Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuwachunguza Wanyama-Pori

Kuwachunguza Wanyama-Pori

Kuwachunguza Wanyama-Pori

HEBU wazia kwamba kifaa kidogo cha kurusha ishara za redio kimewekwa kwenye mgongo wako. Kila unapotembea, kifaa hicho kinawawezesha watu kuchunguza na kuchanganua mwendo wako. Kifaa kama hicho kimewekwa kwenye mgongo wa ndege aina ya wandering albatross anayeitwa Bi. Gibson. Kifaa hicho kidogo huwawezesha watafiti kumchunguza ndege huyo kwa setilaiti zinazopokea ishara zake—na za ndege wengine waliowekwa vifaa hivyo—na kuzirusha tena duniani. Habari zilizopatikana zimefunua mambo ya kushangaza kuhusu ndege hao wenye fahari, na inatumainiwa kwamba habari hizo zitasaidia kuhifadhi ndege hao.

Ripoti moja ya Chuo Kikuu cha La Trobe huko Victoria, Australia, ilisema kwamba watafiti waligundua kuwa ndege hao husafiri kilometa 300 kila siku kwa wastani, na mara kwa mara wao husafiri zaidi ya kilometa 1,000 kwa siku. Ndege hao wana mabawa mapana zaidi kati ya ndege wote ulimwenguni. Mabawa hayo yana upana wa zaidi ya sentimeta 340 kutoka ncha ya ubawa mmoja hadi ncha ya ule mwingine, nayo huwawezesha kuruka juu ya bahari na kusafiri zaidi ya kilometa 30,000 kwa muda wa miezi kadhaa. Uchunguzi kama huo huko Marekani umefunua kwamba ndege aina ya Laysan albatross alisafiri mara nne kutoka Kisiwa cha Tern, kilichoko kaskazini-magharibi ya Honolulu, hadi kwenye Visiwa vya Aleutian—safari ya kilometa 6,000 kwenda na kurudi—ili kutafutia kinda lake la pekee chakula.

Uchunguzi huo mbalimbali uliofanywa kwa kutumia tekinolojia ya hali ya juu umeonyesha ni kwa nini idadi ya ndege wa kike wa wandering albatross imepungua sana kuliko ile ya ndege wa kiume. Iligunduliwa kwamba ndege wa kiume wazalishaji waliwinda samaki karibu na Antaktiki. Ndege wa kike wazalishaji waliwinda upande wa kaskazini zaidi, katika eneo lenye meli za kuvua samaki. Ndege hao walirukia vyambo vilivyovutwa na meli hizo, kisha wakanaswa, na kuzama. Katika makundi fulani ya ndege wazalishaji, idadi ya ndege wa kiume ni mara mbili ya ile ya ndege wa kike. Aina nyingine za albatross zimeathiriwa pia. Katikati ya miaka ya 1990, ndege wapatao 50,000 walikufa kila mwaka nyuma ya meli za kuvua katika bahari za New Zealand. Hivyo, aina nyingi zilikuwa katika hatari ya kutoweka kabisa. Hata imesemwa kuwa ndege wa wandering albatross yumo katika hatari ya kutoweka kabisa huko Australia. Ugunduzi huo umeleta mabadiliko fulani katika mbinu za uvuvi na umepunguza vifo vya ndege wa wandering albatross. Hata hivyo, ndege hao wameendelea kupungua katika maeneo fulani makuu ya kuzalishia.

Kuwafunga Ndege Ukanda

Ijapokuwa vifaa vidogo vya elektroniki vinawasaidia watafiti kuchunguza aina fulani za ndege, mbinu rahisi zaidi na za bei nafuu zimetumiwa kwa miaka mingi. Mbinu moja ni ile ya kuwafunga ndege ukanda. Ndege hufungwa ukanda mdogo wa metali au plastiki kwenye mguu wake kwa uangalifu. Ukanda huo ni kama kibangili kinachofungwa mguuni.

Gazeti la Smithsonian linasema kwamba mbinu ya kuwafunga ndege ukanda ilianza kutumiwa rasmi katika uchunguzi mnamo 1899, wakati mwalimu mmoja wa Denmark, Hans Christian Mortensen, “alipounda kanda zake za metali, na kuziandika jina lake na anwani yake na kisha kuzifungilia kwenye makinda 165 ya kwezi.” Siku hizi, mbinu ya kuwafunga ndege ukanda hutumiwa katika nchi mbalimbali na huwezesha habari muhimu zipatikane kuhusu idadi ya ndege wa aina fulani katika maeneo fulani, kuhamahama kwao, tabia zao, namna wanavyoishi, idadi yao, na idadi ya ndege wanaokufa na wanaozaliwa. Katika maeneo ambako uwindaji unaruhusiwa, mbinu ya kuwafunga ndege ukanda huwezesha serikali kutunga sheria za kuhifadhi ndege wanaowindwa. Mbinu hiyo pia huonyesha jinsi ndege wanavyoathiriwa na magonjwa na kemikali zenye sumu. Ndege fulani wanaweza kuwa na magonjwa ya wanadamu, kama vile uvimbe wa ubongo na ugonjwa wa Lyme. Hivyo, habari kuhusu maumbile na tabia za ndege hao zaweza kutumiwa kulinda afya yetu.

