Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Mama Matatizo Ambayo Akina Hukabili

Mama Matatizo Ambayo Akina Hukabili

Mama Matatizo Ambayo Akina Hukabili

Maisha ya akina mama ni ya kipekee na yenye kupendeza. Wao hufurahia mambo mazuri yasiyo na kifani. Hata hivyo, nyakati nyingine baadhi yao huhisi kana kwamba wamechanganyikiwa kiakili na kihisia kiasi cha kushindwa kuendelea. Helen analinganisha maisha yake na mbio za kuruka viunzi. Na kadiri muda unavyopita viunzi huonekana kuwa vingi zaidi na vya juu zaidi.

Huenda akina mama wakatumia wasaa wao wote kutunza watoto wao hata wasiwe na nafasi ya kutembelea marafiki wao. Esther, aliye na watoto watano, anasema hivi: ‘Ni lazima niwepo sikuzote watoto wanaponihitaji. Mimi huoga na kutayarisha chakula kwa haraka. Sina wasaa wa kusafiri, kuona sehemu mbalimbali, wala kufanya mambo yanayonipendeza. Lakini, sikosi kufua na kukunja nguo vizuri!’

Bila shaka, mama wengi hutaja furaha ya pekee wanayopata wanapolea watoto wao. Esther anasema hivi: “Ninapata nguvu ya kuendelea wakati watoto wanapotabasamu na kusema ‘Asante Mama,’ na kunikumbatia kwa upendo.” *

Mama Wanaofanya Kazi ya Kuajiriwa

Tatizo kubwa la akina mama ni kwamba wengi wao hufanya kazi ya kuajiriwa huku wakifanya pia kazi zote za nyumbani. Akina mama wengi hulazimika kufanya kazi ya kuajiriwa kwa sababu ya mahitaji ya familia. Wanajua kwamba wasipofanya kazi ya kuajiriwa, watoto wao watakosa vitu vingi. Mishahara yao ni muhimu kwa familia, ijapokuwa mara nyingi ni ya kiasi kidogo kuliko mishahara ya wanaume wanaofanya kazi hiyohiyo.

Kwa mfano, asilimia 42 ya wafanyakazi walioajiriwa huko São Paulo, Brazili, ni wanawake. Gazeti moja la huko lilisema kwamba akina mama wasiofanya kazi ya kuajiriwa ni ‘wachache sana.’ Vijijini huko Afrika, ni jambo la kawaida kumwona mama akibeba kuni kichwani na mtoto mgongoni.

Kazi ya Kuajiriwa Inazidi

Tatizo jingine ni kwamba waajiri wengi hutarajia akina mama wafanye kazi kwa muda wa saa nyingi. Na hayo si matatizo yote. Maria, anayeishi Ugiriki, aliombwa na mwajiri wake kutia sahihi hati iliyosema kwamba hangepata mimba kwa muda wa miaka mitatu. Kama angepata mimba, angehitaji kulipa fidia. Maria aliitia sahihi hati hiyo. Lakini alipata mimba mwaka mmoja na nusu baada ya kuajiriwa kazi. Mwajiri wake alimwonyesha hati ambayo Maria alikuwa ametia sahihi. Maria alifikisha kisa hicho mahakamani ili kupinga sera ya kampuni hiyo na sasa anangoja uamuzi wa mahakama.

Huenda waajiri wengine, ambao si wakali hivyo, wakawashurutisha akina mama kurudi kazini haraka iwezekanavyo baada ya kuzaa. Kwa kawaida hawapunguziwi saa za kazi wanaporudi kazini. Kwa hiyo, wajibu wao wa kutunza mtoto mdogo hautiwi maanani. Hawawezi kuomba likizo kwa muda mrefu kwa kuwa wangekosa fedha za kununua mahitaji. Pia, huenda wakakosa mahali pazuri pa kutunzia watoto, na kupokea msaada mdogo sana wa kifedha kutoka kwa serikali.

