Kuutazama Ulimwengu
Kuutazama Ulimwengu
Moshi wa Sigara Huwadhuru Wasiovuta Sigara
Gazeti la Kanada la Globe and Mail linaripoti hivi kuhusu uchunguzi uliofanywa hivi majuzi huko Japani: “Kupumua moshi wa sigara inayovutwa na mtu mwingine kwa dakika 30 tu kunaweza kudhuru moyo wa mtu mwenye afya asiyevuta sigara.” Kwa kutumia mbinu mpya ya kuchunguza mwili wa mwanadamu watafiti kwenye Chuo Kikuu cha Osaka City waliweza kupima jinsi chembe fulani za moyo na mishipa ya damu ya watu wasiovuta sigara inavyoathiriwa wanapopumua moshi wa sigara inayovutwa na watu wengine. Chembe hizo zinapokuwa hazina kasoro zinasaidia damu izunguke ifaavyo kwa kuzuia utando usifanyizwe kwenye kuta za mishipa ya damu na kuzuia damu isigande. Watafiti waliona kwamba damu ilitiririka vizuri zaidi katika mioyo ya watu wasiovuta sigara “kwa asilimia 20 hivi kuliko katika mioyo ya wale wanaovuta sigara. Lakini baada ya kupumua moshi wa sigara kwa dakika 30 tu,” mtiririko wao wa damu ulipunguka kufikia kiwango cha wale wanaovuta sigara. Mtafiti Dakt. Ryo Otsuka anasema hivi: “Jambo hilo linathibitisha moja kwa moja kwamba mtiririko wa damu katika moyo wa watu wasiovuta sigara huathiriwa wanapopumua moshi wa sigara inayovutwa na watu wengine.”
Ramani Zinazoonyesha Sehemu Zenye Taa Nyingi Mno
Jarida la Science linasema kwamba ‘mfumo wetu wa sayari, Kilimia, umepotea. Lakini haujapotea kwa sababu ya msiba mkubwa angani bali kwa sababu mwangaza mwingi wa majiji yetu makubwa huwazuia watu wengi huko Ulaya na Amerika wasione kundi hilo la nyota. Mwangaza huo wote unafadhaisha wataalamu wanaochunguza sayari kwa sababu unaweza kuzuia uchunguzi wao.’ Ili kuwasaidia watu wanaotazama nyota waliokata tamaa, wanasayansi huko Italia na Marekani wamechora ramani mpya zinazoonyesha sehemu zenye taa nyingi mno. Gazeti hilo la Science linasema kwamba ramani za awali zinaonyesha tu mahali ambapo “taa zinatapakaa kwenye mabara usiku.” Lakini, ramani hizo mpya, zinazopatikana kwenye Internet, ‘zinatia ndani ramani za mabara, na ramani chache zilizo na habari nyingi zaidi. Kwa mfano, zinaonyesha mahali ambapo inawezekana kuona nyota katika sehemu mbalimbali za Ulaya.’
Ramani ya Chini ya Bahari
Gazeti la Kanada la Financial Post linaripoti kwamba wanasayansi kwenye Taasisi ya Sayansi ya Bahari ya Bedford huko Nova Scotia ni wa kwanza kutumia tekinolojia mpya ili kuchora ramani ya chini ya bahari. Kwa kutumia mawimbi ya sauti, wanasayansi wanaweza kutengeneza picha ya chini ya bahari zinazoonyesha pande tatu. Katika hatua ya mwisho, “kamera za video zinazoongozwa kutoka mbali hushushwa hadi chini ya bahari na kiasi kidogo cha vitu vilivyoko huko chini huchukuliwa ili vichunguzwe.” Kulingana na ripoti hiyo, “ramani za chini ya bahari zinaweza kuleta faida kubwa sana.” Viumbe wanaoishi chini kabisa baharini wataweza ‘kuvuliwa bila kuharibu sehemu nyingine za chini ya bahari.’ Makampuni ya simu yataweza pia kujua mahali panapofaa na mahali ambapo hapagharimu sana kuweka nyaya za chini ya bahari. Makampuni ya mafuta yataweza kuchimba visima vya mafuta mahali ambapo pana mafuta mengi baharini na mahali ambapo havitaharibu mazingira.” Huenda ramani hizo pia zitawezesha kutolewa kwa mchanga na changarawe, inayopatikana kwa wingi baharini. Gazeti hilo linasema kwamba ‘huenda ikawa jambo hilo halitagharimu sana wala kuleta madhara sana’ kama kuchimba mawe milimani.
