Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuhifadhi Mbegu Haraka

Kuhifadhi Mbegu Haraka

Kuhifadhi Mbegu Haraka

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI UINGEREZA

SISI hutegemea mimea maishani. Mimea ni chanzo cha chakula, mavazi, fueli, vifaa vya ujenzi, na dawa zinazookoa uhai. Wanyama, ndege, na wadudu huitegemea pia. Hata hivyo, watafiti fulani wanasema kwamba robo moja ya mimea iliyoko duniani iko katika hatari ya kutoweka katika muda wa miaka 50 ijayo. Mradi wa Hifadhi ya Mbegu za Milenia ni mradi mkubwa sana kati ya miradi ya kuzuia mimea isitoweke kabisa.

Jengo moja lenye thamani ya dola milioni 120 za Marekani, lililoko kusini mwa Uingereza, litatumiwa kuhifadhi mbegu nyingi sana za mimea ambayo iko katika hatari ya kutoweka. Jengo hilo limetajwa kuwa “Safina ya Noa kwa ajili ya mimea.”

Hifadhi ya Mbegu Ni Nini?

Je, umewahi kupeleka mali zako za thamani katika benki ili zihifadhiwe? Hifadhi ya mbegu hutimiza kusudi kama hilo kwa ajili ya mimea. Ni njia rahisi na ya bei nafuu ya kuhifadhi mmea unaotokeza mbegu, iwe ni mmea mdogo au hata mti mrefu sana. Mbegu zikiisha kuhifadhiwa, si lazima zitunzwe sana. Mbegu nyingi hazichukui nafasi kubwa. Mbegu milioni moja za okidi zaweza kutoshea katika kichupa kidogo cha dawa! Aina nyingine nyingi za mbegu za idadi iyo hiyo, zaweza kutoshea katika chupa ya kuhifadhi chakula. Baada ya kutengenezwa kwa njia maalumu, mbegu hizo zaweza kuhifadhiwa kwa makumi ya miaka au hata kwa karne nyingi, hata zaidi ya muda ambao zingaliweza kusitawi msituni.

Hifadhi za mbegu zimekuwako kwa muda mrefu, japo hapo zamani zilitumiwa hasa kuhifadhi mazao ya biashara. Mnamo mwaka wa 1974, wanasayansi wa bustani za Royal Botanic Gardens, huko Kew, London, walianza kuchunguza namna ya kuhifadhi mbegu za mimea-mwitu kwenye ofisi yao huko Wakehurst Place katika eneo la mashambani la Sussex. Baada ya kuhifadhi aina 4,000 tofauti za mimea kutoka sehemu mbalimbali za ulimwengu, wanasayansi hao walitambua kwamba walihitaji mradi mkubwa zaidi ili kuzuia kutoweka kwa mimea na mazingira yake ulimwenguni pote. Basi, mnamo mwaka wa 1998, hifadhi kubwa ya mbegu ilianza kujengwa huko Wakehurst Place, Kew.

Kutimiza Miradi

Mradi wa kwanza ulikuwa kuhifadhi mbegu za miti, mikwamba, nyasi, vichaka, na mimea-mwitu yote ya Uingereza kufikia mwaka wa 2000. Kati ya mimea 1,440 ya Uingereza, mimea 317 iko katika hatari ya kutoweka. Aina 579 za mbegu zilikuwa zimekwisha kuhifadhiwa huko Kew. Wataalamu na wapenzi wa mimea zaidi ya 250 walisaka mimea iliyosalia. Wapenzi wa mimea walipanda milima, waliteremka magenge, na kupitia kwenye maji ya barafu wakitafuta mimea isiyopatikana kwa urahisi. Kufikia tarehe ya mwisho ya mradi huo, mimea yote ilikuwa imepatikana isipokuwa mimea michache tu isiyopatikana kwa urahisi.

Tangu mwaka wa 2000, lengo kuu limekuwa kukusanya na kuhifadhi asilimia 10, au zaidi ya aina 24,000, ya mimea inayotokeza mbegu. Mradi huo unapasa kukamilika kufikia mwaka wa 2010. Mimea inayokusanywa hasa ni ile inayopatikana katika maeneo yenye ukame. Asilimia 20 ya idadi ya watu ulimwenguni huishi katika maeneo hayo yenye joto na ukame, nao hutegemea mimea maishani. Hata hivyo, kila mwaka maeneo makubwa hugeuka kuwa majangwa. Katika nchi nyingine, harakati za kukusanya mbegu zilianza mwanzoni mwa mwaka wa 1997, na kufikia Februari 2001, watafutaji wa mbegu wa Kew walikuwa wamekusanya mbegu milioni 300 kutoka katika nchi 122. Hivyo, aina 19,000 bado hazijahifadhiwa.

