Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Tetemeko la Ardhi

Tetemeko la Ardhi

Tetemeko la Ardhi

‘TUMEZOEA KUISHI KATIKA DUNIA ILIYO IMARA HIVI KWAMBA DUNIA INAPOANZA KUTIKISIKA TUNABABAIKA SANA.’—“THE VIOLENT EARTH.”

“Kichapo The World Book Encyclopedia chasema kwamba ‘matetemeko ya ardhi ni mojawapo ya matukio yenye kusababisha uharibifu mkubwa zaidi ulimwenguni.’ Maneno hayo ni ya kweli kabisa, kwani nishati ya tetemeko kubwa la ardhi yaweza kuwa mara 10,000 zaidi ya ile ya bomu la kwanza la nyukilia! Jambo hilo linaogopesha hata zaidi kwa kuwa matetemeko hayo yanaweza kutokea katika tabia yoyote ya nchi, msimu wowote, na saa zozote. Na ijapo wanasayansi wanaweza kujua kwa kadiri fulani mahala ambapo matetemeko yenye nguvu yatatokea, hawawezi kutabiri yatatokea lini.

Matetemeko ya ardhi hutokea kwa sababu ya kusonga kwa miamba mikubwa ambayo iko chini ya uso wa dunia. Miamba hiyo husonga daima. Mara nyingi, mawimbi ya tetemeko la ardhi ambayo hutokea huwa dhaifu sana hivi kwamba hayawezi kutambuliwa waziwazi kwenye uso wa dunia, lakini yanaweza kutambuliwa na kurekodiwa na kipima-tetemeko. * Nyakati nyingine, miamba mingi huvunjika na kusongasonga kiasi cha kutetemesha ardhi sana.

Lakini kwa nini miamba hiyo huendelea kusongasonga? ‘Jibu laweza kupatikana katika ile dhana kuhusu mabamba yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia. Dhana hiyo imebadili kabisa maoni ya wanasayansi kuhusu dunia,’ chasema Kituo cha Taifa cha Habari za Matetemeko ya Ardhi (NEIC). ‘Sasa tunajua kwamba kuna mabamba saba makubwa yaliyo kwenye tabaka la nje la dunia ambayo yamegawanyika katika mabamba madogo-madogo. Mabamba yote hayo husonga daima na kwa wakati mmoja. Yanaweza kusonga umbali wa milimeta 10 hadi 130 kila mwaka.’ Kituo cha NEIC chasema kwamba matetemeko mengi ya ardhi hutokea kwenye maeneo membamba ambako mabamba hayo yametengana. Yaelekea asilimia 90 ya matetemeko makubwa ya ardhi hutokea katika maeneo hayo.

Ukubwa na Kiwango

Tetemeko la ardhi laweza kupimwa kulingana na ukubwa au kiwango chake. Katika miaka ya 1930, Charles Richter alibuni kipimo cha kuonyesha ukubwa wa matetemeko ya ardhi. Wakati vituo vya kupima matetemeko ya ardhi vilipoongezeka, vipimo vipya vilibuniwa kwa kutumia uvumbuzi wa Richter. Kwa mfano, kipimo cha nguvu za tetemeko la ardhi huonyesha kiasi cha nishati inayotokezwa kwenye chanzo cha tetemeko la ardhi.

Kwa wazi, nyakati nyingine vipimo hivyo havilingani na uharibifu uliosababishwa na tetemeko la ardhi. Kwa mfano, fikiria tetemeko la ardhi lililotokea kaskazini mwa Bolivia mnamo Juni 1994. Tetemeko hilo lilikuwa na ukubwa wa 8.2 kwenye kipimo cha Richter na yaripotiwa kwamba watu watano tu walikufa. Lakini, mamia ya maelfu ya watu walikufa katika tetemeko la ardhi lililotokea mwaka wa 1976 huko Tangshan, China, ambalo lilikuwa na ukubwa wa 8.0!

Tofauti na kipimo cha ukubwa, kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha jinsi linavyoathiri watu, majengo, na mazingira. Kiwango cha tetemeko la ardhi huonyesha waziwazi hasa jinsi wanadamu wanavyoathiriwa sana nalo. Kwa hakika, matetemeko hayawajeruhi watu moja kwa moja. Badala yake, majeraha na vifo husababishwa na kuta zinazoanguka, mabomba ya gesi yanayolipuka, nyaya za nguvu za umeme zinazokatika, vitu vinavyoporomoka, na kadhalika.

Lengo moja la wataalamu wa matetemeko ni kutoa maonyo kuhusu matetemeko ya ardhi mapema. Programu ya kompyuta inayoitwa Mfumo wa Hali ya Juu wa Kuchunguza Matetemeko ya Ardhi inatayarishwa. Ripoti moja ya shirika la habari la CNN ilisema kwamba programu hiyo, pamoja na uwezo wa kupata habari haraka na pia programu nyingine tata za kompyuta, zitawasaidia wataalamu “kuweza kutambua mara moja mahala ambapo mtikisiko mkubwa wa tetemeko la ardhi umetokea.” Hivyo, jambo hilo litawasaidia wenye mamlaka kutuma msaada kwenye maeneo yaliyokumbwa na msiba.

Pasipo shaka, watu wanapotazamia tetemeko la ardhi wanaweza kupunguza majeraha, uharibifu wa mali na—zaidi ya yote—kuokoa uhai. Hata hivyo, matetemeko ya ardhi yanaendelea kutokea. Hivyo, swali hili lazuka: Watu wamesaidiwaje kukabiliana na hasara?

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Kipima-tetemeko ni chombo kinachopima na kurekodi mtikisiko wa ardhi wakati tetemeko la ardhi linapotokea. Kipima-tetemeko cha kwanza kilibuniwa mwaka wa 1890. Siku hizi kuna vituo zaidi ya 4,000 ulimwenguni pote vinavyopima matetemeko ya ardhi.

[Chati katika ukurasa wa 5]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Idadi ya Matetemeko ya Ardhi

Kionyeshi Ukubwa Wastani wa Kila Mwaka

Kubwa Zaidi 8 na zaidi 1

Kubwa 7-7.9 18

Lenye Nguvu 6-6.9 120

La Kadiri 5-5.9 800

Nguvu Kidogo 4-4.9 6,200*

Dogo 3-3.9 49,000*

Dogo Sana Chini ya 3 Ukubwa wa 2-3:

karibu 1,000 kila siku

Ukubwa wa 1-2:

karibu 8,000 kila siku

* Imekadiriwa.

[Hisani]

Chanzo: National Earthquake Information Center By permission of USGS/National Earthquake Information Center, USA

[Picha katika ukurasa wa 5 zimeandaliwa na]

Mistari inayorekodiwa na kipima-tetemeko kwenye ukurasa wa 4 na 5: Figure courtesy of the Berkeley Seismological Laboratory