Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa

Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa

Kuunganisha Ulimwengu-Mazuri na Mabaya Yanayotarajiwa

‘Kuunganisha ulimwengu ndilo tukio la maana zaidi katika wakati wetu. . . . Linawawezesha mabilioni ya watu kotekote ulimwenguni kupata nafasi za kipekee za kufanya maendeleo.’—MARTIN WOLF, MWANDISHI WA MAMBO YA FEDHA.

“Sisi, watu wa Dunia, ni watu wa familia moja kubwa. Enzi mpya inatokeza magumu na matatizo mapya ulimwenguni, kama vile uharibifu mkubwa wa mazingira, kupunguka kwa mali-asili, vita vya umwagaji-damu na umaskini.”—EDUARD SHEVARDNADZE, RAIS WA GEORGIA.

MNAMO Desemba 1999, mkutano wa Shirika la Biashara Ulimwenguni huko Seattle, Marekani, ulikatizwa na ghasia. Polisi walitumia gesi ya kutoa machozi, risasi za mpira, na gesi kali ili kumaliza ghasia hizo. Kisha wakakamata mamia ya waandamanaji.

Ni nini kilichosababisha ghasia hizo huko Seattle? Ni mahangaiko mengi juu ya kupoteza kazi, mazingira, na ukosefu wa haki katika jamii. Hata hivyo, kwa ufupi, waandamanaji hao waliogopa jinsi ambavyo dunia na watu wangeathiriwa na wazo la kuunganisha ulimwengu.

Watu hawajaacha kuhangaikia jambo hilo. Tangu mwaka wa 1999, maandamano ya kupinga wazo la kuunganisha ulimwengu yameongezeka na kuwa yenye ujeuri hata zaidi. Sasa nyakati nyingine, viongozi wa ulimwengu wanajitahidi kufanya mikutano yao katika maeneo yaliyojitenga na ambako itakuwa vigumu kwa waandamanaji kuvuruga mazungumzo.

Kwa wazi, si kila mtu anaogopa wazo la kuunganisha ulimwengu. Ijapokuwa watu fulani husema kwamba kuunganisha ulimwengu ndicho kisababishi cha matatizo yaliyopo ulimwenguni, wengine wanasema kwamba hilo ndilo suluhisho la matatizo mengi ulimwenguni. Ni kweli kwamba huenda watu wengi wakaona kuwa mjadala huo hauwahusu, kwani wengi hawajafahamu sana maana ya kuunganisha ulimwengu. Lakini hata maoni yako yawe nini, tayari wazo la kuunganisha ulimwengu linakuathiri, na huenda likakuathiri hata zaidi katika siku zijazo.

Ni Nini Maana ya Kuunganisha Ulimwengu?

Usemi “kuunganisha ulimwengu” au “utandaridhi” unafafanua jinsi watu na nchi mbalimbali ulimwenguni zinavyozidi kutegemeana. Jambo hilo limeongezeka sana katika miaka kumi hivi iliyopita, hasa kwa sababu ya maendeleo makubwa ya tekinolojia. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 5.) Sasa, yaonekana kwamba mataifa yameacha kuhusika katika Vita ya Maneno, vizuizi vya biashara vimepungua au kuondolewa, masoko makubwa ya hisa ulimwenguni yamekuwa yakiungana, na usafiri umekuwa rahisi zaidi na wa bei nafuu.

Muungano huo wa ulimwengu ambao unaendelea kuimarika umeleta mabadiliko mengi ya kiuchumi, kisiasa, kitamaduni, na ya kimazingira. Kwa kuhuzunisha, baadhi ya mabadiliko hayo ni mabaya. Kichapo cha Umoja wa Mataifa kinachoitwa Human Development Report 1999 kinasema hivi: ‘Maisha ya watu ulimwenguni pote yameunganishwa zaidi na kwa njia ya moja kwa moja kuliko ilivyokuwa hapo awali. Jambo hilo hutokeza njia nyingi za kufanya mambo mapya ambayo yanaweza kuleta faida au hasara.’ Sawa na mafanikio mengi ya wanadamu, utandaridhi una mazuri na mabaya yake.

