Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kilimo cha Kutumia Mbolea ya Kimaumbile

Kilimo cha Kutumia Mbolea ya Kimaumbile

Kilimo cha Kutumia Mbolea ya Kimaumbile

CHUKUA udongo wa kutosha kutoka kwenye shamba lako la mboga. Je, udongo huo umewekwa dawa nyingi za kuua magugu, wadudu, na wanyama waharibifu hivi kwamba hauna viumbe wowote? Au, je, umejaa minyoo, wadudu, na viumbe wengine wadogo wa kila aina? Iwapo udongo wako una viumbe wengi kama hao, basi huenda, kwa kujua au bila kujua, unafanya kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile.

Mara nyingi, kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile huhusisha kutumia vitu vya asili ili kuboresha udongo. Mojawapo ya malengo ya kilimo hicho ni kuboresha udongo ili mimea iwe yenye afya na isiathiriwe na wadudu waharibifu na magonjwa. Sasa watu katika nchi zinazotumia mbolea ya kemikali wanapendelea kutumia mbolea ya kimaumbile. Kwa nini? Kuna sababu kadhaa.

Kwanza, nyakati nyingine mabaki ya dawa za kuwaua wadudu waharibifu kwenye matunda na mboga yamesababisha hatari kubwa za afya. Kwa mfano, kitabu Pesticide Alert kiliripoti kwamba ‘katika miezi ya Juni hadi Septemba mwaka wa 1985, watu 1,000 hivi huko Kanada na katika majimbo ya Magharibi [mwa Marekani] waliathiriwa na matikiti-maji yaliyokuwa na mabaki ya dawa ya Temik ya kuua wadudu waharibifu.’

Kwa kuongezea, watu wengi huonelea kwamba kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile hulinda mazingira. Wadudu fulani waharibifu wamekuwa sugu kwa sababu ya kupuliziwa dawa za kemikali mara nyingi, hivyo wanasayansi wamebuni sumu hatari zaidi. Kemikali hizo hatari zimeingia ndani ya maji ya chini ya ardhi na zimechafua maji yaliyo muhimu.

Faida nyingine ya kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile ni kwamba maeneo yenye takataka hupungua. Jinsi gani? Takataka nyingi ni majani na mabaki ya vyakula. Badala ya kutupwa, takataka hizo za kimaumbile zaweza kurundikwa na kuachwa zioze ili zitokeze mbolea-vunde. Huenda jambo hilo halipendezi, lakini mbolea hiyo hunufaisha sana mimea!

Hatimaye, watu fulani huona kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile kama njia ya kufanya mazoezi, kuota jua, kutayarisha udongo, na kufurahia kuona mbegu ndogo zikichipuka kuwa mimea yenye afya. Je, unapendezwa na kilimo hicho? Basi, na tuanze kulima! Tutaanza kwanza kwa kuchunguza udongo shambani mwako.

Jinsi Udongo Unavyoboreshwa Shambani Mwako

Mashamba mengi huwa na udongo wa kunata au mchanga. Mchanga una chembe kubwa zinazofanya maji na virutubishi kufyonzwa haraka sana hivi kwamba havinufaishi mizizi. Kwa upande mwingine, udongo wa kunata una tabaka ndogo zinazokaribiana sana hivi kwamba maji hayawezi kupenya tabaka hilo gumu. Hivyo, maji hayo hukosa kupenya na huendelea kutiririka au hulowesha udongo tu na kufanya mizizi ya mimea kukosa hewa.

Mizizi ya mimea husitawi katika udongo unaoweza kuhifadhi unyevu wa kutosha ili kuzuia isinyauke, huku ukiruhusu maji ya ziada yapenye chini zaidi. Wakulima huita udongo wa aina hiyo mboji. Hewa hupenya kwa urahisi katika udongo huo na kuwezesha viumbe vilivyomo kuongeza virutubishi udongoni.

Kiasi kikubwa cha mbolea-vunde chapasa kuongezwa kwenye udongo wa kunata na kwenye mchanga ili uhifadhi unyevu na uruhusu maji ya ziada kupenya. Mbolea hiyo inapoingizwa ardhini, udongo huboreshwa. Hakuna haja ya kutia maji mengi kwani mbolea hiyo huhifadhi unyevu kama sifongo. Mbolea-vunde huwa na mamilioni ya bakteria zenye faida zinazoendelea kusaga takataka zinazooza na kubadili takataka hizo kuwa virutubishi muhimu vinavyofanya mimea isitawi. Mbolea-vunde pia hufanya udongo uwe na asidi na chumvi ya kadiri.

Wakati ambapo mimea fulani yenye mizizi mirefu, kama vile klova na alfalfa, inapopandwa udongoni, hiyo hulainisha udongo mzito na kuongeza mbolea ya kimaumbile. Kutandaza nyasi au unga wa mbao kwenye udongo kunaweza pia kuuboresha.