Kuhifadhi Mbegu

Kwa muda mrefu, watunza-bustani na wakulima wamekusanya na kuhifadhi mbegu. Hata hivyo, mbegu zinazohifadhiwa katika Hifadhi ya Mbegu za Milenia zitadumu kwa muda mrefu kuliko ilivyo kawaida. Hiyo inatokana na jinsi zinavyokaushwa na kugandishwa.

Mbegu zikiisha kukusanywa kwa wingi na kuondolewa takataka, hizo huwekwa katika mifuko ya karatasi au ya vitambaa au hata katika chupa za soda ili zikauke kabla ya kupelekwa huko Uingereza. Wakati huohuo, wakusanyaji hukausha na kuhifadhi mimea ambayo hutokeza mbegu hizo ili ziweze kutambuliwa rasmi huko Kew. Na mitambo maalumu ya setilaiti hutumiwa ili kurekodi mahala ambapo mimea hiyo ilipatikana.

Mbegu hizo zinapopelekwa huko Wakehurst Place, hizo huhitaji kukaushwa mara mbili. Mbegu hizo hukaushwa, husafishwa, kisha hukaushwa tena. Mbegu hizo huwekwa katika vyumba viwili vyenye unyevu kidogo. Cha pili huwa na unyevu kidogo kuliko kile kingine na vyote huwa vikavu kuliko majangwa mengi. Hivyo, unyevu uliomo katika mbegu hizo hupungua kutoka asilimia 50 hivi hadi asilimia 5 hivi. Jambo hilo huzuia mbegu zisiharibike wakati zinapogandishwa na huzuia mbegu zenyewe zisichipue kwa muda mrefu. Kabla ya kuhifadhiwa, mbegu chache hupigwa picha za eksirei ili ijulikane ikiwa ziko sawa au zimeliwa na wadudu. Mbegu nyingine hujaribiwa ili ionekane kama zinaweza kuota. Kwa kweli, baada ya kila miaka kumi, mbegu zitaondolewa kwenye barafu ili ijulikane ikiwa zingali zinaweza kuchipua. Iwapo chini ya asilimia 75 ya mbegu hizo hazichipui, itabidi mbegu mpya zikusanywe.

Sehemu muhimu katika utafiti ni kujua jinsi mbegu zinavyokuwa baada ya kuhifadhiwa kwa muda mrefu na kujua jinsi ya kuzifanya zichipue baadaye. Mwishowe, mbegu hizo huwekwa ndani ya chupa zilizofungwa kikiki na kuhifadhiwa katika jengo kubwa la saruji chini ya ardhi katika friji mbili zilizo kama vyumba. Chupa hizo hupangwa vizuri kwenye rafu, na hudumu hapo katika halijoto ya nyuzi 20 Selsiasi chini ya kipimo cha kuganda.

Je, mbinu hiyo hufua dafu? Naam. Miaka michache iliyopita, mbegu 3,000 za mimea tofauti zilijaribiwa, na asilimia 94 ya mbegu hizo zilichipua. Mbegu hizo zilikuwa zimehifadhiwa kwa muda wa miaka kumi.

Ni kazi ngumu kuhifadhi aina fulani za mbegu. Unyevu wa mbegu hizo ukipungua sana, mbegu hizo hufa. Mbegu hizo zatia ndani za miti fulani ya mwaloni (Quercus), kakao (Theobroma cacao), na za mti unaotoa utomvu wa mpira (Hevea brasiliensis). Lakini mbegu hizo haziwezi kuhifadhiwa zikiwa nyevu kwani maji hayo yakiganda yatapanuka na kupasua kuta za chembe. Wanasayansi wanachunguza mbinu za kushinda tatizo hilo. Suluhisho moja lahusisha kuondoa kiini cha mbegu, kukikausha haraka, na kukihifadhi katika umajimaji wa nitrojeni katika baridi kali sana.

Ni Nani Watakaofaidika?

