Vyakula Bora Unavyoweza Kupata
Vyakula Bora Unavyoweza Kupata
NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI MEXICO
ANGÉLICA na jamaa yake ya watu kumi waliishi katika kijiji kidogo cha mashambani katika jimbo la Oaxaca, Mexico. Walikuwa maskini, na chakula chao kilikuwa chapati za mahindi, maharagwe, mchuzi wa pilipili, wali wenye umajimaji, mkate mtamu, na chai. Angélica anasema hivi: ‘Sisi hatukuwa warefu, tulikuwa wadogo na waliokonda. Tulikuwa wagonjwa mara nyingi—mara tuliumwa na tumbo, mara tulipata vimelea, na mafua.’
Angélica na jamaa yake waliamua kuhamia Mexico City, wakiwa na matumaini ya kupata kazi ambayo ingewawezesha kuinua hali yao ya kiuchumi. Sasa yeye anaamini wanakula vizuri
kwa sababu chakula chao kinatia ndani maziwa, mayai, nyama, malai, aina chache za mboga, na namna nyingi za vyakula vilivyotengenezwa viwandani. Lakini je, chakula chao kimekuwa bora?Ulaji Mbaya Umeenea Kadiri Gani?
Ulimwenguni kote, watu wapatao milioni 800 wamo katika hatari ya kufa kwa sababu ya kukosa chakula cha kutosha. Kulingana na Ripoti ya Afya ya Ulimwengu ya 1998 ya Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), karibu asilimia 50 ya vifo vya watoto wote chini ya miaka mitano vinasababishwa na ulaji mbaya. Mara nyingi, hata wale wanaookoka huendelea kuwa na afya mbaya.
Kwa upande mwingine, wengine wanakadiria kuwa watu milioni 800 wamo katika hatari ya kufa kwa sababu ya kula kupita kiasi. Mlo ambao si kamili waweza kusababisha magonjwa hatari kama vile unene wa kupita kiasi, mafuta kuziba mishipa ya damu, kupanda kwa shinikizo la damu, ugonjwa wa sukari, ugonjwa wa ini, na aina mbalimbali za kansa. Shirika la WHO linasema hivi kwa ufupi: “Ulaji mbaya unatia ndani mambo mengi, kama vile kutokula vya kutosha, kukosa aina fulani za vyakula, na kula kupita kiasi. Ulaji mbaya huua, hulemaza, hukawiza ukuzi, hupofusha, na huathiri ukuzi wa binadamu kwa kadiri kubwa sana katika ulimwengu mzima.”
Katika nchi ileile, kunaweza kuwa na watu wasiokula vya kutosha na pia watu wanene kupita kiasi. Katika nyumba ileile, kunaweza kuwa na watoto wenye utapiamlo na watu wazima ambao ni wanene kupita kiasi daima. Katika visa vingine, watu ambao walikosa chakula cha kutosha wakiwa watoto huwa wanene kupita kiasi wanapokuwa watu wazima. Jambo hilo la mwisho laweza kuwapata wale wanaohamia mjini kutoka mashambani.
Watu wengi hawaelewi jinsi ulaji wao unavyoathiri afya zao. Labda hiyo ni kwa sababu matokeo ya ulaji mbaya hayaonekani mara moja. Lakini chakula bora chaweza kuzuia magonjwa mengi. Kwa kweli, shirika la WHO linakadiria kwamba
asilimia 40 ya visa vya kansa vinaweza kuzuiwa kwa ulaji bora na kwa kufanya mazoezi. Lakini unaweza kuboreshaje chakula chako?Jinsi ya Kuboresha Chakula Chako
Watu fulani hugawanya chakula katika vikundi vitatu vikubwa. Kikundi cha kwanza kinatia ndani nafaka, kama vile mahindi, ngano, mchele, oat, shayiri, rai, na mtama, pia viazi, kama vile viazi ulaya na viazi vikuu. Vyakula hivyo vya wanga huongeza nishati mwilini. Kikundi cha pili kinatia ndani aina za maharagwe kama vile soya, dengu, chick-peas, na broad beans na vyakula vingine vinavyotokana na wanyama, kama nyama, samaki, mayai, maziwa, na vyakula vinavyotengenezwa kwa maziwa. Vyakula hivyo vina protini, madini ya chuma, zinki, na vitamini kadhaa. Kikundi cha tatu kinatia ndani matunda na mboga. Vyakula hivyo vina vitamini na madini muhimu. Pia, vinasaidia mwili kupata nyuzinyuzi na nishati, na ni vyanzo pekee vya vitamini C.
