Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Kuutazama Ulimwengu

Je, Ni Msaada Unaodhuru?

Gazeti la The Daily Yomiuri linasema kwamba mbinu fulani ya kuhifadhi kasa wa Japani aina ya loggerhead inatiliwa shaka. Kufukua mayai ya kasa, kuyaangua kwa mashine, na kisha kuwaachilia kasa wachanga baharini huenda kukaharibu uwezo wao wa kisilika wa kujielekeza wanaposafiri baharini. Gazeti hilo linaripoti kwamba kasa wanaoanguliwa bila msaada wa wanadamu “hugundua mvuto wa sumaku duniani wanapotembea-tembea mchangani, na hivyo wao hukuza uwezo wa kisilika wa kutambua mwelekeo. Kasa wanaoanguliwa katika mashine hufungiwa katika eneo dogo kabla ya kupelekwa baharini, na hivyo wao huzuiwa kukuza uwezo wao wa kisilika wa kutambua mwelekeo na uwezo wao wa kusafiri baharini peke yao.”

Tabasamu Ni Muhimu

Gazeti la The Times la London linasema kwamba “kutabasamu ni njia bora ya kupata marafiki na kuvutia watu.” Mahojiano yaliyofanywa kwa niaba ya shirika la Royal Mail yanaonyesha kwamba jambo la kwanza ambalo watu wengi huona wanapokutana na mtu ni tabasamu yake. Karibu nusu ya wale waliohojiwa walisema kwamba hawangefanya biashara na mtu anayeonekana kuwa hana urafiki. Wakurugenzi wanawake hasa hupenda kuwapandisha cheo wafanyakazi wanaopenda kutabasamu. Brian Bates, mmojawapo wa waandishi wa kitabu The Human Face anasema hivi: “Uchunguzi huo unaonyesha kwamba kutabasamu ni muhimu katika jamii. Sisi hupenda kuwaeleza watu wanaotabasamu siri zetu na matumaini yetu, na kuwapa pesa.” Bates anaendelea kusema kwamba kutabasamu huongeza protini za endorphin zinazopunguza maumivu mwilini, na watu wanaotabasamu bila kujifanya “hufanikiwa zaidi maishani mwao na kazini.”

Saa Zilizo Sahihi Kabisa

Gazeti la The Times la London linaripoti kwamba wanasayansi fulani Wamarekani wamebuni saa ya ioni za zebaki ambayo huonyesha ‘wakati kwa usahihi kabisa kufikia kipimo cha femtosecond moja (sehemu moja ya trilioni elfu moja ya sekunde). Hicho ndicho kipimo kidogo zaidi cha wakati kinachotumiwa na wanasayansi.’ Inasemekana kwamba saa hiyo ni sahihi “karibu mara 1,000 zaidi ya saa za atomi zinazotumiwa kupima Wakati wa Ulimwengu, yaani, wakati unaokubalika kotekote duniani.” Mwanafizikia Scott Diddams anaeleza hivi: ‘Saa hiyo itatumiwa kwanza na wanafizikia kuchunguza ulimwengu kwa undani.’ Hatimaye, itatumiwa vilevile kuboresha mifumo ya simu na setilaiti zinazoongoza vyombo vya kusafiri. Ijapokuwa Diddams anadai kwamba hiyo ndiyo “saa sahihi kabisa ulimwenguni,” anasema kwamba inawezekana kuiboresha.

“Sensa Sahihi Kuliko Zote”?