Kama vile benki za kuhifadhi pesa, Hifadhi ya Mbegu za Milenia hutoa faida. Mbegu mbalimbali hutumiwa katika uchunguzi. Asilimia 25 ya dawa hutengenezwa kwa mimea, lakini asilimia 80 ya mimea ulimwenguni haijachunguzwa. Ni dawa zipi zitakazogunduliwa? Aina moja ya mtambazi (Vicia Faba) inayopatikana Mediterania, imetokeza protini moja ya kugandisha damu ambayo husaidia kutambua magonjwa ya damu yasiyojulikana sana. Huenda pia vyakula, fueli, au nyuzi mpya za nguo zitagunduliwa.

Wanasayansi kutoka nchi nyingine hukaa kwenye Hifadhi hiyo wanapojifunza mbinu za kuhifadhi mbegu na za kuzichipua ili waanzishe hifadhi za mbegu katika nchi za kwao. Kila nchi inayopeleka mbegu zake kwenye Hifadhi hiyo hurudishiwa mbegu nyingi sana na hufaidika kutokana na uchunguzi.

Kwa kuwa mbegu zilizohifadhiwa zinatumiwa kusitawisha ardhi iliyoharibiwa na kuongeza idadi ya mimea iliyo katika hatari ya kutoweka, yatumainiwa kwamba mbinu hizo za kuhifadhi zitazuia kutoweka haraka kwa mimea na kwa viumbe wengi wanaotegemea mimea hiyo.

Mradi Huo Utatimizwaje?

Pasina shaka wanadamu wanakabili hali hatari. Roger Smith, mkuu wa idara ya kuhifadhi mbegu huko Kew, anataja sababu tatu za mradi huo: ‘Sababu ya kwanza ni kwa ajili ya faida yetu wenyewe. Hatufahamu mengi sana kuhusu kila mmea. Hivyo, mmea mmoja unapotoweka tunapoteza ujuzi mwingi sana kuhusu tiba na faida zake za lishe. Sababu ya pili ni ule uhusiano muhimu kati ya viumbe na mimea. Hebu linganisha aina zote za viumbe na wavu. Kila aina ni kama uzi katika wavu. Unafikiri utahitaji kukata nyuzi ngapi ili uharibu wavu huo? Sababu ya tatu na ya maana zaidi ni daraka la kutunza viumbe na mimea. Je, kweli wanadamu wanaoishi sasa wana haki ya kuwanyima wazao wao faida ambazo wangepata kutokana na viumbe na mimea ambayo wao wenyewe walirithi?’

Kungali na magumu makubwa wakati ujao. Steve Alton, mratibu wa mradi huo, anasema hivi: “Tunaweza kuwa na aina nyingi sana za mbegu, lakini iwapo hakuna mahala pa kuzipanda, hakuna haja ya kuzihifadhi.” Je, itawezekana kuhifadhi aina za mimea zilizo katika hatari ya kutoweka huku tukitunza dunia yetu?

Naam, itawezekana. Muumba anaahidi hivi: “Itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote.”—Zekaria 8:12.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 25]

MOJAWAPO YA HIFADHI NYINGI

Bustani za Kew ni mojawapo ya hifadhi 1,300 ulimwenguni pote zinazohifadhi mbegu katika friji za kugandisha. Steve A. Eberhart, mkuu wa Maabara ya Kitaifa ya Kuhifadhi Mbegu huko Colorado, anasema kwamba hifadhi hiyo ya mimea ni salama kama hifadhi ya dhahabu ya Fort Knox.

[Picha]

Mradi wa Hifadhi ya Mbegu za Milenia

[Sanduku katika ukurasa wa 26]

KUKUSANYA AINA ZOTE

Hifadhi za mbegu hutimiza daraka muhimu la kukusanya aina tofauti-tofauti za mmea mmoja. Hivyo, chembe za urithi za aina zote hizo zaweza kutumiwa ili kufanya mmea huo ukinze magonjwa mapya au wadudu wanaoharibu mmea huo. Kwa kupanda mimea fulani pamoja, wanasayansi wanaweza kuboresha mavuno, thamani ya lishe, na uwezo wa mimea wa kukinza magonjwa na wadudu. Kukusanya aina zote za mimea ni muhimu sana.

