Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kutembelea Jiji la Dhahabu Nyeusi

Kutembelea Jiji la Dhahabu Nyeusi

Kutembelea Jiji la Dhahabu Nyeusi

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI BRAZILI

HUENDA hujapata kusikia kuhusu mji wa Ouro Prêto nchini Brazili, lakini katika karne ya 18, idadi ya wakazi wake ilikuwa mara tatu zaidi ya idadi ya watu waliokuwa New York City, na rasilimali zake zilitumiwa wakati mmoja kujenga upya jiji la Lisbon nchini Ureno wakati lilipoharibiwa kabisa na tetemeko la ardhi. Mnamo mwaka wa 1980, Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni, liliongeza mji wa Ouro Prêto kwenye Orodha ya Mirathi ya Ulimwengu. Sasa orodha hiyo inaonyesha maeneo 700 hivi ambavyo ni muhimu sana kwa utamaduni na mambo ya asili. Kwa nini mji wa Ouro Prêto ulipata hadhi hiyo? Fikiria historia ya mji huo wa kipekee.

Kinywaji Chenye Dhahabu

Katika nusu ya kwanza ya karne ya 17, wavumbuzi wengi kutoka Ureno, walioitwa bandeirantes, walienda Brazili kutafuta maeneo mapya, watumwa Wahindi Wekundu, na dhahabu. Kundi moja la wavumbuzi lilifika hadi Mlima wa Itacolomi. Akiwa huko, Duarte Lopes alikwenda kwenye kijito ili apate kukata kiu. Alichota maji kwenye bakuli lake la mbao na kuanza kuyanywa. Kisha akaona vijiwe vidogo vyeusi ndani ya bakuli.

Lopes alimuuzia vijiwe hivyo rafiki yake ambaye, akidhani vilikuwa na thamani kubwa, alivipeleka kwa gavana wa Rio de Janeiro. Gavana alipovichunguza vijiwe hivyo, alitambua kwamba ndani mlikuwa na dhahabu safi sana iliyokuwa imefunikwa na tabaka nyembamba nyeusi ya oksidi ya chuma. Lakini dhahabu hiyo ilikuwa imetoka wapi? Lopes alipoeleza mahali mlima wa Itacolomi ulipokuwa, uchunguzi ukaanza. Mnamo mwaka wa 1698, mvumbuzi aliyeitwa Antônio Dias de Oliveira alipata mlima huo. Watu waliotafuta dhahabu walifika upesi sana katika kituo kilichokuwa karibu na dhahabu, baadaye mahali hapo pakaitwa Vila Rica. Muda si muda, Vila Rica pakawa na wakazi 80,000. Baadaye, pakawa makao makuu ya jimbo la Minas Gerais na kuitwa Ouro Prêto, maana yake “Dhahabu Nyeusi.”

Dhahabu Nyeusi Yasababisha Umwagikaji wa Damu

Kati ya mwaka wa 1700 na 1820, watafutaji wa madini walichimba tani 1,200 za dhahabu—asilimia 80 ya dhahabu iliyochimbwa ulimwenguni pote wakati huo. Lakini dhahabu yote hiyo ilienda wapi? Dhahabu iliyochimbwa iliyeyushwa na kufinyangwa kuwa mikuo ya dhahabu kwenye Casa dos Contos, au Nyumba ya Sarafu. Kutoka hapo, asilimia 20 ya dhahabu hiyo, ambayo ilikuwa thamani ya kodi iliyotozwa, ilipelekwa kwa jamaa ya kifalme ya Ureno.

Wakoloni walipinga kodi hiyo. Mmoja wao alikuwa Felipe dos Santos, aliyewahimiza watafutaji wa madini, wanajeshi, na waumini wa kanisa kupinga mamlaka ya Mfalme wa Ureno. Lakini Wareno walipigana nao. Katika mwaka wa 1720, dos Santos alinyongwa na mwili wake kuburutwa barabarani kwa farasi. Wachimbaji walirudi kwenye migodi yao na kodi ikaendelea kupanda.

Hata hivyo, hilo halikukomesha uasi kwa muda mrefu. Baadaye katika karne hiyo kukatokea Joaquim da Silva Xavier, aliyeitwa kwa jina jingine Tiradentes, maana yake “mtu anayeng’oa jino.” Jina hilo lilihusiana na mojawapo ya kazi zake. Alikuwa sehemu ya kile kikundi cha washairi, wanasheria, na wanajeshi wa Ouro Prêto waliokutana kwa ukawaida katika nyumba ya kasisi aliyeitwa Toledo. Mwanzoni, walipiga gumzo kuhusu mambo ya falsafa, lakini baadaye wakaanza kuzungumza kuhusu siasa ya wakati ule: jinsi koloni za Uingereza huko Amerika Kaskazini zilivyokuwa zimepata uhuru, na jinsi Ufaransa ilivyowakata vichwa wafalme wake. Baadaye, mazungumzo yakawa ya uasi walipoanza kusemezana kwa siri kuhusu jinsi ambavyo Ufalme wa Ureno ulivyokuwa na uonevu mwingi. Malkia wa Ureno, Dona Maria wa Kwanza, alikuwa ameonya kwamba waasi wangekatwa vichwa. Hata hivyo, katika mwaka wa 1788, Tiradentes, ambaye wakati huo alikuwa na cheo jeshini, aliongoza Inconfidência Mineira, au Uasi wa Jimbo la Minas Gerais.