Gazeti la The Wall Street Journal linasema kwamba sensa iliyofanywa Marekani mwaka wa 2000 ilikuwa “sensa sahihi kuliko zote zilizowahi kufanywa.” Hata hivyo, “matokeo ya sensa hiyo ya mwaka wa 2000 yanatia ndani watu milioni 5.77 ambao kulingana na Idara ya Sensa wapo lakini hawakupatikana wakati wa kuhesabu.” Gazeti hilo linaeleza hivi: “Wakati ambapo maafisa wa sensa walikosa watu nyumbani, waliwahesabu kwa ‘kukadiria’ idadi yao kwa kompyuta kupatana na habari mbalimbali, kama vile maelezo ya majirani.” Walifanya hivyo hata wakati ambapo hawakuwa na uhakika kwamba nyumba fulani inakaliwa na watu. Walikadiria idadi ya watu walioishi humo, umri wao, jinsia yao, jamii yao, na kama walikuwa waseja au wamefunga ndoa. Afisa mmoja alisema kwamba makadirio hayo yanaonwa kuwa sahihi “kwa sababu kwa kawaida watu hupenda kuishi karibu na watu wa jamii yao.” Katika majimbo fulani, zaidi ya asilimia 3 ya idadi ya Wamarekani ilikadiriwa kwa njia hiyo, na makadirio yalitumiwa kukisia jamii ya watu zaidi ya milioni 11.

Miti Inayoua?

Kuna ubishi mkali kuhusu miti 400,000 hivi iliyoko kandokando ya barabara mbalimbali huko Ufaransa. Inasemekana kwamba miti inayokua kandokando ya barabara husababisha vifo wakati misiba ya barabarani inapotokea. Gazeti la L’Express la Ufaransa linaripoti kwamba vifo 799 kati ya vifo 7,643 vilivyotokea barabarani mwaka wa 2000 vilihusisha kugonga mti. Lakini, watu wengine husema kwamba kile kinachosababisha vifo hivyo si miti bali ni utumizi wa kileo na kwenda kasi kupita kiasi. Hata hivyo, kati ya miti 10,000 na 20,000 ambayo iko chini ya meta mbili kutoka barabarani itakatwa. Gazeti hilo la Ufaransa lilirejelea makala ya mhariri katika jarida la The Wall Street Journal iliyozungumzia jambo hilo na kusema kwamba yaelekea miti hiyo “imekosea sana kwa kutowaondokea madereva waliolewa.”

Je, Maandishi ya Kichina Yanatoweka?

Gazeti la The Daily Telegraph la London linasema kwamba “Herufi za Kichina, ambazo vizazi vingi vya watoto Wachina wamejifunza kwa taabu, sasa zimo katika hatari ya kutoweka kwa sababu ya kompyuta. Wachina wengi wenye elimu, ambao walijivunia kuweza kukariri herufi hizo 6,000, wanasahau jinsi ya kuandika. Bado wanajua kusoma, lakini hawajui jinsi ya kuandika herufi hizo bila kutumia kompyuta zao.” Hali hiyo inaitwa “‘ti bi wang zi,’ yaani, kusahau herufi mara tu unapoanza kuandika.” Kufikia miaka ya 1980, karibu maandishi yote yaliandikwa kwa mkono, lakini tangu wakati huo, programu za kompyuta za hali ya juu zimetumiwa ili kuandika herufi za Kichina. Hivyo, ustadi wa kuandika herufi maridadi kwa mkono unasahaulika. Jambo hilo “linawatia wasiwasi wataalamu wa lugha, madaktari wa akili, na wazazi. Inasemekana kwamba ustadi huo unaweza kufunua sifa za ndani za mtu, na unathaminiwa sana.”