Minyoo huboresha sana udongo shambani mwako. Minyoo wanapoingia ndani kabisa ya ardhi—kufikia kina cha meta nne—wao huingiza hewa udongoni, huleta madini mbalimbali juu, na kuwezesha maji yapenye vizuri. Wanapofanya mambo yote hayo, wao huacha kinyesi. Kitabu Step by Step Organic Vegetable Gardening husema kwamba kinyesi hicho kina “madini ya nitrojeni, fosforasi, na potasiamu yanayozidi kwa mara tano yale yaliyo katika udongo ulio karibu.”

Vyura, Ndege, na Wadudu Huboresha Shamba

Lakini unaweza kuwamalizaje wadudu waharibifu shambani mwako bila kutumia dawa? Usisahau kwamba zaidi ya kuwaua wadudu waharibifu, dawa hizo huua viumbe muhimu kama vile minyoo na kuvu. Pia, kumbuka kwamba vyura ni muhimu sana katika kilimo. Chura anaweza kula wadudu waharibifu 10,000 kwa muda wa miezi mitatu naye hachagui anachokula. Yeye hula viumbe wanaoharibu mimea kama vile nyenje, wadudu na viwavi wa aina fulani, na konokono.

Ndege pia hula viumbe waharibifu. Kitabu Gardening Without Poisons chasema kwamba ndege aina ya wren alionekana akiwalisha “makinda wake buibui na viwavi 500 alasiri moja katika majira ya kiangazi.” Ukitaka ndege kadhaa aina ya wren au ndege wengine wanaokula wadudu waje shambani mwako basi weka chakula cha ndege na vifaa vya kujenga kiota mahala wanapoweza kuviona. Muda si muda, utaona wakija! Na vipi wadudu? Wadudu wengi wanaoboresha shamba hula wadudu waharibifu. Ukinunua wadudu aina ya ladybug kisha uwaweke shambani mwako, watawamaliza mara moja wadudu aina ya aphid kwani wanapenda kula wadudu hao sana. Mayai ya kivunja-jungu yanaweza pia kununuliwa na kuwekwa shambani. Mayai hayo yakianguliwa, vivunja-jungu watakula wadudu wote walio karibu nao.

Mimea Huzuia Wadudu Waharibifu

Unaweza kutumia mimea fulani kupunguza idadi ya wadudu waharibifu shambani mwako. Panda mimea ambayo huepukwa na wadudu waharibifu karibu na mimea inayohitaji kulindwa. Kwa mfano, minyoo fulani ambayo hula na kudhoofisha mizizi ya mimea mingi haiwezi kukaribia mimea ya matageta. Na vipepeo fulani ambao huharibu kabichi hawakaribii kabichi zilizopandwa karibu na mimea ya rosemary, sage, au thyme. Hata hivyo, tahadhari hii yafaa: Mimea fulani huwavutia wadudu waharibifu.

Mbinu ya kubadilisha mazao shambani ni njia nzuri ya kuzuia wadudu waharibifu na magonjwa. Badala ya kupanda aina moja ya mmea mahala pamoja miaka nenda miaka rudi, huenda ikafaa kupanda mimea tofauti shambani mwako. Kwa njia hiyo utamaliza magonjwa na wadudu waharibifu.

Kilimo cha kutumia mbolea ya kimaumbile chaweza kuwa kigumu, na kinahitaji wakati na subira. Kuboresha udongo wako kwa kutumia mbolea ya kimaumbile kwaweza kuchukua muda wa miezi mingi. Huenda ukakabili vizuizi, na labda ukashawishiwa kunyunyiza kemikali. Lakini kabla ya kufanya hivyo, tua kidogo na ufikirie faida za muda mrefu utakazopata kwa kuepuka kutumia kemikali zenye sumu. Hata hivyo, ukiwa mwenye subira, baada ya muda mfupi huenda shamba lako lililorutubishwa kwa mbolea ya kimaumbile likazaa mboga tamu zisizoweza kuharibiwa kwa urahisi na wadudu waharibifu wala ugonjwa, kama za mashamba mengine. Hiyo haimaanishi kwamba shamba lako halitakumbwa na matatizo kamwe, lakini utafurahia sana matokeo utakayopata. Basi endapo unapenda kilimo, mbona usijaribu kuboresha shamba lako kwa kutumia mbolea ya kimaumbile?

[Picha katika ukurasa wa 17]

Udongo wa kunata

[Picha katika ukurasa wa 17]

Mchanga

[Picha katika ukurasa wa 17]

Udongo wa mboji

[Picha katika ukurasa wa 18]

Viumbe Wanaoboresha Shamba Lako

Chura anaweza kula wadudu waharibifu 10,000 kwa muda wa miezi mitatu

Ndege aina ya “wren” alionekana akiwalisha “makinda wake buibui na viwavi 500 alasiri moja katika majira ya kiangazi”

Minyoo huingiza hewa udongoni na huleta madini mbalimbali juu

“Ladybug” hupenda kula mdudu mharibifu anayeitwa “aphid”

[Picha katika ukurasa wa 18]

Wakati mbolea-vunde inapoingizwa ardhini, udongo huboreshwa