Kuelewa Ugonjwa wa Akili
Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) linaripoti kwamba “robo ya watu wote ulimwenguni wataugua ugonjwa wa akili au wa neva wakati fulani maishani mwao.” Ijapokuwa magonjwa mengi ya akili yanaweza kutibiwa, karibu thuluthi mbili za watu walio na magonjwa hayo hawaendi kupata matibabu. Dakt. Gro Harlem Brundtland, mkurugenzi-mkuu wa shirika la WHO, anasema hivi: “Mgonjwa wa akili hapaswi kuwa na maoni kwamba amejiletea ugonjwa wake. Badala yake, huenda sisi ndio tunapaswa kulaumiwa kwa sababu hatujawashughulikia wagonjwa wa akili na wa ubongo ifaavyo. Ninatumaini kwamba ripoti hiyo itaondoa mashaka na maoni ambayo watu wamekuwa nayo kwa muda mrefu, na kwamba wagonjwa wa akili watashughulikiwa ifaavyo kuanzia leo.” Shirika la WHO linasema kwamba hali ikiendelea namna hii, ‘kufikia mwaka wa 2020, idadi ya watu walioshuka moyo itazidi idadi ya watu wanaougua magonjwa mengine yote ila tu aina moja ya ugonjwa wa moyo.’ Hata hivyo, watu walioshuka moyo wakipata matibabu yanayofaa “wataweza kuishi maisha yenye mafanikio na kufaidi sana jamii zao.”
‘Ubani Unaweza Kudhuru Afya Yako’
Gazeti la New Scientist linaripoti kwamba ‘harufu tamu ya ubani inaweza kudhuru afya yako. Wabudha, Wahindu, na Wakristo wengi hupenda kufukiza ubani nyumbani mwao na mahali pao pa ibada wanapotafakari na kufanya matibabu. Ubani unapofukizwa, watu hupumua moshi wake hatari wenye kemikali zinazosababisha kansa.’ Ripoti hiyo inasema kwamba watafiti kadhaa, walioongozwa na Ta Chang Lin wa Chuo Kikuu cha Taifa cha Cheng Kung huko Tainan, Taiwan, “walichunguza hewa ndani na nje ya hekalu fulani huko Tainan City na kuilinganisha na hewa kwenye makutano ya barabara.” Ripoti hiyo inasema kwamba “viwango vya kemikali ya PAH [polycyclic aromatic hydrocarbons] ndani ya hekalu vilikuwa mara 19 zaidi ya vilivyokuwa huko nje, na juu kidogo kuliko kwenye makutano ya barabara.” Kulingana na gazeti la New Scientist, kiwango cha kemikali moja ndani ya hekalu kilikuwa ‘mara 45 kuliko ndani ya nyumba inayokaliwa na watu ambao huvuta sigara. Kemikali hiyo, ambayo inaitwa benzopyrene, inadhaniwa kuwa kisababishi cha kansa katika watu wanaovuta sigara.’