Ulimwenguni pote, wanadamu hula aina 103 tu za mimea ili kupata zaidi ya asilimia 90 ya kalori. Na zaidi ya asilimia 50 ya vyakula vya wanadamu wote hutayarishwa kwa mazao matatu tu muhimu—mpunga, ngano, na mahindi. Kwa nini hilo ni tatizo?

Zao la aina moja likizalishwa katika maeneo mengi, linaweza kuendelea kuathiriwa na ugonjwa au wadudu wa aina moja. Mfano unaojulikana sana kuhusu jambo hilo ulitokea huko Ireland katika miaka ya 1840. Wakati huo, mimea yote ya viazi iliharibiwa na ugonjwa unaosababishwa na kuvu (Phytophthora infestans). Kuvu hiyo ilisababisha Njaa Kubwa na watu 750,000 walikufa.

[Sanduku katika ukurasa wa 27]

AINA MBALIMBALI ZIMO HATARINI

Kwenye Mkutano wa 16 wa Kimataifa wa Wataalamu wa Mimea uliofanywa Marekani, Dakt. Peter H. Raven aliwatahadharisha wajumbe hivi: “Huenda aina 100,000 kati ya aina zote zipatazo 300,000 zitakuwa zimetoweka au zitakuwa katika hatari ya kutoweka kufikia katikati ya karne [ya 21].” Ripoti moja ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) yasema kwamba tayari aina “nyingi” za mazao ya chakula zimetoweka. Kisababishi kikuu cha kutoweka kwa aina mbalimbali za mimea kinashangaza sana.

Ripoti hiyo ya shirika la FAO ilisema hivi: ‘Aina mbalimbali za mimea zimetoweka hasa kwa sababu ya kuenea kwa kilimo cha kisasa cha kibiashara. Bila kukusudia, uzalishaji wa aina mpya za mazao umesababisha kutoweka kwa mimea tofauti-tofauti ya kienyeji.’

Huko China, aina 10,000 hivi za ngano zilipandwa katika mwaka wa 1949. Leo, aina za ngano zisizozidi 1,000 hupandwa katika nchi hiyo. Nchini Marekani, aina 6,000 hivi za mitofaa zimetoweka katika muda wa miaka 100 iliyopita, na yasemekana kwamba asilimia 95 ya aina mbalimbali za kabichi na asilimia 81 ya aina mbalimbali za nyanya zimetoweka pia.

Vita pia husababisha kutoweka kwa mazao wakati wakulima wanapolazimishwa kuhama mashamba yao kwa muda wa miaka mingi. Hivyo, aina za mazao ya kienyeji hutoweka. Jarida la UNESCO Courier lilisema hivi: “Vita . . . vimeathiri nchi zote zilizoko kwenye pwani ya Afrika Magharibi ambako mpunga ulipandwa hapo kale. Eneo hilo ni muhimu kwa upandaji wa aina mbalimbali za mpunga wa Afrika (Oryza glaberrima), ambao . . . unaweza sasa kuzalishwa pamoja na mpunga wa Asia, mojawapo ya mazao muhimu zaidi ya chakula duniani. Ulimwengu wote utapata hasara kubwa iwapo zao hilo . . . la Afrika ambalo halijachunguzwa sana litaharibiwa kwa sababu ya vita katika eneo hilo.”

Ni Bora Kuliko Hifadhi za Mbegu

John Tuxill, mtafiti wa Taasisi ya Worldwatch, alionya hivi: ‘Tunaendelea kubadilisha chembe za urithi kwa ustadi, lakini hatuwezi kuziumba. Mmea wenye sifa za kipekee ukipotea, hatuwezi kuupata tena.’ Hivyo, pesa nyingi sana zinatumiwa kuhifadhi mbegu kwa njia bora.

Ahadi ambayo Muumba wa mbegu alitoa zamani ni bora zaidi, nayo inatuhakikishia hivi: “Kadiri itakavyodumu nchi, majira ya kupanda na kuvuna . . . hayatakoma.”—Mwanzo 8:22, Biblia Habari Njema.

[Picha katika ukurasa wa 24]

Kukusanya mbegu nchini Burkina Faso

[Picha katika ukurasa wa 25]

Kuhifadhi mbegu katika baridi kali sana

[Picha katika ukurasa wa 26]

Mtaalamu wa mimea kutoka Kenya ajifunza jinsi ya kuchunguza kiwango cha unyevu katika mbegu

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 24]

Picha zote kwenye ukurasa wa 24-27: The Royal Botanic Gardens, Kew