Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Lugha ya Mbugani Siri za Mawasiliano ya Wanyama

Lugha ya Mbugani Siri za Mawasiliano ya Wanyama

Lugha ya Mbugani Siri za Mawasiliano ya Wanyama

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI KENYA

PASINA shaka kwamba uwezo wa kuwasiliana ni mojawapo ya zawadi zenye thamani zaidi ambazo wanadamu walipewa. Kwa kutumia uwezo huo, sisi huwasilisha habari muhimu kwa wanadamu wenzetu iwe ni kwa maneno ama bila kusema, kama vile kwa kutumia ishara. Kotekote ulimwenguni, watu hupigania uhuru wa kusema. Hivyo, watu fulani wamefikiri kwamba wanadamu peke yao ndio wanaoweza kuwasiliana.

Hata hivyo, uchunguzi unaonyesha kwamba wanyama huwasiliana kwa njia tata ambazo mara nyingi ni vigumu wanadamu kuzielewa. Naam, wanyama “huzungumza,” si kwa maneno, bali kwa ishara. Ishara hizo zatia ndani kutikisa mkia, sikio, au kupigapiga mabawa. Njia nyingine za mawasiliano zahusisha kutumia sauti, kama vile kubweka, kunguruma, au sauti za ndege wanapoimba. Wanadamu wanaweza kutambua “lugha” fulani za wanyama kwa urahisi, lakini nyingine zaweza kutambuliwa tu baada ya uchunguzi mwingi wa wanasayansi.

Wanyama Wanaowinda!

Ni katikati ya mwezi wa Julai. Katika Mbuga ya Taifa ya Serengeti huko Tanzania, maelfu ya nyumbu wanaelekea kaskazini kwenye Mbuga ya Wanyama ya Masai Mara nchini Kenya ili kutafuta malisho. Milio ya kwato zao inasikika kwenye nyanda, huku wakiendelea na uhamaji wao wa kila mwaka. Hata hivyo, kuna hatari mbalimbali njiani. Kuna wanyama wanaowinda, kama vile simba, duma, fisi, na chui. Nyumbu hao bado watahatarisha uhai wao kwa kuvuka Mto Mara ulio na mamba wengi. Nyumbu hao huwaepukaje wanyama wanaowinda?

Ili kumkengeusha adui, nyumbu hukimbia umbali mfupi kwa kasi kisha yeye hugeuka ili kumkabili adui, huku akitikisa kichwa chake huku na huku. Nyumbu huyo hurukaruka kwa njia ya ajabu na ya kuchekesha. Hata mnyama mkali sana huzubaa anapoona mchezo huo wa kiajabu. Mnyama anayewinda akiendelea kumkabili, nyumbu huyo huendelea kurukaruka. Jambo hilo humvuruga mnyama anayewinda na laweza kumfanya amwache nyumbu na kuondoka. Mchezo huo wa kiajabu wa nyumbu umemfanya aitwe mcheshi wa nyanda.

Swalapala wanajulikana kwa uwezo wao wa kuruka juu sana. Wao wako katika jamii moja na nyumbu. Watu wengi huonelea kwamba uwezo huo wa kuruka huwawezesha wanyama hao kukimbia haraka sana na kuonekana kuwa wenye madaha. Hata hivyo, swalapala hutumia uwezo wake wa kuruka juu ili kumzuia mnyama anayewinda asimnase miguuni. Yeye huruka kufikia meta 9, na anapofanya hivyo ni kana kwamba anamfanyia mzaha mnyama anayewinda kwa kusema, “Nifuate ikiwa unaweza.” Ni wanyama wachache tu wanaoweza kuthubutu kuruka ili kumkamata swalapala!

Saa za Kula

Ni lazima wanyama wengi wanaowinda wajifunze stadi za kuwinda ili wawe wawindaji bora. Wanyama wachanga hupaswa kutazama kwa makini wakati wazazi wao wanapowafundisha kuwinda. Katika mbuga moja ya wanyama barani Afrika, duma mmoja aliyeitwa Saba alionekana akiwafundisha watoto wake jinsi ya kuwinda. Baada ya kumnyemelea swalatomi mmoja kwa zaidi ya saa moja, Saba alimshambulia swala huyo maskini na kumnyonga, lakini hakumuua. Muda mfupi baadaye, Saba alimwangusha swala huyo aliyeshtuka mbele ya watoto wake. Kwa kushangaza, watoto hao walisita kumrukia swala huyo. Duma hao wachanga walielewa ni kwa nini Mama aliwaletea mnyama aliye hai. Alitaka wajifunze jinsi ya kumwua swala huyo. Duma hao wachanga na wachangamfu walimwangusha swala huyo kila alipojaribu kujinyanyua ili atoroke. Swala huyo alichoka na akafa. Saba alionekana kuwa ameridhika huku akitazama kutoka mbali.

