Linda Uwezo Wako wa Kusikia!
Linda Uwezo Wako wa Kusikia!
“Zaidi ya watu milioni 120 ulimwenguni wana matatizo ya kusikia.”—Shirika la Afya Ulimwenguni.
UWEZO wetu wa kusikia ni zawadi inayopaswa kuthaminiwa. Hata hivyo, kadiri tunavyoendelea kuzeeka, ndivyo uwezo wetu wa kusikia unavyoendelea kupunguka. Ulimwengu wa sasa unatokeza sauti nyingi tofauti-tofauti na makelele ambayo yanaelekea kuharibu uwezo wa kusikia mapema zaidi. Mwanasayansi mashuhuri katika Taasisi Kuu ya Viziwi huko St. Louis, Missouri, Marekani, anasema hivi: “Karibu robo tatu ya matatizo ya kusikia ambayo Mwamerika mmoja anakabili yanatokana na yale ambayo amesikiliza maishani mwake bali si kwa sababu ya uzee tu.”
Kusikiliza sauti kubwa, hata kwa muda mfupi kwaweza kuharibu sehemu za ndani za sikio lako zilizo nyororo. Hata hivyo, mara nyingi, matatizo ya kusikia husababishwa na “kazi zenye makelele, makelele unayosikia wakati unapofanya mambo unayoyapenda, na burudani zenye kelele,” ndivyo anavyosema mtaalamu wa uwezo wa kusikia Dakt. Margaret Cheesman. Unaweza kufanya nini ili kulinda uwezo wako wa kusikia? Ili kujibu swali hilo, ni muhimu kujua mambo fulani kuhusu jinsi uwezo wako wa kusikia unavyofanya kazi.
Sauti Tunazosikia
Mazingira tunamoishi yanazidi kuwa na makelele mengi zaidi. Kila siku wengi wanakabiliana na sauti za aina tofauti kuanzia za magari, mabasi, na malori barabarani, hadi sauti za juu sana za mashine za umeme kazini.
Nyakati nyingine sisi huzidisha tatizo kwa kuweka sauti za juu katika vifaa tunavyosikiliza. Njia moja ya kusikiliza muziki inayopendwa na wengi ni kutumia vidude vya kusikiliza vinavyovaliwa masikioni ambavyo vimeunganishwa na kifaa kinachobebeka cha kuchezea kaseti au CD. Kulingana na Marshall Chasin, mmoja wa waanzilishi wa Vyama vya Wanamuziki vya Kanada, uchunguzi uliofanywa nchini humo na katika Marekani unaonyesha kwamba vijana wanaendelea kupoteza uwezo wao wa kusikia kwa sababu ya kutumia vidude
vya kusikiliza muziki vinavyovaliwa masikioni huku wakiweka sauti ya juu kupita kiasi.Ni kiasi gani cha sauti kinachoweza kusemwa kuwa cha kupita kiasi? Sauti inaweza kukadiriwa kwa kutumia vipimo vitatu—muda wa kuisikiliza, frikwensi, na kiasi cha sauti yenyewe. Muda wa kusikiliza ni kipindi cha wakati ambao mtu anakabiliana na sauti fulani. Frikwensi hupimwa kulingana na mizunguko ya sauti katika kila sekunde, au hezi. Vipimo vya frikwensi ya sauti ya kawaida inayosikika vizuri ni kuanzia mizunguko 20 hadi 20,000 kwa kila sekunde.
Kiasi cha sauti, au ukubwa wake, hupimwa kwa kipimo kinachoitwa desibeli (dB). Kiasi cha sauti cha maongezi ya kawaida ni desibeli 60 hivi. Wataalamu wa sauti wanasema kwamba kadiri unavyosikiliza sauti inayozidi desibeli 85, ndivyo unavyokabili uwezekano mkubwa zaidi wa kupoteza uwezo wako wa kusikia hatimaye. Kadiri sauti inavyozidi kuwa kubwa ndivyo inavyoharibu uwezo wa kusikia haraka zaidi. Ripoti moja katika gazeti la Newsweek inasema hivi: “Sikio lako linaweza kustahimili kwa saa mbili iwapo unafanya kazi na mashine ya umeme ya kutoboa mashimo (100dB), lakini haliwezi kustahimili zaidi ya nusu saa katika chumba cha kuchezea michezo ya video chenye makelele mengi (110dB). Kila ongezeko la desibeli 10 katika kiasi cha sauti linamaanisha kwamba kelele inayoweza kuharibu sikio imeongezeka mara 10.” Utafiti umethibitisha kwamba sauti za kuanzia desibeli 120 hivi husababisha uchungu. Jambo la kushangaza ni kwamba redio fulani za nyumbani zinaweza kutoa sauti ya zaidi ya desibeli 140!—Ona sanduku.