Mataraja ya Ulimwengu Wenye Ufanisi Zaidi

Amartya Sen, mshindi wa Tuzo ya Nobeli ya Uchumi alisema kwamba utandaridhi “umetokeza maendeleo ya kisayansi na ya kitamaduni ulimwenguni na pia kuwafaidi watu wengi kiuchumi.” Pia, kichapo cha Human Development Report 1999 kinasema kwamba utandaridhi “unatokeza njia nyingi zinazoweza kutumiwa kumaliza umaskini katika karne ya 21.” Matarajio hayo mazuri yametokana na jinsi ambavyo utandaridhi umetokeza ufanisi mwingi sana. Leo mapato ya familia ya kawaida ulimwenguni yameongezeka mara tatu kuliko yalivyokuwa miaka 50 iliyopita. *

Wachanganuzi fulani wanaona faida nyingine ya kuunganisha uchumi wa ulimwengu: Wanaonelea kwamba jambo hilo litazuia mataifa kushiriki katika vita. Katika kitabu chake kinachoitwa The Lexus and the Olive Tree, Thomas L. Friedman anasema kwamba utandaridhi ‘unawachochea watu sana wasipigane na kuongeza gharama za vita sana kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya kisasa.’

Watu wanaposhirikiana mara nyingi, umoja unaweza kuongezeka ulimwenguni pote. Mashirika fulani ya haki za binadamu yametumia Internet ili kufanikisha harakati zao. Kwa mfano, mkataba wa kimataifa wa kupiga marufuku mabomu ya ardhini ambao ulifanywa mwaka wa 1997 ulifaulu kwa kadiri fulani kwa sababu kompyuta zilitumiwa kuunganisha na kuwasiliana na mashirika mbalimbali ulimwenguni pote yaliyounga mkono harakati hiyo. Njia hiyo ya kuwahusisha watu wa kawaida ilitajwa kuwa “njia mpya ya kufanya mashauriano ya kimataifa, huku serikali na raia wakiungana kupambana na tatizo linalowahusu wanadamu ulimwenguni pote.”

Licha ya matokeo hayo mazuri, bado watu wengi wanahofu kwamba madhara ya utandaridhi ni mengi kuliko faida zake.

Kuhofu Kwamba Ulimwengu Utagawanyika Zaidi

Huenda hangaiko kuu kuhusu utandaridhi ni jinsi ambavyo umezidisha ile tofauti kati ya matajiri na maskini. Ijapokuwa ni wazi kwamba utajiri wa ulimwengu umeongezeka, ni watu wachache zaidi na nchi chache zaidi zilizo na utajiri huo. Sasa mali halisi za watu 200 matajiri zaidi ulimwenguni ni nyingi kuliko jumla ya mapato ya watu bilioni 2.4 hivi wanaoishi duniani—asilimia 40 ya watu wote duniani. Na ijapokuwa mapato yanaendelea kuongezeka katika nchi tajiri, mapato ya wastani katika nchi 80 zenye umaskini yamepungua katika muda wa miaka kumi iliyopita.

Hangaiko jingine la maana linahusu mazingira. Utandaridhi wa kiuchumi umechochewa na shughuli za biashara zinazokazia faida za kiuchumi kuliko kuhifadhi mazingira. Agus Purnomo, msimamizi wa Hazina ya Mazingira ya Ulimwenguni Pote huko Indonesia, anaeleza tatizo hilo hivi: ‘Tunataka maendeleo daima. Nina wasiwasi kwamba baada ya miaka kumi, tutakuwa tumefahamu umuhimu wa kutunza mazingira, lakini hakutakuwa na viumbe wa kuhifadhi.’

Watu pia wanahangaikia kazi zao. Imekuwa rahisi zaidi kupoteza kazi na mapato kwa sababu mashirika yanayoungana ulimwenguni pote na mashindano makali katika biashara yanalazimu makampuni kuboresha huduma zao. Makampuni yanayohangaikia kupata faida kubwa huona kwamba ni jambo la busara kuwaajiri na kuwafuta wafanyakazi kwa kutegemea faida inayopatikana, lakini jambo hilo huwaletea watu matatizo makubwa.

Kuongezeka kwa mikopo na fedha za kigeni ulimwenguni pote kumetokeza tatizo jingine. Watega-uchumi wa kimataifa wanaweza kukopesha nchi zinazoendelea fedha nyingi sana lakini baadaye kuondoa fedha zao kwa ghafula wakati hali ya uchumi inapozorota. Wakati fedha hizo zinapoondolewa nchi zinazohusika zinaweza kukumbwa na matatizo ya kiuchumi. Mnamo mwaka wa 1998, watu milioni 13 walifutwa kazi huko Asia Mashariki kwa sababu ya hali mbaya za kiuchumi. Huko Indonesia, mapato halisi ya wale wafanyakazi ambao hawakufutwa kazi yalipungua kwa asilimia 50.

