Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Jengo Lenye Maduka Mahali pa Biashara na Starehe

Jengo Lenye Maduka Mahali pa Biashara na Starehe

Jengo Lenye Maduka Mahali pa Biashara na Starehe

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AUSTRALIA

WATU fulani hupenda sana kwenda madukani kununua vitu hali wengine huchukia sana jambo hilo. Hata hivyo, watu wengi wameanza kufurahia kwenda madukani tangu majengo yenye maduka yalipoanza kujengwa.

Wazo la kuwa na maduka mbalimbali mahali pamoja si jambo jipya. Majengo yenye maduka ni kama yale masoko ya kale yaliyokuwa na mfuatano wa maduka. Masoko hayo yalikuwa vituo vya biashara na vya kupigia gumzo. Mnamo mwaka wa 1859, Aristide Boucicaut, mfanyabiashara Mfaransa, alitumia wazo hilo alipoanzisha duka kubwa lenye bidhaa tofauti-tofauti zilizopangwa katika sehemu kadhaa. Hivyo, bidhaa mbalimbali zingeweza kupatikana humo. Maduka hayo makubwa yaliongezeka haraka katika sehemu nyingi za Ulaya na Marekani.

Frank Woolworth ni kati ya watu walioanzisha maduka ya aina hiyo. Kufikia Machi 1912, alikuwa ameanzisha maduka makubwa 600. Hatimaye, maduka makubwa na yale yaliyouza bidhaa maalumu yakaanzishwa katika jengo moja kama yale majengo yenye maduka ya leo. Kwa ujumla, majengo yenye maduka yamewasaidia wauzaji wa rejareja kupata faida kubwa, kwani biashara katika jengo moja lenye maduka mengi yaweza kutokeza dola milioni 200 za Marekani kwa mwaka.

Jambo moja kuu linalozingatiwa katika majengo yenye maduka ni kuwastarehesha wanunuzi. Njia moja ya kufanya hivyo ni kuwaandalia chakula. Mikahawa na maduka ya kuuza vitafunio huwafanya wanunuzi wafurahi na kushiba na hivyo kukaa kwa muda mrefu katika majengo hayo. Mbinu nyingine ya kuwafanya watu wanunue vitu ni kuwavutia kwa vitu wanavyotamani badala ya vitu wanavyohitaji. Gazeti moja lilisema kwamba jengo lenye maduka ni mahali ‘ambapo mwanamke anayeishi viungani anaweza kutazama bidhaa tofauti-tofauti zenye thamani ya mamilioni ya dola zikiwa zimepangwa nyuma ya kioo kinachomulikwa kwa taa.’

Baada ya kuwavutia wanunuzi, hatua inayofuata ni kuwafanya wanunue bidhaa. Njia bora ya kufanya hivyo ni kuwafanya wafurahie kununua bidhaa! Watangazaji wa biashara hujaribu kuwavutia watu wa jinsia zote. Hata hivyo, kama ilivyotajwa hapo juu, wanawake ndio wanaolengwa hasa. Kwa muda mrefu, wasimamizi wa majengo yenye maduka na watangazaji wa biashara wamewashawishi wanawake na hata akina mama walio na watoto kununua vitu katika maduka yao. Zaidi ya kununua bidhaa, wateja hupata nafasi ya kupiga gumzo na kukusanyika wanapokuwa katika majengo yenye maduka kwani kuna sehemu za kuwatunzia watoto, sehemu za kuwaburudisha vijana, sinema, na vyumba vya kuchezea michezo ya kompyuta. Na wanunuzi hukutana na kupumzika mikahawani. Kwa kujali mapendezi ya wanunuzi wanaopenda michezo, jengo moja lenye maduka mengi huko Australia lina sehemu ya mchezo wa kuteleza kwenye barafu, na jingine lina sehemu ya mchezo wa kuviringisha mipira.

Inaonekana kwamba vijana hupenda sana kwenda kwenye majengo yenye maduka. Kijana mmoja anasema hivi: “Marafiki wangu wengi huja hapa. Kila mara ninapokuja hapa, mimi hukutana na mtu fulani ninayemjua. . . Sisi hukutana kwenye meza hii.” Wazee wengi pia hupenda kwenda kwenye majengo yenye maduka. Mwanamke mmoja wa miaka 86 anasema hivi: “Mimi huja hapa kukutana na marafiki. Hapa ndipo mahali penye watu walio na urafiki zaidi. . . . Kama si mahali hapa, singefurahia maisha.”

Kwa upande mwingine, wanunuzi wengi wanakubali kwamba kusudi la jengo lenye maduka ni kuuza bidhaa kama vile kitabu Shelf Life kilivyosema. Jarida la The Humanist linaongeza kusema kwamba majengo yenye maduka ni “sehemu ya jamii yetu inayowafanya wanadamu kuwa wenye thamani kwa sababu tu ya fedha walizo nazo.” Bila shaka, katika mazingira kama hayo, ni lazima mtu awe na usawaziko ili kuepuka kunaswa na mtego wa kutamani mali.—Mathayo 6:19-21.

Hatari za Ununuzi

Watu fulani hawapendi kwenda kwenye majengo yenye maduka kwa sababu wao huogopa sehemu zilizosongamana watu wengi. Na ni kweli kwamba majengo mengi yenye maduka huwa na watu wengi mno, hasa mwishoni mwa juma. Kwa mfano, kila mwaka watu wapatao milioni 19 hutembelea jengo moja lenye maduka huko Sydney, Australia. Idadi hiyo inalingana na idadi ya watu huko Australia. Lakini sio wanunuzi tu wanaohangaishwa na umati wa watu. Inaonekana kwamba visa vya wizi katika maduka huongezeka wakati vijana wengi wanapokwenda kwenye majengo yenye maduka. Ndiyo sababu gazeti la SundayLife! linasema hivi: “Tatizo moja kuu katika maduka hayo ni jinsi ya kushughulika na vijana wengi wanaokusanyika huko.”

Tatizo jingine ambalo wenye maduka fulani hukabili ni kuongezeka kwa kodi mara kwa mara. Mwenye duka mmoja alilalamika hivi: “Biashara kadhaa zinafilisika kwa sababu hiyo.” Gazeti la Forbes linaeleza tatizo hilo kwa kusema hivi: ‘Majengo yenye maduka yanaweza kupambwa kisha wapangaji wapya wanaopenda madoido wakaingia kwenye maduka hayo. Lakini wapangaji hao hulipa pesa nyingi.’ Makala hiyo pia inatabiri kwamba huenda biashara zinazoendeshwa katika majengo yenye maduka huko Marekani zitapata hasara. Hizo ni habari mbaya kwa yale majengo 1,900 yenye maduka nchini humo. Makala hiyo inasema hivi: “Wanunuzi wanapungua.”

Majengo yenye maduka yatapatwa na nini wakati ujao? Kama mambo mengi maishani yalivyo, jambo hilo halijulikani kwa sasa. Lakini kuna jambo linalojulikana wazi: Sikuzote watu watapenda kwenda mahali ambapo wanaweza kununua bidhaa huku wakistarehe!