Kwa upande mwingine, akina mama wengine hufanya kazi ya kuajiriwa kwa sababu wanataka kutimiza miradi fulani, bali si kwa sababu ya magumu ya kifedha. Baada ya kuzaliwa kwa kila mmojawapo wa watoto wake wawili, Sandra aliamua kurudi kazini. Anasema kwamba alipojikuta nyumbani peke yake na mtoto mchanga, ‘nyakati nyingine alisimama kwenye dirisha kutazama nje, na kufikiria kile ambacho watu wengine walikuwa wakifanya.’ Na akina mama wengine hufanya kazi ya kuajiriwa ili waepuke mfadhaiko wa kutunza watoto. Gazeti la Daily Telegraph la Uingereza liliripoti hivi: “Wazazi wengine hubaki kazini kwa muda wa saa nyingi zaidi kwa kuwa kuna utulivu huko. Jambo hilo hupunguza hata zaidi muda wanaotumia pamoja na watoto wao, na watoto wao huzidi kuwa wachokozi, wasiotii na wasiojali.”

Kufanya Kazi Zote Sawasawa

Kufanya kazi ya kuajiriwa na kazi ya nyumbani si rahisi. Akina mama wengi wangekubaliana na mama mmoja anayeishi Uholanzi aliyesema hivi: ‘Mimi huchoka sikuzote. Hata mimi huamka nikiwa nimechoka. Ninaporudi nyumbani baada ya kazi, mimi huwa nimechoka sana. Watoto husema, “Mama amechoka sikuzote,” na hiyo hunifanya nijihisi kuwa nina hatia. Sitaki kukosa kwenda kazini, lakini ninataka vilevile kuwa mama mwenye urafiki anayeweza hali zote. Lakini sijafaulu kuwa mama mkamilifu jinsi ambavyo ningetaka.’

Yeye ni mmojawapo wa mamilioni ya mama walioajiriwa ambao wanaamini kwamba watoto hawataumia sana maadamu wanatumia muda mfupi pamoja nao ifaavyo. Lakini yeye ameona kwamba jambo hilo halijaleta matokeo mazuri. Mama wengi siku hizi wanasema kwamba wao huchoka na kufadhaishwa wakifanya kazi za nyumbani na pia kazi ya kuajiriwa, na kwamba hawalipwi vya kutosha.

Wanawake wanapotumia muda mrefu mbali na watoto, watoto hukosa kile ambacho wanahitaji sana, yaani, wakati na utunzaji wa mama yao. Fernanda A. Lima, mtaalamu wa akili ya watoto huko Brazili anasema kwamba hakuna anayeweza kutimiza daraka la mama vizuri jinsi mama anavyofanya. Anasema hivi: “Miaka miwili ya kwanza ya mtoto ni muhimu zaidi. Mtoto mdogo hivyo hawezi kuelewa kwa nini mama yake hayupo.” Mtu mwingine anaweza kumsaidia mtoto na mahitaji yake, lakini hawezi kuwa mama yake kamwe. Lima anasema: “Mtoto mchanga huhisi kwamba mama yake hamjali.”

Kathy, anayefanya kazi ya kuajiriwa na aliye na binti mdogo, alisema hivi: ‘Ninahisi kana kwamba ninamtoroka [ninapomwacha kwenye nyumba ya kutunzia watoto]. Inanihuzunisha kujua kwamba ninakosa kuona mtoto wangu akikua, na kwamba anawapenda zaidi watunzi wake kuliko mimi.’ Mhudumu mmoja wa abiria wa ndege huko Mexico alisema: “Baada ya muda, mtoto wako hakufahamu wala kukuheshimu kwa kuwa humlei. Wanajua kwamba wewe ni mama yao, lakini wao humpenda zaidi yule mwanamke anayewatunza.”

Kwa upande mwingine, akina mama wanaobaki nyumbani ili watunze watoto wao hupuuzwa na kushushwa hadhi kwa sababu kazi ya kuajiriwa husifiwa sana katika jamii. Katika jamii kadhaa, mwanamke asiyeajiriwa haheshimiwi, kwa hiyo wanawake hulazimika kutafuta kazi ya kuajiriwa, hata ikiwa mishahara yao haihitajiki.