Kwa sababu nzuri basi, watu wanatarajia mambo mabaya na vilevile mazuri kutokana na utandaridhi. Je, unapaswa kuogopa utandaridhi? Au, je, unaweza kutarajia kwamba utandaridhi utakuwezesha kufanikiwa maishani? Je, matokeo ya utandaridhi yametufanya tutarajie mazuri wakati ujao? Makala yetu inayofuata itajibu maswali hayo.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 12 Hata hivyo, makadirio ya wastani, hasa yale ya ulimwenguni pote, yanaweza kupotosha. Katika sehemu nyingi, mapato ya familia hayajaongezeka hata kidogo katika miaka 50 iliyopita, na katika sehemu nyingine mapato ya familia yameongezeka sana.

[Blabu katika ukurasa wa 3]

Mali halisi za watu 200 matajiri zaidi ulimwenguni ni nyingi kuliko jumla ya mapato ya asilimia 40 ya watu wote duniani

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]

VYOMBO VYA TEKINOLOJIA VINAVYOUNGANISHA ULIMWENGU

Maendeleo ya tekinolojia yamebadili mawasiliano kabisa katika kipindi cha miaka kumi iliyopita. Sasa ni rahisi zaidi kupata habari na kuwasiliana na watu haraka na kwa bei nafuu karibu katika sehemu zote ulimwenguni.

TELEVISHENI Siku hizi watu wengi ulimwenguni wanaweza kutazama televisheni, hata kama hawana televisheni zao. Kufikia mwaka wa 1995, kulikuwa na televisheni 235 kati ya kila watu 1,000 ulimwenguni. Idadi hiyo ilikuwa karibu mara mbili ya ilivyokuwa mwaka wa 1980. Watu walio katika maeneo ya mbali sana wanaweza kupata habari kutoka sehemu zote za ulimwengu kwa kutumia kifaa kidogo chenye umbo la sahani kinachopokea ishara za televisheni kutoka kwenye setilaiti. Francis Fukuyama, ambaye ni profesa wa uchumi wa kisiasa, anasema hivi: “Siku hizi, hakuna nchi ambayo haiwezi kupata habari za ulimwengu.”

INTERNET Kila juma watu wapatao 300,000 huanza kutumia Internet. Mnamo mwaka wa 1999, ilikadiriwa kwamba kufikia mwaka wa 2001 watu milioni 700 wangekuwa wameunganishwa kwenye Internet. Mwandishi Thomas L. Friedman anasema hivi: “Tokeo ni kwamba watu wengi sana wanajifunza kuhusu maisha ya watu wengine wengi, bidhaa zao, na dhana zao kuliko katika kipindi kingine cha historia.”

SIMU Gharama za simu zimeshuka sana kwa sababu ya mifumo ya setilaiti na kebo zilizotengenezwa kwa nyuzinyuzi za kioo. Mnamo mwaka wa 1930, bei ya kupiga simu kwa dakika tatu kutoka New York hadi London ilikuwa dola 245 za Marekani, lakini ilishuka hadi senti 35 za Marekani mnamo mwaka wa 1999. Mitandao ya kurusha ishara za redio imewawezesha watu wengi kuwa na simu za mkononi sawa na vile kompyuta zilivyo nyingi leo. Inakadiriwa kwamba kufikia mwisho wa mwaka wa 2002, watu bilioni moja watakuwa na simu za mkononi, na simu hizo zitawawezesha wengi wao kutumia Internet.

KIDUDE KIDOGO CHA KUPITISHA UMEME Vifaa vyote hivyo vilivyotajwa hapo juu, ambavyo vinaendelea kuboreshwa, vinategemea vidude vidogo vya kupitisha umeme. Katika muda wa miaka 30 iliyopita, uwezo wa vidude hivyo wa kupokea na kuhifadhi habari umeongezeka mara mbili baada ya kila miezi 18. Sasa habari nyingi zaidi zinahifadhiwa katika vidude hivyo vidogo sana kuliko wakati mwingine wowote.