Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Karne ya Ujeuri

Karne ya Ujeuri

Karne ya Ujeuri

ALFRED NOBEL aliamini kwamba amani ingeweza kudumishwa iwapo mataifa yangekuwa na silaha hatari. Kwani, mataifa yangeweza kuungana upesi na kumwangamiza adui yeyote. Aliandika kwamba “jambo hilo lingekomesha vita kabisa.” Nobel alionelea kwamba hakuna taifa lolote timamu ambalo lingezusha mapigano iwapo lingeathiriwa vibaya na mapigano hayo. Lakini matukio ya karne iliyopita yameonyesha nini?

Miaka isiyozidi 20 baada ya kifo cha Nobel, Vita ya Kwanza ya Ulimwengu ilianza ghafula. Silaha mpya zilizo hatari zilitumiwa katika mapigano hayo, kama vile bunduki za rashasha, gesi yenye sumu, vifaa vya kurusha mafuta moto, vifaru, ndege, na nyambizi. Wanajeshi wapatao milioni kumi waliuawa, na zaidi ya milioni ishirini wakajeruhiwa. Ukatili uliofanywa katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu uliwafanya watu watamani tena amani. Kwa hiyo, Ushirika wa Mataifa ukaanzishwa. Rais Woodrow Wilson wa Marekani, ambaye alihusika sana katika harakati hizo, alishinda Tuzo ya Nobeli ya Amani mwaka wa 1919.

Hata hivyo, matumaini ya kukomesha vita yaliambulia patupu mnamo mwaka wa 1939, wakati Vita ya Pili ya Ulimwengu ilipozuka. Katika njia nyingi vita hiyo ilikuwa yenye kuogofya kuliko Vita ya Kwanza ya Ulimwengu. Wakati wa mapigano hayo, Adolf Hitler alipanua kiwanda cha Nobel huko Krümmel kikawa mojawapo ya viwanda vikubwa zaidi vya silaha huko Ujerumani, kikiwa na zaidi ya wafanyakazi 9,000. Kisha, mwishoni mwa vita hiyo, kiwanda cha Nobel kiliharibiwa kabisa na ndege za vita za Mataifa ya Muungano, ambazo ziliangusha zaidi ya mabomu elfu moja. Inashangaza kwamba mabomu hayo yalitengenezwa kwa vifaa ambavyo Nobel alibuni.

Mbali na zile vita mbili za ulimwengu, kulikuwa na mapigano mengi madogo-madogo katika karne iliyofuata kifo cha Nobel. Silaha ziliongezeka sana katika kipindi hicho, na nyingine zikawa hatari zaidi. Hebu fikiria baadhi ya silaha za vita ambazo zilitumiwa sana baada ya kifo cha Nobel.

Silaha nyepesi. Hizo zatia ndani bastola, bunduki, makombora, bunduki za rashasha, na silaha nyingine zinazobebeka kwa urahisi. Silaha nyepesi si bei ghali na ni rahisi kuzidumisha na kuzitumia.

Je, silaha hizo zimekomesha vita kwa kuwaogopesha raia? La hasha! Katika gazeti la Bulletin of the Atomic Scientists, Michael Klare anaandika kwamba silaha nyepesi ndizo “silaha kuu ambazo zimetumiwa katika mapigano mengi sana baada ya kile kipindi cha Vita ya Maneno.” Kwa kweli, katika mapigano ya hivi karibuni silaha nyepesi zilisababisha asilimia 90 ya vifo na majeruhi. Silaha hizo zilitumiwa kuua zaidi ya watu milioni nne katika miaka ya 1990 peke yake. Katika visa vingi, silaha nyepesi hutumiwa na vijana ambao wako tayari kuvunja sheria za vita na ambao hawajazoezwa kuwa wanajeshi.

Mabomu ya ardhini. Kufikia mwisho wa karne ya 20, mabomu ya ardhini yalikuwa yakiwalemaza watu 70 hivi kwa wastani kila siku! Wengi waliolemazwa walikuwa raia, bali si wanajeshi. Mara nyingi, mabomu ya ardhini hayatumiwi kuua, bali hutumiwa kulemaza na kuwatisha watu wanaoathiriwa nayo.

Ni kweli kwamba jitihada nyingi zimefanywa katika miaka ya hivi majuzi kuondoa mabomu ya ardhini. Lakini watu fulani wanasema kwamba kwa kila bomu moja linaloondolewa, mabomu mengine 20 hutegwa na kwamba huenda ikawa kuna mabomu milioni 60 yaliyofukiwa ardhini ulimwenguni pote. Ingawa mabomu ya ardhini hayawezi kutofautisha kati ya mwanajeshi na mtoto anayecheza karibu na eneo lililotegwa, bado silaha hizo hatari zinaendelea kuundwa na kutumiwa.

