Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mmea Duni Lakini Tata

Mmea Duni Lakini Tata

Mmea Duni Lakini Tata

Dhana ya mageuzi ya kikemikali husema kwamba mabilioni ya miaka iliyopita, uhai ulianzishwa duniani na utendaji wa ghafula wa kemikali.

Dhana hiyo haikukusudiwa kuonyesha kwamba ndege, wanyama watambaazi, au viumbe wengine tata walitokea wenyewe tu. Badala yake, inasemekana kwamba utendaji wa ghafula wa kemikali ulitokeza viumbe na mimea duni sana kama vile mwani na viumbe wengine wenye chembe moja.

Kutokana na yale yanayojulikana kuhusu viumbe hao wenye chembe moja, je, ni jambo la akili kudai kwamba mimea hiyo ni duni sana hivi kwamba ilitokea tu kwa ghafula? Kwa mfano, je, ni kweli kwamba mwani wenye chembe moja ni mmea duni? Acheni tuchunguze aina moja ya mwani. Huo ni mwani aina ya Dunaliella unaoainishwa katika jamii ya mwani wa Volvocales. Mwani huo una rangi ya kijani-kibichi na una chembe moja.

Mimea ya Kipekee Yenye Chembe Moja

Chembe za miani ya Dunaliella zina umbo la yai na ni ndogo sana—zina urefu wa mikroni kumi hivi. Chembe 1,000 zikiunganishwa pamoja ncha hadi ncha zitafikia urefu wa sentimeta moja. Kwenye ncha moja ya kila chembe kuna nyuzi mbili zinazofanana na kamba za mijeledi. Nyuzi hizo huwezesha miani hiyo kuogelea. Chembe za Dunaliella huwa kama chembe za mimea na hutengeneza nishati kupitia usanidimwanga. Chembe hizo hufanyiza chakula kwa kutumia kaboni dayoksaidi, madini, na virutubishi vingine vinavyofyonzwa ndani ya chembe, nazo huongezeka zinapojigawanya.

Miani hiyo inaweza kusitawi hata katika maji yaliyojaa chumvi. Miani hiyo ni mojawapo ya vitu vichache vinavyoweza kusitawi na kuongezeka katika Bahari ya Chumvi. Kiasi cha chumvi kilichomo ndani ya bahari hiyo ni mara nane ya kiasi cha chumvi kilichomo katika bahari nyingine. Mimea hiyo inayosemwa kuwa duni, inaweza pia kusitawi wakati chumvi inapoongezeka au kupungua kwa ghafula.

Kwa mfano, fikiria mwani wa Dunaliella bardawil, unaopatikana katika maji ya chumvi katika jangwa la Sinai. Wakati wa dhoruba ya mvua, chumvi hupungua katika maji hayo. Na wakati jua kali linapovukiza maji, chumvi nyingi sana huwepo majini. Lakini mmea huo huendelea kusitawi wakati wa mabadiliko hayo kwa sababu unaweza kutokeza na kurundika gliserini kwa kadiri inayofaa. Mwani wa Dunaliella bardawil unaweza kutokeza gliserini haraka sana mara tu baada ya kiasi cha chumvi kubadilika. Mwani huo huongeza au kupunguza gliserini ili kuiweza hali hiyo. Jambo hilo ni muhimu kwani katika maeneo fulani, kiasi cha chumvi chaweza kubadilika sana baada ya muda wa saa chache tu.

Mwani wa Dunaliella bardawil huchomwa na jua kali sana kwa sababu unapatikana katika maji yenye kina kifupi jangwani. Rangi fulani ya asili ndani ya chembe huilinda dhidi ya joto hilo ambalo linaweza kuiharibu. Mwani wa Dunaliella huwa na rangi nyangavu ya kijani-kibichi wakati unapopandwa katika eneo lenye virutubishi, kama katika eneo lenye nitrojeni ya kutosha. Katika hali hiyo, mmea huo huwa na rangi ya asili ya kijani-kibichi ambayo hulinda chembe. Nitrojeni inapopungua na kunapokuwa na ongezeko la chumvi, halijoto, na mwangaza, rangi ya mmea huo wa kijani-kibichi hubadilika na kuwa rangi ya machungwa au nyekundu. Kwa nini? Katika mazingira hayo magumu, utendaji fulani tata wa kemikali hutokea. Ile rangi ya kijani-kibichi hupungua sana, na rangi nyingine ya asili, inayoitwa beta-carotene, hutokezwa. Chembe ingekufa iwapo haingeweza kutokeza rangi hiyo ya asili. Rangi hubadilika kwa sababu beta-carotene hutokezwa kwa wingi hivi kwamba inafanyiza asilimia 10 ya uzani wa mwani.

