, hasa walimu wa hesabu na sayansi. Wanaweza kupata kazi bora mahali pengine. Kwa hiyo, walimu wengi wa nchi nyingine wameajiriwa.”

Bila shaka, ualimu ni kazi ngumu. Basi, ni nini kinachowachochea walimu? Kwa nini wao huendelea kufundisha na kuvumilia? Sehemu ya mwisho itazungumzia maswali hayo.

[Blabu katika ukurasa wa 9]

Inakadiriwa kwamba bastola 135,000 hupelekwa kwenye shule za Marekani kila siku

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 10]

Mwalimu Mwenye Matokeo

Ungemfafanua mwalimu mzuri jinsi gani? Je, ni mtu ambaye anaweza kumsaidia mtoto kukariri mambo na kupita mitihani? Au ni mtu ambaye humfundisha mtoto kuuliza maswali, kufikiri, na kutumia akili? Ni nani ambaye humsaidia mtoto kuwa raia bora?

“Tunapotambua kwamba sisi walimu ni wasafiri wenzi pamoja na wanafunzi wetu katika safari ndefu na ngumu ya maisha, tunapoanza kuwatendea kwa heshima na hadhi wanayostahili, ndipo tunapoanza kuwa walimu bora. Kuwa mwalimu bora ni rahisi hivyo, na vilevile vigumu hivyo.”—To Teach—The Journey of a Teacher.

Mwalimu bora hutambua vipawa vya kila mwanafunzi, naye hujua jinsi ya kujenga vipawa hivyo. William Ayers alisema: “Itatubidi kugundua njia bora ya kufundisha, ualimu unaojenga uwezo, uzoefu, stadi, na vipawa . . . Nakumbuka maneno ya mzazi mmoja Mhindi Mwekundu aliyekuwa na mvulana mwenye umri wa miaka mitano aliyesemekana kuwa haelewi mambo haraka: ‘Wind-Wolf anajua majina ya zaidi ya ndege 40 na jinsi wanavyohama. Anajua kwamba tai huwa na manyoya 13 mkiani. Anahitaji tu mwalimu anayeelewa vipawa vyake.’”

Ili kumsaidia kila mtoto ifaavyo, ni lazima mwalimu atambue kile kinachompendeza na kumsisimua mtoto; kinachomkasirisha na kumfurahisha. Mwalimu bora huwapenda watoto.

[Hisani]

United Nations/Photo by Saw Lwin

[Sanduku katika ukurasa wa 11]

Je, Ni Lazima Masomo Yafurahishe Sikuzote?

Mwalimu William Ayers aliorodhesha mambo kumi ambayo watu huamini kuhusu ualimu lakini yasiyo ya kweli. Mojawapo ni: “Walimu bora hufundisha kwa kuwafurahisha wanafunzi.” Anaongeza: “Ucheshi hupotosha fikira, huburudisha. Wacheshi hufurahisha. Mizaha huchekesha. Masomo yanaweza kumhusisha mwanafunzi, kumvutia, kumstaajabisha, kumvuruga akili, na mara nyingi kumfurahisha sana. Ni sawa ikiwa masomo hufurahisha, lakini si lazima mwalimu awachekeshe wanafunzi. Mwalimu anahitaji kuwa na maarifa, uwezo, stadi, busara, na ufahamu juu ya mambo mengi, na ni lazima awe mtu anayewafikiria na kuwajali wengine.”—To Teach—The Journey of a Teacher.

Sumio, anayeishi huko Nagoya City, Japani, ameona kwamba wanafunzi wake wana tatizo hili: “Wanafunzi wengi wa shule ya sekondari hawapendezwi na chochote kingine isipokuwa tu kujifurahisha na kufanya mambo yasiyotaka jitihada zozote.”

Rosa, mshauri mmoja wa wanafunzi huko Brooklyn, New York, alisema hivi: “Wanafunzi wengi huona kwamba masomo huchosha, mwalimu huchosha, na wanataka kila kitu kiwafurahishe. Hawaelewi kwamba watanufaika na masomo kadiri wanavyotia bidii.”

Kwa sababu vijana wengi wanataka tu kufurahishwa, hawataki kufanya bidii na kujitahidi. Sumio, aliyenukuliwa juu, alisema hivi: “Tatizo ni kwamba hawaoni manufaa ya baadaye. Ni wanafunzi wachache sana wa shule ya sekondari wanaotambua kwamba wakitia bidii sasa, watanufaika wakati ujao.”

[Picha katika ukurasa wa 7]

DIANA, MAREKANI

[Picha katika ukurasa wa 8]

‘Utumizi na uuzaji wa dawa za kulevya umeenea sana lakini hugunduliwa mara chache.’—MICHAEL, UJERUMANI

[Picha katika ukurasa wa 8]

“Ujeuri na utumizi wa dawa za kulevya nyumbani huwaathiri watoto moja kwa moja.”—AMIRA, MEXICO

[Picha katika ukurasa wa 9]

‘Tunapaswa kuwaona walimu kuwa wataalamu, wala si mayaya wenye cheo cha juu.’—SANDRA FELDMAN, MSIMAMIZI WA SHIRIKA LA WALIMU LA MAREKANI