Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Jicho Kubwa

Hapo zamani ilisemekana kwamba kiti cha pweza wa brittle hakuwa na macho na aliishi katika sehemu za chini za bahari zenye giza. Watafiti walishangazwa sana na jinsi kiumbe huyo alivyoonekana kuwa aliwatambua maadui na kuwatoroka. “Sasa wanasayansi wamegundua siri ya kiumbe huyo,” laripoti gazeti la The New York Times. “Mwili wa kiumbe huyo huwa jicho moja kubwa.” Kiti cha pweza wa brittle hutumia lenzi nyingi ndogondogo kufanyiza kitu kinachoaminika kuwa jicho moja kubwa. Isitoshe, lenzi hizo ndogo zaweza “kupitisha mwangaza mara 10 zaidi ya zile lenzi ndogo za kisasa zinazotengenezwa katika maabara,” yasema ripoti hiyo. Dakt. Joanna Aizenberg, aliyeanzisha uchunguzi huo, alisema hivi: “Uchunguzi huo unaonyesha jinsi viumbe vinavyoweza kutokeza vitu vya ajabu hata kuliko tekinolojia ya kisasa.”

Bakteria Sugu

Gazeti la National Post la Kanada laripoti kwamba kuna viumbe wengi sana duniani, hata kilometa kadhaa chini ya ardhi. Profesa Terry Beveridge wa Chuo Kikuu cha Guelph asema hivi: “Bakteria hizo zaweza kuwa chini sana ya ardhi ya Dunia hivi kwamba maji ya mvua yanaweza kuzifikia baada ya miaka 50,000. Bakteria hizo huishi bila mwangaza, usanidimwanga, na hazina sukari wala protini za kula.” Bakteria hizo huishi vipi katika hali hizo? Gazeti la Post lasema kwamba watafiti wa Kanada na Marekani wamegundua kwamba bakteria ya Shewanella hujiambatisha kwenye chuma chenye oksijeni na kula “elektroni za madini ili ipate nishati ya kuiwezesha kuishi.” Wanasayansi wanakadiria kwamba makumi ya maelfu ya vijidudu mbalimbali huishi kina kirefu sana chini ya ardhi. Lakini ni asilimia 10 hivi ya vijidudu hao ambao wameainishwa kikamili.

Ugonjwa wa Malale Umerudi Tena

Jarida la British Medical Journal laripoti kuwa “watafiti wamesema kwamba ugonjwa wa malale umetokea tena na kuambukiza watu wengi katika sehemu fulani za Afrika.” Pierre Cattand, wa Shirika la Kumaliza Ugonjwa wa Malale barani Afrika, asema hivi: ‘Watu milioni 60 wamo hatarini, lakini ni watu milioni tatu au nne tu wanaochunguzwa. Hivyo, kila mwaka watu 45 000 hivi hugunduliwa kuwa wameambukizwa ugonjwa huo. Yakadiriwa kwamba kwa sasa angalau watu 300 000 hadi 500 000 wameambukizwa ugonjwa huo.’ Ugonjwa huo huambukizwa na mbung’o, na ilidhaniwa kwamba ulikuwa umemalizwa katika miaka ya 1960. Maeneo yaliyo katika hatari kubwa ya kukumbwa na ugonjwa huo na yanayohitaji msaada wa kimataifa ni Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na upande wa kusini wa Sudan.

Wacheki Wakataa Dini

Takwimu zilizochapishwa na Idara ya Takwimu ya Jamhuri ya Cheki zaonyesha kwamba katika muda wa miaka kumi iliyopita, Wacheki wengi wamekataa dini. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 2001, ni Wacheki milioni 2.7 tu waliojitambulisha kuwa Wakatoliki, hali mnamo mwaka wa 1991 kulikuwa na Wakatoliki milioni 4 katika nchi hiyo. Katika kipindi hichohicho, asilimia 32 ya waumini wa Kanisa Protestanti waliacha kushirikiana na kanisa hilo na asilimia 46 ya waumini waliacha kushirikiana na Kanisa la Hus. Mbona watu hao waliacha dini? Muda mfupi baada ya kuanguka kwa Ukomunisti, Wacheki walijitambulisha bila hofu kuwa washiriki wa kanisa. Hata hivyo, siku hizi asilimia 60 hivi ya Wacheki hawafuati dini. Sasa Jamhuri ya Cheki, nchi ya Jan Hus, ambaye alijulikana sana kwa kuleta mabadiliko ya kidini, ni mojawapo ya nchi za Ulaya zenye watu wachache sana wanaofuata dini.

Maoni Mazuri Kuhusu Kazi Yanabadilika

Gazeti la The Futurist laripoti kwamba ‘asilimia 55 ya wakurugenzi wakuu waliohojiwa [huko Marekani] walisema kwamba kubadilika kwa maoni mazuri kuhusu kazi kutaathiri sana matokeo ya makampuni wakati ujao.’ Gazeti hilo lasema kwamba huenda hali hiyo ikasababishwa na mambo kadhaa. Mojawapo ya sababu hizo ni kwamba watoto fulani “waliona wazazi wao wakiachishwa kazi japo walikuwa wamefanya kazi kwa uaminifu.” Kwa sababu hiyo, watu wengi waliozaliwa kuanzia mwaka wa 1960 na kuendelea wameona kazi kuwa “njia ya kupata mahitaji yao: pesa, raha, na wasaa.” Makala hiyo yasema kwamba kwa sababu hiyo, “watu hawachochewi tena kufanya kazi kwa sababu ya mshahara mnono wala kwa sababu wana kazi ya kudumu.” Kuongezeka kwa zoea la kuchelewa kufika kazini na kutumia vibaya likizo ya ugonjwa ni mambo mawili yanayoonyesha jinsi ambavyo wafanyakazi wamebadili maoni yao mazuri kuhusu kazi.

