Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kupata Hazina Katika Mji wa Lulu

Kupata Hazina Katika Mji wa Lulu

Kupata Hazina Katika Mji wa Lulu

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

BROOME ni mji ambao uko kaskazini-magharibi mwa Australia na umezingirwa na ufuko wa bahari. Jangwa Kuu la Mchanga limeanzia upande wa kusini-mashariki wa mji huo na kuelekea katikati ya Australia. Bahari ya Hindi iko upande wa magharibi wa mji huo, nayo inaelekea hadi pwani ya Afrika. Tufani huvuma mara nyingi kwenye sehemu hiyo iliyoko kaskazini-magharibi mwa bara hilo.

Hapo zamani, kulikuwa na chaza wengi wenye lulu katika bahari ya eneo hilo la kitropiki hivi kwamba Broome uliitwa Mji wa Lulu. Eneo la Broome lilitembelewa na maharamia, watumwa, na wauzaji wa lulu.

Uvumbuzi wa Haramia

Ijapokuwa Mholanzi Dirck Hartog alitembelea eneo hilo la mbali katika mwaka wa 1616, pwani ya magharibi ya Australia haikujulikana sana hadi mwaka wa 1688. Katika mwaka huo, Mwingereza William Dampier, aliyekuwa mwandishi, mchoraji, na haramia, alifika kwenye pwani hiyo bila kutarajia. Alikuwa akisafiri katika meli yake ya maharamia iliyoitwa Cygnet. Dampier aliporudi katika nchi yake, aliandika matukio ya safari yake. Maandishi na michoro yake iliwavutia sana wananchi wenzake hivi kwamba Jeshi la Wanamaji la Uingereza lilimpa meli na kumwagiza asafiri ili kuchunguza eneo la New Holland, jina la kale la Australia.

Dampier alisafiri kwa meli iliyoitwa Roebuck, lakini safari yake haikufua dafu. Hakuvumbua eneo jipya, na safari yake ilisimama wakati meli yake kuukuu ilipovunjika na kuzama. Dampier aliokoka, na kwenye rekodi za safari yake aliandika kwamba alivumbua chaza wenye lulu.

Utajiri Wapatikana kwa Vifungo vya Nguo na kwa Vifo

Watu walianza kutia maanani uvumbuzi wa Dampier baada ya miaka 160. Mnamo mwaka wa 1854, lulu zilianza kukusanywa toka katika eneo ambalo Dampier aliliita Ghuba ya Shark. Lakini kazi hiyo haikufaulu sana. Wakati huohuo, chaza mkubwa anayeitwa Pinctada maxima alipatikana karibu na eneo hilo, katika Ghuba ya Nichol. Chaza huyo, ambaye ni mkubwa kama sahani, alitengeneza lulumizi bora kupita zote katika koa lake. Lulumizi hizo zilitafutwa sana ili zitumiwe kutengeneza vifungo vya nguo.

Kufikia miaka ya 1890, lulumizi zenye thamani ya pauni 140,000 hivi za Uingereza zilikuwa zikisafirishwa kila mwaka hadi Uingereza kutoka kwenye maeneo yenye chaza huko Broome. Ijapokuwa lulu nyingi zenye thamani zilipatikana katika koa za chaza, vito hivyo havikuonwa kuwa muhimu sana. Wauzaji wa lulu walitajirika hasa kutokana na koa la chaza. Na mara nyingi utajiri huo ulipatikana kwa vifo.

Hapo mwanzoni, wauzaji wa lulu waliwashawishi au kuwalazimisha wenyeji Waaborijini kupiga mbizi ili watafute lulu. Muda si muda Waaborijini wakazoea kazi hiyo. Lakini kazi ya kutafuta lulu kwa kupiga mbizi ni hatari na wapiga-mbizi kadhaa walizama au waliuawa na papa. Wapiga-mbizi wengi pia walikufa kwa sababu ya kudhulumiwa sana na waajiri wao. Wapiga-mbizi wengine kutoka Malasia na Java walipelekwa huko ili kuwasaidia Waaborijini. Chaza walipokwisha katika maji yenye kina kifupi, wapiga-mbizi walishuka chini zaidi kwa kutumia kofia maalumu ya kupigia mbizi ambayo ilikuwa imebuniwa karibu na wakati huo.