Huko Marekani na Australia, mwani wa Dunaliella umepandwa katika vidimbwi vikubwa ili kutokeza beta-carotene inayouzwa kwa minajili ya kutumiwa katika lishe. Kwa mfano, kuna vidimbwi vikubwa katika eneo la kusini na magharibi mwa Australia. Beta-carotene yaweza pia kutengenezwa viwandani. Hata hivyo, ni makampuni mawili tu yaliyo na mitambo tata na ya bei ghali inayoweza kutengeneza beta-carotene kwa wingi. Wanadamu wametumia miaka mingi na pesa nyingi wakifanya utafiti na kubuni mitambo ya kutengeneza beta-carotene, lakini mwani wa Dunaliella unaweza kuitokeza kwa urahisi sana. Ijapokuwa ni mdogo sana hivi kwamba hauonekani kwa macho, mwani huo duni hutokeza rangi hiyo mara tu mazingira yanapobadilika.

Jambo jingine la kustaajabisha kuhusu mwani wa Dunaliella linaonekana katika mwani aina ya Dunaliella acidophila, ambao ulipatikana kwa mara ya kwanza mnamo mwaka wa 1963 katika chemchemi na udongo wenye salfa yenye asidi. Maeneo hayo yalikuwa na asidi sulfuriki kali sana. Uchunguzi uliofanywa kwenye maabara umeonyesha kwamba aina hiyo ya Dunaliella inaweza kusitawi katika umajimaji wenye asidi sulfuriki. Ukali wa asidi hiyo unazidi ule wa limau kwa mara 100. Mwani wa Dunaliella bardawil unaweza pia kusitawi katika mazingira yenye chumvi nyingi sana. Mambo hayo yanaonyesha jinsi mwani wa Dunaliella unavyoweza kubadilika sana kulingana na mazingira.

Mambo Kadhaa ya Kufikiria

Mwani wa Dunaliella una sifa za kustaajabisha. Hata hivyo, hayo ni baadhi tu ya mambo yanayowezesha viumbe na mimea yenye chembe moja kudumu na kusitawi katika mazingira yanayobadilika na nyakati nyingine yaliyo magumu. Sifa hizo huwezesha mwani wa Dunaliella kusitawi, kufyonza chakula kinachofaa, kuchuja vitu hatari, kuondoa taka, kuepuka au kushinda magonjwa, kukinza hatari, kuongezeka, na kadhalika. Wanadamu hutumia chembe trilioni 100 hivi kufanya mambo hayo!

Basi, je, ni jambo la busara kusema kwamba mwani huo wenye chembe moja ni mmea duni tu, usio na maana, na kwamba eti ulitokea tu kutokana na asidi amino chache zilizokuwa katika umajimaji wenye uhai? Je, ni jambo la akili kusema kwamba mimea hiyo yenye kustaajabisha ilitokea tu? Ni jambo la akili kukubali kwamba mimea na viumbe wote walifanyizwa na Mbuni stadi aliyeumba uhai kwa kusudi fulani. Akili na ufundi wa aina hiyo, ambao hatuwezi kuuelewa kikamili, ulihitajika ili kuumba viumbe na mimea tata ambayo hutegemeana.

Kuchunguza Biblia kwa uangalifu, bila kutia ndani maoni ya kidini na ya kisayansi, hutoa majibu yenye kuridhisha kuhusu chanzo cha uhai. Mamilioni ya watu, kutia ndani wengi waliojifunza sayansi, wameboresha maisha yao kwa kufanya uchunguzi huo. *

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 15 Twawatia moyo wasomaji wetu wachunguze vichapo hivi, Je, Kuna Muumba Anayekujali? na Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation?, vilivyochapishwa na Mashahidi wa Yehova.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Kushoto kabisa: Kutokeza “beta-carotene” kwa ajili ya biashara kwa kutumia mwani wa “Dunaliella”

Kushoto: Mwani wa “Dunaliella” wenye rangi ya machungwa na kiasi kikubwa cha “beta-carotene” umeonyeshwa kwa kipimo kikubwa

[Hisani]

▼ © AquaCarotene Limited (www.aquacarotene.com) ▸

[Picha katika ukurasa wa 26]

“Dunaliella”

[Hisani]

© F. J. Post/Visuals Unlimited

[Picha katika ukurasa wa 27]

Picha ya hadubini yaonyesha kiini (N), kloroplasti (C), na “Golgi” (G)

[Hisani]

Image from www.cimc.cornell.edu/Pages/ dunaLTSEM.htm. Used with permission