Wanyama fulani hupiga kelele nyingi wanapotafuta chakula. Kundi la fisi-madoa hukoroma, hunguruma, na kuchekacheka wanapomfukuza mnyama ambaye wanawinda. Fisi anapomuua mnyama, yeye huwakaribisha fisi wengine kwenye karamu hiyo kwa “kicheko” chake cha kuudhi. Hata hivyo, nyakati nyingine fisi hawawindi. Wao hupenda kudoea chakula cha wanyama wengine wanaowinda kwa kuwachokoza. Ha! hata wamejulikana kwa kuwasumbua simba wanaokula kiasi cha kufanya simba waache mlo wao! Wao hufanyaje hivyo? Wao ni machachari kwelikweli. Wao huzusha ghasia nyingi kwa kupiga kelele ili kuwasumbua simba wanaokula. Simba wakipuuza kelele zao, fisi hupiga kelele nyingi zaidi na kuzusha fujo nyingi hata zaidi. Mara nyingi simba hao waliovurugwa huacha mzoga wanaokula na kuondoka.

Nyuki hutafuta chakula kwa njia tata sana. Uchunguzi tata wa kisayansi umeonyesha kwamba nyuki hucheza dansi ili kuwaarifu nyuki wengine kuhusu mahala penye chakula, aina ya chakula, na hata ubora wa chakula hicho alichopata. Nyuki huyo hubeba vipande vya chakula kwenye mwili wake, kama vile umajimaji mtamu au chavua, na kuwapelekea nyuki waliomo mzingani. Nyuki huyo hucheza dansi ya kuzunguka-zunguka ili kuwaelekeza nyuki wengine mahala ambapo chakula hicho kipo na umbali ambao watasafiri. Jihadhari! Nyuki anapokuzunguka-zunguka, huenda ikawa anakusanya habari muhimu ili awaeleze nyuki wengine wakati anaporudi mzingani. Huenda akadhani kwamba amepata mlo anaponusia marashi yako!

Kuendelea Kuwasiliana

Mngurumo wa simba ni mojawapo ya sauti chache za kustaajabisha unazoweza kusikia usiku wakati ambapo kumenyamaza. Watu wamedokeza sababu kadhaa kueleza jinsi simba wanavyowasiliana. Mngurumo wa simba huonya wote kwamba amewasili katika eneo hilo na kwamba yeyote hapaswi kuthubutu kukanyaga hapo. Hata hivyo, simba, ambaye hupenda kuishi na wenzake, hunguruma pia ili kuwasiliana na simba wengine katika kundi lake. Mngurumo huo si mkali sana. Inasemekana kwamba usiku mmoja, simba mmoja alinguruma baada ya kila dakika 15 hadi simba mwingine katika kundi lake alipomjibu kutoka mbali. Simba hao waliendelea kuwasiliana kwa dakika 15 hadi walipokutana. Kisha wakanyamaza.

Mawasiliano hayo huboresha uhusiano kati ya wanyama na kuwalinda dhidi ya hali ngumu za hewa. Kuku hutoa milio kadhaa ili kuwaeleza vifaranga wake mambo tofauti. Hata hivyo, kuku hutoa sauti ndogo jioni, ambayo ni tofauti kabisa na milio yake mingine, ili kuwaonyesha vifaranga wake kwamba amerudi nyumbani kulala. Vifaranga hutii mwito wa Mama na kujikusanya chini ya mabawa yake ili kulala.—Mathayo 23:37.

Kupata Mwenzi

Je, umewahi kutua kidogo na kusikiliza nyimbo za ndege? Je, wewe huvutiwa na uwezo wao wa kuimba? Hata hivyo, je, ulijua kwamba kusudi lao si kutumbuiza watu? Wao huimba ili kuwasilisha ujumbe muhimu. Ijapokuwa nyakati nyingine ndege huimba ili kumiliki eneo fulani, wao hufanya hivyo hasa ili kuwavutia wapenzi. Kitabu The New Book of Knowledge chasema kwamba ndege wanapopata wenzi “muda wanaotumia kuimba hupungua kwa asilimia 90.”

Hata hivyo, nyakati nyingine wimbo ulio bora hautoshi kupata mwenzi. Ndege fulani wa kike hudai eti “mahari” itolewe kabla ya kukubali kuambatana na ndege wa kiume. Hivyo, mnana wa kiume hulazimika kujenga kiota ili uchumba uendelee. Ndege wengine wa kiume huthibitisha kuwa wataweza kulisha familia kwa kumlisha ndege wa kike kihalisi.