Kutembelea Makaburi Kupitia Internet

Gazeti la The Japan Times laripoti kwamba sasa kituo fulani cha Internet kinawawezesha watu kutembelea makaburi ya mfano kwenye kompyuta. Marafiki na watu wa ukoo wanaweza kutembelea makaburi kupitia Internet. Picha ya bamba linalowekwa kwenye kaburi huonekana kwenye kompyuta pamoja na picha na maelezo mafupi kuhusu maisha ya mtu aliyekufa. Nafasi huachwa ili watu waandike ujumbe wao. Wabudha wanaweza kuacha matunda, maua, vijiti vya ubani, na vileo kwenye makaburi hayo ya mfano kwa kubonyeza kipanya cha kompyuta. Tadashi Watanabe, msimamizi wa kampuni hiyo inayotoa huduma za mazishi kwenye Internet, asema kwamba “watu fulani wanasema kuwa hiyo ni mbinu nzuri sana inayowasaidia watu wasioweza kutembelea makaburi mara nyingi, kama vile wale wanaoishi katika nchi ambayo iko mbali na kaburi.”

Onyo Kuhusu Aktiki

Gazeti la The Globe and Mail la Kanada lasema hivi: ‘Kufikia katikati ya karne hii, asilimia 80 ya eneo la Aktiki litaharibiwa sana iwapo viwanda vitaendelea kuongezeka huko.’ Ripoti moja ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Mazingira yasema kuhusu athari nyingi zinazoletwa na maendeleo ya wanadamu katika eneo la Aktiki. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, iwapo maendeleo ya kiviwanda yataendelea kwa kiwango kilekile kama ilivyotukia kutoka mwaka wa 1940 hadi 1990, matokeo yatakuwa mabaya sana. Inasemekana kwamba uharibifu huo unaweza kusambaa kwenye maeneo mengine pia, kwani wanyama wengi wa eneo hilo huhamahama. Gazeti hilo lasema kwamba “tayari kati ya asilimia 10 hadi 15 ya eneo la kaskazini ya dunia limeathiriwa [vibaya sana] na maendeleo ya kiviwanda.”

Watoto Wanene Kupita Kiasi Waongezeka

Gazeti la The Times la London lilisema hivi lilipokuwa likizungumzia uchunguzi wa hivi majuzi uliochapishwa katika jarida la British Medical Journal: ‘Idadi ya watoto wanene kupita kiasi imeongezeka kwa karibu mara mbili katika miaka kumi iliyopita. Mtoto mmoja au zaidi kati ya watoto watano walio chini ya umri wa miaka minne ni mzito kupita kiasi, na mtoto mmoja kati ya kila watoto kumi ni mnene kupita kiasi.’ Dakt. Peter Bundred wa Chuo Kikuu cha Liverpool asema kwamba akina mama wengi huwapa watoto wao “vyakula vinavyonunuliwa vikiwa tayari, vilivyo na mafuta mengi sana,” na kuwatumbuiza kwa kuwaachilia watazame televisheni. Wengi wa watoto hao wanapofikisha umri wa kwenda shuleni, wao hupelekwa shuleni kwa gari badala ya kutembea na baada ya shule wao hutazama televisheni badala ya kucheza nje. Bundred asema hivi: “Hii ndiyo mara ya kwanza ambapo tumeona watoto wa kila umri wakinenepa haraka.”

Haki ya Kukubali Baada ya Kuarifiwa

Miaka kumi baada ya kutoa tangazo la kwanza mnamo Januari 1991, Wizara ya Afya ya Italia imetangaza tena kwamba mgonjwa hapaswi kutiwa damu kabla ya kuarifiwa yanayohusika na kukubali jambo hilo. Tangazo hilo, la Januari 25, 2001, lililochapishwa katika Gazetta Ufficiale della Repubblica Italiana (Gazeti Rasmi la Jamhuri ya Italia), lasema hivi: “Mgonjwa anapoarifiwa kwamba huenda akapatwa na madhara kwa kutiwa damu au visehemu vya damu na/au vitu vilivyotolewa katika damu, anapaswa kuandika iwapo amekataa au kukubali kabla ya kupewa matibabu hayo.”

Wanawake Wajawazito Wanapigwa

Gazeti la The Independent la London lasema kwamba ‘wanawake wajawazito na watoto wao huathiriwa sana wanapopigwa na wapenzi wao kuliko wanavyoathiriwa na magonjwa yanayotokea wakati wa kipindi cha ujauzito.’ Uchunguzi uliofanywa na Chuo cha Royal cha Madaktari wa Uzazi kuhusu ujeuri nyumbani ulionyesha kwamba theluthi moja ya visa vya kupigwa kwa wanawake vilianza walipokuwa wajawazito. Uthibitisho unaendelea kuonyesha kwamba wanaume fulani huwa wajeuri kwa sababu ya kumwonea wivu mtoto anayetarajiwa.’ Profesa James Drife wa Chuo cha Royal cha Madaktari wa Uzazi alisema kwamba ‘walistaajabishwa sana walipoona idadi ya wanawake wajawazito waliopigwa huko Uingereza.’ Uchunguzi kama huo huko Marekani ulionyesha kwamba kati ya wanawake watano wajawazito wanaokufa, mmoja huuawa. Hivyo, “kisababishi kikuu cha vifo vya wanawake wajawazito [huko] ni mauaji.”