Mama Anafanya Kazi Zote Nyumbani

Tatizo jingine la akina mama ni kwamba: Baada ya kufanya kazi siku nzima na kurudi nyumbani wakiwa wamechoka, wao hawapumziki bali wanaanza kazi za nyumbani. Kwa kawaida, akina mama hutarajiwa kutunza nyumba na watoto, wawe wameajiriwa kazi au la.

Ijapokuwa akina mama wengi hufanya kazi ya kuajiriwa kwa muda mrefu kuliko waume wao, nyakati nyingine akina baba hao hawawasaidii na kazi za nyumbani. Gazeti la The Sunday Times la London lilisema hivi: ‘Huku Uingereza, akina baba hawapatikani nyumbani. Uchunguzi mpya unaonyesha kwamba wanaume hutumia dakika 15 tu kwa siku pamoja na watoto wao. . . . Wanaume wengi hawafurahii sana kutumia wakati pamoja na familia zao. . . . Kwa kulinganisha, akina mama Waingereza wanaofanya kazi ya kuajiriwa hutumia dakika 90 kila siku pamoja na watoto wao.’

Waume wengine hulalamika kwamba wake zao hawapendi kusaidiwa kufanya kazi za nyumbani kwa sababu wanataka kazi hizo zifanywe kama vile wanavyozifanya. Waume husema: “Usipofanya vile wanavyofanya umekosea.” Ni wazi kwamba ikiwa mama-watoto aliyechoka atasaidiwa na mume wake, ni lazima akubali njia mbalimbali za kufanya kazi hizo. Kwa upande mwingine, mume hapaswi kutumia jambo hilo kama udhuru wa kutosaidia.

Matatizo Mengine

Desturi zinaweza kuongeza magumu. Huko Japani, akina mama hutarajiwa kulea watoto wao jinsi wengine wanavyofanya. Ikiwa watoto wengine hujifunza kupiga piano au kuchora, mama hulazimika kuruhusu watoto wake wafanye vivyo hivyo. Shule huwashurutisha wazazi kuwaruhusu watoto wao kushiriki katika shughuli zilezile za baada ya shule ambazo watoto wengine hushiriki. Mtu asipofanya hivyo, anaweza kuonewa na watoto, walimu, wazazi wengine, na watu wa ukoo. Tatizo hilo hukumba wazazi katika nchi nyingine vilevile.

Huenda watoto wakatarajia wazazi wawape vitu vingi kwa sababu ya matangazo mengi ya biashara na jinsi ambavyo ununuzi hukaziwa siku hizi. Katika nchi zilizoendelea, huenda akina mama wakahisi kwamba wanapaswa kuwapa watoto wao kila kitu wanachotaka kwa sababu watoto wengine wanapewa vitu hivyo na mama zao. Wasipoweza kufanya hivyo, huenda wakahisi wameshindwa.

Mazungumzo haya kuhusu akina mama wa siku hizi hayapaswi kutufanya tusithamini kazi ya mamilioni ya mama wanaojitahidi na wanaojitolea sana kutimiza mojawapo ya miradi muhimu, yaani, kulea watoto watakaoendeleza jamii ya binadamu. Kazi hiyo ni pendeleo. Biblia inasema hivi: “Watoto ni baraka na zawadi kutoka kwa BWANA.” (Zaburi 127:3, Contemporary English Version) Miriam, aliye na watoto wawili, anawawakilisha mama hao anaposema: “Licha ya magumu, akina mama hupata furaha isiyo na kifani. Sisi akina mama huhisi uradhi tunapowaona watoto wetu wakikubali mazoezi na nidhamu wanayopewa, na hivyo kuwa watu wanaotegemeka katika jamii.”