Je, Kuwafunga Ndege Ukanda Ni Ukatili?

Katika nchi ambako ndege hufungwa ukanda, kuna kanuni zinazodhibiti utendaji huo, na wale wanaofanya kazi hiyo hupaswa kuwa na leseni. Shirika la Kuhifadhi Viumbe la Australia lasema kwamba huko Australia, ‘watu wanaowafunga ndege ukanda huzoezwa kikamili jinsi ya kuwakamata na kuwafunga ndege bila kuwajeruhi. Kwa kawaida wao huzoezwa kwa miaka miwili na hufanya mazoezi mengi.’ Kuna sheria kama hizo pia huko Ulaya, Kanada, Marekani, na katika nchi nyinginezo.

Kanda zinazotumiwa huwa na umbo, ukubwa, na rangi mbalimbali na hutengenezwa kwa vifaa tofauti-tofauti. Kanda nyingi hutengenezwa kwa alumini au plastiki, lakini ndege wanaoishi kwa muda mrefu au wale wanaokaa katika maeneo yenye maji ya chumvi hufungwa kanda za feleji isiyoshika kutu au kanda zilizotengenezwa kwa vifaa vingine visivyoathiriwa na kutu. Kanda zenye rangi mbalimbali hufanya iwe rahisi kuwatambua ndege kutoka mbali. Ijapokuwa ndege hufungwa kanda kadhaa, hawahitaji tena kukamatwa ili watambuliwe.

Watafiti wanazingatia sana kwamba, mbinu yoyote ya kuwatambulisha ndege hao isiwasumbue wala kuathiri tabia yao, miili yao, muda wa kuishi, uhusiano na ndege wengine, mazingira yao, au kuhatarisha maisha yao. Kwa mfano, kitambulisho chenye rangi nyangavu kilichowekwa kwenye ubawa chaweza kufanya ndege aonekane wazi na adui au kuathiri kujamiiana kwake. Aina fulani za ndege hunya kwenye miguu yao, hivyo kuwafunga ndege hao ukanda kwaweza kutokeza maambukizo. Katika maeneo yenye baridi, barafu yaweza kugandamana kwenye kanda na kusababisha hatari, hasa kwa ndege wa majini. Hayo ni baadhi tu ya mambo yanayohusika katika kuwapa ndege kitambulisho. Lakini bado yanaonyesha kwamba ujuzi mwingi wa kisayansi kuhusu maumbile ya ndege unahitajiwa ili mradi huo ufue dafu, na wakati huohuo usiwadhuru ndege.

Vipi Ukimpata Mnyama Aliye na Ukanda au Kitambulisho?

Nyakati nyingine kanda au vitambulisho vyaweza kuwa na namba ya simu au anwani, hivyo unaweza kuwasiliana na mtu anayemiliki mnyama huyo au kituo kinachoshughulikia vitambulisho hivyo. * Hivyo, unaweza kumweleza mtu anayemiliki mnyama huyo wakati na mahala ambapo ulipata kitambulisho hicho na labda pia habari zaidi. Kwa mfano, kama ni samaki, habari hizo zaweza kumsaidia mwanabiolojia kujua umbali na mwendo ambao samaki huyo amesafiri tangu alipowekwa kitambulisho na kuachiliwa huru.

Kutokana na kazi ya watafiti ulimwenguni pote na jitihada za watu wanaojali ambao huripoti vitambulisho na kanda wanazopata, habari za kushangaza kuhusu wanyama-pori zinagunduliwa. Kwa mfano, mfikirie ndege mmoja aina ya chamchanga anayeitwa red knot. Ndege huyo ana uzani wa gramu 100 hadi 200. Sasa wanasayansi wamegundua kwamba kila mwaka ndege wengine wa red knot huhama kutoka kaskazini kabisa mwa Kanada hadi kwenye ncha ya Amerika Kusini na kisha kurudi. Huo ni umbali wa kilometa 30,000 hivi!