Ili kukusaidia kuelewa kwa nini sauti kubwa zinaweza kuharibu uwezo wako wa kusikia, hebu tuchunguze kile kinachofanyika sauti inapoingia masikioni mwako.
Jinsi Masikio Yetu Yanavyofanya Kazi
Sehemu ya nje ya sikio ina umbo ambalo huiwezesha kuchota mawimbi ya sauti na kuyaingiza kwenye mfereji wa sikio, ambapo yanaweza kufikia kiwambo cha sikio. Mawimbi hayo hufanyiza mitetemo katika kiwambo cha sikio, nacho hutokeza mitetemo kwenye mifupa mitatu iliyomo katika sikio la kati. Kisha, mitetemo hiyo hupitishwa hadi kwenye sikio la ndani, ambamo kuna kifuko kilichojaa umajimaji ambacho kinazingirwa na mfupa. Katika sehemu hiyo mitetemo husafiri kupitia umajimaji ulio katika komboli, ambayo ni sehemu ya sikio la ndani yenye umbo la konokono na ina chembe zilizo kama nywele. Umajimaji ulio katika komboli huchochea sehemu ya juu ya chembe hizo zilizo kama nywele ili zitokeze misukumo ya neva inayoweza kutambuliwa. Hatimaye misukumo hiyo ya neva husafirishwa hadi kwenye ubongo ambamo zinageuzwa na kutambuliwa kuwa sauti.
Mfumo wa ubongo unaoshughulikia hisia na msukumo husaidia ubongo kuamua ni sauti zipi zinahitaji kupewa uangalifu na ni zipi ambazo zitapuuzwa.
Kwa kielelezo, huenda mama asishughulike anaposikia sauti ya mtoto akicheza, lakini ataitikia mara moja mtoto anapolia akiomba msaada. Kusikiliza kwa masikio yote mawili ni muhimu sana kwani huturuhusu kupata sauti kwa njia nzuri kutoka pande zote na hutusaidia kutambua upande ambao sauti inatoka. Hata hivyo, wakati wa mazungumzo, ubongo wetu unaweza kuelewa ujumbe mmoja tu kwa wakati mmoja. Kitabu kinachoitwa The Senses kinasema hivi: “Hiyo ndiyo sababu, mtu anapoongea kwa simu, hawezi kusikia yale ambayo mtu mwingine aliye karibu naye anasema.”Jinsi Makelele Yanavyoharibu Uwezo Wetu wa Kusikia
Ili uelewe jinsi sauti kubwa zinavyoharibu uwezo wetu wa kusikia, fikiria mfano unaofuata. Ripoti moja kuhusu usalama kazini inafananisha chembe zilizo kama nywele katika sikio la ndani na zao la ngano shambani na kulinganisha sauti zinazoingia humo na upepo. Upepo mwanana, kama sauti ndogo, utafanya sehemu ya juu ya mmea wa ngano kuyumbayumba, lakini ngano haitaharibika. Hata hivyo, upepo mkali utaongeza mkazo kwenye shina la mmea wa ngano. Upepo mkali wa ghafula, au upepo mwanana unaoendelea kwa muda mrefu waweza kuharibu mmea na kuufanya unyauke.