Silaha za nyuklia. Wakati silaha za nyuklia zilipobuniwa, iliwezekana kuharibu jiji zima kwa sekunde chache tu, bila wanajeshi kupigana vita. Kwa mfano, fikiria ule uharibifu mkubwa uliotokea wakati mabomu ya nyuklia yalipoangushwa huko Hiroshima na Nagasaki mnamo mwaka wa 1945. Watu fulani walipofushwa na ule mwangaza mwingi kupita kiasi. Wengine waliathiriwa na sumu ya mnururisho. Wengi wakafa kwa sababu ya joto jingi na moto. Inakadiriwa kwamba watu 300,000 hivi walikufa katika majiji hayo mawili!

Huenda watu fulani wakasema kwamba kutupa mabomu katika majiji hayo kulizuia vifo vingi ambavyo vingetokea iwapo mapigano hayo yangeendelea bila matumizi ya silaha za nyuklia. Hata hivyo, watu fulani walishtuka sana walipoona jinsi watu wengi walivyoangamia, na wakaanza kuwashawishi wenye mamlaka kuzuia matumizi ya silaha hizo hatari ulimwenguni pote. Naam, wengi walihofu kwamba mwanadamu alikuwa amebuni njia ya kujiangamiza.

Je, silaha za nyuklia zimeleta amani kwa kiasi fulani? Wengine wanakubali jambo hilo. Wanasema kwamba silaha hizo hatari hazijatumiwa vitani kwa zaidi ya miaka 50. Hata hivyo, maoni ya Nobel kwamba silaha za kuwaangamiza watu wengi zingekomesha vita si ya kweli, kwani vita zinaendelea kwa kutumia silaha nyingine. Isitoshe, kulingana na Kamati ya Sera ya Nyuklia, maelfu ya silaha za nyuklia ziko tayari kutumiwa wakati wowote. Na katika wakati huu ambapo ugaidi umechacha sana, wengi wanaogopa kile kinachoweza kutukia magaidi wakipata vifaa vya kutengeneza mabomu ya nyuklia. Hata silaha hizo zikiwa mikononi mwa watu wenye idhini ya kuzimiliki bado kuna wasiwasi kwamba kosa moja tu linaweza kusababisha msiba ulimwenguni kwa bomu la nyuklia. Kwa wazi, silaha zinazosababisha uharibifu haziwezi kuleta amani ambayo Nobel alitabiri.

Silaha za kibiolojia na za kemikali. Kupigana kwa kutumia vijidudu huhusisha matumizi ya bakteria hatari au virusi, kama vile bakteria ya kimeta au virusi vya ndui. Ndui ni hatari sana kwani watu huambukizwa ugonjwa huo kwa urahisi. Pia kuna silaha za kemikali, kama vile gesi ya sumu. Kuna aina nyingi za silaha za kemikali, na ijapokuwa zimepigwa marufuku kwa miaka mingi, zingali zinatumiwa.

Je, silaha hizo kali na madhara yanayosababishwa nazo zimewafanya watu ‘waogope na kuvunja majeshi yao,’ kama vile Nobel alivyotabiri? Sivyo hata kidogo, kwani zimewafanya watu waogope sana wakifikiri kwamba huenda zikatumiwa siku moja—hata na watu wasiojua kuzitumia. Zaidi ya miaka kumi iliyopita, mkurugenzi wa Shirika la Marekani la Kudhibiti na Kupunguza Silaha alisema hivi: “Silaha za kemikali zinaweza kuundwa na mtu yeyote katika gereji lake, maadamu amejifunza mambo machache kuhusu kemia katika shule ya sekondari.”

Pasina shaka kwamba karne ya 20 ilikuwa na vita nyingi zilizosababisha uharibifu mkubwa kuliko katika kipindi kinginecho chote. Sasa mwanzoni mwa karne ya 21, matumaini ya kupata amani yanaonekana kuwa ndoto tu hata zaidi—hasa baada ya mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea huko New York City na Washington, D.C., mnamo Septemba 11, 2001. Steven Levy aliandika hivi katika gazeti la Newsweek: “Yaelekea hakuna mtu yeyote anayethubutu kuuliza iwapo tekinolojia ya hali ya juu itatumiwa kuwaimarisha watu waovu.” Kisha aliongeza hivi: ‘Ni nani ambaye angejua jinsi ya kushughulikia hali kama hiyo? Wanadamu wana tabia ya kukimbilia kufanya mambo wanayoona kuwa ni maendeleo halafu kuchanganua matendo yao baadaye. Tunakosa kufikiria kwamba msiba mkubwa sana unaweza kutokea huku tukifanya mambo yanayowezesha msiba wenyewe utokee.’