Mpelelezi mmoja alifichua majina ya wale waliopanga njama hiyo. Mmoja baada ya mwingine, walikamatwa na kuhamishwa huko Afrika ambako walifia. Tiradentes aliteseka katika jela lisilo na hewa ya kutosha huko Rio de Janeiro hadi aliponyongwa na kukatwa kichwa katika Aprili 21, 1792. Kichwa chake kiliwekwa juu ya mlingoti katikati mwa jiji la Ouro Prêto, na sehemu za mwili wake uliokatwa katika vipande vinne zilitundikwa kando ya barabara tofauti-tofauti. Kwa muda fulani, jambo hilo likazuia waasi wengine ambao wangetokea. Lakini miaka 30 baadaye, mnamo mwaka wa 1822, Brazili ilipata uhuru kutoka kwa Ureno.

Hazina za Sanaa, Historia, na Dini

Wakati ulipopita, dhahabu ya Ouro Prêto ilimalizika, na mji huo ukaacha kuwa muhimu. Lakini bado ulibaki na vyombo vya kale pamoja na kumbukumbu nyingine za historia yake. Baadhi ya vitu hivyo vinaweza kupatikana katika Jumba la Makumbusho la Inconfidência lililoko katika eneo la Praça Tiradentes. Jumba hilo la makumbusho, ambalo wakati mmoja lilikuwa ukumbi wa mji na jela, sasa linahifadhi kumbukumbu za sanaa, historia, na msiba uliopata mji huo.

Baadhi ya vitu ambavyo vinaonyeshwa ni hati ya agizo la kuuawa kwa Tiradentes, iliyotolewa na Dona Maria wa Kwanza, na vipande vya nguzo vilivyotumiwa kumnyonga. Mabaki ya miili ya watu waliohusika katika uasi pamoja na Tiradentes yamezikwa chini ya mawe yaliyopangwa katika safu kama vitanda vilivyo katika chumba kikubwa cha kulala. Katika orofa nyingine, kuna vyumba vyenye vitu vya kale vya wakati wa ukoloni na wa utawala wa maliki.

Mambo ya Kuwafurahisha Wale Wanaopenda Vito

Ukitembea hadi mwisho wa Praça Tiradentes utaona sehemu nyingine yenye hazina nyingi—lile Jumba la Kifalme la Gavana, ambalo lilitumiwa kupokea magavana na maraisi wa Majimbo mengine. Sasa, hapo ndipo ilipo Escola de Minas, taasisi ya elimu ya juu kuhusu ufundi wa kuchimba migodi, jiolojia, na sayansi ya metali. Jumba la makumbusho la taasisi hiyo linajivunia mkusanyo wa sampuli 20,000 za aina 3,000 za madini, vito, fuwele, na hata dhahabu nyeusi ya ouro prêto.

Leo dhahabu haipatikani sana katika sehemu hiyo. Hata hivyo, bado kuna aina kadhaa za beroli kama zumaridi na beroli ya bluu na topazi ya manjano aina ya imperial. Miaka 50 iliyopita, ni wataalamu wachache tu ndio waliojua ufundi wa kukata vito. Lakini leo kuna wengi wanaotafuta vito kwa udi na uvumba na pia kuna maduka mengi ya vito katika eneo la Praça Tiradentes. Wauzaji wa vito watakuonyesha jinsi ya kuvitambua na kukufahamisha kwa wakataji na wasafishaji ambao wamo katika vyumba vya nyuma. Wakataji watakuonyesha jinsi ya kuvikata vito hivyo. Ukarimu huo unaonyesha jinsi wenyeji wanavyojivunia kuishi katika mji wenye historia ya kupendeza.

Ikiwa unapanga kutembea Brazili, hakikisha umezunguka Ouro Prêto, eneo ambalo utafurahia kupiga picha.

[Ramani katika ukurasa wa 22]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

Ouro Prêto

[Hisani]

Ramani: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Wakati oksidi ya chuma inapotolewa, mawe meusi huwa vipande vya dhahabu

[Picha katika ukurasa wa 23]

Mji wa Ouro Prêto na Mlima wa Itacolomi ukionekana kwa mbali

[Picha katika ukurasa wa 24]

Jumba la Makumbusho la Inconfidência huko Praça Tiradentes

[Picha katika ukurasa wa 24]

Zumaridi, topazi ya manjano aina ya “imperial,” na beroli ya bluu

[Hisani]

Vito: Brasil Gemas, Ouro Preto, MG