Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Picha Zenye Kuvutia Kwenye Miamba Huko Val Camonica

Picha Zenye Kuvutia Kwenye Miamba Huko Val Camonica

Picha Zenye Kuvutia Kwenye Miamba Huko Val Camonica

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI ITALIA

KWA maelfu ya miaka, picha hizo zimeonyesha jinsi watu walivyoishi zamani za kale. Picha za uwindaji, kilimo, vita, na ibada zimechongwa kwenye mawe katika mtindo fulani. Katika sehemu maridadi ya Val Camonica katika Milima ya Alps huko kaskazini mwa Italia, miamba imepambwa na maelfu ya picha za aina hiyo.

Leo, watu wanaotembelea Val Camonica mapema asubuhi baada ya jua kuchomoza wanaweza kuziona picha hizo waziwazi. Lakini ni nani waliozichonga, na kwa nini?

Watu wa Camunian

Bonde hilo maridadi liliitwa kwa jina la wakazi wake wa kale, yaani watu wa Camunian. Wanatajwa kwa mara ya kwanza katika historia mwaka wa 16 K.W.K., wakati waliposhindwa na Waroma na kupoteza uhuru wao. Hata hivyo, uchongaji wa picha za Val Camonica ulianza miaka mingi kabla ya jeshi la Roma kufika huko.

Picha hizo zinaonyesha vitu kama vile silaha, vyombo, mifugo, na ramani za vijiji. Kwa hiyo, wataalamu wanasema kwamba wasanii waliozichonga walikuwa wa jamii ya watu waliofanya kazi nyingi mbalimbali. Yaonekana walifanya kazi nyingi, kama vile uhunzi, kutengeneza nguo, kilimo, kufuga wanyama, na biashara.

Picha nyingi zilichongwa katika milenia ya kwanza K.W.K., ijapokuwa nyingine ni za kale zaidi. Utamaduni wa watu wa Camunian ulifikia kilele chake kati ya mwaka wa 1000 na 800 K.W.K. Maelfu ya picha za kipindi hicho zinaonyesha mambo mbalimbali kuhusu maisha yao. Picha hizo zinaonyesha watu waliokamatwa vitani wakiwa wamefungwa pamoja, na wanaume wenye mikuki waliopanda farasi. Pia kuna picha za wahunzi, farasi wanaovuta mizigo, magari ya farasi, na vilevile majengo yaliyoimarishwa kwa nguzo.

Wasanii Waliochochewa na Milima

Wataalamu wanasema kwamba wale waliochonga picha hizo walikuwa ‘wasanii na vilevile makuhani,’ yaani, wanaume waliosukumwa na imani ya kidini na ya mizungu. Huenda walijitenga katika mahali pa faragha mbali na vijiji na miji ili waweze kufikiri na kutafakari. Huenda watu wa Camunian walichochewa hasa kufanya hivyo kwa sababu ya matukio mawili ya ajabu ya asili ambayo hutukia huko siku chache kila mwaka.

Katika majira fulani ya mwaka, jua huchomoza nyuma ya mlima mrefu wa Pizzo Badile. Katika siku fulani kabla ya mapambazuko, miale ya jua humulika mlima huo na kutokeza kivuli kikubwa. Kivuli hicho huzungukwa na miale miangavu na anga jeupe. Ono hilo lenye kuvutia bado linaitwa “roho ya mlima.” Jua hutua upande ule mwingine wa bonde, nyuma ya ufa mwembamba katika Mlima Concarena. Kabla tu ya jua kutua, mwale mwangavu ambao huonekana ni kana kwamba unagawanya mlima huo, huangaza kwa dakika chache anga linaloanza kuwa jeusi, kisha linafifia. Yaelekea kwamba wakazi wa kale wa bonde hilo wasioelewa sababu za matukio hayo walifikiri yalisababishwa na viumbe wa roho.

Picha nyingi zinapatikana kwenye Mlima Pizzo Badile na kwenye maeneo yaliyo karibu. Picha zilichongwa kwa vifaa vilivyotengenezwa kwa mawe, pembe, mifupa, na pembe za ndovu. Nyakati nyingine wasanii walichonga mchoro kwa kutumia kifaa chenye ncha kali. Picha nyingine hazikuchongwa sana, na nyingine zilichongwa sana hata kufikia zaidi ya sentimeta tatu miambani. Yaelekea wasanii walitumia pia rangi mbalimbali, ingawa rangi hizo sasa haziwezi kuonekana kwa macho.

Picha Zilikuwa Aina ya Sala

Huenda watu wa Camunian waliabudu jua. Kuna picha nyingi zinazoonyesha mtu anayeomba mbele ya kisahani huku akiwa ameinua mikono. Huenda kisahani hicho kiliwakilisha jua. Ingawa Ausilio Priuli, ambaye ni mtaalamu wa vitu vya kale, anasema kwamba “ibada ya mungu wa jua” ilikuwa dini kuu, anataja pia “dini ndogo-ndogo.” Anasema hivi: “Matukio ya kidini yaliyochongwa mara nyingi yalitia ndani maandamano, dansi za upatanisho, utoaji wa dhabihu, mapambano ya kidini, na sala za watu wote. Uchongaji ulikuwa aina ya sala.” Lakini waliomba nini?

Emmanuel Anati, mtaalamu wa sanaa ya kale ya miamba, anasema kwamba uchongaji wa picha ‘ulionwa kuwa jambo la lazima ili kuhakikisha mafanikio ya uchumi na ya kijamii, na uhusiano mzuri pamoja na roho.’ Yaelekea kwamba watu wa Camunian waliamini kwamba wangepata mazao mazuri kwa kuchonga picha za watu wanaolima, kuboresha maeneo ya malisho kwa kuchonga picha za mifugo, kupata ushindi vitani kwa kuchonga picha za vita, na kadhalika.

Val Camonica ni kati ya Mirathi ya Ulimwengu ambayo inahifadhiwa na Shirika la Elimu, Sayansi, na Utamaduni la Umoja wa Mataifa. Jambo la kupendeza ni kwamba miamba yenye picha zilizochongwa na kupakwa rangi inapatikana katika angalau nchi 120 huko Afrika, Amerika Kaskazini na Kusini, Asia, Australia, Ulaya, na kwenye visiwa vingi. Na picha zilizochongwa miambani kotekote ulimwenguni zinaonyesha matukio yaleyale. Picha hizo zinaonyesha tamaa ya wanadamu ya kujieleza na ya kutafuta msaada kwa viumbe wa roho.

[Picha katika ukurasa wa 26]

Miale ya jua inapenya ufa kwenye Mlima Concarena

Val Camonica ni mojawapo ya Mirathi ya Ulimwengu

Picha zilizochongwa miambani ili kuhakikisha mafanikio katika uwindaji

Picha ya mwanadamu anayeomba akiwa ameinua mikono

[Hisani]

▼ Mlima Concarena: Ausilio Priuli, “IL Mondo dei Camuni”; rock carvings and human figure: Parco nazionale delle incisioni rupestri: su concessione del Ministero per i Beni e le Attività Culturali. Ogni riproduzione è vietata