Hadi sasa, historia imeonyesha kwamba kuunda mabomu makali na silaha hatari hakujaleta amani ulimwenguni. Basi, je, amani ya ulimwenguni pote ni ndoto tu?

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Kupunguza Nishati ya Nitrogliserini

Mnamo mwaka wa 1846, Ascanio Sobrero, Mwitaliano aliyekuwa mtaalamu wa kemia, alivumbua umajimaji mzito wa mafuta wenye kulipuka unaoitwa nitrogliserini. Umajimaji huo ulikuwa hatari. Vipande vya glasi vilivyotokezwa na mlipuko vilimkata-kata Sobrero usoni, na hatimaye akaacha kutumia umajimaji huo. Isitoshe, Sobrero alishindwa kufumbua fumbo fulani kuhusu umajimaji huo: Umajimaji huo ulipomwagwa na kugongwa kwa nyundo, yale matone yaliyogongwa ndiyo tu yaliyolipuka, bila kuathiri mafuta yale mengine.

Nobel alifumbua fumbo hilo alipobuni kilipushaji fulani kwa kutumia kiasi kidogo cha kilipukaji ambacho kingeweza kuwasha kiasi kikubwa cha kilipukaji kingine. Kisha, mnamo mwaka wa 1865, Nobel alibuni fataki ya aina fulani—kidude kidogo chenye chumvi ya zebaki ambacho kiliingizwa ndani ya chombo chenye nitrogliserini kisha kikawashwa kwa fyuzi.

Hata hivyo, bado ilikuwa hatari kutumia nitrogliserini. Kwa mfano, mnamo mwaka wa 1864, mlipuko uliotokea katika karakana ya Nobel nje ya jiji la Stockholm uliwaua watu watano—kutia ndani ndugu mdogo wa Nobel aliyeitwa Emil. Kiwanda cha Nobel huko Krümmel, Ujerumani, kililipuliwa mara mbili. Pia, watu fulani waliathiriwa vibaya walipotumia umajimaji huo ili kuwasha taa zao, kupaka viatu rangi, au kuitia kwenye magurudumu ya magari yaliyoendeshwa na farasi. Hata wakati milima ilipolipuliwa, mafuta mengine yalipenya nyufa na kusababisha misiba baadaye.

Mnamo mwaka wa 1867, Nobel alifanya umajimaji huo wa mafuta kuwa mgumu kwa kuchanganya nitrogliserini pamoja na kiselga. Kiselga ni kifaa ambacho kinaweza kunyonya unyevunyevu lakini hakiwezi kulipuka. Basi, Nobel akatengeneza baruti kali. Ijapokuwa baadaye Nobel aliunda vilipukaji vya hali ya juu, inasemekana kwamba baruti kali ni mojawapo ya vitu muhimu sana alivyovumbua.

Vilipukaji ambavyo Nobel aliunda vimetumiwa pia kufanya mambo mengine mbali na vita. Kwa mfano, vilitumiwa sana katika ujenzi wa njia za chini kwa chini za St. Gotthard (1872-1882), kulipua magenge yaliyoko chini ya maji kwenye Mto East huko New York (1876, 1885), na katika kuchimba Mfereji wa Corinth huko Ugiriki (1881-1893). Hata hivyo, tangu wakati ambapo ilibuniwa, baruti kali imetumiwa hasa kuharibu na kuua.

[Picha]

Kituo cha polisi huko Kolombia kiliharibiwa kwa vilipukaji vyenye baruti kali

[Hisani]

© Reuters NewMedia Inc./CORBIS

[Picha katika ukurasa wa 4]

Miaka isiyozidi 20 baada ya kifo cha Nobel, silaha mpya hatari zilitumiwa katika Vita ya Kwanza ya Ulimwengu

[Hisani]

U.S. National Archives photo

[Picha katika ukurasa wa 6]

Watu waliojeruhiwa na mabomu ya ardhini huko Kambodia, Iraq, na Azerbaijan

[Hisani]

UN/DPI Photo 186410C by P.S. Sudhakaran ▼

UN/DPI Photo 158314C by J. Isaac

UN/DPI Photo by Armineh Johannes

[Picha katika ukurasa wa 6]

Kulingana na Kamati ya Sera ya Nyuklia, maelfu ya silaha za nyuklia ziko tayari kutumiwa wakati wowote

[Hisani]

UNITED NATIONS/PHOTO BY SYGMA ▸

[Picha katika ukurasa wa 7]

Watu wengi walitambua jinsi silaha za kemikali zilivyo hatari wakati gesi ya “sarin” ilipotumiwa kwenye njia ya magari-moshi yanayopita chini ya ardhi huko Tokyo mnamo mwaka wa 1995

[Hisani]

Asahi Shimbun/Sipa Press

[Picha katika ukurasa wa 5 zimeandaliwa na]

UN/DPI Photo 158198C by J. Isaac