Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Zabibu Zilizoganda Zinazotokeza “Divai ya Dhahabu”

Zabibu Zilizoganda Zinazotokeza “Divai ya Dhahabu”

Zabibu Zilizoganda Zinazotokeza “Divai ya Dhahabu”

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KANADA

Ni wakati wa baridi kali katika eneo la Kanada la Niagara. Wafanyakazi wenye ujasiri wanakabiliana na baridi ya siku hiyo wanapoenda kwenye mashamba ya mizabibu. Pepo baridi zaweza kufanya halijoto ionekane kuwa kama nyuzi 40 Selsiasi chini ya kiwango cha kuganda. Mbona wavunaji hao wanataka kutembea katika halihewa mbaya ili kukusanya zabibu zilizoganda na zilizo ngumu kama gololi? Ni kwa sababu divai tamu sana yenye rangi ya dhahabu hutengenezwa kwa zabibu hizo zilizonyauka—divai ya barafu.

Kupima Wakati na Halijoto kwa Njia Barabara

Mwandishi Mmarekani Mark Twain alisema kwamba hakuna “mbuni mkubwa” kama aksidenti. Mnamo mwaka wa 1794 huko Franconia, Ujerumani, watengenezaji wa divai walisaga na kukamua zabibu zilizoganda baada ya dhoruba ya theluji. Divai iliyotengenezwa kwa zabibu hizo ilikuwa na sukari nyingi. Lakini, kwa kuwa divai hiyo ilikuwa na asidi nyingi, sukari hiyo ilipunguka ifaavyo. Hata hivyo, ili divai ya barafu itengenezwe kila mwaka, watengenezaji wa divai hukabili magumu fulani. Ni lazima halijoto iwe chini ya nyuzi 7 Selsiasi chini ya kiwango cha kuganda kwa siku kadhaa ili umajimaji wa zabibu ugande ifaavyo. Umajimaji wa zabibu hauwi mtamu wakati zabibu zinapoyeyushwa ghafula. Kukiwa na baridi kali sana, zabibu hizo ngumu hazitatokeza umajimaji mwingi zinapokamuliwa. “Hiyo si kazi rahisi,” ndivyo anavyosema mtengenezaji mmoja wa divai huko Niagara. “Ni lazima kuwe na halijoto inayofaa kabisa.”

Tabia ya nchi kusini mwa Kanada, hasa katika eneo la Niagara, inafaa kabisa kwa utengenezaji wa divai ya barafu. Katikati ya miezi ya Novemba hadi Februari, halijoto huwa chini ya nyuzi 7 Selsiasi chini ya kiwango cha kuganda. Watengenezaji wa divai wamefanikiwa sana kutengeneza divai ya barafu kwa kutumia zabibu za Riesling na Vidal, japo zabibu za aina nyingine zimetumiwa pia. Ijapokuwa nchi nyingine pia hutengeneza divai ya barafu, Kanada ndiyo nchi inayotengeneza divai hiyo kwa wingi sana ulimwenguni na imeshinda tuzo kwenye mashindano kadhaa ya kimataifa ya divai.

Kwa Nini Divai Hiyo Ni Tamu Sana?

Divai ya barafu ni tamu sana kwa sababu umajimaji wa zabibu hizo huwa na sukari nyingi sana. Asilimia 80 ya tunda la zabibu huwa na maji. Zabibu huchumwa na kukamuliwa zikiwa zimeganda. Ni lazima watengenezaji wakamue zabibu hizo nje au waache mlango wa jengo la kukamulia likiwa wazi ili zabibu hizo zidumu zikiwa zimeganda. Kiasi kikubwa cha maji, ambayo huganda haraka kuliko sukari, huwa barafu. Hivyo, zabibu zilizoganda zinapokamuliwa, umajimaji unaopatikana huwa na sukari nyingi sana. Mwandishi mmoja wa makala maalum za magazeti alisema kwamba umajimaji huo ni “mtamu sana.”

Ijapokuwa Kanada huwa na majira ya baridi kali sana, Niagara iko kusini zaidi ya lile eneo maarufu la Burgundy huko Ufaransa. Hivyo, kwa kuwa eneo la Niagara huwa na jua kwa muda mrefu na joto kali katika mwezi wa Julai—wakati ambapo mizabibu husitawi sana—zabibu za eneo hilo hufaa kabisa kutumiwa kutengeneza divai ya barafu yenye sukari nyingi sana. Baada ya kiangazi, hali ya hewa hubadilika sana hivi kwamba zabibu hukauka na kuwa tamu zaidi.

Ladha ya “Divai ya Dhahabu”

Kilogramu moja ya zabibu za kawaida huhitajiwa ili kutengeneza chupa moja ya divai ya mililita 750. Hata hivyo, ikitegemea upepo na mwangaza wa jua wakati wa majira ya baridi kali, kilogramu moja ya zabibu kavu yaweza kutokeza mililita 150 tu au hata chini ya hapo! Hivyo, divai ya barafu ni ghali sana na mara nyingi huuzwa katika chupa za mililita 375.

Mtengenezaji mmoja wa divai alisema kwamba divai ya barafu hunukia “kama kokwa za lichi,” na ina ladha ya “matunda ya kitropiki, na ladha kidogo ya umajimaji wa pichi na maembe.” Huenda hapo kwanza ukaona divai hiyo kuwa tamu kupita kiasi, lakini ‘asidi hupunguza utamu huo mwingi na kufanyiza ladha nzuri ya kileo.’

Divai ya barafu haipendwi tu nchini Kanada. Divai hiyo huuzwa katika maeneo mengi, hasa katika Asia Mashariki. Hivyo, watu katika nchi hizo hutumia divai hiyo tamu badala ya kileo cha cognac.

Viwanda vya kutengeneza divai huko Niagara vimeripoti kwamba watu fulani wamejitolea kusaidia kuvuna zabibu wakati wa baridi kali. Ujira wao huwa nini? Wao hupewa chupa ya mililita 375 ya “divai ya dhahabu.”

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Zabibu: © Bogner Photography

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

Julianna Hayes, BCWine.com