Vijana Wanaotaka Kupunguza Uzito

Gazeti la Globe and Mail linasema kwamba asilimia 27 ya wasichana Wakanada 1,739 wenye umri wa kati ya miaka 12 hadi 18 ambao walihojiwa hivi majuzi wana dalili za matatizo ya kula. Waliohojiwa walikuwa watu wanaoishi mjini, wanaoishi karibu na mjini, na watu wa mashambani, nao walijibu maswali yaliyohusu maoni yao kuhusu kula na umbo la miili yao. Uchunguzi huo ulionyesha kwamba baadhi ya wasichana wenye umri wa miaka 12 hula kupita kiasi, kisha husafisha tumbo (kwa kujitapisha), au wao hutumia dawa za kupunguza uzito, dawa za kuharisha, na dawa za kuongeza mkojo, ili kupunguza uzito. Dakt. Jennifer Jones, mwanasayansi anayefanya utafiti kwenye Taasisi ya Afya ya Chuo Kikuu cha Toronto, anasema kwamba wasichana hasa “wanapaswa kuwa na maoni yanayofaa kuhusu chakula na mazoezi. Wanapaswa kuelewa miili yao na hawapaswi kuiga miili ya watu wanaoonyeshwa katika matangazo ya biashara, katika magazeti, na katika video za roki.” Gazeti la Globe linaongeza kwamba “wasichana wengi wanaobalehe hawajui kwamba ni jambo la kawaida kunenepa katika kipindi hicho na kwamba jambo hilo ni muhimu ili mtu akomae ifaavyo.”

Wanafunzi Hutumia Dawa Shuleni

Gazeti la Südwest Presse la Ujerumani linaripoti kwamba watoto wengi zaidi wanatumia dawa kwa sababu ya mfadhaiko wanaopata shuleni. Inasemekana kwamba mtoto 1 kati ya watoto 5 wa shule za msingi hutumia dawa za kupunguza wasiwasi au dawa za kuboresha vipawa. Katika shule za sekondari, mwanafunzi 1 kati ya wanafunzi 3 hutumia dawa hizo. Hata hivyo, Albin Dannhäuser, msimamizi wa Shirika la Walimu wa Bavaria, anasema kwamba kutumia dawa za kutuliza mfadhaiko au kuboresha matokeo shuleni si suluhisho bora, kwa sababu hakuwasaidii watoto kutatua matatizo yao. Anawashauri wazazi kutotarajia mengi mno kutoka kwa mtoto wao, bali “wafikirie afya yake ya mwili na akili na vilevile wazingatie kujenga utu imara.”

Magugu Yanayoudhi Hutumiwa

Gazeti la India Today linasema kwamba “magugu sugu kama vile gugu-maji, lantana, na parthenium yamewafadhaisha waendelezaji wa ardhi.” Mmea wa Lantana camara uliingizwa India na Waingereza mwaka wa 1941 ili upandwe kama nyua za miti, na sasa umeenea kwenye ekari 200,000 za ardhi na haiwezekani kuumaliza kwa kuung’oa, kwa kemikali za kuua magugu, wala kwa vitu vya asili. Sumu ya gugu hilo huzuia mimea mingine kusitawi na vijiji kadhaa vimehamishwa baada ya gugu hilo kuingia katika maeneo fulani. Hata hivyo, gugu hilo limewaletea wenyeji wa kijiji cha Lachhiwala faida za kiuchumi. Wao hutumia mmea wa lantana pamoja na udongo kujenga nyumba na vibanda vya kuku. Gugu hilo, ambalo haliathiriwi na wadudu na wanyama waharibifu, hutolewa maganda yake na kutumiwa kutengeneza fanicha na vikapu bora. Majani ya mmea huo hutumiwa kutengeneza dawa za kufukuza mbu na vilevile vijiti vya ubani. Mizizi ya mmea huo husagwa na kutumiwa kuzuia magonjwa ya meno.

Athari ya Kukata Tamaa

Dakt. Stephen L. Stern wa idara ya magonjwa ya akili kwenye Kituo cha Sayansi ya Tiba cha Chuo Kikuu cha Texas huko San Antonio anauliza hivi: “Ni kwa nini watu fulani hufa huku wengine walio na magonjwa kama yao wakiendelea kuishi? Sababu moja huenda ikawa kwamba watu fulani wana tumaini huku wengine hawana.” Uchunguzi wa Wamarekani wazee 800 unaonyesha kwamba mara nyingi watu ambao wamekata tamaa hufa mapema. Hata hivyo, watafiti wanasema kwamba watu wanapokosa tumaini wao huathiriwa kwa njia tofauti-tofauti ikitegemea mambo yaliyowapata utotoni, utamaduni, hali ya uchumi, na iwapo wameshuka moyo.