Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mwangaza Hutokeza Usingizi Mtamu

Mwangaza Hutokeza Usingizi Mtamu

Mwangaza Hutokeza Usingizi Mtamu

JE, WEWE hukosa usingizi? Hasa ikiwa wewe ni mzee, huenda tatizo likawa kwamba hupati mwangaza wa kutosha mchana. Hivi majuzi, watafiti huko Japani walifanya uchunguzi kuhusu wazee wanaokosa usingizi katika makao ya kuwatunza wazee, na wakagundua kwamba wazee hao walikosa usingizi kwa sababu ya kutopata mwangaza wa kutosha kila siku. Wakati huohuo, vipimo vya damu vilionyesha kwamba wazee hao walikuwa na kiasi kidogo cha homoni inayoitwa melatonin.

Homoni ya melatonin hutokezwa na tezi fulani yenye umbo la pia ubongoni. Ripoti moja ya jarida la The Journal of Clinical Endocrinology & Metabolism ilisema kwamba katika hali za kawaida, utaratibu wa kila siku wa kutokeza melatonin hufanya kiasi chake katika damu kuwa ‘kingi sana wakati wa usiku na kidogo sana wakati wa mchana.’ Hata hivyo, wazee wasipopata mwangaza wa kutosha mchana, kiasi cha melatonin katika damu hupungua. Yaonekana kwamba mwili hushindwa kutambua kati ya mchana na usiku, na watafiti wanaonelea kwamba jambo hilo huathiri usingizi.

Ripoti hiyo yasema kwamba wazee wanaokosa usingizi walipopelekwa mahala penye mwangaza fulani karibu na wakati wa adhuhuri kwa muda wa saa nne (kutoka saa nne hadi saa sita na kutoka saa nane hadi saa kumi) kwa kipindi cha majuma manne, homoni ya melatonin iliongezeka “kufikia kiasi kile cha vijana waliochunguzwa.” * Na wazee hao walipata usingizi mtamu zaidi.

Kutokana na matokeo ya uchunguzi huo, watafiti “walionelea kwamba wazee, hasa wazee wanaokosa usingizi, wanapokaa tu ndani ya nyumba kila siku, hawapati mwangaza wa kutosha kuuwezesha mwili kubadilikana kulingana na wakati.” Kwa kuwa wazee fulani hutumia vidonge fulani vya melatonin ili kuwasaidia kupata usingizi, ripoti hiyo yasema hivi: ‘Kwa kuzingatia athari za kutumia vidonge vya melatonin kwa muda mrefu, kuota jua la adhuhuri kwaweza kuwa njia bora ya kujitibu, yenye matokeo, na iliyo salama kwa wazee hao wanaokosa usingizi kwa sababu ya upungufu wa homoni ya melatonin.’

Basi iwapo wewe hukaa ndani ya jengo kwa muda mrefu na hukosa usingizi, jaribu kukaa nje kwa vipindi virefu zaidi—au angalau uruhusu mwangaza wa kutosha uingie nyumbani mwako wakati wa mchana, na ufanye chumba cha kulala kiwe na giza wakati wa usiku. Utagundua kwamba mwangaza hutokeza usingizi mtamu.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Uchunguzi huo ulitia ndani vikundi viwili: vijana kumi na wazee kumi wenye afya bora wanaokaa katika makao hayo pamoja na wazee hao wanaokosa usingizi.