Twaweza kulinganisha jambo hilo na yale makelele yanayogonga chembe nyororo zilizo kama nywele katika sikio la ndani. Mlio mkubwa wa ghafula unaweza kuharibu sehemu za sikio la ndani na kuacha makovu ambayo huharibu kabisa uwezo wa kusikia. Zaidi ya hilo, sauti kubwa zinazoendelea kwa muda mrefu zinaweza kuharibu kabisa zile chembe dhaifu zilizo kama nywele. Zikiharibika, haziwezi kukua tena. Tokeo ni mvumo sikioni—milio kama ya nyuki, kengele, au mngurumo unaosikika masikioni au kichwani.
Linda na Kudumisha Uwezo Wako wa Kusikia
Ingawa mtu anaweza kuzaliwa na matatizo ya kusikia ama akayapata kupitia msiba usiotazamiwa, tunaweza kujitahidi kulinda na kudumisha uwezo wetu wa kusikia wenye thamani. Ni jambo la hekima kujifunza kimbele kuhusu hatari zinazohusika. Kama vile mtaalamu mmoja wa sauti alivyosema, ‘kungojea mpaka tatizo litokee ndipo uchukue hatua ni kama kuanza kutumia kifaa cha kuzuia mbu baada ya kuambukizwa malaria.’
Jambo la maana mara nyingi ni jinsi tunavyosikiliza bali si kile tunachosikiliza. Kwa mfano, ukitumia vidude vya kusikiliza muziki vinavyovaliwa masikioni, unaweza kuweka sauti ndogo ambayo inaweza kukuruhusu kusikia sauti nyingine. Iwapo redio katika gari lako au nyumbani mwako imefunguliwa sauti ya juu hivi kwamba huwezi kusikia watu wanapozungumza, hiyo ni ishara ya kwamba sauti hiyo imepita kiasi na inaweza kuharibu uwezo wako wa kusikia. Wataalamu huonya kwamba kusikiliza sauti ya desibeli 90 kwa muda wa saa mbili au tatu kunaweza kuharibu masikio yako. Wanapendekeza kuvalia vifaa vya kulinda masikio katika mazingira yenye makelele.
Wazazi wanapaswa kukumbuka kwamba ni rahisi kwa watoto kuharibika masikio kuliko watu wazima. Kumbuka kwamba vitu vya kuchezea vinavyotoa sauti za juu vyaweza kusababisha hatari. Kwani, vitu kama hivyo vinaweza kutoa sauti ya desibeli 110 vinapotikiswa!
Masikio yetu yana viungo vyororo, vidogo, na vya ajabu. Masikio hutuwezesha kusikia sauti zote mbalimbali na zenye kupendeza katika mazingira yetu. Kwa kweli, uwezo huo wa kusikia ambao ni muhimu sana unastahili kulindwa.
[Sanfuku katika ukurasa wa 20]
Makadirio ya Vipimo vya Desibeli vya Sauti Fulani za Kawaida
• Kupumua—desibeli 10
• Mnong’onezo—desibeli 20
• Mazungumzo—desibeli 60
• Wakati wa msongamano wa magari —desibeli 80
• Kifaa cha kusaga chakula—desibeli 90
• Gari-moshi linalopita—desibeli 100
• Msumeno wa umeme—desibeli 110
• Ndege ya jeti inayopita—desibeli 120
• Mlio wa bunduki—desibeli 140
[Sanduku katika ukurasa wa 21]
Huenda Ikawa Unaanza Kupoteza Uwezo Wako wa Kusikia Iwapo
• Unaongeza sauti ya redio au televisheni huku watu wengine wakiona kwamba sauti hiyo ni kubwa kupita kiasi
• Unaendelea kuwaomba wengine warudie yale ambayo wamesema
• Mara nyingi unakunja uso, kuegama, na kugeuza kichwa ili usikie yale ambayo mwenzako anasema
• Unaona ni vigumu kusikia wakati wa mikutano ya hadhara au wakati kuna makelele, kama kwenye vikusanyiko vya kirafiki au katika duka lililo na watu wengi
• Unategemea wengine mara nyingi ili kusikia yale yanayosemwa
[Mchoro katika ukurasa wa 20]
(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)
Sehemu ya nje ya sikio
Mifupa mitatu katika sikio la kati
Kiwambo cha sikio
Komboli
Mishipa ya neva inayoelekea kwenye ubongo