Hamia kwenye habari

Hamia kwenye yaliyomo

Maajabu ya Yai la Mbuni

Maajabu ya Yai la Mbuni

Maajabu ya Yai la Mbuni

NA MWANDISHI WA AMKENI! NCHINI AFRIKA KUSINI

YAI LA MBUNI lililomo katika mashine ya kuangulia halionyeshi ishara yoyote ya mambo yanayoendelea ndani yake wala matukio yenye kuvutia yatakayoanza hivi karibuni. Hata hivyo, hapa penye shamba hili la kufuga mbuni tunaweza kujifunza kuhusu maajabu yote ya mbuni, kuanzia kutagwa kwa mayai.

Kuyatunza Mayai

Mbuni jike hutaga mayai meupe-meupe katika kiota sahili mchangani. Kila moja lina uzito wa kilogramu 1.45 hivi. * Kisha, kila siku, wafanyakazi huchukua mayai yaliyotagwa na kuyaweka katika mashine za kuangulia. Yatakaa humo kwa majuma sita hivi.

Mayai hayo yanayoanguliwa hutunzwa vizuri. Mashine za kuangulia zina halijoto ya nyuzi 37 Selsiasi, na joto hilo linafaa kabisa ili vifaranga wakue ndani ya mayai. Kila siku, mayai hayo hupinduliwa kwa mashine au na mtu ili kiini cha yai kisigandamane na utando wa ganda. Hivyo ndivyo mbuni anavyopindua mayai yake katika kiota chao cha mchanga mbugani.

Kuchungulia Ndani ya Yai

Hata hivyo, tunaweza kujua kile kinachoendelea ndani ya yai namna gani? Mfugaji anachukua yai moja kwa uangalifu, na kuliweka kwenye tundu lililoko katika sehemu ya juu ya sanduku lenye taa nyangavu ndani. Kwa njia hiyo, mfugaji anaweza kuona kile kinachoendelea ndani ya yai. Mfugaji huyachunguza mayai kwa njia hiyo kwa ukawaida ili ajue jinsi vifaranga wanavyoendelea kukua. Endapo mfugaji anaona kwamba yai fulani halina ukuzi wowote ndani yake baada ya kulichunguza mara kadhaa, hatalirudisha katika mashine ya kuangulia.

Yai la mbuni linakaa katika mashine ya kuangulia kwa siku 39. Na kifaranga wa mbuni anakua humo kwa njia ya ajabu. Wakati huohuo, mfuko wa hewa huanza kutokea na hatimaye mfuko huo utachukua thuluthi ya nafasi iliyomo ndani ya yai. * Vifaranga walio ndani ya mayai hufinywa sana, nao wanaanza kujitayarisha kutoka hivi karibuni. Hata hivyo, kwanza ni lazima mfuko wao wa kiini cha yai uanze kuingia matumboni mwao kupitia kiunga-mwana na kitovu chao. Jambo hilo ni muhimu sana kwa kuwa mfuko huo wa kiini cha yai una lishe watakayohitaji hivi karibuni kutoka katika yai na kuanza maisha yao.

Kutoka Katika Mayai

Hatimaye, siku muhimu imefika, nasi tuko tayari kuona tukio la pekee. Kwanza, ni lazima vifaranga wadogo wapasue ule utando na kuingia katika mfuko wa hewa ili waweze kuvunja ganda lenyewe baadaye. Vifaranga wa ndege wengine wana kitu kigumu kwenye ncha ya mdomo wao cha kuvunjia ganda, lakini mbuni wana utando unaokinga mdomo wao laini. Kifaranga huelekeza mdomo wake kwenye ganda huku akitumia upande wa nyuma wa shingo yake kusukuma utando unaomtenganisha na mfuko wa hewa. Baada ya jitihada nyingi za kusukuma, utando huo unavunjika hatimaye, na sasa kifaranga anaweza kutumia nafasi yote iliyomo ndani ya yai.—Ona mchoro wa A.

Mwishowe kifaranga anavuta pumzi kwa mara ya kwanza! Sasa mapafu yake madogo yanafanya kazi. Hata hivyo, kwa sababu ya jitihada hizo zote hewa imekwisha ndani ya yai hilo dogo. Kwa hiyo, kifaranga hawezi kusalimu amri, ni lazima aendelee kupambana na kuvunja ganda. Kwa nguvu yake yote kifaranga hugonga ganda kwa ncha ya mdomo wake. Ghafula, kifaranga aliyechoka sana huona mwangaza hafifu kupitia ufa mdogo katika ganda, na kupitia ufa huo sasa anaweza kupumua hewa safi.—Ona mchoro wa B.