Ukanda uliokuwa kwenye mguu wa ndege mmoja red knot aliyekuwa mzee lakini mwenye afya, ulifunua kwamba huenda ikawa alikuwa akisafiri umbali huo kwa miaka 15. Naam, huenda ndege huyo mdogo alikuwa amesafiri umbali wa kilometa 400,000—mbali zaidi kuliko umbali wa wastani kutoka duniani hadi mwezini! Mwandishi wa mambo ya mazingira Scott Weidensaul alisema hivi huku akimshika ndege huyo mdogo sana wa kustaajabisha: ‘Nimeshangazwa na kustaajabishwa sana, nami ninawaheshimu ndege hao wanaosafiri kotekote katika dunia hii kubwa.’ Kwa kweli, kadiri tunavyojua mengi zaidi kuhusu viumbe wa dunia, ndivyo tunavyozidi kumhofu na kumheshimu yule “Aliyezifanya mbingu na nchi . . . na vitu vyote vilivyomo,” Yehova Mungu.—Zaburi 146:5, 6.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 13 Kanda au vitambulisho vyaweza kuchakaa sana hivi kwamba habari zilizoandikwa hazisomeki. Hata hivyo, habari hizo zaweza kusomeka kwa kutumia asidi maalumu. Kila mwaka, Maabara ya Kufunga Ndege Ukanda huko Marekani husoma mamia ya kanda zisizosomeka kwa kutumia njia hiyo.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

NJIA ZA KUWATAMBULISHA NA KUWACHUNGUZA WANYAMA

Mbali na ndege, kuna viumbe wengi wanaotiwa alama ili wachunguzwe. Mbinu zinazotumiwa kutia alama hutegemea malengo ya wanasayansi na pia miili na tabia za wanyama wanaohusika. Zaidi ya kutumia kanda za kufungwa mguuni, watafiti hutumia vibandiko vidogo, tepe zenye bendera ndefu nyembamba, vitambulisho, rangi, michoro kwenye ngozi, alama zinazowekwa kwa chuma chenye moto, kanda za shingo, vifaa vya kurusha ishara za redio, kompyuta ndogondogo, vishale vidogo visivyoshika kutu (vilivyo na vitambulisho vyenye rangi mbalimbali), kukata kipande cha kidole kikubwa cha mguu, sikio, na mkia, na mbinu na vifaa vinginevyo. Baadhi ya mbinu na vifaa hivyo havigharimu pesa nyingi lakini vingine ni ghali sana. Kwa mfano, kuna kifaa kimoja cha elektroniki chenye kamera ndogo ya video kinachogharimu dola 15,000 za Marekani na hutumiwa kuchunguza jinsi sili wanavyopiga mbizi.

Kifaa kimoja cha elektroniki chaweza kuingizwa ndani ya ngozi au mwili wa mnyama aliyepewa dawa ya kulala na kisha kifaa kingine maalumu kilichoko nje ya mwili wake hupokea habari hizo. Ili kumchunguza tuna wa bluefin, wanasayansi huingiza kompyuta ndogo ndani ya samaki huyo. Kwa muda wa miaka tisa, kompyuta hizo ndogo hukusanya na kuhifadhi habari kuhusu halijoto, kina ambacho samaki huyo amesafiri, kiasi cha mwangaza, na wakati. Kompyuta hiyo inapotolewa, habari nyingi hupatikana, kutia ndani umbali ambao samaki huyo amesafiri. Umbali huo waweza kuhesabiwa kwa kulinganisha vipimo vya kila siku vya mwangaza wa mchana na vipimo vya wakati.

Nyoka wanaweza kutiwa alama kwa kukata magamba fulani ya ngozi yao; kasa wanaweza kutiwa alama kwenye gamba lao; mijusi wanaweza kutiwa alama kwa kukata sehemu fulani ya kidole kikubwa cha mguu; na mamba wanaweza kutiwa alama ama kwa kukata kidole kikubwa cha mguu au kwa kuondoa magamba fulani magumu kwenye mikia yao. Wanyama fulani wana maumbile yanayowatofautisha wazi hivi kwamba ni rahisi kuwatambua kwa picha.

[Picha]

Dubu mweusi anawekwa kitambulisho kwenye masikio; samaki wa mtambo-bunduki amewekwa kitambulisho kinachofanana na spageti; vitambulisho kwenye mikia ya mamba wa Marekani

Kozi-kipanga amewekwa kifaa cha kurusha ishara za redio kwenye setilaiti

Kifaa cha kupima umbali kimewekwa ndani ya trauti wa “rainbow”

[Hisani]

Dubu: © Glenn Oliver/Visuals Unlimited; mtambo-bunduki: Dr. James P. McVey, NOAA Sea Grant Program; mamba wa Marekani: Copyright © 2001 by Kent A. Vliet; kozi aliyeonyeshwa kwenye ukurasa wa 2 na 15: Photo by National Park Service; watu waliobeba samaki: © Bill Banaszewski/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 13]

Mwewe wa “sharp-shinned” anafungwa ukanda

[Hisani]

© Jane McAlonan/Visuals Unlimited