Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kinywaji Chenye Kuburudisha Kutokana na Mmea wa Kigeni

Kinywaji Chenye Kuburudisha Kutokana na Mmea wa Kigeni

Kinywaji Chenye Kuburudisha Kutokana na Mmea wa Kigeni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI NIGER

JE, WEWE hufurahia kinywaji baridi katika siku yenye joto? Jamaa nyingi katika Afrika Magharibi hufurahia kinywaji kitamu chenye rangi ya kuvutia, chenye afya, cha bei rahisi, na ambacho kimetengenezwa kutokana na mmea. Kinywaji hicho kinaitwa bissap, na kinatengenezwa kutokana na mmea wa kitropiki unaoitwa haibiskasi. Mmea huo unaweza kukua hadi urefu wa meta mbili au zaidi. Huo hukuzwa katika maeneo mbalimbali ulimwenguni lakini hasa katika maeneo makavu zaidi kama yale yanayopatikana katika nchi za Niger, Mali, na Senegal.

Jinsi ya Kutayarisha Bissap

Weka kijiko kimoja cha kula cha sehemu za kijani za ua la mmea huo ndani ya lita moja hivi ya maji. Chemsha mchanganyiko huo na kuuacha kwa dakika 15 hadi 20. Ukiisha kuchuja sehemu za mmea, kinywaji chawa tayari kunywewa ama kikiwa baridi au moto, ama kikiwa na sukari au la. Kwa sababu leo tunataka kutayarisha kinywaji baridi ambacho watoto watafurahia, tutaongeza sukari. Jamaa nyingine huongeza pia ladha ya mnanaa au vanila. Kinywaji hicho chenye rangi nyekundu-nyangavu huwekwa ndani ya vifuko vidogo vya plastiki, ambavyo hufungwa kwa kutiwa fundo mdomoni. Sasa kinywaji kiko tayari kunywewa na watoto wanaokipenda! Watoto hufurahia kutoboa pembe ya kifuko hicho na kufyonza kinywaji wanachokipenda. Bila shaka, wengine hufurahia kukinywa kwa kutumia bilauri.

Zaidi ya kuwa kitamu, kinywaji cha bissap husemwa kuwa chenye afya. Kina kalisi, fosforasi, madini ya chuma, vitamini A na C na vitu vinginevyo! Wengine husema kwamba kinywaji hicho pia hutuliza akili, kinaongeza kiasi cha mkojo, na pia kusaidia utendaji wa ini. Kwa vyovyote vile, zaidi ya kuwa mmea maridadi, tunafurahi kwamba unatoa kinywaji chenye afya kinachoburudisha.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]

Photo by Kazuo Yamasaki