Ni nini kinachoweza kuwasaidia akina mama kufurahia zawadi yao zaidi? Sehemu inayofuata ina mawaidha mbalimbali.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 4 Mfululizo huu unazungumzia hasa hali ya akina mama walioolewa. Wakati ujao, gazeti la Amkeni! litazungumzia magumu ya akina mama wasio na wenzi wa ndoa.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

“Siku ya Mama”

Ufukara, ukosefu wa elimu, waume wazembe, kupigwa mara nyingi, na ugonjwa wa UKIMWI hukumba akina mama kusini mwa Afrika. Katika Siku ya Mama ya hivi majuzi, gazeti la The Citizen, la Afrika Kusini liliripoti hivi: “Maelfu ya wanawake watapigwa au kubakwa na wenzi wao, na wengine watauawa katika Siku ya Mama.” Matatizo hayo huwafanya maelfu ya akina mama wa Afrika Kusini wawatupe watoto wao kila mwaka. Katika kipindi cha miaka miwili cha hivi karibuni, watoto waliotupwa waliongezeka kwa asilimia 25. Jambo baya hata zaidi ni idadi inayoongezeka ya wanawake wanaojiua. Hivi majuzi, mwanamke aliyeishi katika eneo lenye umaskini alishika watoto wake watatu na kusimama kwenye reli wakati gari-moshi lilipopita. Wote wakafa. Ili kujiruzuku, baadhi ya akina mama hufanya kazi ya umalaya na kuuza dawa za kulevya au kuwatia moyo binti zao wafanye hivyo.

Inaripotiwa kwamba huko Hong Kong “akina mama fulani vijana huwaua watoto wao au huwatupa katika mapipa ya takataka wanapojifungua kwani hawawezi kuwatunza watoto hao.” “Gazeti la South China Morning Post lilitaja kwamba wanawake wengine walioolewa huko Hong Kong “wamefadhaika hivi [kwamba] wao hupata ugonjwa wa akili kiasi cha kujiua.”

[Sanduku katika ukurasa wa 7]

Akina Mama Katika Nchi Mbalimbali

Hakuna wakati

❖ Uchunguzi uliofanywa huko Hong Kong ulionyesha kwamba asilimia 60 ya akina mama walioajiriwa kazi hawahisi kwamba wanatumia wakati wa kutosha pamoja na watoto wao. Na asilimia 20 ya watoto walio na umri usiozidi miaka mitatu, ambao wazazi wao hufanya kazi ya kuajiriwa, hawaishi nyumbani wakati wa siku za kazi. Kwa kawaida watoto hao hukaa kwa babu na nyanya.

❖ Wanawake huko Mexico hutumia miaka 13 hivi maishani kutunza angalau mtoto mmoja mwenye umri usiozidi miaka mitano.

Akina mama na kazi ya kuajiriwa

❖ Nchini Ireland asilimia 60 ya wanawake hawafanyi kazi ya kuajiriwa bali wao hukaa nyumbani ili kutunza watoto. Asilimia 40 hivi ya wanawake hufanya hivyo nchini Hispania, Italia, na Ugiriki.

Kusaidia kufanya kazi za nyumbani

❖ Asilimia 80 ya wake wasioajiriwa kazi huko Japani walisema kwamba wangetaka mtu mmoja wa ukoo awasaidie kufanya kazi za nyumbani, hasa wanapokuwa wagonjwa.

❖ Nchini Uholanzi wanaume hutumia muda wa saa 2 hivi pamoja na watoto, na dakika 42 kufanya kazi za nyumbani. Wanawake hutumia muda wa saa 3 hivi pamoja na watoto na saa moja na dakika 42 kufanya kazi za nyumbani.

Akina mama wenye kazi nyingi mno

❖ Zaidi ya asilimia 70 ya akina mama huko Ujerumani huhisi kwamba wana kazi nyingi mno. Na asilimia 51 hivi huwa na matatizo ya uti wa mgongo na vifupa vyake. Zaidi ya theluthi ya mama hao huhisi wamechoka na kushuka moyo daima. Asilimia 30 hivi huumwa na kichwa au kuugua kipandauso.

Akina mama wanaopigwa

❖ Asilimia 4 ya wanawake waliohojiwa huko Hong Kong, walisema kwamba walipigwa na wenzi wao walipokuwa wajawazito.

❖ Uchunguzi uliofanywa na gazeti la Focus huko Ujerumani ulionyesha kwamba karibu mama 1 kati ya 6 alikubali kwamba mtoto wake alikuwa amempiga angalau mara moja.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Kazi ya akina mama yaweza kufadhaisha sana, kwani wanawake wengi hufanya kazi ya kuajiriwa na kutunza familia zao