Kulingana na Dakt. Héctor Bourges, mkurugenzi Sayansi ya Tiba na Lishe katika Taasisi ya Kitaifa ya Lishe ya Salvador Zubirán (INNCMSZ) nchini Mexico, chakula bora lazima kiwe kamili, cha kutosha, na kiwe kimesawazishwa. Anapendekeza kwamba “tutie ndani angalau aina moja kutoka kwa kila kikundi cha chakula kwenye kila mlo na tuvibadili vyakula hivyo kadiri tuwezavyo, na pia tubadili jinsi ambavyo tunavitayarisha.”
Fikiria hali ya María. Yeye na familia yake waliishi huko Atopixco, ambalo ni eneo la mashambani katika jimbo la Hidalgo, Mexico. Walikuwa maskini hohehahe, na chakula chao cha kila siku kilikuwa chapati za mahindi, maharagwe, tambi, wali, na mchuzi wa pilipili. Tofauti na jamaa ya Angélica, iliyotajwa mwanzoni, chakula chao kilitia ndani mboga ndogo-ndogo kama mung’unye, chayotes, viyoga, na mimea kama purslane na pigweed, na mingi kati ya mimea hiyo ilipatikana mashambani. Pia, walikula matunda mara kwa mara wakati yalipopatikana kwa wingi. Jitihada zao ziliwaletea afya bora.
Dakt. Adolfo Chávez, msimamizi wa Idara ya Lishe na Elimu ya Lishe ya taasisi ya INNSZ, anapendekeza kwamba vyakula vinavyotokana na wanyama viongezwe kwenye vyakula vingine lakini visiliwe peke yake. Kwa mfano, unaweza kutayarisha chakula kwa kuchanganya mayai machache na viazi, mboga, au maharagwe. Dakt. Chávez anasema hivi: “Katika elimu ya lishe, mbinu hiyo huitwa ‘mbinu ya kuongezea.’” Hata hivyo, zingatia onyo hili: Sikuzote osha matunda na mboga vizuri, hasa ikiwa yataliwa bila kupikwa.
Lazima pia chakula kimfae kila mtu, na ni lazima mambo kama vile umri, jinsia, na namna ya mtu ya maisha yazingatiwe. Wengine hupendekeza kwamba watu wazima wale sehemu mbili za matunda na/au mboga kwenye kila mlo na kuongeza kiasi cha nafaka na maharagwe wanayokula. Wengine wanapendekeza kwamba vyakula vinavyotokana na wanyama vitumiwe kwa kiwango kidogo katika kila mlo, huku samaki, nyama ya kuku iliyoondolewa ngozi, na nyama isiyo na mafuta vikipewa nafasi ya kwanza. Pia, inapendekezwa kwamba mafuta na sukari zipunguzwe.
Hata wale wanaoishi katika nchi zinazoendelea na ambao wanakabiliana na umaskini wanaweza kuboresha chakula chao. Jinsi gani? Kwa kuteua vyakula bora mbalimbali na kuvichanganya, kama vile kuchanganya nafaka na aina za maharagwe. Kwa kutumia kiasi kidogo cha nyama na mayai ili kuboresha lishe. Kwa kutumia kwa faida mboga za kijani kibichi zinazositawi katika eneo lako na matunda yanayopatikana katika msimu huo.
Muumba wetu hutoa “chakula katika nchi” ili wanadamu wakifurahie. (Zaburi 104:14) Biblia inasema hivi kwenye Mhubiri 9:7: “Wewe enenda zako, ule chakula chako kwa furaha.” Bila shaka, tunaweza kufurahia manufaa za vyakula bora vitamu ambavyo Muumba wetu ametupatia tunapovitumia kwa kiasi na usawaziko.
[Picha katika ukurasa wa 26]
KIKUNDI CHA KWANZA: nafaka na viazi
[Picha katika ukurasa wa 26]
KIKUNDI CHA PILI: aina za maharagwe, nyama, samaki, mayai, maziwa, na vyakula vinavyotengenezwa kwa maziwa
[Picha katika ukurasa wa 26]
KIKUNDI CHA TATU: matunda na mboga