Kurekebisha Marumaru Iliyochakaa
Gazeti la The Times la London linasema kwamba “wanasayansi wamegundua njia ya ajabu ya kukuza marumaru kwa muda wa siku chache kwa kutumia bakteria.” Bakteria ndogo sana zinazopatikana udongoni zinakuzwa kwenye maabara katika umajimaji wenye pektini. Chakula chao chenye madini kinapoisha, bakteria hizo hufa na kuwa kalisi-kaboni safi, yaani, umajimaji wenye marumaru. Wakati michongo na vitu vingine vya marumaru ambavyo vimechakaa kwa sababu ya kuzeeka au kwa sababu ya hali ya hewa vinapopuliziwa umajimaji huo, vinafunikwa kwa utando mwembamba wa marumaru unaoshikamanisha jiwe. John Larson, msimamizi wa idara ya kuhifadhi michongo kwenye Majumba ya Makumbusho na Maonyesho huko Merseyside, Uingereza, anasema kwamba marumaru ya hali ya juu haipatikani kwa wingi siku hizi na kiasi kikubwa cha marumaru kinaweza kufanyizwa haraka kwa kutumia mbinu hiyo mpya bila madhara yoyote na kwa bei nafuu.
Wizi Katika Jina la Mungu
Deborah Bortner, msimamizi wa Shirika la Kulinda Watega-Uchumi la Amerika Kaskazini, anasema hivi: “Nimefanya kazi ya kuchunguza shughuli za kutega uchumi kwa miaka 20, na nimeona fedha nyingi zikiibwa kwa jina la Mungu kuliko katika njia nyingine yoyote. Unapotega fedha uwe macho hata ikiwa yule unayefanya biashara naye anasingizia kupendezwa na dini au imani yako.” Kulingana na gazeti la Christian Century, “katika miaka mitatu iliyopita, maafisa wanaochunguza shughuli za kutega uchumi katika majimbo 27 wamechukua hatua dhidi ya makampuni mengi na watu waliojisingizia kupendezwa na mambo ya kiroho au imani ya kidini ili kufanya watega-uchumi kuwaamini. . . . Katika kisa kinachojulikana sana kilichoendelea [kwa zaidi ya miaka mitano],” shirika moja la Kiprotestanti “lilikusanya zaidi ya dola milioni 590 za Marekani kutoka kwa watega-uchumi zaidi ya 13,000 kotekote nchini. Maafisa wanaochunguza shughuli za kutega uchumi walifunga shirika hilo mwaka wa 1999, na watatu kati ya wasimamizi wake walikubali mashtaka ya ulaghai.” Gazeti la Christian Century linaripoti kwamba “watu walipoteza jumla ya dola bilioni 1.5 za Marekani” katika visa vingine vitatu.
Ongezeko la Joto la Dunia Husababisha Misiba
Gazeti la Uingereza la Guardian Weekly linasema hivi: “Baada ya kuripoti kuhusu ongezeko kubwa la idadi ya misiba iliyosababishwa na hali ya hewa katika miaka ya mwishomwisho ya 1990,” shirika la Msalaba Mwekundu linaonelea kwamba ‘misaada inayotolewa na mataifa haitatosha ili kushughulikia hasara inayosababishwa na ongezeko la joto la dunia. Katika Ripoti ya Misiba Duniani ya kila mwaka, Shirikisho la Kimataifa la Mashirika ya Msalaba Mwekundu na ya Mwezi Mwekundu linasema kwamba misiba kama vile mafuriko, dhoruba, maporomoko ya ardhi, na ukame, ilitokea mara 200 hivi kila mwaka kabla ya mwaka wa 1996. Idadi hiyo iliongezeka hatua kwa hatua kufikia 392 katika mwaka wa 2000.’ Roger Bracke, msimamizi wa idara ya kutoa msaada ya shirikisho hilo, anadhani kwamba idadi ya misiba ya asili itaendelea kuongezeka na alisema hivi: “Msaada unaotolewa una mipaka fulani; tunahofia kwamba siku moja tutashindwa kutoa msaada.” Kulingana na gazeti la Guardian, “thuluthi mbili ya watu [milioni 211] walioathiriwa na misiba ya asili kila mwaka katika miaka kumi iliyopita walikumbwa na mafuriko. Asilimia 20 ya watu hao waliathiriwa na njaa, na hiyo ilisababisha vifo vingi kuliko msiba mwingine, yaani, asilimia 42 hivi ya vifo vyote vilivyosababishwa na misiba ya asili.”