“Sodoma na Gomora” Zafilisika

Mashua zilizotumiwa katika biashara hiyo ya lulu ziliongezeka kufikia zaidi ya 400. Kulikuwa na Waasia, Wazungu, na Waaborijini, na mara nyingi mchanganyiko wa tamaduni hizo ulisababisha uhalifu mwingi. Mtafutaji mmoja wa lulu alisema hivi kuhusu hali ya wakati huo: ‘Broome lilikuwa eneo lenye ufanisi, lenye uovu, na mahala ambapo watu wabaya hawakuadhibiwa. Makasisi walipolinganisha eneo hilo na Sodoma na Gomora, watu waliona maneno yao kuwa sifa nzuri kwa maendeleo ya jamii badala ya kuyaona kama maonyo kwamba Mungu atawaadhibu wakati ujao.’

Hata hivyo, vita ya kwanza ya ulimwengu ilipozuka, biashara ya lulumizi iliteketea, na uchumi wa Broome ukazorota. Biashara ya lulumizi ilianza tena kwa muda mfupi katikati ya vita ya kwanza na vita ya pili ya ulimwengu. Lakini baada ya vita ya pili ya ulimwengu, Broome ilipata hasara nyingine. Plastiki zilibuniwa, na punde si punde vifungo vya plastiki vikapendwa zaidi ya vifungo vya lulumizi.

Kutengeneza Lulu Zenye Thamani

Baada ya vita ya pili ya ulimwengu, watu fulani kutoka Australia walitembelea maeneo ya kutengeneza lulu huko Ago, Japani. Kokichi Mikimoto alikuwa ameboresha ufundi wa kutengeneza lulu huko kwa kuingiza changarawe katika makoa ya chaza. Kitabu Port of Pearls chasema kwamba Mikimoto aliwaambia Waaustralia hao kuwa ‘wangeweza kutengeneza lulu nzuri hata zaidi huko kwao kwa kutumia chaza wao wakubwa.’ Waaustralia hao walitumia shauri lake, na kufikia miaka ya 1970, chaza wa Australia walikuwa wakitengeneza lulu kubwa na zenye thamani zaidi ulimwenguni.

Ijapokuwa lulu zinazotengenezwa katika sehemu nyingi za ulimwengu zina kipenyo cha milimeta 11, lulu za Bahari ya Kusini zaweza kufikia kipenyo cha milimeta 18. Mkufu mmoja tu wa lulu hizo kubwa unaweza kuwa na thamani ya dola 500,000 za Marekani. Basi ndiyo sababu vito hivyo vya mviringo vyaweza kulinganishwa na almasi zinazopatikana kwenye sakafu ya bahari!

[Picha katika ukurasa wa 14, 15]

William Dampier

Mpiga-mbizi akusanya makoa ya chaza karibu na pwani iliyoko kaskazini ya Broome

Mtaalamu aondoa lulu kutoka kwenye chaza

Mojawapo ya meli zilizotumiwa hapo awali kutafuta lulu ilirekebishwa ili itumiwe tena baharini

Lulu huwa na rangi mbalimbali (ukubwa wa picha umeongezwa)

[Hisani]

William Dampier: By permission of the National Library of Australia - Rex Nan Kivell Collection, NK550; mpiga-mbizi: © C. Bryce - Lochman Transparencies; mkufu na mtaalamu: Courtesy Department of Fisheries WA, J. Lochman; meli: Courtesy Department of Fisheries WA, C. Young; picha ya lulu iliyopigwa karibu: Courtesy Department of Fisheries WA, R. Rose