Njia tata za kuwasiliana huwawezesha wanyama kupata mahitaji yao, kupunguza vita, na kuishi pamoja kwa amani. Kwa kuwa uchunguzi unaendelea kufanywa kuhusu mawasiliano ya wanyama, tungali tunatarajia kufahamu mambo mengi kuhusu “lugha ya wanyama.” Hata ingawa hatuelewi kwa ukamili jinsi ambavyo wao huwasiliana, mawasiliano hayo humtukuza yule aliyeyaanzisha, Yehova Mungu.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 18, 19]

“Sauti Ndogo” ya Tembo

Alasiri moja yenye joto kali, wageni fulani wanatembelea makao ya tembo katika Mbuga ya Taifa ya Amboseli nchini Kenya. Tembo hao hawatishiki wakati wageni hao wanapoingia katika makao yao. Hata hivyo, tembo hao wanawasiliana kwa sauti mbalimbali za juu sana na za chini. Baadhi ya milio yao haiwezi kusikika na wanadamu lakini ni mikubwa sana hivi kwamba tembo aliye kilometa kadhaa kutoka hapo anaweza kuisikia.

Wataalamu wa tabia za wanyama wangali wanashangazwa na zile njia tata ambazo tembo hutumia kuwasilisha ujumbe muhimu. Joyce Poole ametumia zaidi ya miaka 20 akichunguza jinsi ambavyo tembo wa Afrika huwasiliana. Amekata kauli kwamba viumbe hao wakubwa, wanaojulikana kwa pembe zao zinazopendwa, huwa na hisia ambazo ni wanyama wachache tu walio nazo. Poole anasema hivi: ‘Unapowatazama tembo wa kundi moja wakisalimiana au wakisalimiana na kundi jingine wanalopenda au wakati tembo mchanga anapozaliwa, utaona kwamba wana hisia nyingi kama vile shangwe, furaha, upendo, urafiki, uchangamfu, ucheshi, huruma, na heshima.’

Wanapokutana baada ya muda mrefu, wao husalimiana kwa fujo, huku wakikimbia pamoja wakiinua vichwa vyao na kukunja na kuchezesha masikio. Nyakati nyingine, tembo anaweza kuingiza mkonga wake ndani ya mdomo wa tembo mwenzake. Ni kama kwamba tembo hufurahi sana wanapokutana na ni kana kwamba wao huambiana hivi, “Lo! Nimefurahi sana kukuona!” Jambo hilo huimarisha muungano wao ambao ni muhimu ili kuendeleza jamii yao.

Yaonekana kuwa tembo pia hucheka. Poole anasema aliwaona tembo wakisogeza kona za midomo yao kana kwamba walikuwa wakitabasamu, huku wakitikisa vichwa vyao kama kwamba walikuwa wakicheka. Wakati mmoja Poole alicheza na tembo hao. Tembo hao walitenda kwa njia ya kiajabu sana kwa dakika 15. Miaka miwili baadaye, tembo fulani walioshiriki katika mchezo huo walionekana ni kama walikuwa “wakitabasamu” na Poole labda wakikumbuka jinsi walivyocheza pamoja naye. Mbali na kufurahiana wanapocheza, tembo pia huiga milio. Poole alipokuwa akifanya uchunguzi fulani, alisikia mlio uliokuwa tofauti na milio ya kawaida ya tembo. Mlio huo ulipochanganuliwa, ilisemekana kwamba tembo hao walikuwa wakiiga sauti za malori yaliyokuwa yakipita hapo karibu. Na walifurahia kufanya hivyo! Ni kana kwamba tembo hujaribu kutumia kila njia ili kujifurahisha.

Mambo mengi yamesemwa juu ya jinsi ambavyo tembo huonekana kuwa wanaomboleza wakati tembo mwenzao anapopatwa na maafa. Wakati fulani, Poole alimwona tembo-jike akisimama kwa siku tatu karibu na mtoto wake aliyekufa alipozaliwa. Poole alisema hivi kuhusu kisa hicho: “Uso” wake “ulikuwa kama wa mtu mwenye majonzi na aliyeshuka moyo: aliinamisha kichwa chake na masikio yake, kona za mdomo wake zilikuwa zimekunjamana.”

Watu wanaowaua tembo kwa ajili ya pembe zao hawafikirii ‘uchungu wa kihisia’ wa tembo mayatima ambao yawezekana waliona mama zao wakiuawa. Tembo hao wachanga hupelekwa kwenye makao ya wanyama mayatima, nao huwa na “majonzi” mengi sana katika siku chache za kwanzakwanza. Mtunzaji mmoja kwenye makao hayo aliripoti kwamba aliwasikia tembo mayatima “wakilia kwa sauti” asubuhi. Athari zaweza kuonekana miaka kadhaa baada ya mauaji hayo. Poole anadokeza kwamba tembo hao wanajua kuwa wanadamu ndio wanaowatesa. Tunatazamia wakati ambapo wanadamu na wanyama wataishi pamoja kwa amani.—Isaya 11:6-9.

[Picha katika ukurasa wa 16, 17]

Polisi wa “Cape” wanasalimiana kama kawaida

[Picha katika ukurasa wa 17]

Nyumbu anacheza dansi ya kiajabu ili kumkengeusha adui

[Picha katika ukurasa wa 17]

“Kicheko” cha kuudhi cha fisi

[Hisani]

© Joe McDonald

[Picha katika ukurasa wa 18]

Nyuki anacheza dansi