Baada ya kupumzika, kifaranga hupata nguvu ya kuendelea kuvunjavunja ganda kwa kutumia mguu wake wa kulia na mdomo wake mdogo wenye utando wa kinga. Kisha, kifaranga huyo hupasua kwa nguvu ganda na kujaribu kukaa vizuri. Mbuni huyo mchanga aliyetoka tu kuanguliwa hutazama mazingira yake kwa mshangao na kujaribu kujiendesha kwa madaha na kwa kujitumaini kwa kadiri awezavyo.—Ona mchoro wa C.

Kwa nini mfugaji hamsaidii kifaranga huyo mdogo anapopambana sana kutoka katika yai? Hiyo ni kwa faida ya kifaranga huyo kwa sababu inachukua muda fulani kwa kiini cha yai kuingia tumboni mwa kifaranga kupitia kitovu chake, kisha kitovu hicho hufungika. Mtu akijaribu kumsaidia kiumbe huyo dhaifu ili kuharakisha atoke anaweza kumjeruhi au kusababisha ugonjwa mbaya.

Hata hivyo, mwishowe vifaranga hao wadogo wamefaulu kutoka katika mayai yao. Sisi watazamaji, tunavutiwa sana kuona vifaranga hao wachovu wakiibuka katikati ya vipande vingi vya maganda.

Vifaranga Wanakutana na Wazazi Walezi

Baada ya muda mfupi, manyoya mororo ya vifaranga hao wanaovutia hukaushwa na hewa yenye joto ya mashine ya kuangulia. Kisha, wao hupelekwa nje kwenye kizimba kidogo kwenye jua. Inaonekana wanafurahia jambo hilo sana! Mwishowe wanaweza kutembeatembea kwa miguu yao midogo inayotetemeka-tetemeka.

Kesho yake ndiyo siku muhimu kwa ndege hao wenye manyoya mororo. Wanapelekwa kwa wazazi wao walezi, mbuni wakomavu watakaowatunza kwa muda wa miezi mitatu ijayo. Hadi wakati huu, vifaranga hao hawajasikia njaa kwa sababu wamepata lishe kutokana na kiini chao cha yai. Hata hivyo, siku kadhaa baada ya kuanguliwa wanaanza kusikia njaa. Lakini watakula nini? Tunashangaa kuona kwamba vifaranga hao wanaanza kula mavi ya mbuni wanaowalea! Mfugaji anaeleza kwamba huenda jambo hilo likasaidia kujenga mfumo wao wa kinga ambao haujakomaa.

Ona jinsi vifaranga hao wanavyojaribu sana kwenda sambamba na wazazi wao walezi wenye miguu mirefu! Bila shaka jambo hilo si rahisi. Lakini vifaranga wa mbuni hukua haraka sana—sentimeta 30 kwa mwezi. Kwa hiyo, baada ya mwezi mmoja tu wanaweza kufuatana na mbuni wakubwa bila shida.

Vifaranga hao watakapokuwa na umri wa miezi sita watakuwa mbuni wakomavu, na watafikia urefu wa meta mbili na nusu hivi. Ni vigumu kuwazia kwamba miezi saba tu iliyopita viumbe hao wenye miguu mirefu na shingo ndefu walikuwa mayai yasiyoweza kusogea katika mashine ya kuangulia kwenye shamba la kufuga mbuni.

[Maelezo ya Chini]

^ fu. 5 Ili upate habari zaidi kumhusu mbuni, tafadhali, ona makala ya “Mwenye Mwendo wa Kasi, Asiyepuruka, na Anayevutia Sana—Mbuni,” katika toleo la Amkeni! la Julai 22, 1999, ukurasa wa 16-18.

^ fu. 9 Yai la mbuni “lina vitundu vingi vinavyowezesha hewa kuingia ndani ya yai. Kwa sababu ya mvukizo unaoanza baada ya yai kutagwa, nafasi ya hewa hutokea katikati ya tando mbili za ganda katika upande mnene wa yai.”—Ostrich Farming in the Little Karoo.

[Mchoro katika ukurasa wa 23]

(Ona mpangilio kamili katika nakala iliyochapishwa)

JINSI KIFARANGA ANAVYOANGULIWA

A

B

C

[Hisani]

Michoro ni ya: Dr. D. C. Deeming

[Picha katika ukurasa wa 23]

Siku muhimu—vifaranga wanatoka katika mayai!

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 25]

John Dominis/Index Stock Photography