Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kazi Nyingi za Akina Mama

Kazi Nyingi za Akina Mama

Kazi Nyingi za Akina Mama

10:50 asubuhi. Akiwa amesinzia, Alex, yule mtoto mdogo, analia na kumwendea mama yake Helen. Wale watoto wengine wawili—Penny (5) na Joanna (12)—na mumewe, Nick, wamelala fofofo. Helen anamwinua Alex hadi kitandani na kumnyonyesha. Anashindwa kupata usingizi tena.

11:45 asubuhi. Helen anakwenda jikoni kimya, anatengeneza kahawa, na kusoma.

12:15–1:20 asubuhi. Nick anaamka. Helen anawaamsha Penny na Joanna, anatayarisha kiamsha-kinywa, na kufanya kazi ya nyumbani kidogo. Nick anaondoka saa 1:15 kumpeleka Joanna shuleni, kisha anakwenda kazini. Mama ya Helen anafika ili kumtunza Alex.

1:30 asubuhi. Helen anampeleka Penny kwenye shule ya watoto wadogo. Anaposafiri akielekea kazini Helen anafikiria wajibu na kazi za akina mama. Anasema hivi: “Sijawahi kufanya kazi ngumu kama hiyo.”

2:10 asubuhi. Ofisini Helen anakuta kazi nyingi. Anahofia kwamba huenda akapoteza kazi akipata mimba tena. Familia huhitaji mshahara wake pia.

4:43 asubuhi. Baada ya Helen kumaliza mazungumzo kwa simu kuhusu watoto wake, mfanyakazi mwenzake anamliwaza kwa kusema: “Unawatunza watoto wako vizuri sana.” Machozi ya Helen yanatiririka.

6:05 mchana. Anapokula mkate, Helen anakumbuka jinsi hali ilivyokuwa kabla ya binti yake wa kwanza kuzaliwa. Wakati huo alikuwa amepanga kufanya mambo mengi sana wakati ambapo angekuwa na wasaa. Anasema hivi: ‘Kumbe nilikuwa nikiota ndoto!’

9:10 alasiri. Baada ya mama yake kumpigia simu mara kadhaa na kusimulia michezo ya Alex, Helen anataja uhusiano wake wa pekee pamoja na watoto wake: “Sijawahi kumpenda mtu yeyote jinsi ninavyowapenda watoto wangu.” Upendo huo ulimsaidia kushinda magumu ya kwanzakwanza yasiyotarajiwa.

11:10 jioni. Baada ya kumchukua Joanna shuleni, Helen anashughulikia mambo mbalimbali. Anampigia Nick simu na kumkumbusha kwamba yeye ndiye anayepaswa kumchukua Penny shuleni.

12:00–1:30 jioni. Helen anapofika nyumbani Nyanya anapumzika. Na sasa ni zamu ya Helen kumtunza Alex. Kisha Helen anafanya kazi za nyumbani na kutayarisha chakula cha jioni. Anapoulizwa kuhusu mahitaji ya mtoto mdogo, Helen anahema na kusema: “Mtoto mchanga anahitaji mikono ya mama, mwili wake, maziwa yake; na humzuia mama asilale.”

2:30–4:00 usiku. Helen anamsaidia Joanna kufanya kazi za shuleni na kumnyonyesha Alex. Anafanya kazi nyingine za nyumbani, huku Nick akimsomea Penny kwa muda wa nusu saa.

5:15 usiku. Baada ya Penny na Joanna kwenda kulala, Helen anamshika Alex ambaye hajalala bado, kisha Alex anashikwa na usingizi. “Ninafikiri amelala,” Helen anamwambia Nick, ambaye tayari anasinzia-sinzia.